Mwakilishi
wa Kampuni ya kuzalisha vifaa vya umeme ya Elsewedy Electric ambaye ni
Mkurugenzi Mkaazi wa Afrika Mashariki wa Kampuni hiyo injinia Ibrahim
Qamar kutoka nchini Misri anayewekeza nchini Tanzania amesema kuimarika
kwa Sera, Sheria na mazingira mazuri ya Uwekezaji Nchini Tanzania ikiwa
ni pamoja na amani na utulivu; ndio sababu kubwa zilizomfanya aje
kuwekeza nchini.
Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Dkt. Maduhu Isaac Kazi (Mwenye
Tai Nyekundu Kulia) akiwa katika Picha ya Pamoja na Injinia Ibrahim
Qamar, Mwakilishi Mwekezaji wa Kampuni ya Elsewedy ya Misri anaewekeza
Nchini kwa kujenga Kiwanda cha Vifaa vya umeme na Chuo cha fani ya Umeme
Bw.
Qamar amesema miongoni mwa masuala ambayo wawekezaji wengi huyaangalia
kwa makini kwenye nchi wanazotaka kuwekeza ni pamoja na Utawala bora,
ulinzi wa mitaji yao pamoja na masoko ya uhakika mambo ambayo Tanzania
imeyapa kipaumbele na hivyo kumfanya yeye na wawekezaji wengine
kufikiria na kuamua kuwekeza Tanzania
Bw.
Qamar alitembelea ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC mwishoni
mwa juma lililopita na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa
Kituo hicho Dkt. Maduhu Kazi ambapo alimwambia kutokana na kazi nzuri
wanayoifanya, ameamua kuwekeza katika miradi miwili mikubwa ikiwa ni
pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha kutengeneza vifaa vya Umeme pamoja na
Chuo cha mafunzo ya umeme, uwekezaji ambao unatarajia kufanyika kwa
awamu mbili na baadae huenda atafanya uwekezaji katika viwanda vya
kutengeneza vifaa na kujenga miundombinu ya kuzalisha umeme wa jua na
upepo.
Awamu ya kwanza
ya uwekezaji huu ambao unapanga kuwekeza mtaji wa Dola za Marekani
milioni kumi na tano (15) na kuzalisha ajira za moja kwa moja mia moja
kumi na tano (115) unatarajia kuanza mara moja baada ya taratibu za
ardhi kukamilika katika wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam.
Mwekezaji huyu pia aliishukuru TIC kwa jitihada za kuhakikisha
inasimamia upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji huo ambao utakuwa
na tija kubwa kwa Taifa na Jamii ya Tanzania.
“TIC mnafanya kazi kubwa
ya kuhakikisha wawekezaji tunapata fursa ya kuwekeza hapa Tanzania,
mmetusaidia sana kupata ardhi kule kigamboni ambayo tulikuwa tukiihitaji
kwa muda mrefu na kulikuwa na ucheleweshaji katika hatua za kuipata,
lakini niseme tu, baada ya TIC kuingilia kati suala hili, nimeona
mafanikio makubwa sana na nawaahidi sitawaangusha katika uwekezaji huu
mkubwa ambao najua utakuwa na manufaa kwa pande zote mbili" alisema Injinia Qamar.
Aidha alitaja kusudio lake la ujenzi wa Kiwanda na Chuo cha masuala ya Umeme
"Nakusudia
kujenga kiwanda cha vifaa vya umeme vikiwepo Mita, Waya na Transifoma,
pia tutafungua chuo cha masuala hayo nikutaarifu tu kuwa awamu ya kwanza
tutaianza mara moja, pale taratibu za kupata ardhi zitakapokamilika
ambapo naona tupo katika hatua za mwisho kabisa na mimi nimeshajipanga
vizuri kabisa ili niweze kuanza” alisema Bw. Qamar.
Mkurugenzi Mtendaji
wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt. Maduhu Isaac Kazi (Kulia)
akijadiliana jambo na Mwakilishi wa Kampuni ya Elsewedy ya Misri Injinia
Ibrahim Qamar mapema Juzi katika Ofisi za TIC zilizopo Mtaa wa Shaban
Robert Posta Jijini Sar Es Salaam, katikati ni Mkuu wa Idara ya
Huduma kwa Wawekezaji Bw. Revocatus Arbogast Rasheli akifuatilia kwa
makini mjadala huo.
Pia
alimshumshukuru Mkrugenzi Mtendaji wa TIC Dk. Maduhu Kazi kwa
kutembelea ofisi za kampuni ya Elsewedy Electric Jijini Dar es Salaam
muda kifupi baada ya kuteuliwa kuiongoza taasisi hiyo ya Uwekezaji
nchini ambapo alipata fursa ya kujua mpango wa kampuni wa uwekezaji
pamoja na changamoto zilizokuwa zinaukabili uwekezaji huo hivyo
kukwamisha uwekezaji wa kampuni hiyo nchini ambapo katika ziara hiyo TIC
ilimhakikishia mwekezaji Elsewedy kuwa TIC ingeshughulikia changamoto
hizo kwa kasi sambamba na miradi mingine ambayo uwekezaji wake ulikwama
kwa sababu za kiutendaji.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt
Maduhu Kazi amesema Kituo hicho kinahudumia wawekezaji wote na kwamba
endapo kuna changamoto zozote wanazokutana nazo wasisite kuziwasilisha
katika ofisi za TIC zilizopo katika kanda na hata hapa makao Makuu.
Aidha Dkt. Kazi amesema jitihada alizozifanya Mh. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli katika kuboresha mazingira
ya Uwekezaji na Biashara yamesaidia wawekezaji wengi kuiamini Tanzania
kama nchi salama kwa kuwekeza mitaji yao.
“Milango ya TIC ipo wazi
wakati wote, tunawakaribisha sana na endapo mna changamoto zozote
msisite kuja, hii ni kazi yetu” alisema Dkt Kazi.
Aidha aliwataka
wawekezaji wengine kuja kuwekeza nchini kutokana na kuimarika kwa Sera
na sheria za Uwekezaji zilizofanywa na Serikali ya awamu ya tano hatua
inayoleta manufaa makubwa kwenye sekta ya uwekezaji nchini na kuwezesha
kufikiwa kwa azma ya Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda kama
ilivyobainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
Alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia Oktoba 2015
hadi sasa Serikali imefuta kodi na tozo mbalimbali 168 ambazo zilikuwa
kero kwa wawekezaji na pia katika kipindi hicho hakuna kodi yoyote mpya
iliyoanzishwa na Serikali hatua inayoendelea kuipaisha Tanzania katika
kuvutia Uwekezaji.
0 Comments