Header Ads Widget

Ticker

6/recent/ticker-posts

Waziri Kairuki awakaribisha wawekezaji kutoka Ujerumani




Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki akimkabidhi nyaraka zenye taarifa za uwekezaji  Bw.Uwe Raschke Mkurugenzi wa Bodi ya kampuni ya Bosch baada ya kufanya mazungumzo


6 Februari 2019, TIC, Dar es Salaam; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki amepokea ujumbe wa wafanyabiashara wapatao 11 kutoka nchi ya Ujerumani na kufanya mazungumzo. Ujumbe huo ni kutoka kampuni ya Bosch na umeongozwa na Naibu Balozi wa Ujerumani nchini Mhe. Jörg Herrera. Kampuni ya Bosch ni maarufu katika uwekezaji kwenye mashine za magari, mifumo ya tehama, mashine zinazotumika migodini, mashine za ulinzi na usalama, vifaa vya majumbani (frige, majiko) pamoja na vifaa vingine.

Katika mazungumzo na Waziri, kampuni ya hiyo imeeleza kupendezwa na mazingira ya biashara na uwekezaji yaliyopo nchini kwa sasa na kwamba yamewavutia kuja kuwekeza tofauti na ilivyokuwa awali. Aidha mwakilishi wa kampuni hiyo Bw. Uwe Raschke ameainisha maeneo ambayo kampuni hii ina nia ya kuwekeza kuwa ni kwenye mifumo ya tehema ya usalama katika migodi, viwanja vya ndege, mawasiliano ya reli, mifumo ya magari ya abiria na mizigo, kujenga vituo vya kukagua na kutengeneza magari mabovu automobile repair and inspection centres, kiwanda cha kutengeneza heater za maji zinazotumia gesi na elimu ya utaalam wa ufundi stadi. 


Mheshimiwa Kairuki akizungumza na msafara wa wafanyabiashara kutoka Ujerumani kampuni ya Bosch na wawakilishi wa taasisi za Serikali kwenye ukumbi wa mikutano wa TIC.

 Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Kairuki ameishukuru kampuni ya Bosch kwa kufikiria kuwekeza Tanzania na kwamba uamuzi wao sio wa bahati mbaya  bali ni hakika kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo, soko la uhakika na utayari wa serikali katika kuwasaidia kufanikisha miradi wanayotarajia kuianzisha ikiwamo kupata vibali na leseni za uwekezaji zinazotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) chini ya mfumo wa Huduma za Mahala Pamoja ‘One Stop Facilitation Centre’. Vilevile Mhe. Waziri ameainisha fursa na maeneo ya uwekezaji kwa kampuni hiyo kuwa ni viwanda, madini, tehama, kuunganisha magari, kuzalisha na kusambaza umeme, mafuta na gesi.

Mhe. Waziri akijadiliana jambo na  Naibu Balozi wa Ujerumani nchini Mhe. Jörg Herrera (katikati) pamoja na Bw.Uwe Uwe Raschke
Katika kuhakikisha kwamba ujumbe huo unapata taarifa na ufafanuzi zaidi kuhusu fursa zilizopo na miradi/maeneo ambayo nchi inaweza kushirikiana na kampuni ya Bosch, taasisi mbalimbali za serikali zilishiriki ili kuelezea. Taasisi zilizoshiriki ni Wizara ya Madini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Shirika la Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), Wakala wa Ujenzi (TBA) na wenyeji Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).  Aidha Mhe. Kairuki pia amewataka sekta binafsi kuchangamkia fursa hii na kuangalia namna ambavyo wanaweza kushirikiana na kampuni ya Bosch katika biashara na uwekezaji kwenye maeneo yaliyoainishwa. 

Tayari baadhi ya vifaa vya kampuni ya Bosch vimenunuliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kwa lengo la kutumika kwenye uendeshaji wa shughuli mbalimbali katika uwanja mpya Terminal 3, Julius Nyerere Airport.
Wawakilishi wa taasisi za serikali walishiriki kikao cha Mhe Kairuki na ugeni kutoka Ujerumani
Kampuni ya Bosch imekuwepo Afrika katika nchi takribani 13 lakini bado ilikuwa haijafanya uwekezaji Tanzania. Hivi sasa kampuni hii imeridhishwa na kuvutiwa na mazingira ya uwekezaji yaliyopo nchini na yamewashawishi kufanya maamuzi ya kuja kuwekeza. Taasisi za serikali na sekta binafsi zijipange kutoa ushirikiano utakaohitajika kwa kwa kampuni hii ili kufanikisha uwekezaji wao unaotarajiwa kuleta uwekezaji wa ubia, tekinolojia, uzalishaji wa bidhaa bora zenye gharama nafuu, kutengeneza ajira na kuongeza pato la Taifa kiujumla.  
Timu ya ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Ujerumani katika kikao cha pamoja na Mhe Waziri Kairuki


Post a Comment

0 Comments