Header Ads Widget

Ticker

6/recent/ticker-posts

Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2020/2021

HOTUBA YA WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI MHESHIMIWALUHAGA JOELSON MPINA (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KWA MWAKA2020/2021 A. UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, kutokana na taarifa iliyowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayosimamia Kilimo, Mifugo na Maji iliyochambua Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Fungu 99 – Mifugo na Fungu 64 – Uvuvi) Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2019/2020. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2020/2021. 2. 

Mheshimiwa Spika, Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha hotuba yangu siku ya leo. Aidha, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kushika wadhifa huu. Pia, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuiongoza nchi yetu kwa uhodari na umahiri mkubwa kwa takriban miaka mitano (5) tangu aingie madarakani. Katika kipindi hicho tumeshuhudia maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii, umahiri na uhodari wake katika kuiongoza nchi yetu umegusa na kusisimua Taasisi za Kimataifa, Afrika na Dunia pia amekuwa kiongozi wa mfano na gumzo kila kona Mungu ambariki Rais wetu ili aendeleze mapambano ya kutafuta maendeleo ya kweli ya Watanzania, Waafrika na Dunia.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua anazochukua katika kipindi hiki kigumu cha janga la ugonjwa wa CORONA (COVID – 19) unaoambukizwa na Virusi vya Corona, Rais wetu amewaondolea hofu watanzania na kuweka msimamo usioyumba katika kukabiliana na janga hili jambo lililowezesha watanzania kuendelea na shughuli zao za kiuchumi huku wakichukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo. 

Mheshimiwa Spika, nawapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Ally Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna wanavyomsaidia Mhe. Rais kuiongoza vema nchi yetu kwa hekima na busara.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwasilisha hotuba yake iliyotoa mwelekeo wa utendaji wa sekta zote katika Serikali. Pia, namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) Waziri wa Fedha na Mipango, kwa wasilisho lake la Mpango wa Bajeti ambao umefafanua vizuri mipango na mikakati ya Serikali katika mwaka wa fedha 2020/2021 wenye lengo la kuimarisha na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii nchini. 

Mheshimiwa Spika, napenda pia kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuliongoza vizuri Bunge letu Tukufu. Uongozi wenu bora umewezesha Bunge la 11 kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Mahamoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini na Makamu wake Mhe. Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Morogoro kwa ushirikiano, maelekezo na ushauri mzuri walioutoa wakati wa kupitia Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2019/2020 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2020/2021. 

Aidha, napenda kuwapongeza Mhe. Justine Monko, Mbunge wa Singida Kaskazini, Mhe. Miraji Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashiriki, Mhe. Dkt. John Daniel Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki kwa kuchaguliwa na kisha kuapishwa na Bunge lako Tukufu ili wawatumikie wananchi waliowachagua.

Mheshimiwa Spika, Wizara ilipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Mhe. Balozi. Dkt. Augustine Philip Mahiga, Mbunge wa Kuteuliwa na Waziri wa Sheria na Katiba; Mhe. Ajali Rashid Akbar, Mbunge wa Newala Vijijini; Mhe. Askofu Dkt. Getrude Pangalile Rwakatare, Mbunge wa Viti Maalum Morogoro; na Mhe. Richard Mganga Ndassa, Mbunge wa Sumve; Naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa salaam za pole kwa familia za marehemu, ndugu na wananchi ambao walikuwa wanatumikiwa na Wabunge hao. Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, AMINA. 

Aidha, naomba nitumie fursa hii kuwapa pole Waheshimiwa Wabunge waliopata ajali mbalimbali na waliougua katika kipindi cha mwaka 2019/2020.

Napenda pia kuwapa pole wale waliopoteza ndugu zao na wapendwa wao kutokana na Ugonjwa wa Corona (COVID – 19)(COVID – 19), ninawaombea kila la kheri wale ambao wameambukizwa ugonjwa huo ili Mungu awape afya njema mapema iwezekanavyo. 

Tuendelee kuzingatia maelekezo ya kitaalamu yanayotolewa na viongozi mbalimbali kwa ajili ya tahadhari huku tukiendelea kufanya kazi kwa bidii ili uchumi wetu usitetereke.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nichukue nafasi hii ya pekee kumpongeza Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kumshukuru Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Hamis Ulega, Mbunge wa Jimbo la Mkuranga kwa jinsi alivyonisaidia katika kuiongoza wizara hii hakika wananchi wa Mkuranga wamepata mwakilishi makini ndani ya Bunge na Serikali na ninaamini kwamba wataendelea kumuunga mkono, pia nawashukuru Makatibu Wakuu wa Wizara Dkt. Rashid Adam Tamatamah (Uvuvi) na Prof. Elisante Ole Gabriel (Mifugo) kwa kuwa kiungo kikubwa cha watumishi na kuwezesha kutekeleza majukumu ya wizara kwa ufanisi. Aidha, ninawashukuru kwa dhati na kuwapongeza watumishi wote wa Wizara yangu kwa kazi nzuri mnayofanya.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa mara nyingine tena niwapongeze na kuwashukuru wananchi wa Jimbo ninaloliwakilisha, yaani jimbo la Kisesa, lililopo Mkoa wa Simiyu, kwa kunichagua na kwa ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kuwawakilisha na kuwatumikia katikaBunge hili Tukufu.

SEKTA YA MIFUGO (FUNGU 99)

HALI HALISI YA SEKTA YA MIFUGO 

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020 idadi ya mifugo hapa nchini inakadiriwa kuongezeka ikilinganishwa na mwaka 2018/2019 ambapo idadi ya ng’ombe imeongezeka kutoka milioni 32.23 hadi milioni 33.4, mbuzi kutoka milioni 20 hadi milioni 21.29 na kondoo kutoka milioni 5.5 hadi milioni 5.65. Aidha, kuku wameongezeka kutoka milioni 79.1 hadi milioni 83.28 ikiwa kuku wa asili wameongezeka kutoka milioni 38.5 hadi milioni 38.77, kuku wa kisasa wameongezeka kutoka milioni 40.6 hadi milioni 44.51, nguruwe kutoka milioni 2 hadi milioni 2.14 na punda kutoka 636,997 hadi 657,389 (Taarifa ya Uchambuzi wa Sekta ya Mifugo Tanzania 2016/2017 - 2031/2032). Aidha, Sekta ya Mifugo katika mwaka 2019 ilikua kwa asilimia5na kuchangia asilimia7.4katika Pato la Taifa ikilinganishwa na kukua kwa  asilimia 4.9 na kuchangia asilimia 7.2 katika Pato la Taifa mwaka 2018.

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa maziwa umeongezeka kwa asilimia 12.1 kutoka lita bilioni 2.7 mwaka 2018/2019 hadi kufikia lita bilioni 3.0 mwaka 2019/2020 (Taarifa ya Uchambuzi wa Sekta ya Mifugo Tanzania 2016/2017 - 2031/2032), ambapo kati ya hizo, lita bilioni 2.1 zilitokana na ng’ombe wa asili na lita bilioni 0.9 zilitokana na ng’ombe wa kisasa (Kiambatisho Na. 1). Aidha, kati ya ng’ombe milioni33.4waliopo nchini ng’ombe wa maziwa nimilioni1.95(TLMP).

Mheshimiwa Spika, usindikaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita milioni 70.9 mwaka 2018/2019 hadi lita milioni 74.3 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 4.8. Hadi sasa, kuna viwanda vya kusindika maziwa 99 kati ya hivyo, viwanda 91 vinafanya kazi na viwanda 8 havifanyi kazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo migogoro miongoni mwa wanaushirika na kushindwa katika ushindani wa kibiashara.

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa zao la nyama umeongezeka kutoka tani 690,629 mwaka 2018/2019 hadi tani 701,679.1 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 1.6 (Kiambatisho Na. 1). Kati ya hizo, tani 486,736.1 za nyama ya ng’ombe, tani 95,964.2 za nyama ya mbuzi na kondoo, tani 80,601.3 za nyama ya kuku na tani 38,377.4 za nyama ya nguruwe. Aidha, ng’ombe walionenepeshwa wameongezeka kutoka ng’ombe 371,200 mwaka 2018/2019 hadi kufikia ng’ombe 512,256 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia38.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 uzalishaji wa mayai umeongezeka kutoka mayai bilioni 3.58 mwaka 2018/2019 hadi mayai bilioni 4.05mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 13.3 (Kiambatisho Na. 1). Ongezeko hilo limesababishwa na kuongezeka kwa vituo vya kutotolesha vifaranga vya kuku.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2020 jumla ya kilo za ngozi 16,746,589.36 (ng’ombe - 14,449,075.49, mbuzi - 1,775,298.5 na kondoo - 522,215.38) zenye thamani ya shilingi bilioni 23.9 zimezalishwa ikilinganishwa na kilo 16,012,800.71 (ng’ombe - 13,904,620.27, mbuzi 1,653,669.26 na kondoo - 454,511.17) zenye thamani ya shilingi bilioni 22.8 zilizozalishwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2020 jumla ya vipande vya ngozi vyenye uzito wa Kilo 6,747,011 (ng’ombe – 5,948,791, mbuzi/kondoo 114,904 na punda - 683,317) vyenye thamani ya shilingi bilioni 12.90viliuzwa nje ya nchi, katika nchi za Ghana, China, Pakistani, Indonesia, Ethiopia, Nigeria na Italy (Kiambatisho Na. 3) ikilinganishwa na kilo 5,384,735.79 (ng’ombe – 4,588,579.56, mbuzi/kondoo 660,369.69na punda - 114,800.00) vyenye thamani ya shilingi bilioni 13.0 vilivyouzwa nje katika nchi za Nigeria, Ghana, Ethiopia, China, Italy, Kenya, India, Misri, Uturuki, Pakistani na Beninmwaka 2018/2019.

UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2019/2020 NA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2020 /2021

Maeneo ya Kipaumbele katika Mwaka 2019/2020

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 maeneo ya kipaumbele katika Mpango na Bajeti ya Wizara kupitia Idara Kuu ya Mifugo (Fungu 99) yatakayotekelezwa ni pamoja na:

(i) Kuimarisha afya ya mifugo;

(ii) Kuwezesha upatikanaji endelevu wa rasilimali za vyakula vya mifugo na maji kwa ajili ya mifugo; 

(iii) Kuboresha kosaafu ya mifugo ili kuongeza tija na uzalishaji: 

(iv) Kuboresha biashara ya mifugo ndani na nje: 

(v) Kuimarisha huduma za utafiti wa mifugo, huduma za ugani na mafunzo kwa wafugaji na maafisa ugani; 

(vi) Kuanzisha na kuimarisha vikundi na vyama vya ushirika vya mazao ya mifugo; 

(vii) Kusimamia na kuratibu shughuli za taasisi zilizo chini ya Wizara; 

(viii) Kuboresha masuala ya rasilimali watu; 

(ix) Kuboresha utekelezaji wa sera, sheria na kanuni katika sekta ya mifugo;na

(x) Kuimarisha uratibu na usimamizi wa wataalamu wa sekta ya mifugo.
Makusanyo ya Maduhuli

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Fungu 99 ilitarajia kukusanya kiasi cha shilingi 50,000,000,000.00. Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2020 kiasi cha shilingi 38,501,236,284.25 kimekusanywa sawa na asilimia 77 ya lengo la makusanyo kwa mwaka 2019/2020. Hata hivyo, makusanyo hayo ni sawa na asilimia 92.41 ya makusanyo yaliyolengwa kukusanywa ndani ya kipindi cha miezi kumi (10) ambayo ni shilingi bilioni 41.66. Makusanyo hayo hadi Aprili, 2020 (38,501,236,284.25) yameongezeka kwa shilingi 6,361,524,248.03 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2018/2019 ambapo makusanyo yalifikia shilingi 32,139,712,036.22
Fedha Zilizoidhinishwakwa Ajili ya Matumizi ya Kawaida na Maendeleo 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Fungu 99 ilitengewa jumla ya shilingi 31,774,378,000.00. Kati ya Fedha hizo, shilingi 28,774,378,000.00 ni fedha za Matumizi ya Kawaida na shilingi 3,000,000,000.00 ni fedha kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo.

Matumizi ya Bajeti ya Kawaida 22. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Fungu 99 lilitengewa jumla ya shilingi 28,774,378,000.00. Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2020, jumla ya shilingi 22,146,054,084.63zilikuwa zimetolewa, ambazo ni sawa na asilimia 76.96 ya bajeti iliyotarajiwa kwa miezi kumi na miwili, ikiwa ni sawa na asilimia 92.36 ya kipindi cha miezi kumi (yaani hadi 30 Aprili, 2020). Kati ya hizo, shilingi 12,783,043,056.50 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Wizara (PE) na shilingi 9,363,011,028.13 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC).

Matumizi ya Bajeti ya Maendeleo 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Fungu 99 ilitengewa jumla ya shilingi3,000,000,000.00kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo zikiwa ni fedha za ndani ili kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2020 kiasi cha shilingi 328,821,307.00 (sawa na asilimia 10.9) kilipokelewa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.

Sera, Sheria na Kanuni Katika Sekta ya Mifugo.

Sera, Mikakati na Programu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara imeendelea kutoa elimu kuhusu Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 na Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo Tanzania (Tanzania Livestock Master Plan TLMP). Jumla ya wadau 7,835 walipata elimu hiyo kupitia Maonesho ya Sabasaba, Nanenane na Siku ya Chakula Duniani. Aidha, Wizara imesambaza nakala 150 za Sera ya Taifa ya Mifugo na nakala120za Fursa za Uwekezaji kwa wadau katika Sekta ya Mifugo. Vilevile, Wizara imeendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agriculture Sector Development Programme–ASDP II).

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itaendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agriculture Sector Development Programme – ASDP II) na kuandaa Mpango Mkakati wa Wizara kwa mwaka 2020/2021 hadi 2025/2026, kukamilisha tathmini ya Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya mifugo, Wakala, Bodi na Taasisi zilizo chini ya Wizara.

Sheria na Kanuni.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kupitia Sheria za sekta ya mifugo kwa ajili ya kuboresha mazingira na kuwezesha ukuaji wa sekta ya mifugo ambapo marekebisho ya Sheria za Ustawi wa Wanyama SURA 154 na Sheria ya Magonjwa ya Mifugo SURA 156 yamefanyika kupitia Written Laws Miscelleneous Amendments Act 2019, Act No.14 of 2019. Aidha, marekebisho ya Sheria za Tasnia ya Maziwa SURA 262 na Sheria ya Tasnia ya Nyama SURA 412 yamefanyika kupitia Written Laws Miscelleneous Amendments, Act 2020, Act No.1 of 2020.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo SURA 180 yaliyopo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Written Laws Miscelleneous Amendments Act 2020) tayari yameshasomwa kwa mara ya kwanza katika kikao cha Bunge la Mwezi Januari, 2020.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa Kanuni mbalimbali chini ya Sheria ya Magonjwa ya Wanyama SURA 156 na kutangaza katika Gazeti la Serikali kwa ajili ya kuanza kutumika ili kutatua changamoto mbalimbali katika Sekta ya Mifugo (Kiambatisho Na. 4), kanuni hizo ni:

(i) Animal Diseases (Acaricide Application and Management) Regulations, 2019 GN. No. 955; 

(ii) Animal Diseases (Hatcharies and Breeding Flock Farms) Regulations, 2019 GN. No.956; 

(iii)Animal Diseases (Artificial Breeding) Regulations, 2020 GN. No.118 

(iv)Animal Diseases (Regional Veterinary Officers and District Veterinary Oficers) Notice, 2019 GN. No.66; na 

(v) The Animal Diseases (Vaccines and Vaccination) Regulations, 2020 GN. Na. 180

Mheshimiwa Spika, Wizara imefanya marekebisho ya tozo katika Kanuni za Magonjwa ya Wanyama (Animal and Animal Products Movements Control) 2020 na kuwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango. Aidha, kanuni mbalimbali chini ya Sheria ya Veterinari SURA 319 zimeandaliwa na kutangazwa katika Gazeti la Serikali kwa ajili ya kuanza kutumika. Kanuni hizo ni:

(i) The Veterinary (Appointment of Veterinary Inspectors)Notice,2020  GN No.132; 

(ii) The Veterinary (Cancellation of Veterinarians) Notice, 2020 GN No. 133; na 

(iii) The Veterinary (Registration of Veterinarians and Veterinary Practise Facility (Amendment) Regulations, 2020 GN No. 134.

Mheshimiwa Spika, chini ya Sheria ya Tasnia ya Nyama SURA 412 kanuni mbalimbali zimeandaliwa na kutangazwa katika Gazeti la Serikali kwa ajili ya kuanza kutumika. Kanuni hizo ni:

(i) Meat Industry (Import and Export of Livestock, Meat and Meat Products) (Amendment), 2019 GN.No.538; 

(ii) Meat Industry (Registration of Meat Industry Stakeholders) (Amendment), 2019 GN.No.677; na 

(iii) Meat Industry (Inspection of Meat Industry Stakeholders Activities) 2019 GN.No.739.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara imeandaa Kanuni chini ya Sheria ya Tasnia ya Maziwa (SURA 262), Ustawi wa Wanyama (SURA 154) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (SURA 434) ambazo zimepitiwa na kuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kanuni hizo ni:

(i) The Dairy Industry (Registration of Dairy Industry Stakeholders)(Amendment) Regulations, 2020; 

(ii) The Dairy Industry (Raw Milk Transportation) (Amendment)Regulations, 2020; (iii) The Dairy Industry (Treatment and Disposal of Unfit Milk) (Amendment) Regulations, 2020;

(iv) The Dairy Industry (Duties and Powers of the Inspectors and Analysts) (Amendment)Regulations, 2020; 

(v) The Dairy Industry (Raw Milk  Grading and Minimum Quality and Safety Requirement) (Amendment)Regulations, 2020; 

(vi) The Dairy Industry (Import and Export of Milk and Milk Products) (Amendment) Regulations, 2020 

(vii) The Animal Welfare (Impounded Animal)Regulations, 2020 

(viii) The Animal Welfare(Humane Slaughter and Killing of Animals) Regulations, 2020 and 

(ix) Livestock Research  Regulations, 2020

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kuratibu na kuboresha Sheria, Kanuni na Taratibu kuhusu ubora wa bidhaa za mifugo, pembejeo na huduma za kisheria.

Uzalishajiwa Mifugo wa Masoko Huduma ya Uhimilishaji 33. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI pamoja na Public Private Partnership for Artificial Insemination Delivery (PAID), African Dairy Genetic Gain (ADGG) pamoja na Kituo cha Taifa cha uhimilishaji (NAIC) imeandaa na kutekeleza Muundo wa Biashara ya Uhimilishaji (Dairy Business Model) na kufanya majaribio katika maeneo ya mfano (Pilot areas)yaKawe na Mabwepande katika Manispaa ya Kinondoni; Chanika na Kinyerezi katika Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam. Aidha, lengo la Dairy Business Modelni kuzijengea uwezo Halmashauri na wafugaji kuweza kumudu gharama za uhimilishaji kibiashara pindi muda wa utekelezaji wa miradi ya PAID na ADGG utakapomaliza muda wake. Pia, jumla ya ng’ombe 76,612 wamehimilishwa katika Mikoa 21ya Tanzania Bara (Kiambatisho Na.5a).

Mheshimiwa Spika, kati ya ng’ombe waliohimilishwa, ng’ombe 4,668 wamehimilishwa bure na Wizara kupitia kambi za uhimilishaji zilizoanzishwa katika Mikoa ya Dodoma, Simiyu, Katavi, Geita na Kagera (Kiambatisho Na.5b) ambapo kiwango cha ushikaji mimba “conception rate“ ni asilimia 60. Kambi za uhimilishaji zimechochea hamasa kubwa kwa wananchi kuhimilisha mifugo yao ili kuboresha mbari za mifugo. Aidha, Wizara inaendelea kufuatilia viwango vya ushikaji mimba kutoka kwenye mikoa husika.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Kanuni za Uhimilishaji Animal Diseases (Artificial Breeding) Regulations, 2020 GN. No.118 ambazo zimetoa bei elekezi ya kuhimilisha ng’ombe isiyozidi shilingi 10,000 kwa mpandisho mmoja bila kichocheo (Hormone) ikilinganishwa na gharama ya shilingi 25,000 kabla ya kanuni hiyo. Ili kuwezesha mafanikio na ufanisi wa kanuni hizi Wizara imetekeleza yafuatayo:(i) Wahimilishaji 37 katika Halmashauri 8 wamejengewa uwezo kwa vitendo kuhusu uhimilishaji. (ii) Wataalam wa uhimilishaji waliopata mafunzo ya uhimilishaji kwa nadharia na vitendo wameongezeka kutoka 333 2018/2019 hadi kufikia watalam 441 mwaka 2019/2020. (iii) Lita 7,441.25 za kimiminika baridi cha Naitrojeni zilisambazwa kwenye Vituo vya Kanda vya Uhimilishaji. 36. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kuimarisha Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), Vituo saba (7) vya Kanda vya Uhimilishaji na kuwezesha kambi za uhimilishaji kuhimilisha ng’ombe 100,000 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs).

Uzalishajina Usambazaji wa Mitamba 37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 jumla ya mitamba 18,255 ya maziwa imezalishwa kati ya hiyo mitamba 2,349 wametoka kwenye Mashamba ya Serikali (Kiambatisho Na. 6) na mitamba 15,906 kutoka kwa wafugaji binafsi ikilinganishwa na mitamba 619 iliyozalishwa na kuuzwa kutoka katika Mashamba ya Serikali na mitamba 14,460 kutoka kwa wafugaji binafsimwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itanunua mitamba 53 ya boran wazazi kwa ajili ya Shamba la Kuzalisha Mitamba Nangaramo (LMU) na madume matano (5) ya Friesian kwa ajili ya Shamba la Kuzalisha Mitamba Kitulo (LMU). Aidha, uhamasishaji wa wadau ili kuwekeza kwenye mashamba binafsi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mitamba unaendelea.

Uzalishaji waKuku na Mayai 39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, jumla ya vifaranga 70,323,000 vimezalishwa na kusambazwa nchini. Kati ya hivyo,  vifaranga 60,463,872 ni wa nyama, vifaranga 7,860,000 ni wa kuku chotara hususan Sasso na Kroiler na vifaranga 1,999,128 ni wa kuku wa mayai ikilinganishwa na vifaranga 50,928,000 vilivyozalishwa mwaka 2018/2019. Aidha, Wizara ilitoa vibali vya kusafirisha nje ya nchi vifaranga vya kuku wazazi 850,000wa nyama na mayai katika nchi za Kenya, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Comoro, Malawi, Korea Kusini na Uturuki. Vilevile, Wizara imetoa vibali maalum vya kuingiza kuku wazazi 750,000 wa nyama na mayai kutoka Uholanzi, Ufaransa, Zambia na India ikilinganishwa na vifaranga wa kuku wazazi 556,616vilivyoingizwa nchinimwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, vituo vya kutotolesha vifaranga vimeongezeka kutoka vituo 19 mwaka 2018/2019 hadi kufikia vituo 26. Vituo hivyo vipo katika mikoa ya Dar es Salaam (7), Iringa (2), Njombe (1), Pwani (11), Kilimanjaro (2), Arusha (1), Mbeya (1) na Mwanza (1). Aidha, mashamba ya kuku wazazi nchini yameongezeka kutoka 16 hadi 20 katika kipindi hicho yenye uwezo wa kutunza zaidi ya kuku wazazi 1,200,000 (Kiambatisho Na. 7a na 7b).

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara kwa kushirikiana na Kampuni ya AKM Glitters imewezesha upatikanaji wa vifaranga 81,160 katika vikundi 151 kutoka Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Pwani na Rukwa (Kiambatisho Na. 8a na 8b). Aidha, vikundi 27 vya wafugaji kuku na kaya 950 zimepatiwa vifaranga 8,500 katika Wilaya za Bagamoyo (4,500) na Sumbawanga (4,000). Pia, mtandao wa wanawake 400 wanaofuga kuku katika Wilaya ya Mkuranga wamepatiwa vifaranga5,700.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kuratibu na kusimamia uzalishaji wa kuku, vifaranga na mayai. Vilevile, Wizara itaendelea kuhamasisha ulaji wa mayai ili kuongeza kiwango cha ulaji kwa mtu kwa mwaka.

Uzalishaji wa Nguruwe 

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ufugaji na biashara ya nguruwe ambapo hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2020 jumla ya tani 38,377.4 za nyama ya nguruwe zimezalishwa ikilinganishwa na tani 37,773 zilizozalishwa mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 1.6.  ongezeko hili limetokana na kuimarishwa kwa mashamba ya Serikali ya Ngerengere na Kitulo ili yaweze kuendelea kuzalisha mbegu bora za nguruwe. Aidha, Chama cha Wazalishaji Nguruwe nchini (Tanzania Piggery Farmers Association - TAPIFA) kimeendelea kuhamasisha wafugaji wa nguruwe kujiunga na chama ambapo mpaka mwezi Aprili 2020 jumla ya wanachama 220 wanaofuga nguruwe wanaofikia takriban 200,000. 

Pamoja na mafanikio tajwa hapo juu, tasnia hii bado inakabiliwa na gharama kubwa ya vyakula, upatikanaji wa mbegu bora na uhaba wa machinjio na viwanda. Hivyo, Wizara kwa kushirikiana na TAPIFA inaendelea kukabiliana na changamoto kama ifuatavyo:
(i) Kuagiza mbegu bora za nguruwe aina za Camborough, Duroc, Peatrain, Large White na Topic kutoka nchi za Zambia, Rwanda, Afrika ya Kusini na Ufaransa; 

(ii) Kupunguza gharama za vyakula vya nguruwe kwa kusimika mitambo ya kisasa ya kuchanganya vyakula; 

(iii) Kujenga machinjio ya kisasa ya nguruwe katika mkoa Dar es Salaam; na 

(iv) Kuanza usindikaji wa nyama ya nguruwe katika Kiwanda cha Happy Sausage kilichopo Sakina Arusha.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itahimiza sekta binafsi kuzalisha na kusambaza mbegu bora za nguruwe kwa wafugaji ili kuongeza uzalishaji wa nguruwe na bidhaa zake. Aidha, Wizara itaendelea kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji, usindikaji na biashara ya nguruwe. Pia, Wizara itaendelea kuimarisha mashamba yake ya Ngerengere, Kitulo na Mabuki ili yaweze kuendelea kuzalisha mbegu bora za nguruwe. Vilevile, Wizara itaendelea kuimarisha Chama cha Wazalishaji Nguruwe nchini TAPIFA kwa lengo la kuboresha kosaafu za nguruwe.

Haki Miliki za Waboreshaji Mbari za Wanyama

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea na taratibu za kutunga Sheria ya Mbari za Mifugo ili kuanzisha Mfumo wa Kisheria wa Kulinda Haki za Wagunduzi wa Mbari mpya za Wanyama, hifadhi ya kosaafu zilizopo nchini na kusimamia ubora wa mbegu za mifugo. Uwepo wa mfumo huo utatoa hamasa kwa wadau wa sekta binafsi na ya umma kuwekeza kwenye ugunduzi wa mbari mpya za wanyama, uzalishaji wa wanyama bora wa mbegu na kuzalisha mbari zenye tija zaidi katika uzalishaji wa mazao ya mifugo. Vile vile, mfumo huo unalenga kutoa na kulinda haki miliki kwa wagunduzi wa mbari mpya ili waweze kufaidika na uwekezaji wao. Aidha, Sheria hiyo itaanzisha utaratibu wa kuhifadhi na kuendeleza mbari zilizopo nchini pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za wanyama.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara imetambua wadau wanane (8) wa uboreshaji wa mbari za mifugo katika mikoa ya Manyara, Kilimanjaro, Mbeya, Tanga na Morogoro . Aidha, Wizara imetambua vyama vitatu (3) vya wadau wa uzalishaji wa mbari za mbuzi katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Morogoro. 

Kazi wanazofanya wadau hao ni pamoja na kuhifadhi (conservation) mbari za wanyama wa asili, kudumisha ubora wa mbegu za mifugo na kuzalisha mbari mpya za wanyama zenye tija katika uzalishaji wa maziwa, nyama na mayai. Pia, Wizara inaendelea kushirikiana nao katika hatua za kukamilisha uzalishaji mbari mpya.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itafanya tambuzi yakinifu (characterization) ya mbari za wanyama zilizopo nchini, kusajili na kutunza daftari la mbari za wanyama, wanyama wa mbegu na waboreshaji mbari katika mikoa mitatu(3).

Biashara ya Mifugo na Mazao Yake Biashara ya Mifugo 

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara imeendelea kuratibu biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi. Katika mwaka 2019/2020 jumla ya ng’ombe 1,513,926 mbuzi 1,733,463, kondoo 299,157 na punda 198,000 wenye thamani ya shilingi trilioni 1.06 waliuzwa katika minada mbalimbali hapa nchini ikilinganishwa na ng’ombe 2,006,816, mbuzi 1,491,251, kondoo 341,814 na punda 124,000 wenye thamani ya shilingi trilioni 1.3 waliouzwa katika minada mbalimbali hapa nchini mwaka 2018/2019. Sababu za kushuka kwa biashara hii ni pamoja na mwaka 2019/2020 kuwa na mvua nyingi hivyo kuathiri biashara ya mifugo katika minada. Aidha, hadi tarehe 30 Aprili, 2020 jumla ya Shilingi 5,217,369,393.2 zilikusanywa kama Maduhuli ya Serikali.  Pia, Wizara imetoa mafunzo kwa watendaji 26 wa minada kuhusu Sheria na Kanuni za Uendeshaji wa Minada, ikiwa ni pamoja na matumizi ya PoS na taratibu za ukusanyaji na uwasilishaji wa maduhuli ya Serikali.

Udhibiti wa Biashara ya Mifugo na Mazao yake (Operesheni Nzagamba) 49. Mheshimiwa Spika, kabla ya Operesheni Nzagamba kulikuwa na ukwepaji mkubwa wa kulipa maduhuli ya Serikali yahusuyo biashara ya mifugo na mazao yake; uingizaji holela wa bidhaa mbalimbali kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu; na uuzwaji wa bidhaa zisizokidhi viwango. Katika mwaka 2019/2020 Wizara imeendelea kutekeleza operesheni Nzagamba ili kudhibiti utoroshaji wa mifugo na mazao ndani na nje ya nchi na upotevu wa mapato katika maeneo matano ya kimkakati ambayo ni: Nzega (Tabora), Lamadi (Simiyu), Babati (Manyara), Longido (Arusha) na Handeni (Tanga). Kupitia operesheni hiyo hadi kufikia 30 Aprili, 2020mafanikio yafuatayo yamepatikana:

(i) Jumla ya shilingi 5,516,568,128 zimekusanywa ikiwa ni tozo ya kusafirisha mifugo nje ya nchi shilingi 2,993,977,500; tozo ya kusafirisha vyakula vya mifugo nje ya nchi shilingi 885,101,260; vibali kusafirisha mifugo nchini shilingi 1,495,853,468; na faini kwa makosa ya ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika biashara ya mifugo na mazao yake shilingi141,635,900(Kiambatisho Na.10); 

(ii) Jumla ya ngómbe 392,661, mbuzi na kondoo 676,715 walikaguliwa ambapo jumla ya mifugo 3,363 (ngómbe, mbuzi na kondoo) iliyokuwa inatoroshwa kwenda nje ya nchi bila kulipiwa vibali na ushuru ilikamatwa na kutozwa faini yenye jumla ya shilingi 141,635,900. Aidha, ng’ombe 44,791, mbuzi na kondoo 220,033waliuzwa nje ya nchi. Pia, ng’ombe 354,906, mbuzi na kondoo 243,435 walikatiwa vibali ndani ya nchi  na  jumla ya tani 56,986.48 za vyakula vya mifugo zilisafirishwa nje ya nchi; 

(iii) Udhibiti wa utoroshaji wa mifugo na mazao yake nje ya nchi umesaidia kuhamasisha ujenzi wa viwanda vipya vya nyama, maziwa na ngozi; 

(iv) Udhibiti wa uingizaji wa mazao mifugo ambapo jumla lita za maziwa 5,621.3, kilo 303.69 za nyama na bidhaa zake, trei za mayai 1,012 zilikamatwa zikiwa zimeingizwa nchini kinyume cha Sheria; na 

(v) Kuhamasisha matumizi ya mizani katika minada na uanzishaji wa ushirika wa wafanyabiashara wa mifugo. 50. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itajenga minada miwili ya upili; na mmoja wa mpakani; na kukarabati minada ya upili na mipakani na kuwezesha utekelezaji wa doria sita (6) za Mikakati ya Kudhibiti Upotevu wa Mapato yatokanayo na Biashara ya Mifugo na Mazao yake (OperesheniNzagamba). Kodi, Ada na Tozo Katika Sekta ya Mifugo 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 kutokana na malalamiko kutoka kwa wadau juu ya viwango vikubwa vya kodi, ada, ushuru na tozo Wizara imesikia kilio hicho na kufanya mapitio ya kanuni zake za tozo (Animal and Animal Products Regulations, 2007) ili kuondoa malalamiko na kukabiliana na hali ya sasa. Mabadiliko hayo yatabainishwa katika Hotuba ya Waziri wa Fedha atakapowasilisha Bungeni Bajeti ya Serikali. 52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itaendelea kutathmini kodi, tozo na ada mbalimbali zitakazoonekana kuwa kero kwa wazalishaji na wafayabiashara ya mifugo na mazao yake ili kuzifuta au kuzifanyia marekebisho. Zao la Ngozi 

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2020 jumla ya kilo za ngozi 16,746,589.36 (ng’ombe 14,449,075.49, mbuzi 1,775,298.5 na kondoo 522,215.38) zenye thamani ya shilingi bilioni 23.9 zimezalishwa ikilinganishwa na kilo 16,012,800.71 (ng’ombe 13,904,620.27, mbuzi 1,653,669.26 na kondoo 454,511.17) zenye thamani ya shilingi bilioni 22.8 zilizozalishwa mwaka 2018/2019. Kilo za ngozi za ng’ombe 25,500 zenye thamani ya shilingi milioni 14.4 na kilo za ngozi za mbuzi na kondoo 114,500 zenye thamani ya shilingi milioni 202.7 zimesindikwa ikilinganishwa na kilo za ngozi ya ng’ombe 972,866.04 zenye thamani ya shilingi bilioni 2, kilo za ngozi za mbuzi na kondoo 386,135 zenye thamani ya shilingi milioni 867.9 na kilo 114,800 za punda zenye thamani ya shilingi milioni 157.2 zilizosindikwa mwaka 2018/2019. Upungufu wa kilo zilizosindikwa umesababishwa na katazo la uingizaji wa ngozi zilizochakatwa kwa kutumia chrominenasulphide katika soko la Ulaya. Hivyo, Wizara inahamasisha wenye viwanda vya ngozi kubadilisha teknolojia ya usindikaji kutoka kwenye matumizi ya chromine na sulphide kwenda kwenye usindikaji unaozingatia usalama wa mazingira kwa kutumia teknolojia ya kutumia mimea aina ya mimosa (vegetable tanning). 

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kuendeleza Tasnia ya Ngozi (Leather Sector Development Strategy 2016 – 2020). Katika mwaka 2019/2020mafanikio yaliyopatikana ni:

(i) Kuanzisha kituo cha kutoa leseni na vibali vya kusafirisha ngozi nje ya nchi cha Dodoma na kuimarisha kituo cha Dar es Salaam. Hivyo, hadi Aprili 2020 jumla ya kampuni 17 zimepatiwa leseni za usajili wa maghala ya kuhifadhia ngozi (Premises License) na vibali vya kusafirisha ngozi nje ya nchi kwa lengo la kuwezesha biashara ya ngozi (Kiambatisho Na.11); 

(ii) Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kampeni za uhimilishaji, uogeshaji mifugo, chanjo na upatikanaji wa maji na malisho, pia, uhamasishaji wa ujenzi wa machinjio za kisasa na viwanda vya kusindika mazao ya mifugo ambapo mikakati hii imesaidia upatikanaji wa ngozi bora kwa ajili ya uchakataji na usindikaji viwandani. 

(iii)Visu maalum vya kuchunia ngozi za Wanyama vimegawiwa kwa wachunaji wa ngozi wenye leseni katika Kanda za Mashariki, Kaskazini na Ziwa. Jitihada zinaendelea ili kugawa visu hivyo maalum katika kanda zotenane nchini.

(iv)Ili kuwezesha upatikanaji wa ngozi bora kulingana na mahitaji ya wachakataji na wasindikaji wa ngozi, wakaguzi wa ngozi 113 wameteuliwa na wachunaji ngozi 735 wamejengewa uwezo. 

(v) Udhibiti wa utoroshaji na udanganyifu katika biashara ya ngozi kwa kutoza asilimia 80 ya usafirishaji wa ngozi ghafi na asilimia 10 ya usafirishaji wa ngozi zilizosindikwa kufikia hatua ya kati (wet blue) umeimarisha biashara ya ngozi nchini. 

Mheshimiwa Spika, hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zimechochea uwekezaji mkubwa katika tasnia ya ngozi, kwa mfano, ujenzi wa Kiwanda cha Ngozi cha Karanga Moshi wenye thamani ya shilingi bilioni 75 umekamilika kwa asilimia 80 na ujenzi wa Kiwanda cha ACE Leather Morogoro wenye thamani ya Shilingi bilioni 23 (Dola za Kimarekani milioni 10) umakamilika kwa asilima 90. Pia, machinjio 30 zimejengwa na zinaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kuwezesha utekelezaji wa Mpango Shirikishi wa Kuendeleza Tasnia ya Ngozi kwa kuvijengea uwezo vikundi vya wazalishaji wa bidhaa za ngozi katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Geita, Simiyu, Mara na Shinyanga. Aidha, Wizara itaendelea kurasimisha wadau waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa zao la ngozi ambao ni wakaguzi, waweka madaraja na wachunaji. Pia, Wizara itafanya mapitio ya Sheria ya Biashara ya Ngozi Na. 18 ya mwaka 2008 na kanuni zake na kuhuisha Mkakati wa Kuendeleza Tasnia ya Ngoziwa2016 hadi 2020. Machinjio ya Dodoma 

Mheshimiwa Spika, tangu machinjio ya Dodoma ilipokabidhiwa kwa Kampuni ya TMCL mwaka 2008, utendaji wake umekuwa siyo wa kuridhisha. Aidha, majengo, miundombinu ya machinjio, mitambo na vifaa imechakaa bila ukarabati wowote; kuongezeka madeni; kutengeneza hasara kila mwaka na haijawahi kutoa gawio Serikalini. Pia, usimamizi dhaifu na ubadhilifu wa fedha umepelekea Serikali kupata hasara ya shilingi bilioni 42.28 kwa kipindi cha miaka 11. Kutokana na udhaifu huo wa uendeshaji na uchakavu wa machinjio, Wizara ya Mazingira ya UAE inayosimamia ubora wa nyama iliifutia machinjio ithibati ya kuuza nyama katika nchi za Falme za Kiarabu (UAE). 

Kwa kuwa Serikali ilifanya jitihada nyingi kunusuru machinjio hii bila mafanikio, mnamo tarehe 27 Desemba, 2019, Wizara ilirejesha Machinjio hiyo Serikalini. Kutokana na uamuzi huo, kumekuwepo na mafanikio makubwa ambapo ndani ya muda wa miezi minne, uchinjaji wa mifugo umeongezeka kutoka wastani wa ng’ombe 41 kufikia wastani wa ng’ombe 125 kwa siku. Pia, makusanyo ya mapato yameongezeka kutoka wastani wa shilingi 39,843,788 hadi shilingi 90,279,000 kwa mwezi. Katika kipindi cha miezi minne Wizara imeweza kulipia gharama za uendeshaji ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi na kupata faida ambayo sehemu yake kiasi cha shilingi milioni 70 kimetolewa kama gawio kwa Serikali. Hii ni mara ya kwanza kwa Serikali kupata gawio kutoka katika machinjio hiyo. Aidha, Kampuni ya NICOL na NARCO wamekubaliana kuvunja Kampuni ya TMCL bila kwenda Mahakamani. Pia, Serikali inaendelea na ukarabati ili kurejesha ithibati ya kuuza nyama nchiza UAE. 58. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itaendelea kuimarisha machinjio ya Dodoma kwa kuweka usimamizi wa machinjio hiyo chini  ya taasisi za LITA na NARCO.

Rasilimali za Malisho, Vyakula na Maji kwa Mifugo Malisho, Vyakula na Maji kwa Mifugo 59. Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kutekeleza Mkakati wa Upatikanaji wa Malisho na Maji pamoja na kukamilisha maandalizi ya miongozo ya usimamizi wa rasilimali hizo. Katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea na hatua za awali kwa ajili ya ujenzi wa lambo katika Kijiji cha Chamakweza (Bagamoyo), Visima virefu katika Vijiji vya Mpapa (Manyoni) na Nsolanga-Ismani (Iringa)  na ukarabati wa malambo katika Kijiji cha Kimana (Kiteto), Kijiji cha Narakauo (Simanjiro) na kijiji cha Kimokoa (Longido). 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itachimba visima virefu vinne (4) katika Halmashauri za Tanganyika (Tanganyika) na Tunduru (Mkowela). Pia, itakarabati malambo 10 yaliyopo katika Halmashauri za Longido (Kemokoa), Simanjiro (Narakauo), Bukombe (Bukombe), Butiama (Bukabwa), Igunga (Igunga), Kiteto (Kimana), Kishapu (Mwalata), Chunya (Isewe), Kilindi (Lengusero) na Meatu (Isebanda). Pia, Wizara itaendelea kushirikiana na Wizara ya Maji ili miradi ya maji kwa ajili ya binadamu izingatie miundombinu ya maji kwa ajli ya mifugo,naWizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ili uchimbaji wa mashimo kwa ajili ya malighafi ya ujenzi wa barabara yachimbwe kimkakati ili yaweze kutumika kama malambo baada ya miradi ya ujenzi kukamilika. 

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha lishe na upatikanaji wa uhakika wa malisho kwa mifugo, Wizara inaendelea kutoa elimu kwa wafugaji na wadau wengine kuhusu uzalishaji na uhifadhi wa malisho. Katika mwaka 2019/2020, Jumla ya marobota 380,765 ya hei yamezalishwa kati ya hayo marobota 326,655 yamezalishwa katika mashamba ya Serikali (Kiambatisho Na. 12) na marobota 54,110 yamezalishwa kutoka mashamba ya Sekta Binafsi. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 jumla ya tani 127.3 za mbegu bora za malisho na vipandikizi zimezalishwa katika mashamba ya Serikali ikilinganishwa na tani 12.1 za mbegu za malisho zilizozalishwa katika mashamba ya Serikali mwaka 2018/2019. Ongezeko hili limetokana na uzalishaji wa tani 115.2 za vipandikizi zilizozalishwa kwa wingi kutokana na uwepo wa mvua za kutosha misimu ya vuli na masika na Serikali kuwekeza katika ununuzi wa vitendea kazi yakiwepo matrekta na harrow kwa ajli ya shamba la Serikali la mbegu za malisholililopo Vikuge Kibaha, mkoani Pwani.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, viwanda vipya 11 vya kutengeneza vyakula vya mifugo vimeongezeka na kufanya viwanda vya vyakula vya mifugo kufikia 105 ikilinganishwa na viwanda 94 katika mwaka 2018/2019 (Kiambatisho Na. 13). Aidha, katika kuhakikisha upatikanaji wa vyakula vya mifugo vyenye ubora na viwango stahiki unakuwepo, Wizara imeteua Wakaguzi 129 waliopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 109 na 20 ngazi za Mikoa. Pia, ukaguzi wa maeneo ya kuzalisha, kuhifadhi na kuuza vyakula vya mifugo umefanyika katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Iringa, Kilimanjaro, Morogoro, Mbeya, Mwanza, Njombe, Pwani, Ruvuma na Songwe. Jumla ya maeneo 11 ya kuzalisha vyakula, matano (5) ya kuhifadhi na 36ya kuuzia vyakula vya mifugo yamekaguliwa na wadau wamepatiwa vyeti vya usajili baada ya kukidhi vigezo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itaendelea kusimamia na kudhibiti ubora na usalama wa vyakula vya mifugo kwa kufanya ukaguzi katika maeneo 75 ya uzalishaji, uhifadhi na uuzaji wa vyakula vya mifugo ikiwa ni pamojana kutoa mafunzo rejea kwa wakaguzi 159 wa vyakula vya mifugo na maeneo ya malisho. Pia, itaendelea kuimarisha mashamba ya Serikali ya kuzalisha mbegu za malisho na kuwezesha urasimishaji wa aina 10 za mbegu hizo.

Ustawi wa Wanyama 

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na matukio ya ukamataji holela wa mifugo usiyozingatia ustawi na haki za wanyama ambazo ni chakula, maji, malazi, matibabu na uhuru wa kuonesha tabia za uasili. Ukamataji huo umekuwa ukifanywa na Serikali za Vijiji, Halmashauri za Wilaya na Mamlaka za Hifadhi. Ukamataji huu umekuwa ukiambatana na utesaji wa wanyama ikiwemo mifugo kukatwa mapanga, mifugo kupewa sumu na kusababisha vifo pasipo kuzingatia Sheria ya Ustawi wa Wanyama Na. 19 ya mwaka 2008 (Animal Welfare Act No. 19/2008); Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya mwaka 2003 (Animal Diseases Act No. 17/2003) na Sheria ya Nyanda za Malisho Na. 10 ya mwaka 2010 (the Grazingland and Animal Feed Resources Act, No. 10/2010). Jumla ya mifugo 14,668,323 (ngómbe 14,667,175, mbuzi 718, kondoo 248 na punda 182) ilikamatwa kati ya mwaka 2017 na 2019 hususan kutoka mikoa ya Tabora, Mbeya, Dodoma, Geita na Rukwa (Kiambatisho Na. 14). 

Mikoa mingine ambayo kumekuwepo na matukio ya ukamataji wa mifugo kwenye hifadhi za maliasili ni pamoja na Katavi, Mara, Morogoro, Iringa, Simiyu, Tanga,Shinyanga, Manyara, Singida, Arusha, Kilimanjaro, Kigoma na Pwani.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kuratibu na kusimamia haki na ustawi wa wanyama.

Utatuzi wa MigogoroBaina ya Wafugaji na WatumiajiWengine wa Ardhi.

Mheshimiwa Spika, katika kutatua migogoro baina ya wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi, Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliamua kuunda timu ya Mawaziri nane (8) iliyoongozwa na Mhe. William Vangimembe Lukuvi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Isimani ili kupata ufumbuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ya wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi (Kiambatisho  Na. 15b-i). Timu hiyo ilizunguka nchi nzima kwenye maeneo yenye migogoro kwa kutumia ndege maalum ya kijeshi. Ambapo baadaye Mhe. Rais alitoa maagizo yafuatayo:

i. Kurasimisha vijiji 920 ambavyo vinamigogoro ya matumizi ya ardhi na hifadhi, mashamba, ranchi, mapori ya akiba, na vyanzo vya maji visiondolewe katika maeneo vilipo;

ii. Kufuta baadhi ya maeneo ya hifadhi za misitu na maeneo tengefu na kuagiza yagawiwe kwa wananchi kwa ajili ya mifugo, kilimo na makazi. Jumla ya Mapori Tengefu 12 yenye jumla ya ekari 707,659.94 yamefutwa na misitu saba (7) yenye ukubwa wa ekari46,247.56imefutwa.

iii. Hifadhi za misitu 14 na mashamba 16 yasiyoendelezwa yamegwe na kugawiwa kwa wananchi kwa shughuli za mifugo, kilimo na makazi.

iv. Kuweka mwongozo wa matumizi kwa maeneo ya mita 500 katika maeneo ya kinga (buffer zone) na mita 60 katika hifadhi ya vyanzo vya maji ili ziendelee kutumiwa na wananchi kwa namna ambayo haitaathiri mazingira (Kiambatisho Na. 15b-ii).

Mheshimiwa Spika, hivi sasa Wizara nane (8) za kisekta ikiwemo Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Katiba na Sheria (Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali) zinaendelea kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais ambapo utekelezaji wake uko katika hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara yangu ilifanya ziara katika Halmashauri 152 kwa lengo la kukutana, kusikiliza na kutatua  changamoto zinazowakabili wafugaji. Ziara hizo zilipokelewa kwa vilio kwa baadhi ya maeneo ambayo yana migogoro sugu baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Naomba nitoe maelezo kwa muhtasari kuhusu migogoro hiyo kama ilivyowasilishwa wakati wa ziara:

i. Migogoro kati ya wakulima na wafugaji;

a.Wafugaji wanaingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima na kuharibu mazao;

b.Wafugaji kuvamia vyanzo vya maji, kuwapiga na kuwaumiza wakulima na kukataa kuwalipa fidia;

c. Wakulima kuvamia na kufanya shughuli za kilimo katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kulishia mifugo;

d.Wakulima kuziba njia za mifugo za kwenda katika malisho, maji, josho na mnadani, kukata mapanga, kushikilia kwa muda mrefu  mifugo; na

e. Baadhi ya watendaji wa Serikali kulalamikiwa kwa kutokutenda haki na kufanya upendeleo wanapoletewa malalamiko ya wakulima na wafugaji.

ii. Migogoro kati ya Mamlaka za uhifadhi, mashamba ya Serikali na wafugaji.

a.Wafugaji kuvamia na kuingiza mifugo ndani ya  maeneo ya hifadhi na mashamba ya Serikali na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kueneza magonjwa baina ya mifugo na wanyama pori;

b.Kutanua mipaka ya hifadhi na kujumuisha maeneo ya malisho kwenye hifadhi, hifadhi kutokuwa na alama na mipaka inayoonekana hali inayopelekea mifugo kukamtwa hata ikiwa nje ya hifadhi;

c. Maeneo ya malisho kubadilishiwa matumizi bila kuzingatia mahitaji, uanzishwaji wa WMA’s na kukatazwa matumizi mseto katika maeneo hayo kumechangia kupungua kwa maeneo ya malisho nchini;

d.Mifugo kushikiliwa kwa muda mrefu bila kupatiwa huduma muhimu kama maji, malisho, chanjo na matibabu ambapo inapelekea mifugo mingi kufa ikiwa inashikiliwa;

e. Wafugaji wanaposhinda kesi mahakamani hawarudishiwi mifugo yao na pengine hurudishiwa mifugo pungufu kinyume na  hukumu za mahakama;

f. Baadhi ya maaskari wa hifadhi wamekuwa  wakipiga risasi mifugo ili kuwakomoa wafugaji na kupoteza ushahidi, mifugo kuuzwa kiholela wakati  imeshikiliwa;

g.Ukamataji holela wa mifugo usioshirikisha uongozi wa vijiji na wamiliki wa mifugo umepelekea kutofautiana kwa idadi ya mifugo inayokamatwa na inayofikishwa mahakamani;

h.Wanyama pori wakali kama Simba, Chui na Tembo wamekuwa wakishambulia mifugo bila kupata msaada au fidia yoyote;

i. Baadhi ya Mamlaka za Miji zimekuwa zikilazimisha wafugaji kuhamisha mifugo yao bila kuzingatia haki zao katika umiliki wa ardhi;

j. Wafugaji kulalamikia kutozwa faini kubwa kinyume cha Sheria pale mifugo yao inapokamatwa katika maeneo yasiyoruhusiwa,

Mheshimiwa Spika, Wizara iliweza kutatua baadhi ya migogoro papo kwa papo, migogoro mingine inaendelea kufanyiwa kazi na baadhi ya migogoro hiyo imewasilishwa katika Wizara za kisekta na mamlaka husika kwa ajili ya utatuzi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara imeendelea kutatua Migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi  katika maeneo ya Vilima vitatu (Babati), Hifadhi ya Ngorongoro (Ngorongoro), Mvuha (Morogoro vijijini); Ranchi ya Ruvu (Bagamoyo); Kwala (Kibaha); Gwata (Kisarawe); Mindutulieni (Chalinze); Mkiu, Njopeka, Kisegese, Chamgoi, Kifumangao, Mkuruwili na Mtongani (Mkuranga); Msaraza (Pangani), Katambuzi, Katera, Karukwanzi B, Ishaka Ibale na Nyakakoni (Kyerwa), Kahundwe (Karagwe), Ranchi ya Kongwa (Dodoma), Shamba la Kuzalisha Mitamba Hanga Ngadinda na Muhukulu Lilahi (Ruvuma) na Shamba la Kuzalisha Mitamba Mabuki (Mwanza). Aidha, migogoro mikubwa 11 kati ya 17 (sawa na asilimia 64.7) iliyodumu kwa muda mrefu imetatuliwa katika kipindi cha mwaka 2019/2020 katika Mikoa ya Pwani, Dodoma, Morogoro, Ruvuma, Mwanza na Geita. Migogoro iliyotatuliwa ni ya: Ranchi ya Ruvu, Ranchi ya Misenyi, Ranchi ya Kagoma, Kituo cha karantini Kwala, Ranchi ya Kongwa, Gwata Kisarawe, Ranchi ya Dakawa, Hifadhi ya Msitu wa Kigosi ya Geita, Mamlaka ya Pori la Akiba la Mkungunero la Chemba, lililokuwa Shamba la Mifugo Hanga la Madaba na Shamba la Kuzalisha Mitamba Mabuki Misungwi.

Mheshimiwa Spika, Wizara katika jitihada za kupata suluhisho la migogoro kati ya watumiaji mbalimbali wa ardhi imetekeleza yafuatayo:

(i) Imemega maeneo yenye ukubwa wa hekta 29,428.49, katika mashamba na Ranchi za Taifa na kuwapatia wananchi maeneo hayo ili waweze kuendeleza shughuli za kilimo, ufugaji na makazi. Kati ya hekta hizo, hekta 1,800 kutoka katika shamba la Hanga Ngadinda (Ruvuma), hekta 2,208 kutoka Ranchi ya Ruvu, hekta 22,201.094 kutoka Ranchi ya Missenyi, hekta 80.4 kutoka shamba la Taasisi ya Utafiti wa Mifugo – Kongwa na hekta 3,139 kutoka Kituo cha Karantini cha Kwala (Kiambatisho Na. 15a).

(ii)Imefanya ziara katika Halmashauri 152 zenye mifugo ili kusikiliza, kutoa elimu na kutatua migogoro hiyo. Juhudi hizi zimesaidia kupunguza mauaji na kukatana mapanga na hivyo kurejesha amani na utulivu katika maeneo yenye migogoro. Aidha, Jumla ya migogoro 304 imetatuliwa kupitia ziara za viongozi wa Wizara. 

(iii) Inafanya upimaji wa mashamba yote ya Serikali na kuweka mipaka na alama zinazoonekana ambapo hadi mwezi Aprili, 2020 jumla ya mashamba 8 yenye ukubwa wa hekta 23,066.94 yamepimwa na kuwekewa alama zinazoonekana. Mashamba hayo ni Hangangadinga (4,200), Mahukuru Lilahi (3,100), Chibe (2,054), Shishiyu (3,170), Mkwese (5,036), Kinyangiri (3,419.94), Nachingwea (1,497) na Kelema (590). Zoezi la upimaji linaendelea kwa mashamba yaliyobaki. Pia, Halmashauri za Wilaya zimeitikia wito wa kutenga maeneo kwa ajili ya malisho ambapo jumla ya hekta 2,818,687.17 zimetengwa na hekta 108,427.49 zimepimwa.

(iv) Imeunda timu ya watalam kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ambayo inazunguka nchi nzima kutatua migogoro sugu. Timu hiyo inajumuisha wataalam kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara za Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mambo ya Ndani; Usalama wa Taifa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Chama cha Wafugaji. Toka kuzinduliwa kwa timu hiyo mwaka 2018 mafanikio makubwa yamepatikana ambapo jumla ya migogoro sugu 45 imetatuliwa na hivyo kuleta amani na utulivu kwa wananchi.

(v)Wizara inazifanyia mapitio Sheria ya Ustawi wa Wanyama Na. 19 ya mwaka 2008 (Animal Welfare Act No. 19); Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya mwaka 2003 (Animal Diseases Act No. 17) na Sheria ya Nyanda za Malisho Na. 10 ya mwaka 2010 (the Grazingland and Animal Feed Resources Act, No. 10) ili ziweze kutoa ulinzi wa kutosha wa ustawi endelevu wa mifugo. Pia, Wizara imetunga Kanuni za Ukamataji Mifugo (The Animal Welfare (Impounded Animal)Regulations, 2020) ambayo imeweka mwongozo wa namna ya kukamata wanyama, kuwatunza na kuwapa mahitaji muhimu ikiwemo malisho, dawa, chanjo na maji.

Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kutoa elimu kuhusu ufugaji wa mifugo wenye tija, kudhibiti na kutatua migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa rasilimali ardhi inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini. Vilevile, Wizara itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Katiba na Sheria ili kuhakikisha kuwa migogoro ya ardhi inazuiwa na kutatuliwa. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara katika kuhakikisha wafugaji wanapata maeneo ya malisho imetenga na kuwapangisha wafugaji kwa muda wa mwaka mmoja mmoja jumla ya hekta 78,470.97 kutoka kwenye taasisi zake ikiwemo TALIRI (2,501.03), NARCO (59,290), Vituo vya Kupumzishia Mifugo (13,679.94) na Mashamba ya Kuzalisha Mitamba (3,000). Hadi sasa jumla ya ng’ombe 54,852 mbuzi na kondoo 11,578 wanachungwa katika maeneo ya Serikali (Kiambatisho Na. 15c).
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imeandaa na kutekeleza mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji kwa lengo la kupata ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na maeneo ya malisho. Jumla ya vijiji 23 vimetenga hekta 29,786.0 katika Wilaya 8 za Kilindi (2,109.98), Handeni (3,380.01), Namtumbo (11,076.8), Songea (6,353.52), Nyasa (198.78), Mbinga (1,493.66), Ruangwa (407.52),  Liwale (1,216) na Mpwapwa (3,549.72) na kufikia idadi ya vijiji 1,875 ukilinganisha na vijiji 1,852 mwaka 2018/2019 vilivyopimwa na kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Hivyo, maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kwa sasa yamefikia hekta 2,818,687.17 ikilinganishwa na hekta2,788,901.17katika mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaainisha, kutenga, kupima na kutangaza hekta 1,500,000 kwenye Gazeti la Serikali maeneo ya malisho yaliyotambuliwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya ufugaji endelevu. Aidha, itapima na kutenga vitalu katika eneo la Mwisa II Mkoani Kagera  lenye ukubwa wa hekta 121,643.94 kwa ajili kuvimilikisha kwa wafugaji wazawa kwa utaratibu wa mikataba maalumu ili kuweza kufuga kisasa na kibiashara. Kazi ya upimaji na uwekeaji vigingi vya mpaka iko kweye hatua ya mwisho. Aidha, natumia fursa kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Kagera ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Brig. Jen. Michael Gaguti kwa ushirikiano mzuri katika kufanikisha zoezi hili muhimu ambalo sasa litatatua changamoto ya mgogoro wa wafugaji na watumiaji wengine wa Ardhi uliodumu kwa muda mrefu.

Huduma ya Afya ya Mifugo Magonjwa ya Mifugo 

Mheshimiwa Spika, Magonjwa mbalimbali ya mifugo yamekuwa kikwazo katika uzalishaji na biashara ya mifugo. Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuchukua hatua mahsusi katika kukabiliana na magonjwa 13 ya kimkakati (Kiambatisho Na. 16) kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni na haki na ustawi wa wanyama katika utoaji wa tiba  na kinga. Magonjwa hayo ni pamoja na:

(i) magonjwa yaenezwayo na wadudu (Kupe na Mbungó) ambayo ni pamoja na Ndigana Kali, Ndigana Baridi, Mkojo Mwekundu na Moyo Maji yanayosababisha asilima 72 ya vifo vya mifugo. 

(ii) magonjwa ya mlipuko na kuvuka mipaka ambayo ni pamoja na Ugonjwa wa Miguu na Midomo, Homa ya Nguruwe, Mdondo, Homa ya Mapafu ya Ng’ombe (CBPP), Homa ya Mapafu ya Mbuzi (CCPP), Homa ya Bonde la Ufa, Mafua Makali ya Ndege, Sotoka ya Mbuzi na Kondoo, Kimeta, Kutupa Mimba, Mapele Ngozi na Kichaa cha Mbwa. 

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau iliendelea kutekeleza mikakati ya kudhibiti magonjwa ya mifugo yaenezwayo na wadudu. Katika mwaka 2019/2020 mafanikio yafuatayo yamepatikana:

(i) Wizara ilizindua kampeni ya pili ya kuogesha mifugo ambayo ilifanyika tarehe 29 Oktoba 2019 katika  Wilaya ya Mlele Halmashauri ya Mpimbwe. 

(ii) Jumla ya majosho 542 yamekarabatiwa na Wizara (162) na Halmashauri (380) na mapya 85 yamejengwa (Kiambatisho Na. 17a)na(Kiambatisho Na. 17b). 

(iii) Katika mwaka 2019/2020 Wizara ilinunua jumla ya lita 12,549.50 za dawa za kuogesha mifugo aina ya Paranex (Alphacypermethrin) na TikTik (Amitraz) zenye thamani ya Shilingi 440,714,750 ili kuendeleza zoezi la uogeshaji mifugo. Dawa hizi zilisambazwa kwenye majosho 1,738 katika Halmashauri 152 za Mikoa 25 ya Tanzania bara. 

(iv) Kamati 1,036 za usimamizi na uendeshaji wa majosho zimeundwa, kati ya hizo 260 zimefungua akaunti benki (Kiambatisho Na. 18). 

(v) Jumla ya michovyo 211,037,290 imefanyika ambapo michovyo 149,954,080 ya ng’ombe, 45,477,778 ya mbuzi na kondoo 15,605,431 (Kiambatisho Na. 19).

Mheshimiwa Spika, Wizara iliandaa kanuni na mwongozo wa uogeshaji ambao unatoa maelezo ya namna ya uogeshaji mifugo. Kanuni na mwongozo huo viliainisha majukumu mbalimbali ya wadau ikiwemo bei elekezi ya kuogesha mifugo ya shilingi 50 kwa ng’ombe na shilingi10kwa mbuzi au kondoo. 80. 

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau iliendelea kutekeleza mikakati ya kudhibiti magonjwa ya mifugo ya mlipuko na yanayovuka mipaka.  Katika mwaka 2019/2020 mafanikio yafuatayo yamepatikana:

(i) Utoaji wa chanjo umefanyika kwa mbuzi na kondoo 2,557,870 dhidi ya Ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo; ng’ombe 5,557,587 dhidi ya Ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya Ng’ombe (CBPP); ng’ombe 1,036,769, mbuzi 680,906 na kondoo 192,906 dhidi ya Ugonjwa wa Kimeta; ng’ombe 162,843 dhidi ya Ugonjwa wa Kutupa Mimba; mbwa 812,712 na paka 4,152 dhidi ya ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa na Ngómbe 12,419 dhidi ya Ugonjwa wa Miguu na Midomo.

(ii)Maeneo Huru ya Magonjwa ya Mifugo (Disease Free Compartments) yenye ukubwa wa hekta 266,857yameainishwakatika Ranchi za Taifa na vitalu vya watu binafsi kama maeneo yatakayo kuwa huru kwa Ugonjwa wa Miguu na Midomo. Aidha, sampuli 900 zimechukuliwa katika maeneo hayo na zinafanyiwa uchunguzi ili kubaini aina ya vinasaba (serotype) vya ugonjwa vilivyopo ili kuwezesha utengenezaji wa chanjo. 

(iii) Jumla ya dozi 47,347,700 za Chanjo ya Matone ya Ugonjwa wa Mdondo (I2) zimezalishwa na kusambazwa kwenye Mikoa yote nchini ikilinganishwa na dozi 38,245,800 zilizozalishwa katika mwaka 2018/2019. Chanjo hiyo inastahimili hali ya joto hivyo inaweza kutumiwa na wafugaji wa kuku vijijini bila kuharibika. 81.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara itaendelea kutekeleza mikakati ya kudhibiti magonjwa ya mifugo kwa kununua dawa za ruzuku za kuogeshea mifugo lita 19,700, kukarabati majosho 125 na kujenga majosho mapya 20 ili kuwezesha kuongeza uogeshaji wa mifugo kutoka michovyo milioni 211 hadi michovyo milioni 405. Pia, itaendelea kuzalisha chanjo za magonjwa 13 na kusimamia utekelezaji wa utoaji wa chanjo kwenye Halmasahuri zote nchini. Vilevile, katika udhibiti wa Ugonjwa wa Homa ya Nguruwe itahamasisha ufugaji bora wa nguruwe kwa kutengeneza mabanda  bora, kutoa elimu na kupulizia dawa za kuua virusi kwenye mabanda.

Uzalishaji na Usambazaji wa Chanjo 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeandaa utaratibu wa manunuzi ya pamoja (bulk procurement) ya chanjo zote zinazohitajika na ambazo hazijaanza kuzalishwa hapa nchini ili kuongeza upatikanaji wa chanjo kulingana na kalenda ya chanjo, kulinda ubora wa chanjo na kupunguza gharama ya chanjo kwa wafugaji. Sambamba na mpango huo, Wizara imeandaa bei elekezi ya chanjo zote za magonjwa ya kipaumbele zinazozalishwa nchini na zitakazoagizwa kutoka nje ya nchi kuanzia ngazi ya uzalishaji, maduka yanayosambaza pamoja na bei atakayolipa mfugaji kwa kuzingatia Kanuni ya Chanjo na Uchanjaji ya mwaka 2020 GN.180 Animal Disease (Vaccine and Vaccination) Regulations, 2020 GN. No 180). Lengo la bei elekezi ni kuhakikisha kuwa kila mfugaji anachanja mifugo yake kwa kufuata Sheria ili kudhibiti magonjwa hayo kuanzia tarehe 01 Julai, 2020.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kutekeleza utaratibu na usimamizi wa bei elekezi za chanjo 13 za magonjwa ya kimkakati na ununuzi wa chanjo kwapamoja (Bulk Procurement)kwa chanjo zote ambazo hazizalishwi nchini. Aidha jitihada hizi za serikali zitapelekea kupunguza gharama za chanjo kwa asilimia 60. Nitumie nafasi hii kutangaza bei elekezi ambazo wadau wote watapaswa kuzifuata na kuzizingatia (Kiambatisho Na.20na21).

KuimarishaUchunguzi naUpatikanaji wa Taarifa za Magonjwaya Mifugo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara kupitia Vituo vinane (8) vya Kanda vya Uchunguzi na Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mifugokwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa imeendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na utoaji wa taarifa za magonjwa ya mifugo. Jumla ya wataalam 108 kutoka Halmashauri 70 wamepatiwa mafunzo na vifaa vya kielektronic (smartphone) kwa ajili ya ufuatiliaji na utoaji wa taarifa za magonjwa ya mifugo kupitia Mfumo wa Event Mobile Application(EMAi).

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi Aprili 2020 jumla ya matukio 537 ya magonjwa mbalimbali ya mifugo yalitolewa taarifa katika maeneo mbalimbali yakilinganishwa na matukio 1,025 yaliyotolewa taarifa katika mwaka 2018/2019 nchini. Pia, katika matukio hayo mifugo 605,722 ikiwemo ngómbe 432,521, mbuzi 140,180 na kondoo 32,021 ilipatwa na magonjwa na 221,733 kufa kutokana na magonjwa hayo. Mifugo iliyokufa kwa magonjwa ni ngómbe 198,010, mbuzi 21,203 na kondoo 2,520 ambapo mifugo iliyopatwa na magonjwa imepungua kwa asilimia 29 ikiwa ni mifugo 853,180 (ngómbe 627,155, mbuzi 185,038 na kondoo 40,987). Aidha, mifugo iliyokufa imepungua kwa asilimia 37 ikilinganishwa na mifugo iliyokufa kwa magonjwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kuimarisha upatikanaji wa taarifa za magonjwa ya mifugo kwa kuwezesha kutoa mrejesho wa kitaalamu juu ya udhibiti wa magonjwa yanayoambukiza binadamu kutoka kwa wanyama na matumizi sahihi ya pembejeo za Wanyama katika Halmashauri 30 na kuwezesha uchanjaji wa wanyama 25,000,000 dhidi ya magonjwa ya kipaumbele 13. Aidha, Wizara itaimarisha huduma za uchunguzi na matibabu kwa kujenga kliniki na maabara katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Baraza la Veterinari Tanzania

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Baraza la Veterinari Tanzania (Veterinary Council of Tanzania – VCT) ina jukumu la kusimamia maadili ya wataalam wa afya ya wanyama na viwango vya huduma ya Wanyama zinazotolewa na wataalam hao. Katika kipindi cha tarehe 1 Julai, 2019 hadi 30 Aprili, 2020, Wizara, kupitia Baraza la Veterinari Tanzania imetekeleza yafuatayo:

(i) Vituo vya kutoa huduma ya afya ya wanyama 928 vimekaguliwa kati ya 1,900 vilivyotarajiwa kukaguliwa katika mikoa 17. Ukaguzi huu ulilenga kuhakikisha vituo vya afya ya wanyama vinatoa huduma stahiki na zinazokidhi matarajio ya wafugaji (Kiambatisho Na. 22); 

(ii) Vituo 40 vya kutolea huduma ya afya ya wanyama vimefungwa kutokana na kukosa sifa(Kiambatisho Na. 23); 

(iii) Watoa huduma sita (6) wasio na sifa waliokamatwa kwenye minada katika Mikoa ya Singida na Simiyu wakiuza dawa kinyume na taratibu na kuchukuliwa hatua za kisheria; 

(iv) Madaktari wa mifugo 59 wamesajiliwa kati ya 60 waliotarajiwa kusajiliwa na vituo vya afya ya wanyama 250 vimesajiliwa kati ya 400vilivyotarajiwa kusajiliwa; 

(v) Wataalam wasaidizi 200 wameandikishwa kati 500 waliotarajiwa kuandikishwa na kuorodhesha, wasaidizi wa wataalam 305 wameorodheshwa kati ya 500 wanaotarajiwa kuorodheshwa; 

(vi) Leseni 64 zimetolewa kwa wakaguzi wa nyama, wataalam wa maabara na wahimilishaji kati ya leseni 200 zilizotarajiwa kutolewa; 

(vii) Jumla ya maeneo ya kutolea huduma ya afya ya wanyama 1,730 yamesajiliwa, ikiwemo Hospitali moja (1) ya wanyama iliyopo SUA - Morogoro; Kliniki (18); maabara (2) na vituo vya afya ya wanyama (1,709) link https://www.mifugouvuvi.go.tz/publicatio ns/39. 

(viii)Vyuo viwili (2) vipya vimekaguliwa na kutambuliwa kuwa na sifa ya kutoa mafunzo ya Astashahada na Stashahada za afya na uzalishaji wa wanyama ambavyo ni (1) Tanzania Research and Career Development Institute (TRACDI), kilichopo Nzughuni, Dodoma na (2) KARUCO kilichopo Kagera. Vyuo hivyo vitaanza kutoa mafunzo katika mwaka wa masomo 2020/2021. 

(ix) Chuo cha Mahinya (Ruvuma) kimekaguliwa na kuelekezwa kukamilisha hatua zilizobakia za maandalizi kabla ya kutambuliwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara kupitia Baraza la Veterinari Tanzania imeweka utaratibu kwa wahitimu wote wa shahada ya veterinari kupitia mafunzo kwa vitendo (internship) ya mwaka mmoja (1) na wale wa Stashahada ya afya na uzalishaji wa wanyama miezi sita (6) kama ilivyoelekezwa katika Sheria ya Veterinari (SURA 319). Lengo la mpango huu ni kuwajengea weledi na umahiri zaidi wahitimu wote wa Udaktari wa Wanyama na Stashahada ya Afya na Uzalishaji wa Wanyama katika kuwahudumia wafugaji. Utaratibu huu utaanza kutekelezwa katika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara kupitia Baraza la Veterinari Tanzania itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Veterinari (SURA 319) na Kanuni zake kwa kusajili madaktari wa mifugo 70; vituo vya huduma ya afya ya wanyama 400; kuorodhesha na kuandikisha wataalam wasaidizi 1,000; na kutoa leseni kwa wakaguzi wa nyama, wahimilishaji na wataalam wa maabara za veterinari 200. Aidha, Baraza litaendelea kusimamia maadili ya wataalam na viwango vya utoaji huduma ya mifugo kwa kufanya ukaguzi wa vituo vya kutoa huduma ya mifugo katika Halmashauri zote nchini na kusimamia mafunzo kwa vitendo na ya kujiendeleza kwa wataalam kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Utafiti, Mafunzo na  Ugani Uratibu wa Utafiti naMafunzo 

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kusimamia shughuli za Utafiti na Mafunzo ya Mifugo nchini kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA). Aidha, Wizara, imeandaa Ajenda ya Kitaifa ya Utafiti wa Mifugo ya miaka mitano (Livestock Research agenda 2020 -2025) iliyozinduliwa tarehe 16 Novemba, 2019. 

Lengo la Ajenda hii ni kutekeleza vipaumbele vya Serikali, katika kutekeleza ajenda hii kwa ufanisi Wizara imeandaa kanuni za utafiti (Livestock Research Regulations 2020) na Kanzidata ya Watafiti wa Mifugo Nchini (National Livestock Research Database). Matokeo makubwa yanayotarajiwa ni pamoja na:

(i) Kufungua makabati yaliyoficha tafiti zilizofanyika miaka iliyopita kuanzia mwaka 2010, kuziorodhesha na kuwezesha kuwafikia wadau ilikutatua changamoto za Sekta ya Mifugo. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya tafiti 279 zimeorodheshwa. 

(ii) Kupanua wigo wa utafiti kwa kuzitambua na kuziorodhesha tafiti mbalimbali zinazofanywa na watafiti nchini
60
ikijumuisha wanafunzi wa Shahada za Uzamili na Uzamivu. 

(iii) Kuweka msingi wa kisheria katika kusimamia na kutoa wajibu na majukumu kwa watafiti kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa na Serikali katika kufanya tafiti mbalimbali nchini. (iv) Kuwezesha ukusanyaji wa tafiti zote za mifugo zinazofanyika kila mwaka na kuzisambaza kwa wadau, hali ambayo itawezesha wadau mbalimbali kupata taarifa za utafiti kwa urahisi na kwa wakati, pia, kwa upande wa Serikali itasaidia kutunga na kurekebisha sera, sheria, kanuni na miongozo. 

(v) Kuimarisha ushirikiano na mahusiano ya taasisi za utafiti.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara  imeandaa Mpango Mkakati wa Uendelezaji na Uhifadhi wa Kosaafu na Uboreshaji wa Mbari za Mifugo (National Compact Strategies and Action Plan to Implement Global Plan of Action for Animal Genetic Resources in Tanzania). Utekelezaji wa mkakati huo utasaidia:

(i) Kuweka miongozo ya kutambua kabila, koo na mbari za mifugo na kufanya uchambuzi yakinifu wa kosaafu (characterization) pamoja mifumo ya uzalishaji mifugo nchini; 

(ii) Kukuza utumiaji endelevu wa kosaafu kwa kupitia teknolojia za kisasa na maarifa asilia; 

(iii) Kutengeneza mfumo imara na wa uhakika wa Uhifadhi Kosaafu za Mifugo nchini;na 

(iv) Kushawishi jamii za kimataifa katika kuimarisha uwezo wa Taasisi zetu zinazohusika na uendelezaji mbali.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara  ilifuatilia ajira za wahitimu (tracer study) wa Vyuo vya mafunzo ya Mifugo nchini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2014 – 2019). Lengo la ufuatiliaji huo ilikuwa ni kutambua kiwango cha wahitimu walioajiriwa katika sekta za umma na binafsi ndani ya sekta ya mifugo na kuainisha changamoto. Aidha, ufuatiliaji huu umebainisha changamoto kubwa kuwa ni upungufu wa mafunzo ya ujasiriamali katika mitaala na ukosefu wa mitaji kwa wahitimu. Serikali inaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizi ili kuwawezesha wahitimu wengi kujiajiri katika sekta ya mifugo kwa kuhakikisha vituo atamizi (incubation centres), mafunzo kazini (internship) na kupitia upya mitaala.

Mheshimiwa Spika, Wizara, imeandaa Mitaala mitatu (3) ya kozi fupi za umahiri katika Tasnia za maziwa, nyama na ngozi. Lengo la mitaala hii ni kuwezesha upatikanaji wa wataalam mahususi katika viwanda vya Uchakataji na Usindikaji wa mazao yatokanayo na mifugo. Walengwa wa mafunzo haya ni wataalamu wa mifugo na wajasiriamali katika Mnyororo wa thamani wa Sekta ya Mifugo. Mafunzo haya yatatolewa katika Kampasi za LITA na hivyo kutatua tatizo la uhaba wa Wataalamu hawa wa umahiri.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kuratibu na kusimamia utoaji wa mafunzo ya mifugo kwa vyuo vya Serikali na Binafsi vinavyotumia Mitaala ya Wizara iliyopitishwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE). Vyuo binafsi vya Mifugo vinavyotumia Mitaala ya Wizara ni pamoja na Igabiro (Muleba), Hagafilo (Njombe), Kilacha (Moshi), Visele (Mpwapwa), CANRE (Ubungo) na Kaole (Bagamoyo). Aidha, Wizara itaendelea kuwaandaa wakufunzi wa vyuo vya mifugo kutoa mafunzo kwa kutumia mfumo wa Weledi na Stadi Stahiki (yaani Competency-based Education and Training - CBET). Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi na vitengo itaanzisha kanzidata ya TEHAMA (ICT) ya Mafunzo na Ugani. Lengo ni kurahisisha upatikanaji wa taarifa zamafunzo na ugani.

Huduma za Ugani wa Mifugo.

Mheshimiwa Spika; idadi ya watumishi wa ugani kwa sekta ya mifugo bado ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji. Mahitaji ya wataalam wa Ugani wa mifugo kwa sasa ni Wagani 17,848 kwa mchanganuo ufuatao; ngazi ya Mkoa 52, Halmashauri za Wilaya 1,643; Kata 3,834 na vijiji 12,319. Aidha, Wagani wa mifugo  waliopo kwa sasa katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ni 3,795 na hivyo kuwa na upungufu wa Wagani 14,053 kwa kada za uzalishaji, afya ya mifugonanyanda za malisho. Serikaliitaendelea kuongeza idadi ya Maafisa Ugani kadiri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kutoa elimu ya mafunzo rejea  na maarifa mapya kuhusu uzalishaji wa kibiasharakama ifuatavyo:

(i) Wadau 8,158 katika Halmashauri 25 wakiwemo wafugaji 6,030 maafisa ugani 471, wanafunzi wa shule za sekondari na msingi 1,433, wakuu wa shule za sekondari na msingi 87 na watendaji wa kata na vijiji 137. Hivyo, hili ni ongezeko la asilimia 77.4 kutoka 1,840 katika mwaka 2018/2019 hadi kufikia 8,158 mwaka 2019/2020. Mafunzo hayo yametolewa katika Halmashauri za Mvomero, Sumbawanga Mji, Sumbawanga Vijijini, Nkasi, Kalambo, Mpanda, Chato, Tanganyika, Mpimbwe, Nsimbo, Mlele, Meatu, Songwe, Ileje, Tunduma Mji, Mbozi, Momba, Mkuranga, Mbeya Jiji, Mbeya Vijijini, Mbarali, Chunya, Kyela, Busokelo na Rungwe. Mafunzo hayo yalihusu ufugaji bora wa mifugo ya aina mbalimbali.

(ii) Wachunaji wa ngozi 735 na wataalam wa mifugo 94 wamejengewa uwezo kuhusu uchunaji bora wa ngozi unaozingatia mahitaji ya soko kutoka katika Mikoa nane (8) (KiambatishoNa. 24).

(iii)Vyama hai 40 vya ushirika wa wafugaji vimeratibiwa katika Mikoa ya Manyara (2), Iringa (2), Simiyu (1), Tanga (8), Kilimanjaro (6), Arusha (7), Singida (1), Mbeya (11) na Morogoro (2).

(iv)Wafugaji na wadau 115,979 wamepatiwa elimu ya ufugaji bora wa kibiashara kupitia maonesho ya Saba Saba (25,200), Nane Nane (75,089)na Siku ya Chakula Duniani (15,670).

(v) Machapisho mbalimbali kuhusu ufugaji bora vikiwemo vitabu 1,533; vipeperushi 16,260; majarida 500; na mabango 150 yaliandaliwa na kusambazwa.

(vi)Jumla ya Wataalamu 117 walipata mafunzo ya kudhibiti kuenea kwa magonjwa yasiyokuwa na mipaka (Trans Boundary Animal Diseases – TADs) kwa ufadhili wa USAID.

(vii) Mashamba darasa 31 ya malisho yameanzishwa katika Halmashauri 13 za Ikungi, Itigi, Mkalama, Iramba, Singida Manispaa, Singida Vijijini, Manyoni, Monduli,  Rungwe, Njombe vijijini, Mufindi, Kahama na Kishapu.  Aidha, kwa sasa kuna jumla ya mashamba darasa 88 katika Halmashauri 37.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kutoa mafunzo rejea kwa wafugaji 181,000 katika Halmashauri 156 na Maafisa Ugani 200, kuanzisha mashamba darasa 50 katika Halmashauri 30 na kusambaza teknolojia za ufugaji bora kupitia maonesho ya Nane Nane, Saba Saba na Siku ya Chakula Duniani. Aidha, Wizara itaandaa na kusambaza machapisho ya ufugaji bora, kuratibu utoaji wa huduma za ugani nchini, kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika wa wafugaji na kuandaa makala mbalimbali.

Taasisi Zilizo Chini ya Wizara Kampuni ya Ranchi za Taifa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara kupitia Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imetekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja: 

(i) Kutunza jumla ya ng’ombe 14,742, mbuzi 2,920, kondoo 2,889, nguruwe 259 na farasi 31. 

(ii) Kuzalisha na kukuza ndama 4,781 ikilinganishwa na ndama 4,606 waliozalishwa na kukuzwa katika mwaka 2018/2019. 

(iii) Kununua  ng’ombe 2,283 wenye thamani ya shilingi 1,369,800,000 kutoka kwa wafugaji wa asili kwa ajili ya kunenepesha kwa kutumia vyakula vya ziada ili kuzalisha nyama bora na hivyo kuwa sehemu ya soko la uhakika kwa wafugaji nchini ikilinganishwa na ng’ombe 1,343 walionunuliwa katika mwaka2018/2019. 

(iv) Kuuza ng’ombe 4,998 wenye thamani ya shilingi 3,040,309,298 ikilinganishwa na ng’ombe 3,598 wenye thamani ya shilingi 2,572,000,000 waliouzwa katika mwaka 2018/2019. Kati ya ng’ombe hao waliouzwa, ng’ombe 2,283 walinunuliwa kutoka kwa wafugaji na kunenepeshwa na 2,715 walitoka kwenye ranchi.

(v) Jumla ya ekari 6,771 zimefyekwa vichaka kwa ajili ya kuruhusu ukuaji wa malisho. Pia, Kampuni itanunua vifaa vya kisasa kwa ajili uandaaji wa mashamba ya malisho na kuvyeka vichaka. (vi) Kuweka mipaka ya kuonekana katika Ranchi za Missenyi, Ruvu na Uvinza. 

(vii) Kumega eneo lenye ukubwa wa hekta. 24,435.912 kutoka katika Ranchi za Missenyi (22,201.094) na Ruvu (2,234.818 ha) kwa ajili ya matumizi ya kilimo, mifugo na makazi katikavijiji.
 (viii) Yapo maduka7ya nyama katika maeneo ya Bukoba, Dar es Salaam, Dodoma, Kongwa, Hai, Morogoro na Kalambo (Rukwa).

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Kampuni ya NARCO imepanga kutekeleza kazi zifuatazo:

(i) Kuzalisha ng’ombe4,964, mbuzi1,937kondoo 1,317 pamoja na kuzalisha na kuuza nyama tani896; 

(ii) Kununua jumla ya ng’ombe 6,000 wenye thamani ya shilingi 3,600,000,000 na kuuza jumla ya ng’ombe 7,996 kwa thamani ya shilingi 6,272,870,000. 

(iii) Kufyeka vichaka ekari 2,696 na kupima na kuweka  alama za mipaka inayoonekana katika ranchi 11 za Kagoma, Mabale, Kitengule, Kikulula, Kongwa, Mzeri, West Kilimanjaro, Kalambo, Usangu, Mkata, Dakawa;na eneo la Mwisa II. 

(iv) Kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wafugaji 500 katika vijiji vinavyozunguka Ranchi za NARCO; na mafunzo kwa vitendo kwa wanachuo 290 kutoka katika Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo hapa nchini. 

(v) Kufungua maduka mapya mawili (2) ya nyama katika Mikoa ya Mwanza na Arusha. Pia, itanunua magari mawili (2) yenye mfumo baridi (refrigerated trucks) kwa ajili ya kusafirisha nyama.

Bodi ya Nyama Tanzania 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Bodi ya Nyama Tanzania imeendelea kuratibu, kusimamia na kuendeleza tasnia ya nyama nchini ambapo mafanikio yafuatayo yamepatikana:

(i) Vibali 86 vya kuuza nyama nje ya nchi vilitolewa. Aidha, jumla ya tani 692.36 za nyama (nyama ya ng’ombe tani 142.18, mbuzi tani 36.07 na kondoo tani 1.11, punda na tani 513) zenye thamani ya shilingi 2,985,609,691 (Dola za Marekani 1,298,091.17) ziliuzwa  nje katika nchi za Dubai, Iraq, Omani, Comoro, Hongkong na Vietnam ikilinganishwa na kiasi cha tani 1,207.93 zenye thamani ya shilingi 5,207,057,286.21 zilizouzwa nje ya nchi katika mwaka 2018/2019. 

(ii) Vibali 36 vimetolewa kuingiza nyama ndani ya nchi yenye jumla ya tani 243.65 (nyama ya ng’ombe tani 195.12, nguruwe tani 48.53) na thamani ya shilingi 4,066,632,530 (Dola za Marekani 1,768,101.10) kutoka Kenya, Afrika Kusini, Ubelgiji na Uingereza ikilinganishwa na kiasi cha tani 516.63 zenye thamani ya Shilingi 4,970,240,959.00 (Dola za Marekani 2,160,974.33) zilizoingizwa nchini mwaka 2018/2019. 

(iii)Uingizaji wa mazao ya mifugo kutoka nje ya nchi umeshuka kwa asilimia90. 

(iv)Wadau wa nyama 757 wametambuliwa na kusajiliwa katika mikoa 21 (Kiambatisho Na. 25). 

(v) Jumla ya machinjio 31 zimekaguliwa. Kutokana na ukaguzi huo machinjio 8 zimefungwa kutokana na kushindwa kukidhi vigezo, machinjio hizo zipo katika mikoa tisa (9) (Kiambatisho Na.26). 

(vi)Wadau wa nyama 706 wamepatiwa mafunzo juu ya uanzishaji vyama vya ushirika vya mifugo, uzalishaji wa nyama bora na salama, elimu ya biashara ya nyama, utambuzi na usajili wa mifugo na  fursa za uwekezaji katika tasnia ya nyama nchini. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara kupitia Bodi ya Nyama itaendelea kuhamasisha uboreshaji mifugo ili kuimarisha mnyororo wa thamani katika tasnia ya nyama unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje  ya nchi; kuendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza zaidi katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata na kusindika nyama  ili kuziba  pengo la mahitaji ya nyama nchini; kutoa mafunzo ya uzalishaji na uuzaji wa nyama kwa kuzingatia taratibu za usafi;  kutambua na kusajili wadau wa tasnia ya nyama na vyama vyao.

Bodi ya Maziwa Tanzania 

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Bodi ya Maziwa Tanzania imeendelea kusimamia biashara ya maziwa ndani na nje ya nchi ili kuimarisha uzalishaji na biashara ya maziwa na mazao yake. Katika mwaka 2019/2020 jumla ya lita bilioni 3 za maziwa zilizalishwa na vibali 443 vimetolewa ili kuingiza maziwa yenye ujazo wa lita 11,725,859.84 vikiwa na thamani (FOB value) ya Shilingi 15,199,487,699 kutoka nchi za Afrika Kusini; Uganda; Kenya; United Arab Emirates; Uholanzi; na Ireland ikilinganishwa na vibali 692 vilivyotolewa mwaka 2018/2019 kuingiza maziwa yenye ujazo wa lita 18,617,659.07 vikiwa na thamani (FOB value) ya Shilingi 26,224,025,033.80 sawa na upungufu wa asilimia 42.04. Kupungua kwa kiasi cha maziwa kinachoingizwa nchini kumetokana na kuimarika kwa udhibiti wa uingizaji maziwa na mazao yake kutoka nje ya nchi kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani, kuongezeka uzalishaji wa maziwa na kuimarika kwa viwanda vya ndani vya kusindika maziwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Bodi imeendelea kusimamia tasnia ya maziwa ambapo mafanikioyafuatayo yamepatikana:

(i) Programu ya Unywaji Maziwa Shuleni imeratibiwa katika shule 49 za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Njombe, Mbeya na Tanga zenye wanafunzi33,115.

(ii) Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni imeadhimishwa kitaifa Mkoani Iringa tarehe 26 Septemba, 2019 ambapo jumla ya shule 10 zenye wanafunzi 3,400 zilishiriki na pakiti 600 za ujazo wa mililita 250 ziligawiwa kwa wanafunzi.

(iii) Wadau 16,000 wamehamishwa kuwekeza katika tasnia ya maziwa kupitia maonesho ya Saba Saba, Wiki ya unywaji Maziwa shuleni, Nane Nane na Bonanza la michezo.

(iv) ATM tatu (3) za maziwa zimezinduliwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Bodi ya Maziwa kwa kushirikiana na TAMPA imeingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kudurufu mashine hizo na kusambazwa nchini baada ya kuthibitishwa ubora wake.

(v) Wiki ya maziwa itaadhimishwa kielekroniki kuanzia tarehe 28 Mei hadi tarehe 1 Juni, 2020 kwa kuzingatia tahadhari na kujikinga na ugonjwa wa COVID 19. (vi) Wadau 250 wa maeneo ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro, Mbeya, Tanga na Pwani wamesajiliwa ikilinganishwa na wadau 63 waliosajiliwa katika mwaka 2018/2019.

(vii)Ukaguzi umefanyika katika maeneo 160 ya kuzalisha, kusindika, kutunza na kuuza maziwa ikiwemo vioski (19), maduka (62), viwanda (17) na magari ya kusafirisha maziwa(62).

(viii) Wadau 283 wamepatiwa mafunzo, kati ya hao 126 kuhusu  usindikaji maziwa; 135 uzalishaji maziwa na 22 Udhibiti wa Ubora wa Maziwa katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Morogoro na Pwani.

(ix) Vikundi 18 vyenye wanachama 3,182 vimejengewa uwezo katika maeneo ya Kiutawala; Kiufundi na Usimamizi wa Fedha kutoka katika Mikoa ya Iringa (6); Njombe (4); Mbeya (3); Songwe (1); Morogoro (1); Pwani (1); Mwanza (1); na Dar es Salaam (1).

(x) Vituo 10 vya kukusanyia maziwa vimejengwa kwa kushirikiana na sekta binafsi katika mikoa ya Ruvuma (6), Pwani (2) na Dar es Salaam (2).

(xi) Kusimamia upatikanaji wa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo wenye thamani ya shilingi 241,742,000 kwa wafugaji 46  wa vyama vya CHAWAMU na UWAMWA vilivyopo Mkoani Tanga kwa ajili ya kununua mitamba 76 na ujenzi wa mabanda bora 25.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara kupitia Bodi ya Maziwa Tanzania itaendelea kuimarisha na kujenga vituo 50 vya kukusanyia maziwa vyenye uwezo wa lita 135,000 kwa siku katika maeneo yanayozalisha maziwa kwa wingi; kuhamasisha ujenzi wa mabanda  bora ya ng’ombe wa maziwa; uwekezaji katika viwanda vya kusindika maziwa na mazao yake; uhamasishaji wa uundaji wa ushirika wa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa na kuwaunganisha wafugaji hao na taasisi za kifedha ili kupata mitaji na kufuga kwa tija. Aidha, Bodi itaendelea kuhamasisha unywaji wa maziwa kupitia wiki ya maziwa; unywaji wa maziwa shuleni na Bonanza la michezo.
Wakala wa Maabara ya Veterinari.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara kupitia Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imepata mafanikio yafuatayo:

(i) Idadi ya chanjo za  mifugo zinazozalishwa imeongezeka kutoka chanjo nne (4) mwaka 2018/19 kufikia chanjo sita (6) mwaka 2019/2020; 

(ii) Jumla ya dozi 49,008,325 za chanjo za mifugo zimezalishwa na kusambazwa nchini ambapo Halmashauri 40 dozi 1,287,000, wasambazaji wa pembejeo za mifugo na wachanjaji binafsi dozi 47,721,325 (Kiambatisho Na.27); 

(iii) Ujenzi wa jengo jipya litakalotumika katika utengenezaji wa chanjo za bakteria umekamilika kwa asilimia75; (iv) Uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo katika sampuli 13,587 umefanyika ambapo magonjwa muhimu yaliyotambuliwa ni pamoja na Kichaa cha Mbwa, Kimeta, Ugonjwa wa Kutupa Mimba, Nagana, Ndigana Kali, Ndigana Baridi na Homa ya Mapafu ya Ng’ombe; 

(v) Uchambuzi wa ubora wa vyakula vya mifugo katika sampuli 1,260 umefanyika ambapo sampuli 46 sawa na asilimia 6 zilibainika kuwa na upungufu wa nishati na protini; 

(vi) Kituo kipya cha Wakala kimeanzishwa katika Mji wa Sumbawanga kwa ajili ya kuhudumia Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi; 

(vii) Miradi ya kutokomeza ugonjwa wa malale inatekelezwa katika vijiji vya Emboreet, Loibor siret na Kimotorok katika Wilaya ya Simanjiro  ambapo jumla ya mbung’o 5,000 na sampuli 770 za damu za ng’ombe zilikusanywa kwa lengo la kuangalia maambukizi ya ndorobo. Pia, utafiti unaendelea ili kubaini kemikali bora ya kufukuzia/kuvutia mbung’o na jamii ya inzi wasumbufu wa mifugo katika vijiji vya Mwangudo, Sungu, Makao na Mbushi katika Wilaya ya Meatu; 

(viii) Utafiti katika maeneo ya utengenezaji wa chanjo ya Homa ya Mapafu ya Mbuzi (CCPP), uimarishaji wa ufugaji wa kuku wa kienyeji, udhibiti wa ndorobo na uimarishaji wa uwezo wa kudhibiti viini vya magonjwa unaendelea. Utafiti huo umepata ufadhili wenye thamani ya shilingi 1,635,094,800 kutoka International Atomic Energy Agency (IAEA), Biotechnology and Biological Sciences Research Council (BBSRC), BIOINNOVATE na COSTECH. 

(ix) Jumla ya sampuli 82 za dawa za kuogesha mifugo zilifanyiwa uchunguzi ambapo sampuli 71 sawa na asilimia 87 kati ya hizo zilionekana kuwa zinafaa kwa matumizi. 

(x) Ujenzi wa Kliniki ya mifugo katika Wilaya ya Meatu umekamilika kwa asilimia85.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara kupitia Wakala wa Maabara ya Veterinari itaongeza uzalishaji wa chanjo na itaanza kuzalisha wa aina tatu (3)  mpya za chanjo ambazo ni Chanjo ya Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa, Sotoka ya Mbuzi na Kondoo na Homa ya Mapafu ya Mbuzi. Pia, Wakala utaendelea kuchunguza na kutambua magonjwa ya mifugo yanayotokea nchini kwa kupima sampuli 35,000, kufanya uchambuzi wa ubora wa vyakula kwenye sampuli 5,000 na kuchunguza nguvu za dawa za josho katika sampuli 300 kutoka maeneo yaliyoonesha usugu wa dawa za kuogeshea mifugo. Aidha, TVLA itaendelea kufanya tafiti za magonjwa ya mifugo na wadudu waenezao magonjwa hayo. Pia, TVLA itaanzisha kituo kipya cha uchunguzi na utambuzi wa magonjwa katika Mkoa wa Simiyu ili kuigawa Kanda ya Ziwa yenye mikoa sita (6) inayohudumiwa na kituo kimoja cha Mwanza.

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) ilitekeleza miradi ya utafiti 39 katika nyanja za utafiti wa ng’ombe wa maziwa; ng’ombe wa nyama; mbuzi; kondoo; kuku; malisho; na sayansi ya jamii na uchumi. Mafanikio yaliyopatikana nikama ifuatavyo:

(i) Ng’ombe bora wa maziwa 119 wenye mchanganyiko wa damu za Sahiwal na Friesian na Danish Red); (Sahiwal na Mpwapwa); Mpwapwa na Danish Red walizalishwa. 

(ii) Ng’ombe chotara wa nyama 77 wenye mchanganyiko wa damu za Mpwapwa na Boran; Mpwapwa na Sahiwal; na Sahiwal, MpwapwanaBoranwalizalishwa. 

(iii) Ng’ombe chotara 141 wenye sifa mchanganyiko ya kuzalisha nyama na maziwa (dual purpose) walisambazwa kwa wafugaji kwa ajili ya kuboresha uzalishaji katika mikoa nane (8) ikiwepo Pwani; Mwanza; Simiyu; Morogoro; Tanga; Geita; Dodoma na Mbeya ikilinganishwa na ng’ombe 130 waliosambazwa katika mwaka 2018/2019. 

(iv) Ziara ya mafunzo kwa wafugaji 20 kutoka Halmashauri ya Longido kwenda nchini Kenya ili kujifunza na kupata uzoefu wa umuhimu wa uhimilishaji ilifanyika. Kutokana na ziara hiyo Ushirika wa Wafugaji wa Ng’ombe aina ya Sahiwal Longido (UWASALO) wenye wanachama 42 umeundwa kwa lengo la kuunganisha wadau na kurahisisha uratibu. 

(v) Jumla ya mbuzi 1,472 wamenenepeshwa kupitia Kituo Atamizi kinachoendeshwa na TALIRI kwa ushirikiano na PASS. Aidha, ujenzi wa mabanda 10 yenye uwezo wa kunenepesha mbuzi 2,000, Ofisi (1), machinjio (1), maduka ya kuuzia nyama (10) na mgahawa (1) umefanyika. 

(vi) Kupitia uhawilishaji kiinitete (MOET), jumla ya viinitete 34 vilivunwa na kupandikizwa kwa ng’ombe waleaji mimba 34. Vilevile, mtambo wenye thamani ya shilingi milioni 189 wa kuzalisha kimiminika cha hewa baridi ya Naitrojeni wenye uwezo wa kuzalisha lita 65 kwa siku umenunuliwa na kusimikwa kwenye maabara ya bayoteknolojia iliyopo Mpwapwa.

(vii) Ufuatiliaji wa mwenendo wa uzalishaji kwa kutumia Teknolojia ya TEHAMA umefanyika kwa wafugaji 19,000 ambapo ng’ombe wa maziwa 179,197 wanafuatiliwa ufanisi wao katika mikoa ya Arusha (31,803); Kilimanjaro (31,081); Tanga (59,589); Iringa (28,458); na Mbeya (28,262). Mfumo huo unawezesha wafugaji kupata ushauri wa kitaalam kulingana na hali ya ng’ombe wake. 

(viii) Jumla ya vifaranga 2,400 vya kuku wa asili aina ya Horasi vilianguliwa kwa ajili ya tathmini ya ukuaji na uzalishaji.  Utafiti huu wa kupata kuku wa asili utafanyika kwa kipindi cha miaka 5 hadi 8 kwa lengo la kupata kuku wenye wastani wa uzito wa kilo 1.5 katika umri wa wiki 16 na uwezo wa kutaga mayai200hadi240kwa mwaka. 

(ix) TALIRI imesambaza kuku chotara aina ya Sasso 32,000 na Kroiller 11,000 kwa kaya za wafugaji 1,864 katika Mikoa ya Dodoma, Tanga, Mtwara, Singida, Mbeya, Simiyu na Mwanza.
(x) Ili kutekeleza utafiti wa kuku, TALIRI imenunua vifaa na mitambo mbalimbali vikiwemo; mashine ya kuangulia vifaranga (egg incubator) yenye uwezo wa kuatamisha mayai5,280,Vizimba(cages) tisa(9) vyenye uwezo wa kubeba kuku 432, Mashine ya kusaga na kuchanganya chakula cha kuku yenye uwezo wa kuchakata tani 1.0hadi1.5 kwa saamoja. 

(xi) Wataalam 16 walipatiwa mafunzo ya uhimilishaji mbuzi ambapo mbuzi 181 wamehimilishwa kwenye Halmashauri ya Siha. Vilevile, mbuzi 134 walisambazwa kwa wafugaji katika maeneo ya Kwimba, Ulanga, Bariadi, Tanga, Pwani, Morogoro, Chato, Nyamagana, Meatu, Misungwi, Bagamoyo, Dodoma Mjini na Ilala. Aidha, mbuzi 119 aina ya Malya, Gogo White, Sonjo RednaPare Whitewalizalishwa. 

(xii) Vitalu 90 vyenye aina sita (6) za Mikunde na nne (4) za nyasi kwa ajili ya majaribio ya urasimishaji wa mbegu za malisho vimestawishwa kwenye Vituo vya Mpwapwa, Uyole na Tanga. 108. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TALIRI inatekeleza utafiti kwa kufuata Agenda ya Utafiti wa Mifugo nchini. 

Aidha, TALIRI imeanzisha kanzidata ya kitaifa ya tafiti za mifugo (National Livestock Research Database) ambapo jumla ya Tafiti 433 zimekusanywa kutoka Taasisi zinazofanya tafiti za mifugo nchini ambazo ni Vyuo Vikuu (187); Taasisi za Utafiti (210); Taasisi za Wizara (27) na Mashirika
yasiyo ya Serikali (9). Tafiti hizo zinapatikana kupitia tovuti ya TALIRI http://research.taliri.go.tz
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TALIRI imebaini aina saba (7) za magugu sumbufu katika maeneo ya machunga nchini yanayohitaji kupata ufumbuzi kwa haraka. Magugu hayo ni Gugu la Kongwa (Mahata); Gugu la Siam (Amachabongo), Gugu caroti; Gugu la Cordifolia, Gugu la Jaegeri, Gugu mti Prosopis (Mrashia) na Gugu Ndulele. Aidha, TALIRI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine inafanya utafiti wa kudhibiti gugu “Mahata” kwa kutumia njia za kemikali, kibaiolojia na matumizi dawaza miti ya asili.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara kupitia TALIRI itaratibu tafiti zote nchini, kutathmini na kuendeleza utafiti wa mifugo na malisho ili kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa, nyama, mayai na ngozi kuchangia uchumi wa viwanda. Aidha, Taasisi itaimarisha miundombinu ya mashamba ya utafiti katika kanda saba (7). Pia, TALIRI kwa ushirikiano na PASS itanenepesha mbuzi 4,000 na Kuzalisha mbuzi 1,500 kwa njia ya uhimilishaji. Vilevile, TALIRI kupitia Mradi wa ADGG, itafanya maonesho ya Gwaride la pili la ng’ombe bora wa Maziwa kwa njia ya TEHAMA katika kipindi hiki cha Janga la ugonjwa wa Corona (COVID–19).

Wakala wa Mafunzo ya Mifugo

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara kupitia Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) imedahili wanafunzi wa ngazi ya Astashahada na Stashahada 3,634 ukilinganisha na wanafunzi 2,536 waliodahiliwa mwaka 2018/2019.

Idadi hii ni ongezeko la wanafunzi 1,098, sawa na asilimia 43.3. Idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu masomo katika mwaka 2019/2020 kutoka Vyuo vya Serikali ni 1,678 ukilinganisha na wanafunzi 1,208 waliohitimu mwaka 2018/2019, ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 470, sawa na asilimia 38.9. Idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu masomo kutoka vyuo binafsi ni 407.

Aidha, jumla ya wafugaji 594 wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi katika Kampasi za Wakala ukilinganisha na wafugaji 363 waliopatiwa mafunzo katika mwaka 2018/2019, ikiwa ni ongezeko la wafugaji 231 sawa na asilimia 63.6. Pia, jumla ya wafugaji 1,468 wamefikiwa na wanachuo wakati wa mafunzo yao kwa vitendo.

MheshimiwaSpika, ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi waliodahiliwa katika mwaka huu na LITA, miundombinu mbalimbali imeboreshwa.  Miundombinu iliyokarabatiwa ni pamoja na Hosteli tatu (3) katika Kampasi ya Tengeru; Hosteli mbili (2) katika Kampasi ya Buhuri; Hosteli mbili (2) katika Kampasi ya Temeke; Hosteli moja (1) katika Kampasi ya Morogoro; Hosteli mbili (2) katika Kampasi ya Mpwapwa; Madarasa matatu (3) katika Kampasi ya Morogoro; Kumbi mbili (2) za mihadhara katika Kampasi za Morogoro na Mpwapwa; Maabara mbili (2) katika Kampasi za Tengeru na Temeke,  Maktaba mbili (2) katika Kampasi za Madaba na Tengeru na  vyoo vitano (5) katika Kampasi za Morogoro, Mabuki, Tengeru, Mpwapwa na Buhuri. Miundombinu iliyojengwa upya ni vyoo vitatu (3) vya wanafunzi katika Kampasi za Morogoro, Mabuki na Kikulula.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara kupitia LITA imefanya utafiti wa ajira za wahitimu wa Vyuo vya Mifugo nchini (2014 – 2019). Katika kipindi tajwa wanafunzi 8,132 walihitimu masomo katika ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada ambapo matokeo ya awali kwa wahitimu 776 sawa na asilimia 9.5 ya wahitimu wote ndio waliofanikiwa kuajiriwa katika Sekta za Umma (651), walioajiriwa katika Sekta Binafsi (60) na waliojiajiri katika Sekta Binafsi (65) ndani ya Sekta ya Mifugo hadi sasa na asilimia 90.5 hawajulikani kazi wanazofanya baada ya kuhitimu masomo yao. Aidha, changamoto kubwa zimeainishwa katika utafiti huu na maeneo pendekekezwa ya utatuzi yameainishwa ambapo Serikali inayafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara kupitia LITA itatekeleza yafuatayo:

(i) Kudahili wanafunzi 4,000 wa ngazi ya Astashahada na Stashahada. 

(ii) Kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo mabweni/hostel, madarasa, maktaba, vyoo na maabara ili kuwezesha utoaji wa mafunzo ya muda mrefu na mfupi.

(iii) Kuandaa Mpango wa utoaji mafunzo ya muda mfupi kwa Wafugaji na wajasiriamali wengine ili kuongeza uzalishaji na tija katika Sekta ya Mifugo. Aidha, Mafunzo hayo yatatolewa katika miezi ya Machi, Aprili, Agosti, Septemba na Oktoba kila mwaka. Miongozo ya utekelezaji wa Mpango huu inaandaliwa kwa kushirikiana na chama cha wafugaji Tanzania ambapo katika awamu ya kwanza kaya 1,500 za wafugaji zitafikiwa. Lengo la mpango huu ni kuzifikia kaya za wafugaji milioni 4.6 ndani ya miaka mitano ijayo.


SEKTA YA UVUVI (FUNGU 64) HALI YA SEKTA YA UVUVI 

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Uvuvi ni moja kati ya sekta muhimu za kiuchumi hapa nchini. Shughuli za uvuvi hapa nchini zinahusisha uvuvi kwenye maji ya asili na ukuzaji viumbe maji. Katika mwaka 2019, Sekta ya Uvuvi ilichangia asilimia 1.71 ya Pato la Taifa na imekua kwa asilimia 1.5 Aidha, Sekta ya Uvuvi huchangia katika kuwapatia wananchi uhakika wa chakula, lishe, kuongeza kipato, fedha za kigeni na kupunguza umaskini. Vilevile, inakadiriwa kuwa zaidi ya Watanzania milioni 4.5 wanategemea shughuli zinazohusiana na uvuvi. 116. Mheshimiwa Spika, shughuli za uvuvi kwenye maji ya asili huendeshwa na wavuvi wadogo ambao huchangia zaidi ya asilimia 95 ya samaki wote wanaozalishwa nchini na asilimia tano (5) iliyobaki huchangiwa na uvuvi wa kibiashara. Aidha, uvuvi wa kibiashara hufanyika katika maji ya Kitaifa kwa uvuvi wa samaki aina ya Kambamiti na kwenye Ukanda wa Uchumi wa Bahari kwa kuhusisha meli za kigeni. Katika mwaka 2019/2020 jumla ya wavuvi 202,053 wanaotumia vyombo vya uvuvi 58,930 walivua kiasi cha tani 392,933.0 za samaki zenye thamani ya shilingi trilioni1.85(Kiambatisho Na. 28).

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhamasisha shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji ambapo kwa mwaka 2019/2020, jumla ya vifaranga 21,676,187 (Kiambatisho Na. 29) vimezalishwa kutoka katika vituo vya binafsi na Serikali ambapo uzalishaji wa mazao ya viumbe maji ulifikia tani 18,716.56. Kati ya tani hizo, tani 17,233 ni za samaki wenye mapezi, tani 73.56 ni za Kambamiti, tani 1,410ni za mwani pamoja na vipande 550 vya lulu kutoka kwa wakuzaji viumbe maji 28,009. 118. Mheshimiwa Spika, samaki huchangia takriban asilimia 30 ya protini inayotokana na wanyama. Ulaji wa samaki kwa mtu kwa mwaka hapa nchini umeongezeka kutoka kilo 8.2 mwaka 2018/2019 hadi kufikia kilo 8.5 mwaka 2019/2020. Aidha, kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa wastani wa ulaji samaki duniani kote ni kilo 20.3 kwa mtu kwa mwaka (FAO, 2018). Serikali itaendelea kuhamasisha ulaji wa samaki miongoni mwa watanzania. 

Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa za utafiti, wingi wa samaki katika maji yetu umeongezeka kutoka tani 2,803,000 mwaka 2018/2019 hadi kufikia tani 3,274,165 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 16.8. (Kiambatisho Na. 30).  Ongezeko hilo limetokana na juhudi za Serikali katika kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi kupitia doria na operesheni maalum dhidi ya uvuvi na biashara haramu ya samaki na mazao yake ikiwa pamoja na kutoa  elimu ya uvuvi endelevu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Sekta ya Uvuvi imeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo:

i.Kutokuwepo kwa Bandari ya Uvuvi na hivyo kupoteza mapato ambayo yangepatikana kutokana leseni na tozo kwa meli zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari; 

ii.Kutokuwa na meli za kutosha za kitaifa kwa ajili ya uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari;

iii.Kuendelea kuwepo kwa uvuvi na biashara haramu ya samakina mazao ya uvuvi;

iv.Upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa unaokadiriwa kufikia asilimia  40; 

v.Uhaba wa vifaranga na vyakula vya samaki vyenye ubora; 

vi.Uhaba wa Maafisa Ugani wa Uvuvi ikilinganishwa na mahitaji; na vii.Uhaba wa huduma za kifedha kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi kukua na kutumia teknolojia za kisasa.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizi Wizara imeandaa na kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo: 

i.Kukamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi; 

ii.Kukamilisha taratibu za kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO 2018) na kununua meli za uvuvi katika maji ya kitaifa,  pamoja na kutoa leseni kwa meli kubwa zinazomilikiwa na Sekta Binafsi; 

iii.Kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mkakati wa Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali za Uvuvi Nchini; 

iv.Kuendelea kuimarisha ushirikiano na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekta Binafsi katika kujenga na kuboresha masoko, mialo na kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kutengenezazana za uvuvi; 

v.Serikali pamoja na Sekta Binafsi zitaendelea kuimarisha vituo vya kuzalisha vifaranga, kuongeza upatikanaji wa samaki wazazi na kuboresha vitotoleshi na kuhamasisha kuanzisha viwanda vya kuzalisha vyakula bora vya samaki; 

vi.Kuongeza upatikanaji wa Maafisa Ugani wa Uvuvi kwa kuimarisha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi na kuhamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekta Binafsi kuajiri Wagani wa Uvuvi ili kukidhi mahitaji; na 

vii.Kuimarisha Dawati la Sekta Binafsi la Wizara ili kuwaunganisha wavuvi na Taasisi za fedha kwa ajili ya kupata mikopo yenye masharti nafuu na kuwahamasisha wavuvi kuanzisha vyama vya ushirika ili waweze kukopesheka.

MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2019/2020 

Makusanyo ya Maduhuli kwa Mwaka 2019/2020. 

Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara ilitarajia kukusanya kiasi cha Shilingi 32,301,458,000 kupitia Fungu 64. Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2020 kiasi cha Shilingi 24,484,806,549.62 sawa na asilimia 75.80 ya lengo zilikuwa zimekusanywa kutoka Sekta ya Uvuvi. Hata hivyo, makusanyo hayo ni sawa na asilimia 91 ya makusanyo yaliyolengwa kukusanywa ndani ya kipindi cha miezi kumi (10) ambayo ni shilingibilioni 26.9.  (Kiambatisho Na. 32).

Mheshimiwa Spika, fedha hizi zimekusanywa kutoka vyanzo vifuatavyo: leseni za kusafirisha samaki na mazao yake (Export Licences); leseni za uingizaji mazao ya uvuvi (Import Licences); ushuru wa mrabaha (Export Royalty); Mrabaha wa kuingiza mazao ya uvuvi nchini (Import Royalty), leseni za uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa bahari Kuu, Tozo ya Maabara; leseni za uvuvi wa kambamiti, mauzo ya vifaranga vya samaki na faini kwa makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria za uvuvi.

Makusanyoya Maduhulikwa Mwakawa Fedha 2019/2020 

Makadirio ya Ukusanyaji wa Maduhuli kwa Mwaka 2020/2021 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara kupitia Fungu 64 inatarajia kukusanya kiasi cha Shilingi 33,000,000,000. Vyanzo vikuu vya fedha hizo ni pamoja na; leseni za kusafirisha samaki na mazao yake (Export Licences); leseni za uingizaji mazao ya uvuvi (Import Licences); ushuru wa mrabaha (Export Royalty); Tozo ya Maabara; mauzo ya vifaranga vya samaki; mauzo ya mazao ya uvuvi na faini kwa makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria za uvuvi. Fedha Zilizoidhinishwa 125. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Fungu 64 ilitengewa jumla ya Shilingi 33,127,378,551.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 18,432,461,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi14,694,917,551.00ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Matumizi yaBajeti ya Kawaida. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Fungu 64 lilitengewa jumla ya Shilingi 18,432,461,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 11,557,566,693 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Wizara (PE) na Shilingi 6,874,895,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC). Hadi kufikia tarehe 15 Aprili, 2020, jumla ya Shilingi 12,668,326,728.20 zilikuwa zimetolewa, sawa na asilimia 68.72kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Shilingi 7,385,963,728.20 ni fedha za mishahara ya watumishi (PE) na shilingi 5,282,363,000.00 ni fedha za matumizi mengineyo Matumizi ya Bajeti ya Maendeleo 127. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Fungu 64 ilitengewa kiasi cha Shilingi 14,694,917,551 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwa ni fedha za ndani na nje. Kati ya fedha hizo Shilingi 3,000,000,000.00 ni fedha za ndani na Shilingi 11,694,917,551 ni fedha za nje. Hadi kufikia  tarehe 30 Aprili, 2020, jumla ya Shilingi 6,783,584,061.19 sawa na asilimia 46.16 kutoka vyanzo vya ndani na nje zilitolewa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi 426,312,537.92 ni fedha za ndani na shilingi 6,357,271,523.27ni fedha za nje.

MAENEO YA VIPAUMBELE KATIKA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2020/2021

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara kwa kushirikiana na wadau itatekeleza vipaumbele mbalimbali ili kuifikisha nchi yetu kwenye uchumi wa viwanda. Vipaumbele hivyo ni pamoja na:

i.Kuimarisha usimamizi, udhibiti na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi; 

ii.Kuongeza na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali yatokanayo na Sekta ya Uvuvi;

iii.Kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari na Bahari Kuu; 

iv.Kuimarisha usimamizi na uthibiti  wa ubora, usalama na viwango vya samaki na mazao ya uvuvi; 

v.Kuimarisha miundombinu na kukuza biashara yamazao yauvuvi; 

vi.Kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi za Uvuvina Ukuzaji Viumbe Maji; 

vii.Kuongeza upatikanaji wa vifaranga bora vya samaki; na 

viii.Kuimarisha Utafiti, Huduma za Ugani na Mafunzo ya Uvuvi.

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU KATIKA MWAKA 2019/2020 NA MPANGO WA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

Sera, Sheriana Kanuni

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara imefanya mapitio na kutunga Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali zinazosimamia Sekta ya Uvuvi ikiwemo: 

i.Kuandaa Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Uvuvi na kusimamia utekelezaji wake (Tanzania Fisheries Sector Development Master Plan). 

ii.Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 imefanyiwa mapitio na marekebisho katika kifungu cha 8, 40, na 47 ili kuwa na adhabu zinazoendana na ukubwa wa makosa; 

iii.Muswada wa “Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu – The Deep-Sea Fisheries Management and Development Act, 2020” umewasilishwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa 17 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muswada huo unategemewa kuwasilishwa kwa mara ya Pili na ya Tatu katika Mkutano wa 19 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

iv.Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 imefumuliwa na kuandaliwa Sheria mbili zilizotenganisha masuala ya uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji, na pia kuondoa kasoro zilizopo ili kukidhi mahitaji ya sasa; 

v.Sheria mpya ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu inaandaliwa ili kuongeza wigo wa maeneo ya hifadhi hadi kwenye maji baridi; 

Mheshimiwa Spika, Wizara imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wavuvi na wadau wa mazao ya uvuvi kuhusu utekelezaji wa Kanuni ya Uvuvi ya mwaka 2009, kwa kuwa Kanuni hizo zimepitwa na wakati na kwa kuwa tafiti mpya zimefanyika pamoja na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, Wizara imezifumua Kanuni za Uvuvi za mwaka 2009 na kuandaa Kanuni mpya za Uvuvi za mwaka 2020. 

Baadhi ya mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika Kanuni mpya ni kama ifuatavyo:

i.Kuruhusu matumizi ya taa za nguvu ya jua (solar) katika maeneo ya mavuvi katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Bahari ya Hindi; 

ii.Kuruhusu matumizi ya nyavu za makila za kuunganisha kufikia ukomo wa macho 78 katika Ziwa Victoria na macho 144 katika Ziwa Tanganyika uvuvi wa samaki aina ya Sangara na Migebuka;

iii.Kuruhusu matumizi ya ringnetkatika uvuvi wa dagaa Ziwa Tanganyika umbali mita 1,000 kutoka mwaloni, peninsula na kisiwa; 

iv.Kuruhusu nyavu za makila za ukubwa wa macho ya inchi 1.5 kwa ajili ya uvuvi wa samaki aina ya vitui na mantura katika Ziwa Nyasa; 

v.Kuweka na kuzingatia kipimo kisichopungua sentimita 2 kwa samaki wabichi na sentiminta 3 kwa samaki waliokaushwa kutoka katika kipimo kilichokubalika kisheria kwa samaki aina ya Sangara; 

vi.Kuruhusu misimu ya uvuvi wa samaki aina ya Kambamiti katika kipindi cha kuanzia tarehe 1 Machi hadi tarehe 30 Septemba kwa Kanda ya Kaskazini na kuanzia tarehe 1 Aprili hadi tarehe 31 Agosti ya kila mwaka kwa Kanda ya Kusini; 

vii.Kuruhusu uuzwaji wa Pweza wenye uzito kuanzia gramu 440 baada ya kuchakatwa; 

viii.Kuruhusu uvuvi wa Kambakoche aina ya Pakupaku (Sandy lobster) kuanzia gramu 250; 

ix.Kuruhusu kuvuliwa kwa samaki jamii ya Perege wenye urefu kuanzia sentimita 20 katika Ziwa Rukwa, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa, Mabwawa ya Mtera na Nyumba ya Mungu; 

x.Kuruhusu samaki wasiochakatwa (whole fish) waliotolewa matumbo kuuzwa katika masoko ya Kikanda na Kimataifa;
97
xi.Kuruhusu biashara ya mabondo chini ya urefu wa sentimita 12 au uzito wa gramu 13 kwa mabondo mabichi na urefu wa sentimita 8 au uzito wa gramu 4 kwa mabondo makavu; na 

xii.Kuweka miongozo ya usimamizi wa uvuvi katika maji madogo kwenye maziwa ya Eyasi, Manyara, Kitangiri, Rukwa, Singidani, Basuto, Burigi na bwawa la Bahi na mto Kilombero.
Mheshimiwa Spika, Wizara imesikia kilio cha wavuvi na kufanya maboresho ya ada mbalimbali za leseni. Mabadiliko haya yataonekana katika muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2020/2021.

Uboreshaji wa ada za leseni na tozo za uvuvi unalenga kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Uvuvi na kukuza biashara ya samaki na mazao yake.

Mheshimiwa Spika, Wizara ipo katika hatua za mwisho kutangaza Kanuni za kutekeleza Ajenda ya Taifa ya Utafiti wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji ili kuongeza matumizi ya tafiti katika Sekta ya Uvuvi. Aidha, Wizara imeandaa na kufanya maboresho ya Kanuni za Tozo ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu ambazo zinatarajiwa kuanza kutumika katika mwaka wa fedha 2020/2021. 133. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itakamilisha mapitio ya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 na kuandaa Muswada wa Sheria mpya ya Uendelezaji Ukuzaji Viumbe Maji na Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu. 

Aidha, itasimamia utekelezaji wa maboresho ya kanuni na tozo mbalimbali yaliyofanyika.  Vilevile, Wizara itakamilisha kuandaa Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Uvuvi na kusimamia utekelezaji wake (Tanzania Fisheries Sector Development Master Plan).

MWENENDO WA UVUNAJI WA RASILIMALI ZA UVUVI 

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia uvunaji na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi nchini. Katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2019 hadi mwezi Machi 2020 jumla ya tani 392,933.0 za samaki wenye thamani ya shilingi trilioni 1.85 walivunwa ikilinganishwa na tani 389,459.40 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.83 zilizovunwa katika kipindi kama hiki mwaka 2018/2019 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia0.89. Ongezeko hilo limechangiwa na kuimarika kwa usimamizi wa Sekta ya Uvuvi uliopelekea kuongezeka kwa wingi wa samaki katika maji asili, hususan katika Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kusimamia biashara ya samaki na mazao ya uvuvi nje ya nchi kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa. Hadi kufikia mwezi Machi 2020, tani 32,388.88 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 102,458 wenye thamani ya shilingi bilioni 436.96 waliuzwa nje ya nchi na kuiingizia Serikali mrabaha wa shilingi bilioni 19.1 (Kiambatisho Na. 33) ikilinganishwa na tani 38,114.72 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 46,098 wenye thamani ya shilingi bilioni 491.15 waliouzwa nje ya nchi na kuliingizia Taifa mrabaha wa shilingi bilioni 15.63 katika mwaka 2018/2019 kwa kipindi kama hicho. Hata hivyo, mauzo ya mazao ya uvuvi nje ya nchi yalifikia shilingibilioni 691kuishia Juni, 2019

Mheshimiwa Spika, sehemu kubwa ya mazao ya uvuvi yanayosafirishwa nje ya nchi ni kutoka Ziwa Victoria ambayo yamechangia tani 30,012.91 sawa na  asilimia 92.66 ya mauzo yote. Mazao ya samaki aina ya Sangara yalikuwa tani 22,714.87 sawa na asilimia 70.13 ya mauzo yote yaliyosafirishwa nje ya nchi katika Mwaka 2019/2020 (Kiambatisho Na. 34a na 34b). Mazao mengine kutoka Ziwa Victoria yanajumuisha Dagaa na Furu. Aidha, mauzo ya mabondo yalipungua kwa asilimia 35.6 ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2020 mauzo ya mabondo nje ya nchi yalikuwa tani 569.43 zenye thamani ya shilingi bilioni 130.05 na kuingiza mrabaha wa shilingi bilioni 3.93 ikilinganishwa na tani 884.30 zenye thamani ya shilingi bilioni 178.31 zilizoingiza mrabaha wa shilingi bilioni 2.87 mwaka 2018/2019 katika kipindi husika.

Mheshimiwa Spika, kushuka kwa kiasi cha mauzo ya  mazao ya uvuvi nje ya nchi yakiwemo mabondo kumetokana na kuyumba kwa soko la bidhaa hizo kunakosababishwa na sababu mbalimbali zikiwemo ushindani katika soko na kwa sehemu kubwa mlipuko wa ugonjwa wa Corona. Aidha, kutokana na kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Corona (COVID – 19)mashirika mengi ya ndege kama vile Kenya Airways, Emirates, Qatar Airways na Ethiopia Airways yaliyokuwa yakisafirisha bidhaa hizo yamesitisha safari zake. Vilevile, ndege za mizigo zimeweka masharti ya kuwepo kwa mzigo usiopungua tani nane (8) kutoka kiwanja cha ndege Mwanza na mzigo usiopungua tani 26 kutoka uwanja wa Julius Nyerere International Airport. Hali hiyo imesababisha kuchelewa kwa usafirishaji wa mizigo kutoka katika viwanja vya ndege hivyo. Pia, gharama ya usafirishaji wa bidhaa hizo imepanda kutoka dola za kimarekani2.5hadi kufikia3.8kwa kilo.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2020, jumla ya tani 8.18 za samaki wenye thamani ya shilingi milioni 161.01 wameingizwa nchini ikilinganishwa na tani 7,760.12 zenye thamani ya shilingi bilioni 15.31 zilizoingizwa nchini katika kipindi kama hiki mwaka 2018/2019 (Kiambatisho Na. 36). Uingizaji wa samaki kutoka nje umepungua kwa asilimia 99.9 kutokana na kuimarika kwa uzalishaji na upatikanaji wa samaki katika soko la ndani.

USIMAMIZI NA UDHIBITI WA RASILIMALI ZA UVUVI NA MAPAMBANO DHIDI YA UVUVI HARAMU

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kuimarisha Kanda Kuu tatu (3) na Vituo 30 vya Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali za Uvuvi nchini kwa kuvipatia vitendea kazi na watumishi  ili kupambana na uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi. Aidha, Wizara imeanzisha vituo vipya vinne (4) vya Bwawa la Nyumba ya Mungu, Bwawa la Mtera, Ziwa Rukwa na Rorya ili kupanua wigo wa kupambana na uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi.

Mheshimiwa Spika, Usimamizi na udhibiti wa rasilimali za uvuvi nchini ni jukumu la kila mtanzania kwa kuzingatia Katiba ya Nchi kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 26 na 27 na kwa mujibu wa sheria zingine za nchi. Pia, jukumu hili limeainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 20152020. 

Lengo la usimamizi na udhibiti ni kuhakikisha kuwa rasilimali za uvuvi zinakuwa endelevu kwa ajili ya kizazi kilichopo na vizazi vijavyo. 

eshimiwa Spika, kabla ya awamu ya tano kuanza uvuvi haramu katika maji yetu ulikuwa umekithiri kwa kiwango cha kutishia uwepo wa rasilimali za uvuvi. Mnamo mwezi Desemba, 2017 Wizara yangu ilifanya tathmini ya kina kuhusu Utendaji wa Sekta ya Uvuvi na kiwango cha Uvuvi haramu katika maeneo ya mavuvi na kubaini mambo yafuatayo: 

i.Kukithiri kwa uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi katika Ziwa Victoria ambalo huchangia asilimia 64 ya mavuno ya samaki nchini. Aidha, tathmini hiyo ilibaini kuwa asilimia 96.6 ya samaki aina ya Sangara waliokuwa wanavuliwa walikuwa wachanga chini ya urefu wa sm 50. Vilevile, samaki aina ya Sangara waliokuwa wanavuliwa ambao wanakidhi viwango kisheria walikuwa wamebaki asilimia 3 tu na samaki wazazi walikuwa wamebakia asilimia0.4tu; 

ii.Kuongezeka kwa matumizi ya zana haramu, hususan makokoro toka 1,665 mwaka 2006 hadi kufikia makokoro 3,216 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 93; nyavu za timba ziliongezeka toka 4,801 mwaka 2006 hadi 19,382 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia300;

iii.Kukithiri kwa matumizi ya milipuko katika uvuvi ukanda wa bahari na uvuvi holela katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ) na utoroshaji wa mazao ya bahari kwenda nje ya nchi; 

iv.Upotevu wa mapato yatokanayo na Biashara ya mazao ya uvuvi nje ya nchi, mfano lango la Tunduma pekee tani 7,000 zilipitishwa kuelekea katika nchi jirani za Zambia na Malawi lakini ni tani3,000tu ndizo zilizolipiwa ushuru na kwa upande wa mpaka wa Kagera tathmini ilionesha kuwa takriban tani 100 zinatoroshwa kila wiki kuelekea katika nchi ya Uganda; 

v.Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU's) kutowajibika ipasavyo; na 

vi.Ushirikiano hafifu kati ya BMUs, Serikali za Vijiji, Kata na Halmashauri Ngazi ya Wilaya. 142. 

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Wizara yangu iliamua kuendesha doria na operesheni dhidi ya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Mabwawa ya Nyumba ya Mungu na Mtera na Bahari ya Hindi.  Operesheni hizo zimedumu kwa kipindi chote cha miaka mitatu (2017/2018 hadi 2019/2020). Operesheni hizo ni pamoja na: 

i.Operesheni Sangara 2018 iliyofanyika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Mabwawa ya Nyumba ya Mungu na Mtera; 

ii.Operesheni MATT iliyofanyika katika Mwambao wa Bahari ya Hindi; na 

iii.Operesheni Jodari iliyofanyika katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ) 143. Mheshimiwa Spika, matokeo ya mapambano dhidi ya uhalifu huo kwa kipindi cha miaka mitatu (2017/2018, 2018/2019 na 2019/2020 ) ni pamoja na kukamatwa nyavu haramu za makila 1,162,555; makokoro 17,924; nyavu za timba 69,437; nyavu za dagaa 13,224; kamba za kokoro zenye urefu wa mita 1,893,097; ndoano 4,652,697; nyavu za ringnet 1,375; nyavu za tembea 6,953; samaki wachanga kilo 423,882; Kaa hai wachanga kilo 5,676; mabomu vipande 4,583; detonator 2,534; mbolea ya urea kilo 626; na watuhumiwa 14,384. Aidha, vifaa vingine vilivyokamatwa ni pamoja na injini za boti 2,404; magari 7,240; pikipiki 704; mitungi ya gesi 624 (Kiambatisho Na. 37). 

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi hicho chote cha miaka mitatu mfululizo (2017/2018 hadi  mwezi Machi, 2020), Wizara imefanikiwa kudhibiti uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi kwa asilimia zaidi ya 80 katika maji baridi na asilimia 100 kwa uvuvi wa kutumia mabomu kwa ukanda wa pwani ya bahari yetu. 

Mheshimiwa Spika, kufuatia operesheni JODARI iliyofanyika mwezi Januari hadi Februari, 2018 kwa kushirikisha Kikosi kazi cha Taifa cha Kuzuia na Kupambana na Uharibifu wa Mazingira (National Multi-Agency Task Team NMATT), meli ya Buah Naga 1 ilikamatwa ikiwa na mapezi ya papa bila miili ambapo Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara iliwahukumu mmiliki, nahodha na wakala kifungo cha miaka 20 au kulipa faini ya shilingi bilioni 1. Watuhumiwa hao walishindwa kulipa faini hiyo na wanatumikia kifungo. Aidha, meli ishirini (20) zenye kupeperusha bendera ya China zilikimbia bila kuhakikiwa mavuno (catch verification) na kushusha samaki wasiolengwa (by-catch) kabla ya kuondoka katika maji ya Tanzania kinyume na Kanuni za Uvuvi wa Bahari Kuu ya 10(1)(a) na 10(1)(c) ya Mwaka 2009 na marekebisho yake ya Mwaka 2016. 146.

Mheshimiwa Spika, hatua mbalimbali zimefanyika kuhakikisha kuwa wamiliki wa meli hizo wanalipa faini, ikiwa ni pamoja na kuwaandikia barua wakala na wamiliki wa meli  hizo kuwataka kukubali makosa na kulipa faini kwa mujibu wa sheria za Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, kuwasilisha shauri hili katika Kamisheni ya Jodari ya Bahari ya Hindi (IOTC), na kufanya mazungumzo kati ya Ujumbe wa Tanzania na China kwenye IOTC mjini Hyderabad, India mwezi Juni 2019. 

Katika mazungumzo hayo ilikubalika kuwa kila upande ufanyie kazi makubaliano yaliyofikiwa kwa kuzishirikisha Serikali kwa hatua zaidi. Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu tayari imefanya mawasiliano na Kiongozi wa Ujumbe wa China - IOTC ili kujua msimamo wa serikali ya China wa kuwataka wamiliki wa meli hizo kulipa faini ili ya jumla ya shilingi bilioni 20 ili kulimaliza suala hilo kabla ya Mkutano wa IOTC unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba,2020. 

Mheshimiwa Spika, mapambano hayo yameleta mafanikio makubwa katika Sekta ya uvuvi na Taifa kwa ujumla. Mafanikio yaliyopatikana ni kama ifuatavyo:

i.Kuimarika kwa usimamizi na udhibiti wa rasilimali za uvuvi nchini, uvunaji wa rasilimali za uvuvi na hivyo kusababisha samaki kuongezeka kutoka tani 387,543 waliovuliwa mwaka 2017/2018 na kufikia tani 448,467mwaka 2019/2020. 

ii.Kuongezeka kwa wingi wa samaki aina ya Sangara kutoka tani 417,936 mwaka 2016 hadi kufikia tani553,770mwaka 2018 na tani816,964 mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la asilimia47.5. Aidha, dagaa waliongezeka kutoka tani 660,333 mwaka 2018 kwa ziwa lote hadi kufikia tani 936,247 mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 41.8 na kwa upande wa Tanzania dagaa waliongezeka kutoka tani 340,422 mwaka 2018 hadi tani512,840mwaka 2019. 

iii.Kupungua kwa samaki wachanga aina ya Sangara wenye urefu wa chini ya sentimita 50 kutoka asilimia 96.6 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia62.8mwaka 2018; 

iv.Kuongezeka kwa samaki aina ya Sangara wenye urefu wa kuanzia sentimita 50 hadi 85 kutoka asilimia 3.3 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia32.0mwaka 2018; 

v.Kuongezeka kwa samaki aina ya Sangara wenye urefu wa juu ya sentimenta 85 kutoka asilimia 0.4 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 5.2mwaka 2018; 

vi.Kuongezeka kwa wastani wa urefu wa Sangara kutoka sentimeta 16 mwaka 2017 hadi kufikia sentimeta 25.2mwaka 2018; na 

vii.Kupungua kwa uingizaji wa samaki kutoka nje ya nchi kutoka thamani ya shilingi bilioni 56 mwaka 2016/2017 hadi shilingi milioni 161.01 Machi, 2020 sawa na upungufu wa asilimia 99.7. Hivyo, kusaidia kupunguza matumizi ya fedha za nje katika mwaka 2019/2020; 

viii.Kuongezeka kwa upatikanaji wa samaki uliosababisha kushuka kwa bei ya mazao ya uvuvi katika soko la ndani toka wastani wa shilingi 9,000 kwa kilo ya samaki aina ya Sangara mwaka 2017/2018 hadi shilingi 4,500 mwaka 2019/2020. Vilevile, bei ya samaki aina ya Sato imeshuka kutoka wastani wa shilingi 9,500 mwaka  hadi shilingi 7,500 mwaka 2019/2020. 

Mheshimiwa Spika, Aidha, kuimarika kwa uzalishaji wa mazao ya uvuvi, kumewahamasisha wadau wa sekta kuanzisha viwanda vya kuchakata samaki hapa nchini, katika ukanda wa Ziwa Victoria ambako kuna viwanda tisa (9) vinavyofanya kazi, viwanda vipya vinne (4) viko kwenye hatua ya ujenzi, kuongezeka kwa maghala ya ugandishaji/kuhifadhia (Cold rooms) samaki na mazao ya uvuvi kutoka nane (8) mwaka 2017/2018 hadi 90 mwaka 2019/2020. Maghala hayo kwa sasa yanauwezo wa kuhifadhi wastani wa tani350kwa siku. 

Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuimarika kwa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2019 jumla ya Shilingi Bilioni 33.796 zimekusanywa sawa na asilimia 156.94 ya lengo la kukusanya Shilingi bilioni 21.534. Vilevile, mauzo ya samaki nje ya nchi yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 379 kwa miaka miwili iliyopita na kufikia shilingi bilioni 691.88 katika mwaka wa fedha 2018/2019 kiasi ambacho hakijafikiwa katika kipindi chochote kile. 

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020 pekee, Wizara imeendeshaoperesheni maalum na doria zenye sikukazi 7,472 kwenye maji, nchi kavu na maeneo ya mipakani ambapo zana haramu mbalimbali zilikamatwa zikiwemo; nyavu za makila 166,177, makokoro 808, nyavu za timba 31,671, nyavu za dagaa 547, kamba za kokoro zenye urefu wa mita 149,071, ndoano 12,000, mitumbwi 736, boti 56, nyavu za ring net 204, vyandarua 22, katuli 10, injini za boti 275 na kasia 8. Pia, magari 8, pikipiki 36, baiskeli 6, samaki wachanga kilo 28,450, kaa hai wachanga kilo 30, kambakoche hai wachanga kilo 46, simbi kilo 22,000, pamoja na watuhumiwa 2,040 walikamatwa na kufunguliwa kesi mahakamani na wengine kutozwa faini. 

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kudhibiti Uhalifu wa Mazingira (National Mult-Agency Task Team NMATT) imeendesha operesheni nne (4) ambapo (3) zilifanyika katika Ukanda wa Pwani na (1) katika Ukanda wa Ziwa Victoria. Aidha, jumla ya raia wa kigeni 25 walikamatwa katika Ukanda wa Ziwa Victoria. Pia, zana haramu mbalimbali zikiwemo; makokoro 105, nyavu za makila 8,445, nyavu za timba 201, kamba za kokoro zenye urefu wa mita 20,705, nyavu za ring net 55, mitumbwi 30, magari 5, mitungi ya gesi20na watuhumiwa101walikamatwa. 

Mheshimiwa Spika, nyavu haramu zilizokamatwa wakati wa doria na operesheni hizo ziliteketezwa kwa idhini ya Mahakama. Samaki wachanga waliokamatwa waligawiwa katika Taasisi za umma zikiwemo shule za Sekondari na kwenye vituo vya kulelea watoto na watu wenye mahitaji maalum (Kiambatisho Na. 38). Pia, vifaa mbalimbali vilivyokamatwa vikiwemo magari manne (4), baiskeli sita (6), pikipiki (36), injini (275), maboti (56) na mitumbwi (680) vilikabidhiwa kwa wahusika baada ya kukidhi matakwa ya kisheria. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, utafiti wa kuangalia wingi na mtawanyiko wa samaki kwa kutumia njia ya mwangwi  (Acoustic Survey) katika Ziwa Victoria ulifanyika, ambapo matokeo yanaonyesha kuwa samaki aina ya dagaa waliongezeka kutoka tani 660,333 mwaka 2018 kwa ziwa lote hadi kufikia tani 936,247 mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 41.8 na kwa upande wa Tanzania dagaa waliongezeka kutoka tani 340,422 mwaka 2018 hadi tani 512,840 mwaka 2019. Aidha, samaki aina ya Sangara wameongezeka kutoka tani 553,770 mwaka 2018 hadi tani 816,694 kwa ziwa lote, mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 47.5. Kwa upande wa Tanzania, Sangara waliongezeka kutoka  tani 301,460 mwaka 2018 hadi  tani 422,076 mwaka 2019. Kuongezeka kwa wingi wa Sangara kunatokana na juhudi za Serikali katika kupiga vita uvuvi haramu. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara kwa kushirikiana na wadau, itaendelea kuimarisha shughuli za usimamizi na ulinzi wa rasilimali za uvuvi kwa kufanya doria za kawaida zenye siku kazi 7,800. Aidha, Wizara itafanya Operesheni Maalum kila robo mwaka na kuiwezesha NMATT kutekeleza majukumu yake kwa kufanya operesheni maalum 10. Vilevile, Wizara itaimarisha vituo tisa (9) katika Ukanda wa Ziwa Victoria; Bahari ya Hindi na Mashariki; na Nyanda za Juu Kusini. Pia, itaendelea kufanya kaguzi kwenye maeneo ya bandari, mipakani, vizuizi, masoko na mialo ya kupokelea samaki.

HIFADHI ZA BAHARI NA MAENEO TENGEFU

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) iliendelea kulinda na kusimamia maeneo yaliyohifadhiwa katika Bahari ya Hindi ambayo ni Hifadhi za Bahari tatu (3) na Maeneo Tengefu (15) kwa kufanya jumla ya doria zenye sikukazi 797 hadi kufikia Machi, 2020 ikilinganishwa na doria zenye sikukazi 677 kwa kipindi kama hicho Machi 2019. 

Matokeo ya doria hizo ni kukamatwa kwa kilo 83 za makome, vipande 108 vya nyavu haramu, michinji 2 na fito 10 za mikoko iliyovunwa kinyume na sheria. 156. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia MPRU iliendelea kutoa gawio la maduhuli kwa Halmashauri na Vijiji vilivyomo ndani ya maeneo ya Hifadhi ambazo maduhuli hukusanywa. Katika mwaka 2019/2020, jumla ya shilingi 232,968,726 zilitengwa na kutolewa kwa ajili ya kugharamia shughuli za uhifadhi na miradi ya maendeleo katika vijiji vilivyomo ndani ya Hifadhi ya Kisiwa cha Mafia. 

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi, 2020 jumla ya wageni 30,412 walitembelea maeneo ya Hifadhi za Bahari ikilinganishwa na wageni 46,304 kwa mwaka 2018/2019. Kupungua kwa idadi ya watalii katika maeneo ya hifadhi kumetokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID – 19)ambao umesababisha kusitishwa kwa safari za ndege za kimataifa na hivyo kuzuia kuja kwa watalii kutoka nje ya nchi. 158. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara kupitia MPRU itaendelea kulinda, kutunza na kusimamia mifumo ikolojia katika maeneo yaliyohifadhiwa kwa kufanya doria za sikukazi 800. Aidha, MPRU itaendelea kutekeleza Mkakati wa Kujitangaza na Kuongeza Mapato kwa kutangaza maeneo yaliyohifadhiwa ikiwa pamoja na vivutio vya utalii vilivyomo. Vilevile, MPRU itaboresha miundombinu katika maeneo ya utalii wa kiikolojia (eco tourism) ili kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi na hivyo kuongeza mapato.

UVUVI KATIKA BAHARI KUU 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli kutokana na uvuvi wa Bahari Kuu zilifanyika ikiwa ni pamoja na Serikali kuondoa tozo ya Dola za Kimarekani 0.4 kwa kilo ya samaki wanaolengwa kutoka Bahari Kuu kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Novemba 2019 hadi Novemba 2020 kama ilivyoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 883 la mwaka 2019. 

Baada ya Serikali kuondoa tozo hiyo mashirika ya meli kutoka nchi za Ufaransa, Uhispania na Ushelisheli zilileta maombi ya leseni za uvuvi ili kufanya uvuvi katika Bahari Kuu. Hata hivyo, baada ya kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 mashirika hayo yametoa taarifa za kusitisha nia hiyo. Aidha, Mamlaka imefanikiwa kutoa leseni za uvuvi wa Bahari Kuu kwa meli (2) zenye bendera ya Tanzania (AL-MAIDA na SEHEWA 02) na kuiingizia Mamlaka kiasi cha Shilingi 31,920,817 zilizotokana na ada ya leseni. Vilevile, doria za anga zenye jumla ya masaa 72 zilifanyika na kuonesha kuwa hakukuwa na meli zenye kuvua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ) nchinikinyume cha Sheria. 160. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Mamlaka inafanya tafiti tatu za Analysis of Tuna and Tuna like species, Stock Structure and Genetic connectivity na Study on Oceanographic Factors influencing spatial distribution of Tuna and Tuna like species in Tanzania waters katika EEZ zenye lengo la kutoa uelewa juu ya rasilimali inayopatikana na kuwezesha usimamizi endelevu. Vilevile, Mamlaka kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inafanya tafiti za kutambua maeneo yenye samaki wengi katika EEZ na maji ya Kitaifa nchini katika pwani ya Tanga, Wete, Nungwi, Mkinga, Pangani, Bagamoyo, Kinondoni, Mkuranga, Rufiji, Kibiti, Kilwa, Lindi, na Mtwara. 161. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020,

Mamlaka imeendelea kuboresha Mfumo wa Takwimu za Uvuvi kwa kuongeza moduli tatu (3) za Ukaguzi wa Meli, Doria za majini, Dashboard na kuunganishwa na Mfumo wa kufuatilia mienendo ya meli (Vessel Monitoring System VMS). Vilevile, Mamlaka imekamilisha mfumo wa malipo kwa njia za kielektroniki ambapo waombaji wa leseni za uvuvi watafanya malipo kwa njia ya mtandao (online), malipo kwa njia ya QR Code na kwa njia ya kuhamisha kutoka Benki yoyote duniani. Kwa kutumia mfumo huu mapato yote yataonekana katika mfumo Mkuu wa Serikali wa kukusanya mapato (GePG) hivyo kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka  2020/2021, Mamlaka itafanya tafiti nyingine tatu zenye lengo la kutoa uelewa juu ya rasilimali inayopatikana na kuwezesha usimamizi endelevu katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari. Tafiti hizo ni: Tuna Biology, Economic profile na Pole and line fishery. Vilevile, Mamlaka kwa kushirikiana na TAFIRI itaendelea kufanya tafiti za kutambua maeneo yenye samaki wengi katika EEZ na maji ya Kitaifa (Potential Fishing Zones).

Mheshimiwa Spika, Mamlaka itaendelea kusimamia  ulinzi wa rasilimali za uvuvi Bahari Kuu kwa kuendesha doria za anga na majini na kuboresha Mfumo VMS. Aidha, Mamlaka itaandaa Mkakati wa kuongeza uwekezaji kwa kutoa vivutio mbalimbali kwa wawekezaji wazawa ikiwa pamoja na kuwaunganisha na masoko ya nje kwa ajili ya kuuza bidhaa zao. Vilevile, Mamlaka itandaa Mpango Biashara (Business Plan) utakaosaidia kuongeza mapato na kuiwezesha Mamlaka kuweza kujiendesha. SHIRIKA LA UVUVI TANZANIA–TAFICO 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Serikali inaendelea na Mkakati wa kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (Tanzania Fisheries Corporation-TAFICO) ili kuiwezesha Nchi kunufaika na rasilimali za uvuvi, hususan zile zilizopo katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari na Bahari Kuu. Pamoja na mambo mengine Wizara imeendelea kuweka mipaka na alama zinazoonekana na kufanya ukarabati wa mali zilizofanyiwa tathmini yenye thamani ya shilingi bilioni 118. 

Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mpango Biashara wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO Business Plan). Lengo la Mpango huu ni kutoa mwelekeo wa kibiashara wa Shirika kwa kipindi cha miaka 10 ambapo utafanyika kupitia Serikali na Sekta Binafsi kwa njia ya ubia. Mpango huu umeainisha miradi mikubwa mitatu kama ifuatavyo: 

i.Mradi wa uvuvi utakaojumuisha Meli ya Uvuvi wa Mishipi (Longliner), Meli ya Uvuvi Wavu wa Kuzungusha (Purse Seiner), na Meli ya Uvuvi wa Maji ya Ndani (Territorial Waters Fishing Vessel); 

ii.Mradi wa Kuchakata samaki utakaojumuisha Kiwanda cha Kuchakata samaki (Fish Processing Plant), Kiwanda cha Kuzalisha Barafu (Ice Making Plant) na Ghala la Ubaridi la Kuhifadhia Samaki (Cold Storage Facility); na 

iii.Mradi wa Ukuzaji Viumbe Maji (Aquaculture) utakaojumuisha Ufugaji Samaki kwenye Vizimba (Cage Fish Farming) katika Ziwa Victoria na Bahari ya Hindi, Ufugaji Samaki kwenye Mabwawa (Pond Fish Farming), Vitotoleshi vya Kuzalishia Vifaranga vya Samaki (Fish Hatchery) na Kiwanda cha Vyakula vya Samaki (Fish Feed Plant). 

Mheshimiwa Spika, Miradi hiyo mitatu (3) itatekelezwa kupitia miradi midogo kumi yenye thamani ya jumla ya Shilingi 89,282,057,278.00. Miradi hiyo inatarajiwa kuanza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka 2020/2021 (Kiambatisho Na. 40). 

Mheshimiwa Spika, katika mikakati ya kuiwezesha TAFICO, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Uchumi na Jamii - Japan (The Economic and Social Development Programme) imepata msaada wa shilingi bilioni 4.2 kwa ajili kutekeleza miradi mbalimbali ambapo tayari hatua za ununuzi zimeanza kama ifuatavyo: 

i.Ujenzi wa meli yenye urefu wa mita 20 itakayovua katika maji ya kitaifa; 

ii.Usimikaji wa mtambo wa kuzalisha barafu; 

iii.Ujenzi wa ghala la baridi la kuhifadhia samaki (Cold room); 

iv.Ukarabati wa karakana ya uhandisi; na 

v.Ununuzi wa gari maalum la kusambazia samaki na barafu (Refrigerated Truck). 

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na Mazungumzo na Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo Duniani (IFAD) ili kuweza kupata kiasi cha Shilingi Bilioni 68.8 kwa ajili ya kununua meli mbili (2) za longlinner na purse seiner zitakazogharimu kiasi cha shilingi bilioni 55.9 ili kuliwezesha Shirika la TAFICO kuvua katika Bahari Kuu. Aidha, shilingi Bilioni 12.9 zitatumika kuwezesha mradi wa ufugaji viumbe maji. Vilevile, katika vikao vilivyofanyika tarehe 24 Februari hadi 7 Machi 2020 kati ya wajumbe kutoka IFAD na Serikali waliweka ratiba ya utekelezaji na kukubaliana kuanza utekelezaji wa mradi huo mwezi Januari, 2021 (Kiambatisho Na. 41). 

169. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Serikali itanunua Meli tatu (3) za Uvuvi na kuanza uvuvi wa Bahari Kuu na maeneo mengine; kujenga na kuendesha viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi; kuendelea na ukarabati wa majengo na miundombinu ya TAFICO itakayojumuisha gati la kuegeshea Meli za Uvuvi, kusimika mitambo ya barafu, maghala ya baridi pamoja na kuiwezesha TAFICO kuanza miradi ya  ukuzaji viumbe maji. 

UJENZI WA BANDARI YA UVUVI 

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kupitia Mtaalam Mwelekezi ambaye ni Kampuni ya M/S Sering Ingegneria ya Nchini Italia kwa gharama ya shilingi 1,421,041,703.08. Hadi sasa Mtaalam Mwelekezi amewasilisha Ripoti (Interim Report) ya kina ya ukusanyaji wa taarifa muhimu za maeneo yanayofaa kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi. Katika hatua ya ukusanyaji wa taarifa muhimu jumla ya maeneo kumi na moja (11) ya Mbegani-Bagamoyo, Ras Buyuni, Shangani-Mtwara, Bandari ya Lindi, Rushungi, Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje, MoaTanga, Bandari ya Tanga, Mwambani-Tanga na Pangani yalifanyiwa tathmini kwa kuzingatia vigezo vya kimazingira/ikolojia. 

Mheshimiwa Spika, Baadhi ya vigezo hivyo ni uwepo wa miundombinu wezeshi kama vile barabara, upatikanaji wa eneo la kutosha, eneo kutokuwa kwenye hatari za athari za kimazingira (exposure to extreme conditions); matumizi ya ardhi kwenye eneo husika (Land use); na hali ya ikolojia ya pwani (coastal ecology). 

Aidha, vigezo vingine vilivyozingatiwa ni pamoja na ukaribu wa eneo kwenye kina kirefu cha maji; hitaji la kuwa na kinga maji (breakwater), kiasi cha mtaji na gharama za matengenezo; na hitaji la kuchimba ili kuongeza kina cha maji (dredging). Kwa kuzingatia vigezo hivyo, maeneo matatu (3) ya Mbegani Bagamoyo, Kilwa Masoko na Bandari ya Lindi yamependekezwa. Kutokana na kazi hiyo Serikali imemlipa Mtaalam Mwelekezi asilimia 50 sawa na shilingi 710,520,896.54 kulingana na Mkataba uliosainiwa. 

Mheshimiwa Spika, ili kuendelea na hatua inayofuata, Serikali inakamilisha taratibu za kuchagua eneo moja kati ya matatu yaliyopendekezwa. Aidha, baada ya Serikali kufanya uamuzi wa eneo linalofaa kujenga Bandari ya Uvuvi Mtaalam Mwelekezi atafanya upembuzi wa kina (bathymetric, topographic and geotechnical survey) na kisha kuandaa michoro, kuainisha gharama za ujenzi na kuwasilisha taarifa ya mwisho (Final Report). Baada ya kuwasilisha taarifa ya mwisho Mtaalam Mwelekezi atalipwa sehemu ya mwisho ya malipo ya asilimia 50 sawa na shilingi 710,520,896.54 kulingana na mkataba uliosainiwa. 

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuwezesha ujenzi wa bandari ya uvuvi, mazungumzo yanaendelea baina ya Serikali ya Tanzania na Korea ya Kusini kwa ajili ya kupata ufadhili wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi katika eneo litakalopendekezwa. Aidha, Randama ya Makubaliano (MoU) kati ya nchi hizi mbili umeandaliwa na taratibu za kuusaini zinaendelea. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Serikali itakamilisha upembuzi wa kina na kuanza ujenzi wa Bandari ya Uvuvi katika eneo litakalochaguliwa. Aidha, uwepo wa Bandari ya Uvuvi utawezesha meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari Kuu kutia nanga, kushusha mazao ya uvuvi na kupata huduma mbalimbali zikiwemo mafuta na chakula. Aidha, kuwepo kwa Bandari ya Uvuvi kutawezesha ukuaji wa biashara ya mazao ya uvuvi, kuongeza ajira, kuchochea uwekezaji na ujenzi wa viwanda, kuongeza fedha za kigeni, kuongeza mchango wa Sekta ya Uvuvi katika Pato la Taifa na hivyo kuiwezesha nchi kunufaika kikamilifu na rasilimali za uvuvi.

UKUZAJI VIUMBE MAJI 175. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara imeendelea kuimarisha vituo vinne (4) vya Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji vya Kingolwira - Morogoro, Mwamapuli – Tabora, Ruhila – Ruvuma na Nyengedi – Lindi ili kuongeza uzalishaji wa samaki kwa kufanya yafuatayo: 

i.Kununua samaki wazazi 27,640 na kuwagawanya katika vituo; 

ii.Kusimika happa net 60 kwa ajili ya kutunzia samaki wazazi; na 

iii.Kununua matanki 22 kwa ajili ya kulelea vifaranga na kukarabati mabwawa nane (8). 

Mheshimiwa Spika, maboresho hayo yamesababisha kuongezeka kwa uzalishaji vifaranga kufikia 4,146,840 kutoka vifaranga 478,300 vilivyozalishwa kutoka katika vituo vya wizara, Taasisi zilizo chini ya Wizara na Taasisi zingine za Serikali katika mwaka 2018/2019. Aidha,  vifaranga 1,500 vimepandikizwa katika bwawa linalomilikiwa na wananchi katika Wilaya ya Msalala ili kuongeza upatikanaji wa samaki katika maeneo hayo. 

Mheshimiwa Spika, Wizara imefanya kaguzi mbili (2) zenye sikukazi 88 katika vitotoleshi, mashamba ya ufugaji wa samaki na viwanda vya kutengeneza vyakula vya samaki katika mikoa 11 nchini. Aidha, kaguzi nyingine mbili (2) zenye sikukazi10 zimefanyika katika shamba la ufugaji wa kambamiti la Alphakrust Limited lililopo Mafia.  Kaguzi hizo zilionesha kuwa  wadau wa ukuzaji viumbe maji walio wengi wanafuata sheria na kanuni zilizopo. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeandaa miongozo saba (7) kuhusu: Uzalishaji Vifaranga vya Samaki; Uzalishaji Vyakula vya Samaki na Ulishaji; Ufugaji Samaki kwenye Vizimba; Ukulima wa Mwani; Ufugaji Samaki kwenye Mabwawa; Ufugaji wa Kaa na Udhibiti wa Magonjwa ya Samaki. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kuhamasisha jamii kuwekeza katika ukuzaji viumbe maji kwa kutoa elimu. Jumla ya wadau 7,072 walipata elimu ya mbinu bora za ufugaji wa samaki na kilimo cha  mwani kupitia maonesho ya Nane Nane (2,876), Siku ya Chakula Duniani (231) na katika vituo vya Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji (3,965) ikilinganishwa na wadau 6,695 waliopatiwa elimu kwa mwaka 2018/2019. Aidha, Wizara imeandaa na kusambaza vipeperushi 7,300 kuhusu kanuni bora za ukuzaji viumbe maji. 

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji. Katika mwaka 2019/2020, kumekuwa na ongezeko la vizimba 23 vya kufugia samaki na kufanya idadi ya vizimba kufikia 431 ikilinganishwa na vizimba 408 vilivyokuwepo mwaka 2018/2019. Mtawanyiko wa vizimba hivyo ni: Ziwa Victoria (370), Ziwa Tanganyika (9) na katika malambo mbalimbalinchini (52). 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itakarabati na kujenga vituo sita (6) vya kuzalisha vifaranga vya samaki na kuendeleza ukuzaji viumbe maji katika maeneo ya Mwamapuli-Tabora, Ruhila-Ruvuma, Kingolwira-Morogoro, Nyengedi-Lindi, MachuiTanga, na Rubambagwe-Geita. Aidha, vituo hivi vitazalisha vifaranga milioni 8 na tani 60 za samaki na pia vitakuwa mashamba darasa kwa ajili ya kutoa elimu ya ufugaji bora  wa samaki. Vilevile, vitotoleshi vya sekta binafsi vitahamasishwa kuzalisha vifaranga milioni 22 na hivyo kufikia jumla ya vifaranga milioni 30 kwa mwaka kutoka wastani wa uzalishaji wa sasa ambao ni vifaranga milioni22kwa mwaka. 

Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kusimamia na kuendeleza matumizi ya teknolojia mpya za kuongeza thamani katika mazao ya viumbe maji bahari hususani mwani kwa mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Tanga pamoja na kuanzisha kituo kimoja (1) cha Ukuzaji Viumbe Maji bahari katika ukanda wa Pwani. 

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhamasisha uzalishaji wa chakula cha samaki nchini kupitia sekta binafsi ambapo tani 58.45 zenye thamani ya shilingi 175,350,000 zimezalishwa na viwanda 12 vilivyopo nchini. Aidha, tani 276.7 za chakula cha samaki zenye thamani ya shilingi 1,125,062,200 zimeingizwa nchini. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kusimamia na kutoa ushauri katika vitotoleshi 21 vya sekta binafsi na mashamba 100 ya ukuzaji viumbe maji katika mikoa ya Ruvuma, Kigoma, Mwanza, Mbeya, Katavi na Pwani. Pia, Wizara itaendelea kutoa mafunzo  ya mbinu bora za ukuzaji viumbe maji na kuhamasisha uwekezaji. Aidha, Wizara itapandikiza vifaranga vya samaki katika malambo 12 yaliyoko kwenye mikoa ya Rukwa, Arusha, Mtwara, Ruvuma, Kilimanjaro, Simiyu, Dodoma, Kagera, Njombe, Shinyanga  na Tabora. 185. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kufanya kaguzi zenye sikukazi 200 katika viwanda vya kutengeneza vyakula vya samaki, vitotoleshi vya vifaranga vya samaki, na mashamba ya ufugaji samaki  katika mikoa 11 nchini (Mwanza, Mara, Geita, Morogoro, Mbeya, Pwani, Dar es Salaam, Ruvuma, Kilimanjaro, Arusha na Kagera). Aidha, Wizara  itaanzisha mashamba darasa manne (4) katika Halmashauri za Wilaya za Njombe, Mwanga, Meatu, na Mkuranga.

UTHIBITI WA UBORA NA USALAMA WA MAZAO YA UVUVI 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kuthibiti ubora na usalama wa samaki na mazao yake kwa kufanya kaguzi katika mialo, masoko, viwanda na maghala ya kuhifadhia samaki na mazao yake ili kuchochea biashara  ndani na nje ya nchi.Aidha viwanda12 vya wachakataji wakubwa na viwanda vinne (4) vya wachakataji wa kati vimefanyiwa ukaguzi na kukidhi viwango vya ubora na usalama wa kuchakata mazao ya uvuvi kwa ajili ya soko la Kikanda, Kimataifa likiwepo Soko la nchi za Jumuiya ya Ulaya (Kiambatisho Na. 42). Aidha, viwanda vidogo 33 vya uchakataji, maghala 39 ya kuhifadhi samaki wakavu na maghala 34 ya kupokelea samaki hai  yamefanyiwa ukaguzi na kukidhi viwango vya ubora na usalama. Pia, jumla ya  kaguzi 7,520 za mazao ya uvuvi zilifanyika katika viwanda, maeneo ya mipakani, viwanja vya ndege na bandarini. 

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa imefanya kaguzi za kawaida 264 katika maeneo ya wachakataji wadogo na vyombo 862 vya usafirishaji wa mazao ya uvuvi.  Pia, kaguzi 158 zimefanyika katika mialo  ya Ukanda wa Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika  na Pwani ya Bahari ya Hindi. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara kupitia Maabara za Nyegezi-Mwanza na Dar es Salaam imefanya uhakiki wa ubora na usalama wa mazao ya uvuvi kwa kufanyia uchunguzi  sampuli 2,848 za minofu ya samaki, dagaa, maji na udongo ili kubaini uwepo wa vimelea, kemikali na madini tembo. Matokeo ya chunguzi hizo yalibaini kuwa mazao hayo yamekidhi viwango vya usalama na ubora kwa ajili ya matumizi ya binadamu na wanyama. 

Mheshimiwa Spika, Maabara Nyegezi-Mwanza imeendelea kupata hati ya umahiri katika kiwango cha ISO/IEC 17025:2017 kutoka Taasisi ya Ithibati ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika-SADC (SADCAS). Aidha, idadi ya wataalam wa Maabara walioidhinishwa na kutambuliwa kimataifa wameongezeka kutoka 7 mwaka 2018/2019 hadi 11 mwaka 2019/2020. 190. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itafanya kaguzi za kina 120 katika viwanda na kaguzi za kawaida 1,500 katika mialo, masoko, maghala, na vyombo vya usafirishaji mazao ya uvuvi; Wizara itahakiki usalama na ubora wa samaki na mazao yake kabla ya kusafirishwa ndani na nje ya nchi kwa kufanya kaguzi 8,080. Pia, Wizara itatoa mafunzo kwa wadau 100 kuhusu teknolojia za kisasa, ufungashaji na uwekaji lebo unaozingatia uhifadhi wa mazingira, miundombinu inayohusika na upokeaji na uchakataji, utangazaji masoko na usafirishaji wa samaki na mazao ya uvuvi. 

Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kukarabati mialo 20 katika Ukanda wa Ziwa Victoria (11), Ukanda wa Pwani (4), Ziwa Tanganyika (2), Ziwa Nyasa (2) na Bwawa la Nyumba ya Mungu (1). Pia, Wizara itafanya ukarabati wa masoko ya samaki 15 katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Iringa, Pwani, Ruvuma, Tanga, Kagera, Mtwara na Geita, ili kuhakikisha kuwa mahitaji ya msingi ya kulinda afya za walaji yanazingatiwa. 192. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itaendelea kuboresha shughuli za Maabara katika maeneo yafutayo: 

i. Kuongeza idadi ya sampuli zitakazofanyiwa chunguzi kufikia 6,000 kwa minofu ya samaki, dagaa, maji na udongo ili kubaini uwepo wa vimelea, kemikali na madini tembo ikilinganishwa na sampuli 2,848 zilizochunguzwa mwaka 2019/2020. 

ii. Kuboresha mifumo ya usimamizi ya maabara ili kuendelea kukidhi vigezo vya kiwango kipya cha ISO/IEC 17025:2017. 

iii. Kusimamia maabara ndogo za viwanda vya kuchakata samaki na kuhakiki mifumo ya uchakataji katika viwanda hivyo.

HUDUMA ZA UGANI WA UVUVI 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kutoa huduma za ugani nchini licha ya kuwa na Wagani 677 ukilinganisha na hitaji la sekta ya kuwa na wagani 16,000 na hivyo kuwa na upungufu wa wagani 15,323. Aidha, Wizara imeendelea kuwasiliana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI ili kuzielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuajiri Maafisa Ugani. Vilevile, Wizara imeendelea kuhamasisha Sekta binafsi kuwekeza katika kutoa huduma za ugani ili  kuongeza upatikanaji wa huduma  hizo katika maeneo mbalimbali nchini. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara ilishiriki katika maonesho mbalimbali ya kitaifa ikiwa ni pamoja na Maonesho ya biashara ya kimataifa – Sabasaba, Nanenane, na siku ya chakula Duniani ambapo zaidi ya wadau 33,742 walitembelea mabanda ya Wizara na kupata ufahamu juu ya Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 2015, Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake na kupatiwa elimu ya Uvuvi na Ukuzaji viumbe maji kwa ujumla wake. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imetambua Vyama vya Ushirika vya Wavuvi 102,kuwezesha kuanzishwa kwa vyama vipya 14 na kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa vyama viwili (2). Vilevile, vyama vitano (5) vimepatiwa  Injini za Boti 5 na vyama 14 viko katika hatua za mwisho za kupatiwa mikopo. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imezindua Agenda ya Taifa ya Utafiti wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji (The Fisheries and Aquaculture Research Agenda 2020 – 2025). Agenda hiyo imeainisha maeneo matano (5) ya vipaumbele ambavyo ni: mfumo wa ikolojia ya viumbe maji; uvuvi endelevu katika maji ya asili; Ukuaji wa tasnia ya Ukuzaji viumbe maji; Masoko na biashara ya samaki na mazao yake; na masuala mtambuka. 

Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kusambaza teknolojia mbalimbali za uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kwa kufanya yafuatayo:

i. Kutoa mafunzo rejea kwa wadau 5,008 wa Sekta ya Uvuvi katika Halmashauri 23 nchini (Kiambatisho Na. 43) kuhusu matumizi ya zana halali za uvuvi, ukuzaji bora wa Viumbe Maji na uhifadhi bora wa mazao ya uvuvi. 

ii. Kuandaa na kurusha hewani vipindi 30 vya redio, vipindi 10 na makala 22 za luninga kupitia  Shirika la TBC. Vipindi hivyo vilihusu ufugaji na upatikanaji wa vifaranga bora vya samaki; uchimbaji; utunzaji wa mabwawa na upandikizaji wa vifaranga pamoja na  ufugaji wa samaki katika mabwawa na vizimba. Pia, nakala 11,250 za machapisho  yaliyohusu ufugaji bora wa samaki, athari za uvuvi haramu na uhifadhi bora wa mazao ya uvuvi yalichapishwa na kusambazwa kwa wadau mbalimbali. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia FETA ilifanya tathmini ya kufahamu walipo wahitimu wa kada za uvuvi kwa kufanya ufuatiliaji (Tracer Study) kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2019 waliohitimu katika vyuo vya FETA (Kiambatisho Na. 44), SUA na CKD. Matokeo ya tathmini hiyo yalionesha kuwa asilimia 28 ya vijana wote waliohitimu katika kipindi hicho hawana ajira. Aidha, Wizara inafanya mapitio ya mitaala ili kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji ya soko la ajira kwa wakati uliopo na baadae.

Mheshimiwa Spika, pia, Wizara imeelekeza vyuo vinavyotoa taaluma za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kuweka mkazo katika mafunzo yanayohusu ujasiriamali, ubunifu na mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi waliodahiliwa katika vyuo hivyo. Vilevile, Wizara inandaa utaratibu wa kuwaunganisha wahitimu wasio na ajira na Dawati la Sekta Binafsi ili kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuanzisha shughuli za ujasiliamali.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itaandaa na kurusha hewani vipindi 30 vya redio, 10 vya luninga kuhusu masuala ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji. Aidha, Wizara itahamasisha na kutoa mafunzo rejea kwa wadau 25,000 ili kuwa na Uvuvi endelevu. Vilevile, Wizara itaendelea kusambaza matokeo ya tafiti za kiteknolojia kwa wadau mbalimbali na itawawezesha wanafunzi wa Uzamili na Uzamivu kufanya tafiti za kipaumbele zinazohusiana na masuala ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji ili kuendeleza na kutekeleza Agenda ya Taifa ya Utafiti wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji “2020-2025”.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itaendelea kuviwezesha vyama vya ushirika vya wavuvi na wakuzaji viumbe maji kwa kuvipatia vifaa na zana za uvuvi ili kuongeza tija katika sekta. Aidha, Wizara itaendelea kushiriki na kuhamasisha  wadau kushiriki katika maonesho ya Kitaifa (Sabasaba, Nanenane, Siku ya Chakula Duniani na Mvuvi day) ili waweze kujifunza teknolojia mbalimbali za uvuvi pamoja na kubadilishana uzoefu.

TAASISI  YA UTAFITI  WA  UVUVI  TANZANIA –TAFIRI 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imefanya tafiti mbalimbali ambazo zimesaidia katika kusimamia na kuendeleza Sekta ya Uvuvi nchini na kuchangia katika ukuzaji wa uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla. Tafiti hizo zilifanyika kwa samaki wa maji ya asili na ukuzaji viumbe maji. Tafiti zilifanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo maziwa makuu, bahari, na mabwawa (Kiambatisho Na. 45).

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TAFIRI, imeandaa Agenda ya Utafiti wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji (National Fisheries and Aquaculture Research Agenda), kanuni za utafiti wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji (Fisheries and Aquaculture Research Regulations). Aidha, TAFIRI imeandaa kanzidata ya tafiti za uvuvi na ukuzaji viumbe maji nchini (National Fisheries and Aquaculture Research Database), ambapo katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, TAFIRI imetoa machapisho 112, na vyuo vikuu vimezalisha tasnifu za Uzamili (Master’s) na Uzamivu (PhD) 35 katika kipindi husika. Utekelezaji wa Agenda ya Utafiti ya Taifa utaleta faida zifuatazo:

i. Kuwezesha kufungua makabati yaliyohifadhi tafiti zilizo fanyika miaka ya nyuma kutoka mwaka 2015 hadi 2020, kutafsiri matokeo na kuziorodhesha tafiti hizo pamoja na kuzifikisha kwa watumiaji;

ii. Kupanua wigo wa kufanya tafiti kwa kuzitambua na kuziorodhesha tafiti zote kwenye masuala  ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji zinazofanywa na watafiti nchini kwa kujumuisha  tafiti zinazofanywa na wanafunzi wa shahada za Uzamili (Masters) na Uzamivu (PhD) wakati wa kukamilisha masomo yao;

iii. Kuweka misingi ya kisheria kwa kutoa miongozo,  wajibu na majukumu kwa watafiti wote kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa na Ajenda ya Utafiti;

iv. Kuorodhesha na kuweka tafiti zote pamoja ili kurahisisha utunzaji, usambazaji  na utumiaji wa taarifa zinazotokana na tafiti husika; na

v. Kuwezesha uratibu wa shughuli za utafiti  ili kupata muunganiko wa taarifa kuhusu tafiti za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, tafiti mbalimbali zimeendelea kufanyika. Kupitia Mradi wa SWIOFish utafiti wa uvuvi wa Pweza na mazingira yake katika maeneo ya Mtwara (Msangamkuu na Mgao), Tanga (Kwale na Mtambwe), Pwani (Jojo, Jibondo na Bwejuu) na Lindi (Songosongo) unaendelea ambapo matokeo ya utafiti yatasaidia katika uhifadhi na uvuvi endelevu wa rasilimali ya pweza. Pia, utafiti huu utasaidia katika mchakato wa kulipatia zao la Pweza Nembo ya Kiikolojia (Ecolabeling) inayotolewa na Taasisi ya Marine Stewardship Council.

Mheshimiwa Spika, Nembo ya Kiikolojia itasaidia Pweza wa Tanzania kuuzwa katika soko la Kimataifa na kuongeza thamani ya Pweza wetu katika soko la Dunia. Mpaka sasa zoezi la kupata Nembo ya Kiikolojia limefikia asilimia 79. Kwa sasa, Wizara kupitia TAFIRI na kwa kushirikiana na WWF inaandaa mkakati wa uvunaji wa Pweza (Octopus Harvesting Strategy) ambao utawezesha kuongeza asilimia hadi 81 kuelekea kupata Nembo ya Kiikolojia.

Mheshimiwa Spika, kupitia TAFIRI, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (The Nature Conservancy - TNC) imefanya utafiti ili kubaini madhara yauvuviwa Ringnet katika Ziwa Tanganyika. Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa ringnet inaweza kutumika kuvua samaki katika Ziwa Tanganyika lakini ufanyike kuanzia umbali wa mita 1,000 kutoka ufukweni na kwenye visiwa. Ruhusa hiyo inahusu uvuvi wa usiku tu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara kupitia TAFIRI itasimamia kikamilifu utekelezaji wa Ajenda ya Taifa ya Utafiti wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji. Pia, itaendelea kufanya tafiti za ufugaji wa samaki nchini ili kupata mbegu bora ya samaki iliyoratibiwa kijenetiki; vyakula bora vya samaki vilivyotokana na malighafi asili inayopatikana katika eneo la wafugaji samaki; teknolojia bora na rahisi ya ufugaji samaki katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na ufugaji wa vizimba katika Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Mheshimiwa Spika, TAFIRI itaendelea kufanya tafiti za kuendelea kujua wingi, aina na mtawanyiko wa samaki katika Maziwa Makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa), Maziwa ya Kati, Maziwa Madogo, mito na mabwawa; na kuainisha rasilimali za uvuvi katika Bahari ya Hindi, hasa zile ambazo ni muhimu kwa chakula na uchumi kwa wavuvi na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, TAFIRI itafanya tafiti katika Bahari ya kitaifa (Territorial waters) na katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (Exclusive Economic Zone - EEZ) kuchunguza bailojia, ikolojia na wingi wa makundi ya samaki aina ya jodari na jamii zake na mazingira ya bahari yanayovutia uwepo wa samaki hao wanaopatikana Bahari ya Hindi.

WAKALA WA ELIMU NA MAFUNZO YA UVUVI –FETA

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) imeendelea kutoa mafunzo mbalimbali katika Tasnia ya Uvuvi. Katika kipindi hicho FETA ilidahili jumla ya vijana 1,103 kwa masomo ya Astashahada na Stashahada katika Kampasi za Mbegani, Nyegezi na Kigoma. Aidha, Wizara iliwezesha mafunzo ya muda mfupi kwa washiriki 2,176 yaliyofanywa na FETA

Mheshimiwa Spika, FETA imetoa mafunzo kwa washiriki kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Kenya, Uganda, Afrika ya Kusini, Namibia, Angola, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Somalia na Madagascar. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2018/2019 na 2019/2020, kupitia msaada kutoka Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), FETA ilitoa mafunzo kwa maafisa uvuvi 45kutoka Jamhuri ya Somalia. 212. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia FETA ilifanya tathimini ya kufahamu waliko wahitimu wa kada za uvuvi (Tracer Study) waliohitimu kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2019 katika kampasi za FETA, SUA na CKD. Matokeo ya tathimini kwa vyuo vyote vitatu yalionesha kuwa asilimia 61 ya wahitimu hao wameajiriwa (Serikalini asilimia 52, sekta binafsi asilimia 9), asilimia 3 wamejiajiri, asilimia 36 hawana ajira. Matokeo ya tathimini kwa FETA yameonyesha kuwa asilimia 49 ya wahitimu hao wameajiriwa (Serikalini asilimia 23, sekta binafsi asilimia 26),  asilimia 6 wamejiajiri, asilimia 28 hawana ajira na asilimia 17 wanaendelea na elimu ya juu. Maoni ya waliofuatiliwa yanaonesha kuwa elimu inayotolewa na vyuo husika inakidhi mahitaji ya Sekta.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 FETA imejenga mifumo miwili ya utotoleshaji wa vifaranga vya samaki itakayokuwa na uwezo wa kutotolesha vifaranga 500,000 kwa wiki kwenye kampasi zake za Mikindani –Mtwara na Nyegezi – Mwanza.  Aidha, FETA imezalisha jumla ya vifaranga 2,767,400 katika vituo vyake vya Nyegezi – Mwanza, Mbegani – Pwani na Gabimori–Mara.

Mheshimiwa Spika, FETA ikishirikiana na TASAC ipo katika hatua za mwisho za kuridhiwa kwa Itifaki ya Standards of Training, Certification and Watch Keeping for fish Vessels Personel (STCW – F). Faida zitakazopatikana baada ya Itifaki hiyo kuridhiwa ni pamoja na:

i. Vyeti vitakavyotolewa kwa wahitimu wa vyuo vya mafunzo ya uvuvi nchini vitatambuliwa kimataifa;

ii. Kuongezeka kwa fursa za ajira za kimataifa kwa wataalam wa vyombo vya uvuvi;

iii. Uwepo wa wakaguzi na waangalizi (inspectors and observers) wenye weledi utahakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari;

iv. Kuimarika kwa vyuo vya ndani vya mafunzo ya uvuvi na kutambulika kimataifa;

v. Kuwa na viwango bora vya ufundishaji wa wanafunzi katika vyuo vya uvuvi nchini;

vi. Kuimarika kwa usalama wa wafanyakazi katika vyombo vya uvuvi hivyo kupungua kwa ajali; vii. Kuimarika kwa ulinzi, usalama na uhifadhi wa mazingira ya bahari;

viii. Kuimarika kwa upatikanaji wa takwimu na taarifa mbalimbali za uvuvi; na

ix. Wahitimu wa mafunzo ya uendeshaji wa meli na usalama kuwa na sifa ya kufanya kazi Bahari Kuu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itahakikisha kuwa miundombinu ya kufundishia katika vituo vya FETA vya Gabimori - Rorya na Mikindani - Mtwara inaboreshwa ili kuanza kutoa mafunzo. Kwa sehemu kubwa, vituo hivi viwili, vitajikita katika kutoa elimu ya ufugaji samaki, kuzalisha vifaranga vya samaki na kuvisambaza kwa wananchi na kutoa huduma za ushauri na ugani katika Kanda husika. Aidha, FETA itaendelea kutoa elimu na mafunzo ya uvuvi, uchakataji na ufugaji samaki kwa nadharia na vitendo ili kuongeza tija katika Sekta ya Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, vilevile, FETA imeandaa mpango wa kutoa mafunzo ya siku saba (7) kwa wadau wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji 3,210. Mafunzo hayo yatakuwa yakitolewa katika kipindi cha miezi minne (4) katika kampasi za FETA husuan wakati wa likizo ya wanachuo.

MIRADI YA MAENDELEO YA SEKTA YA UVUVI 

I Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish)

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kutekeleza Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka Sita (2015 hadi 2021). Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa thamani ya shilingi 39,486,528,000.00. Lengo kuu la mradi huo ni kuimarisha usimamizi madhubuti wa uvuvi katika ngazi ya kijamii, kitaifa na kikanda. Katika mwaka 2019/2020, mradi umetenga kiasi cha shilingi: 11,094,917,551.00 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi mbalimbali ikiwemo:

i. Kuimarisha na kuijengea uwezo Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Taasisi zake (TAFIRI, FETA na MRPU) kwa kuwezesha mafunzo mbalimbali na vitendea kazi kwa watumishi wake;

ii. Ujenzi wa miundombinu ya kuimarisha sekta ya Uvuvi kama vile Maabara ya Utafiti wa Uvuvi Dar es Salaam, nyumba za watumishi katika Hifadhi ya Bahari ya Silikanti Tanga (TACMP) na ofisi ya Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia; ukarabati wa miundombinu ya soko la Feri - Dar es Salaam; na ujenzi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Bahari (National Mariculture Resource Centre) Kunduchi, Dar es Salaam.

iii. Ununuzi wa Boti, vifaa vya doria, Vifaa vya utafiti – TAFIRI pamoja na kutoa mafunzo stahiki kwa walengwa;

iv. Kuwezesha  mafunzo kwa Vikundi 50 vya Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) kuhusu masuala ya utawala bora na uongozi ikiwa pamoja na kuwanunulia vitendea kazi mbalimbali; na v. Kuwezesha mapitio ya Sheria ya Uvuvi, kutafsiri na kuchapisha Sera ya Uvuvi katika lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara kupitia mradi wa SWIOFish umetenga bajeti ya shilingi 7,082,358,000 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi mbalimbali ikiwemo: kuiwezesha TAFIRI kufanya tafiti za mavuvi ya kipaumbele; kuimarisha ushiriki wa jamii za wavuvi katika usimamizi na ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi; kuwezesha Doria katika ulinzi wa rasilimali za uvuvi; kuiwezesha Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU); kuimarisha Mfumo wa Taarifa zinazohusu Uvuvi kulingana na matakwa ya kikanda; na kuwezesha kurejea Mpango wa Usimamizi wa Samaki wanaopatikana katika tabaka la juu la maji.

Mheshimiwa Spika, mradi wa SWIOFish utaboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo: kuendelea na ujenzi wa maabara ya TAFIRI; kukamilisha ujenzi wa  nyumba za watumishi wa MPRU Tanga; kuendelea na ujenzi wa jengo la ofisi MPRU - Mafia; ukarabati wa miundombinu ya soko la Feri-Dar es Salaam; na ujenzi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Bahari (National Mariculture Resource Centre) Kunduchi, Dar es Salaam.

II Mradi wa Usimamizi wa Samaki wanaopatikana katika Tabaka la Juu la Maji 220. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) inatekeleza Mradi wa Kuwezesha Utekelezaji wa Mpango wa Usimamizi wa Samaki wanaopatikana katika Tabaka la Juu la Maji (Project to Support the Implementation of the Tanzania Small and Medium Pelagic Fisheries Management Plan) katika Ukanda wa Bahari ya Hindi. Mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi (18) kuanzia mwezi Agosti, 2019 kwa thamani ya shilingi 228,737,551. Lengo la Mradi huo ni kuimarisha uendelevu wa samaki wanaopatikana katika Tabaka la Juu la Maji wakiwemo dagaa ambao huchangia takribani theluthi moja ya mavuno ya samaki wanaopatikana katika Bahari ya Hindi.

Mheshimiwa Spika, kupitia mradi huo Wizara imetekeleza kazi zifuatazo:

i. Kutoa mafunzo kuhusu Mzunguko wa Usimamizi wa Uvuvi kwa wadau 30 wanaohusika katika kutekeleza Mpango wa Usimamizi wa Samaki wanaopatikana katika Tabaka la Juu la Maji. Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha uwezo wadau katika kutekeleza Mpango huo.

ii. Kufanya maandalizi ya Mpango wa Mafunzo kwa kuzingatia dhana ya usimamizi wa uvuvi unaozingatia ikolojia na mazingira (Ecosystem Approach to Fisheries Management). Mpango huu utakaotumika kutoa mafunzo kwa wadau wanaohusiana na utekelezaji wa Mpango wa Usimamizi wa Samaki Wadogo na wa Kati Wanaopatikana katika Tabaka la Juu la Maji ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali hiyo;

iii. Kufanya tathmini ya Mfumo wa Wizara wa Ukusanyaji, Uhifadhi na Uchakataji wa Takwimu za Uvuvi ili kubaini changamoto zilizopo. Kufahamika kwa changamoto hizi kutawezesha Serikali kuhuisha Mfumo uliopo na kuandaa Mkakati ya Usimamizi wa Takwimu Nchini utakayowezesha upatikanaji wa takwimu na taarifa sahihi za uvuvi kwa wakati;  na

iv. Kufanya mapitio ya Mpango wa Usimamizi wa Samaki wanaopatikana katika Tabaka la Juu la Maji kwa kufanya tathmini ya hali halisi ya utekelezaji wa Mpango ili kubaini changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango tangu ulipoandaliwa Mwaka 2013 pamoja na fursa mpya zilizopo kwa sasa. Taarifa hii itaiwezesha Serikali kuandaa Mpango mpya na kuweka mikakati ya usimamizi itakayoendana na hali halisi ya rasilimali husika.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itaendelea kutekeleza Mradi huo kwa kufanya yafuatayo:

i. Kutoa mafunzo kwa wadao 50 wakiwemo Maafisa Uvuvi Wilaya, Wakusanya Takwimu za Uvuvi na  Vikundi shirikishi vya usimamizi wa rasilimali za Uvuvi (BMUs) kuhusu uvuvi endelevu; na

ii. Kufanya utafiti kuhusu madhara yatokanayo na uvuvi wa samaki wasiolengwa (Bycatch) kwa samaki wanaopatikana katika tabaka la juu la maji.

MASUALA MTAMBUKA KATIKA SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI 

Dawati la  Sekta Binafsi la Wizara

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Dawati la Sekta Binafsi imeunganisha wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi wanaohitaji huduma za mikopo na bima, hususan kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Katika mwaka 2019/2020, jumla ya Shilingi bilioni 26.1 zimeidhinishwa na TADB ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.7 ikilinganisha na shilingi bilioni 17.3 zilizotolewa katika mwaka 2018/2019. Fedha zilizoidhinishwa na kutolewa katika mwaka 2019/2020 ziko katika mgawanyoufuatao:

i. Uzalishaji wa mifugo na usindikaji wa nyama: kampuni 10 zimeomba mkopo ambapo kiasi cha fedha kilichoidhinishwa na TADB mpaka sasa ni shilingi bilioni 12.9 na shilingi bilioni 10.3tayari zimetolewa

ii. Uzalishaji wa maziwa na usindikaji: kampuni nane (8) na Vyama vya Ushirika vya Msingi viwili (2) vimeomba mkopo ambapo shilingi bilioni 12.2 zimeidhinishwa na shilingi bilioni 1.69 tayari zimetolewa.

iii. Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji: kampuni saba (7) na Vyama vya Ushirika viwili (2) vimeomba mkopo ambapo shilingi milioni 944.2 zimepitishwa na shilingi milioni 323.8 tayari zimetolewa.

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa Sekta za Mifugo na Uvuvi, Dawati limefanikisha masuala yafuatayo:

i. Benki ya TPB imefungua dirisha maalum la mikopo kwa wavuvi. Uzinduzi wa dirisha hilo ulifanyika tarehe 23 Septemba, 2019 Ilemela, Mwanza. 

ii. Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji wa Wavuvi walio katika vyama vya ushirika unaoitwa “Uvuvi Data Base”umeandaliwa. Vyama vya Ushirika 9 na wavuvi 557 kutoka mikoa ya Mwanza, Geita na Kigoma wameingizwa katika mfumo huo utakaowezesha taasisi za fedha kuwatambua na kuwafuatilia wakopaji hivyo kuvutia utoaji wa mikopo kwa wavuvi. 

iii. Shirika la Bima la Taifa (NIC) limekubali kutoa bima kwa mikopo na zana za uzalishaji katika sekta za mifugo na uvuvi. 

iv. Vijarida vya mnyororo wa thamani wa mazao saba (7) ya mifugo na uvuvi vimeandaliwa kwa kushirikiana na ASPIRES-USAID ili kutambua changamoto za uzalishaji katika Sekta za Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara kupitia Dawati la Sekta Binafsi imeshughulikia hoja za kampuni za Sekta Binafsi kwa Taasisi za Serikali ili kuharakisha upatikanaji wa huduma zinazochelewesha ufanisi. Pia, Dawati limeshiriki kwenye mijadala ya kisera iliyotoa fursa za kujengwa na upanuzi wa kiwanda cha maziwa cha Galaxy Food and Beverages (Arusha); kiwanda cha ngozi cha ACE Leather Ltd (Morogoro); kiwanda cha dawa za mifugo cha Farm Access (Arusha); viwanda vya nyama vya Nguru Hills (Morogoro); Tan Choice (Pwani); na Kiwanda cha Mabondo (Kagera). Vilevile, katika kipindi hiki cha Mlipuko wa CORONA (COVID – 19), Dawati limewaunganisha wasafirishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi kusafirisha mazao nje ya nchi kupitia TAHA. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara kupitia Dawati la Sekta Binafsi itaendelea kuainisha, kuratibu na kufuatilia changamoto na kuzitafutia ufumbuzi kwa haraka ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara katika Sekta za Mifugo na Uvuvi. Aidha, Dawati litaendelea kuhamasisha uwekezaji katika Sekta za Mifugo na Uvuvi ikiwemo: uwekezaji katika viwanda vya kusindika mazao ya mifugo (nyama, maziwa na ngozi), vyakula vya mifugo, ufugaji samaki katika vizimba, mabwawa, uzalishaji wa vifaranga na vyakula bora vya mifugo na samaki.
UtawalaBora, Jinsia na UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imehamasisha watumishi kupima afya zao kwa hiari na kuwawezesha watumishi wanaoishi na Virusi vya UKIMWI kupata huduma ya lishe. Aidha, Wizara imetekeleza Mkakati wa Kuzuia na Kuziba Mianya ya Rushwa kwa kuanzisha mfumo wa malipo kwa njia ya kielektroniki katika vituo vyake pamoja na kutoa elimu kwa watumishi na wadau wa Sekta ya Mifugona Uvuvi. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeajiri watumishi wapya 52 wakiwemo Maafisa Mifugo (25), Maafisa Uvuvi (5), Manahodha (2), Wateknolojia wa Maabara (2), Wahasibu (2) na watumishi wa Kada Mtambuka saba (16). Aidha, vikao vitatu (3) vya Kamati ya Ajira vimefanyika ambapo watumishi tisa (9) wamepandishwa vyeo, watano (5) wamethibitishwa kazini baada ya kumaliza vizuri muda wa majaribio. Pia, taarifa za kiutumishi na mishahara ya watumishi 465 zimehakikiwa kupitia Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Utumishi na Mishahara (HCMIS) na watumishi 53 wamepatiwa mafunzo ya Itifaki, Sheria, Kanuni na miongozo ya kazi. Vilevile, Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Utumishi na Mishahara (HCMIS) na Mfumo wa Malipo ya Mishahara kwa watumishi (GSPP) imeendelea kusimamiwa. Aidha, watumishi 20 wamewezeshwa kushiriki mafunzo ya muda mrefu na watumishi25mafunzoya muda mfupi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itatekeleza Mkakati wa Kuzuia na Kuziba Mianya ya Rushwa na kuelimisha watumishi wote kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya kazi katika Utumishi wa Umma. Pia, Mkataba wa Huduma kwa Mteja utafanyiwa mapitio na Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji Kazi (OPRAS) utasimamiwa.  Aidha, Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Utumishi na Mishahara (HCMIS) na Mfumo wa Malipo ya Mishahara ya watumishi (GSPP) itawezeshwa. Vilevile, michezo kwa watumishi mahali pa kazi itapewa umuhimu unaostahili.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaajiri watumishi 235 wakiwemo 173 wa Sekta ya Mifugo na 62 wa Sekta ya Uvuvi, watumishi 111 wanatarajiwa kupandishwa vyeo na watumishi 23 wanatarajiwa kuthibitishwa kazini. Aidha, Wizara itafanya uhakiki wa watumishi 465, watumishi 400 wataelimishwa kuhusu kupima afya zaokwa hiari na watumishi wanaoishi na Virusi vya UKIMWI watahudumiwa. Vilevile, vikao vinne vikiwemo viwili (2) vya Kamati ya Ajira na viwili (2) vya Baraza la Wafanyakazi vitawezeshwa, pia majukumu ya Vyama vya Wafanyakazi, michezo na mabonanza yatawezeshwa.
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara imeanzisha Mfumo wa Mawasiliano Kielektroniki (e-office) kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi. Mfumo huo umewezesha kuongezeka kwa kasi ya utendaji kazi, kupunguza gharama za uendeshaji wa ofisi, kuwezesha upatikanaji wa taarifa za ofisi kwa haraka. Aidha, watumishi 99 wa Wizara wamepatiwa mafunzo ya kutumia mfumo huu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake hususan ya ukusanyaji wa maduhuli ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi kwa kutumia mifumo ya TEHAMA. Katika utekelezaji huo, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeanza kukusanya maduhuli kwa njia ya kieletroniki yatokanayo na vibali vya Afya ya Wanyama (Animal Health Movement Permit) kupitia mfumo wa makusanyo wa Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS) ambao unasimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI. Kupitia mfumo wa makusanyo wa TAMISEMI (LGRCIS) wastani wa makusanyo umeongezeka kutoka Shilingi 1,884,822,638.55kwa kipindi cha Julai hadi Aprili 2018/2019 hadi kufikiaShilingi 3,795,970,430.02 kwa kipindi kama hicho 2019/2020; uwazi umeongeza kwenye makusanyo na umewezesha ufuatiliaji wa karibu wa makusanya yatokanayo na mifugo. Pia, mfumo huu umeisaidia upatikanaji wa taarifa za mifugo inayokaguliwa kwenye minada ya awali. Vibali vya Afya ya Wanyama ni kasma inayokusanywa na Mamlaka za Serikali Mitaa (MSM) kwenye minada 504 ya awali nchini. Aidha, mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo wa makusanyo wa LGRCIS yametolewa kwa watumishi 163 kutoka Halmashauri117zenye minada ya awali.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kukamilisha ujenzi wa mfumo wa kielektroniki (Fisheries Licence Online Application) utakaowezesha wafanyabiashara wa samaki na mazao yake kuomba leseni na vibali vya kusafirisha samaki na mazao yake ndani na nje ya nchi. Lengo likiwa ni kuongeza ufanisi na kurahisisha biashara ya samaki na mazao yake. Aidha, wizara imeimarisha na kusimamia Mfumo wa kukusanya maduhuli ya Serikali (Fisheries Revenue Collection System) ambao umeunganishwa na mfumo wa Serikali wa GePG (Government Electronic Payment Gateway) na Mfumo wa kielektroniki wa Kukusanya na Kutunza Takwimu za Uvuvi (Electronic Catch Assessment Survey - eCAS). Aidha, Wizara imesambaza mashine sita (6) za kielektroniki za kukusanyia maduhuli (Point Of Sales - POS) katika vituo  vya kukusanyia mapato  na hivyo kuwezesha idadi ya vituo vyenye POS kufikia.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara imepanga kuboresha na kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kwa kutumia mifumo ya kieletroniki katika ukusanyaji maduhuli yatokanayo na Sekta ya Mifugo na Uvuvi kwenye minada, masoko na mialo ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuboresha mazingira ya kufanya biashara. Pia, Wizara itaendelea kutumia mfumo wae-officekatika Idara na taasisi zake ili kufikia lengo la kutumia karatasi chache (less paper) na baadaye kutotumia karatasi (paperless).

Mawasiliano Serikalini

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara imeendelea kutoa taarifa mbalimbali kwa wadau wa mifugo na uvuvi zikiwemo taarifa za uzinduzi wa kampeni za uogeshaji mifugo kupitia majosho, taratibu za uendeshaji wa minada ya mifugo nchini, uzinduzi wa ajenda za utafiti wa mifugo na uvuvi, uanzishwaji na uendeshaji wa mashamba darasa. Aidha, ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya mifugo yanayopotoshwa katika jamii umetolewa ikiwemo ufafanuzi baada ya kuwepo taarifa zisizo za kweli juu ya VirusivyaCorona (COVID – 19)kuwa na uwezekano wa kusambazwa na mifugo wakiwemo kuku. Hivyo, Wizara ilitoa ufafanuzi kuwa mifugo haiwezi kusambaza virusi hivyo kwa binadamu. Vilevile, Wizara imerusha vipindi maalum 52 vya runinga kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC 1) pamoja na vipindi vya redio kupitia TBC Taifa juu ya elimu mbalimbali kuhusu Sekta za Mifugona Uvuvi.

Mheshimiwa Spika Wizara inavipongeza vyombo mbalimbali vya habari vikiwemo vituo vinavyorusha matangazo katika ngazi ya jamii (community radio and television stations), magazeti, redio, televisheni na mitandao ya kijamii, namna vinavyotoa ushirikiano mkubwa kwa Wizara kwa kuhabarisha umma shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wizara kupitia njia mbalimbali yakiwemo matangazo ya moja kwa moja (mubashara), pamoja na kusambaza taarifa za Wizara zinazotolewa na kusambaza kwa umma kwa kutumiavyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itaendelea kutoa ufafanuzi na taarifa sahihi kwa wananchi juu ya mambo mbalimbali yanayohusu Wizara na taasisi zake pamoja na kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kuutarifu umma juu ya shughuli mbalimbali za Wizara. Aidha, Wizara itaendelea kuandaa vipindi maalum vya redio na televisheni na kuvitangaza ili kuwapatia wananchi fursa ya kupata taarifa mbalimbali hususan kwa wafugaji na wavuvi ili watumie vyema Sekta za Mifugo na Uvuvi katika kukuza uchumi wao na kuongeza pato la Taifa. Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi 

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia hifadhi ya Mazingira katika sekta ya mifugo na uvuvi kwa kutoa mafunzo yanayohusu ufugaji unaohimili mabadiliko ya tabianchi kwa wawezeshaji 84 katika Halmashauri zote za Mikoa ya Dodoma na Singida. Aidha, Wizara imeendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kutekeleza Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo ya vijijini (Ecosystem Based Adaptation for Rural Resilience in Tanzania) katika Halmashauri za Mvomero (Morogoro), Mpwapwa (Dodoma), Kishapu (Shinyanga) na Simanjiro (Manyara). Jumla ya wafugaji 1,400 wamewezeshwa kuibua shughuli zinazoweza kufanyika katika mazingira ya maeneo yao ili kuwawezesha kuwa na ufugaji unaohimili mabadiliko ya tabianchi. Pia, imepata mafanikio makubwa katika kudhibiti uvuvi wa milipuko kwa asilimia 100, ambao huchangia kuharibu mazalia ya samaki (matumbawe) katika mwambao wa Bahari ya Hindi. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara itatoa mafunzo kwa wawezeshaji katika Halmashauri 32 nchini kuhusu ufugaji unaohimili mabadiliko ya tabianchi. Pia, Wizara itaendelea kushirikiana na Ofisi  ya Makamu wa Rais – Mazingira na Wizara ya Kilimo katika kutekeleza Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo ya vijijini (Ecosystem Based Adaptation for Rural Resilience in Tanzania) katika Halmashauri za Mvomero (Morogoro), Mpwapwa (Dodoma), Kishapu (Shinyanga) na Simanjiro (Manyara). Pia, Wizara itashirikiana na Wizara ya Maji katika utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi wa Mkoa wa Simiyu utakaotoa maji kutoka Ziwa Victoria kupitia Miji ya Bariadi, Mwandoya na Meatu (Simiyu). Mradi huu utasaidia kupunguza changamoto ya maji kwa ajili ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 wizara itaendelea kufuatilia athari za mabadiliko ya Tabianchi katika maziwa makubwa na maziwa mengine. Aidha, wizara itaandaa jarida la kufundishia wavuvi na wafugaji wa samaki kuhusu utunzaji wa mazingira. Lengo ni kujenga uelewa wa masuala ya utunzaji wa mazingira kwa wavuvi na wafugaji samaki.
Ushirikianowa Kikandana Kimataifa 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuendeleza Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Kupitia ushirikiano huo, nchi yetu inapata fursa ya kushiriki na kutekeleza Sheria, miongozo, mikataba, itifaki na taratibu mbalimbali za kikanda na kimataifa zenye lengo la kuimarisha Sekta ya Mifugo hususan udhibiti wa magonjwa ya mifugo na biashara ya mazao ya mifugo ikiwemo nyama, ngozi na maziwa. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kushiriki kwenye mikutano, makongamano na warsha mbalimbali zenye lengo la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kusimamia Sekta ya Mifugo. Miongoni mwa mikutano hiyo ni Baraza la Sekta ya Kilimo na Usalama wa Chakula ambao ulijadili maeneo ya Sumu kuvu katika mazao ya Kilimo (Aflatoxin); Afya ya Mimea na Mifugo (Sanitary and Phytosanitary); Udhibiti wa magonjwa ya mifugo yasiyo na mipaka (TADs); Taarifa ya Sera ya Uwekezaji kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Investment Policy); Mkutano wa Eneo Huru la Biashara kwa Afrika (ACfTA); Baraza la Biashara na Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika Mashariki; na Mkutano Mkuu wa SADC kuhusu uwekezaji katika viwanda. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi za kikanda na kimataifa ili kuendeleza Sekta ya Mifugo hususan uwekezaji na biashara ya mifugo na mazao yake. Vilevile, Wizara itaendelea kushiriki katika masuala ya kikanda, kimataifa na kutekeleza mikataba na itifaki mbalimbali za kikanda na kimataifa ambazo nchi yetu ni mwanachama. 

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha mashirikiano ya kikanda na kimataifa ili kusimamia rasilimali za uvuvi katika maji tunayomiliki kwa pamoja na nchi nyingine. Katika mwaka 2019/2020, Wizara imeshiriki katika vikao na warsha mbalimbali kupitia Taasisi za Lake Victoria Fisheries Organisation (LVFO) inayosimamia Ziwa Victoria, Lake Tanganyika Authority (LTA) inayosimamia Ziwa Tanganyika, pamoja na taasisi za IOTC, WIOMSA, SWIOFC, IORA zinazosimamia Ukanda wa Bahari ya Hindi. 

Mheshimiwa Spika, kupitia mashirikiano hayo, Wizara inaratibu na kushiriki katika vikao vya kujadili Mkataba wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) wa kuondoa ruzuku isiyoendana na usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi. Mkataba huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2020. Pia, kupitia LVFO wafanyabiashara wadogo 100 kutoka nchi za Tanzania (25), Kenya (25), Uganda (25) na Burundi (25) walipewa mafunzo kuhusu uchakataji, ufungashaji na kuongeza thamani katika mazao ya uvuvi. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imeendelea kushiriki kwenye mikutano, makongamano na warsha mbalimbali za Kikanda na Kimataifa kwa lengo la kuweka mikakati ya kuendesha operesheni za pamoja dhidi ya Uvuvi Haramu Usioratibiwa na Usiotolewa Taarifa katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika. Aidha, Tanzania ilishiriki katika mafunzo kuhusu mfumo wa kikanda wa kutoa taarifa ya utekelezaji wa Itifaki ya Uvuvi ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) yaliyofanyika nchini Zimbambwe. Pia, katika Mkutano wake wa 17, Bunge lako tukufu  liliridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa kuzuia Uvuvi Haramu, Usioratibiwa na Usiotolewa Taarifa (Port States Measures Agreement-PSMA). 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi za kikanda na kimataifa katika Sekta ya Uvuvi ili kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi. Aidha, Wizara itaendelea kutekeleza mikataba na itifaki mbalimbali za kikanda na kimataifa ambazo nchi yetu ni mwanachama ikiwemo Itifaki ya PSMA.

Uwekezaji na Uwezeshaji katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali kupitia Wizara imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya mifugo na bidhaa zake. 

Kutokana na jitihada hizo mafanikio yafuatayo yamepatikana:

i. Machinjio 21 zinazokidhi viwango vya kimataifa  zenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 3,160,  mbuzi na kondoo 5,650, kuku 35,500,  nguruwe 90 na  punda 200 kwa siku zinafanya kazi(Kiambatisho Na.47).

ii. Viwanda tisa (9) vya kusindika nyama vyenye uwezo wa kusindika jumla ya tani 794 za nyama kwa siku vinafanya kazi (Kiambatisho Na.48). 

iii. Machinjio za kisasa 10 zenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 7,000, mbuzi/kondoo 12,610 na kuku 3,000 kwa siku zinaendelea kujengwa na kukarabatiwa(Kiambatisho Na.49). 

iv. Viwanda 11 visivyofanya kazi vyenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 4,500, mbuzi/kondoo 8,500, kuku 5,000,  punda 200 kwa siku vimehamasishwa kuanza uzalishaji (Kiambatisho Na.50).

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya nyama ili kuzalisha nyama safi na salama kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi. Katika  mwaka 2019/2020 ujenzi wa kiwanda cha Tan Choice Limited kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani umekamilika kwa asilimia 98. Kiwanda hiki kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 1,000 na mbuzi4,500kwa siku.Pia, ujenzi wa kiwanda cha Elia Foods Overseas Ltd kilichopo Longido Mkoa wa Arusha umekamilika kwa asilimia 97.

Kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe1,000na mbuzi4,000kwa siku. Vilevile, ujenzi wa kiwanda cha Binjiang Company Ltd kilichopo Manispaa ya Shinyanga umekamilika kwa asilimia 99. Kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe1,000kwa siku. 

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) inaendelea na upanuzi wa kiwanda cha kuzalisha bidhaa za ngozi cha Gereza la Karanga ambapo kwa sasa upanuzi huo umefikia asilimia 80. Aidha, upanuzi huo utakapokamilika utawezesha kiwanda hicho kusindika futi za mraba 12,500 za ngozi kwa siku; kuzalisha viatu vya kiraia jozi 4,000 kwa siku; kuzalisha soli za viatu 3,000 kwa siku; na kuzalisha bidhaa nyingine za ngozi zikiwemo mikanda, pochi na mabegi. Vilevile, kiwanda cha ACE Leather cha Morogoro kinapanuliwa kwa kuwekewa mtambo wa kisasa utakaowezesha kusindika ngozi kufikia hatua ya mwisho (finished leather) ambapo upanuzi huo umefikia asilimia90. 

Mheshimiwa Spika, ili kuwa na chanjo za magonjwa ya mifugo za kutosha kulingana na mahitaji nchini, Wizara imeendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuzalisha chanjo za magonjwa ya mifugo ambapo katika mwaka 2019/2020mafanikio yafuatayo yamepatikana:

i. Ujenzi wa jengo la kuzalishia chanjo za aina ya bakteria katika Kiwanda cha Serikali cha uzalishaji Chanjo cha Kibaha (TVI) umefikia asilimia 75. Ujenzi wa jengo hilo utakapokamilika mwezi Juni, 2020 utawezesha kiwanda kuzalisha chanjo za Magonjwa 13 ya kipaumbele zinazohitajika hapa nchini ikiwemo chanjo mpya tatu (3) za Magonjwa ya Homa ya Mapafu ya Mbuzi, Sotoka ya Mbuzi na Kondoo na Kichaa cha Mbwa. 

ii. Ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuzalisha chanjo za mifugo cha Hester Biosciences Africa Limited cha Kibaha chenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 18 (Shilingi bilioni 41.4) unaendelea ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia 90. Kiwanda hicho kitakapo kamilika mwezi Juni, 2020 kitazalisha chanjo 27 zinazoagizwa kutoka nje ya nchi ambapo kwa mwaka kiwanda hiki kitaweza kuzalisha jumla ya dozi bilioni 1.5 kwa mwaka kwa ajili ya soko la ndani na soko la nje. 

Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza kwa dhati wawekezaji hawa ambao wameunga mkono Serikali ya awamu ya tano katika kuwekeza kwenye Sekta ya Mifugo. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara imetoa mafunzo kuhusu Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi kwa Vikundi 11 vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi katika Bwawa la Mtera (4) na Ziwa Victoria (7) katika Wilaya za Ilemela na Nyamagana (Mwanza). 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imehamasisha sekta binafsi kuwekeza katika  viwanda vipya vinne (4) ambavyo vipo katika hatua za awali za ujenzi. Viwanda hivyo ni pamoja na Supreme Perch Ltd na Lake Star vya mkoani Kagera, Abajuko Enterprise Ltd cha mkoani Pwani na Pesca Perch Ltd cha mkoani Mwanza. Vilevile, idadi ya maghala ya ugandishaji/kuhifadhia mazao ya uvuvi (cold rooms) imeongezeka kutoka nane (8) mwaka 2017/2018 hadi 90 mwaka 2019/2020 na kupelekea kuongezeka kwa usambazaji na upatikanaji wa samaki na mazao ya uvuvi nchini na nje ya nchi. Maghala hayo kwa sasa yanauwezo wa kuhifadhi wastani wa tani 350 kwa siku. 

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhamasisha wavuvi na wadau wa uvuvi kujiunga pamoja na kuanzisha vyama vya ushirika ili waweze kukopesheka na kuongeza tija katika Sekta ya Uvuvi. Aidha, vyama vya ushirika vya wavuvi vimeunganishwa na taasisi za fedha ambapo mikopo iliyoombwa na kupitishwa ni shilingi bilioni 2.6 na mikopo iliyotolewa ni shilingi milioni 873.8. Pia, Wizara imehamasisha Benki ya Posta Tanzania -TPB kuzindua Akaunti ya Wavuvi (Wavuvi Account) kwa ajili ya mikopo na bima mahususi kwa wavuvi hususan wavuvi wadogo. Juhudi hizi zinalenga kuboresha maisha ya wavuvi na kuongeza kipato ili waweze kuboresha maisha ikiwa ni pamoja na lishe. 

Mheshimiwa Spika, katika kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji, Wizara imetoa vibali 39 bila tozo yoyote katika mwaka 2019/2020. Vibali hivyo ni kama ifuatavyo: ufugaji  samaki kibiashara (11), kuingiza nyavu za kutengeneza vizimba (6), kusafirisha mwani (4), kusafirisha lulu (2), kuingiza vifaranga vya samaki (4), kuingiza samaki wa mapambo (5), na  kuingiza chakula cha samaki(13). 

Mheshimiwa Spika, pia, jumla ya shilingimilioni 4zimetolewa kwa vikundi vya wafugaji samaki katika Wilaya za Mbarali na Chato. Vilevile, jumla ya  injini13za kupachika za boti ambapo injini tatu (3) zenye uwezo wahorsepower15 zimetolewa kwa vikundi vya wavuvi vya Magawa, Kisiju na  Shungubweni katika wilaya ya Mkuranga. Pia injini kumi (10) za boti zenye uwezo wa horsepower 25 zimegawiwa katika kikundi cha wafugaji wa samaki  Mwamapuli (1) kilichopo Wilaya ya Igunga, kikundi cha wavuvi Mbamba bay (1), kikundi cha wavuvi Kyela (1), Vita Fishing Group, Msangamkuu-Mtwara (1), wakulima wa mwani Kweingoma-Handeni (1), Jiwezeshe Group Naumbu - Mtwara (1), Ukerewe (1), Nyamikoma-Busega (1), Kasanga-Kalambo (1) na Kaliua-Tabora(1). 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021 Wizara imetenga shilingimilioni 200kwa ajili ya kusaidia wavuvi, wakuzaji viumbe maji na wadau wengine kupitia vyama Ushirika. Aidha, Wizara itaendelea kuhamasisha wavuvi na wadau wa uvuvi kuanzisha vyama vya ushirika pamoja na kuanzisha miradi ya kuwasaidia wavuvi wadogo. Gawio la Serikali katika Sekta ya Mifugo 258. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Taasisi, Bodi na Wakala zilizopo chini ya Wizara ambazo ni NARCO, LITA, TALIRI, TVLA, Bodi ya Nyama Tanzania, Bodi ya Maziwa Tanzania, Machinjio ya Dodoma, TAFIRI, FETA na MPRU zimetoa gawio kwa Serikali lenye jumla ya shilingi 1,492,500,000 (Kiambatisho Na. 51) ikilinganishwa na shilingi 520,000,000 kilichotolewa mwaka 2018/2019. Aidha, Wizara imeendelea kuhamasisha uwepo wa tija katika taasisi hizo ili kuweza kuchangia zaidi mapato katika mfuko wa Serikali

Michango katika Shughuli za Kijamii. 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Taasisi, Bodi na Wakala zilizo chini ya Wizara zimetoa mchango wa shilingi 560,971,726 (Kiambatisho Na. 51) ikilinganishwa na shilingi 411,793,383 zilizotolewa mwaka 2018/2019. Michango hiyo ni kwa ajili ya kuchangia shughuli za maendeleo ya jamii kwa kukarabati na kujenga miundombinu muhimu ikiwemo ukarabati wa majosho; kuchimba visima vya maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo; kujenga kituo cha kukusanyia maziwa; kusaidia vyama vya ushirika vya wafugaji; uhifadhi na miradi ya maendeleo katika vijiji vilivyomo ndani ya hifadhi ya kisiwa cha Mafia; kutolewa injini za boti kwa vikundi 13 vya uvuvi; na mafunzo kwa jamii kuhusiana na shughuli za uvuvi na ulinzi wa rasilimali za uvuvi.

Mwenendo wa Ukusanyaji Maduhuli ya Serikali  

Mheshimiwa Spika, mwenendo wa ukusanyaji maduhuli kwa Sekta za Mifugo na Uvuvi  umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo katika mwaka wa 2019/2020 Wizara ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 82,301,458,000 hadi kufikia Aprili 2020 ilikuwa imekusanya kiasi cha shilingi 62,985,042,833 sawa na asilimia 76.5 ya lengo. Vilevile, ukusanyaji maduhuli uliongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 21 mwaka 2015/2016 hadi shilingi bilioni 72 mwaka 2018/2019. Aidha, mapato ya Taasisi zilizo chini ya Wizara na mapato ya Halmashauri yanayotokana na shughuli za  Mifugo na Uvuvi yameongezeka kwa kasi kubwa.
HITIMISHO 

Shukrani 

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wale wote waliochangia kwa namna moja au nyingine katika kuiwezesha Wizara kufanikisha majukumu yake. Mafanikio yaliyopatikana katika mwaka uliopita yametokana na ushirikiano na misaada ya kifedha na kiufundi kutoka kwa nchi wahisani, mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, taasisi za fedha za kitaifa na kimataifa, taasisi za hiari zisizokuwa za kiserikali na mashirika ya kidini bila kusahau hamasa na ushiriki wa wananchi wakiongozwa na Waheshimiwa Wabunge na Madiwani. 

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuzitambua na kuzishukuru nchi za Australia, Austria, Brazil, Canada, Jamhuri ya Czech, Hispania, Iceland, Ireland, Japan, Israel, Korea Kusini, Jamhuri ya Watu wa China, Marekani, Misri, Norway, Poland, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na Uswisi  kwa kuchangia katika maendeleo ya Sekta za Mifugo na Uvuvi. 

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutambua na kuzishukuru jumuiya za kikanda ambazo ni Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Nchi za Ulaya (EU). Aidha nashukuru taasisi za Kifedha na Wadau wa Maendeleo ambao ni Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika la Kimataifa la  Ushirikiano la Jamhuri ya Korea (KOICA), Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Jamhuri ya Japan (JICA), Shirika la Misaada la Ireland (Irish Aid), Shirika la Misaada la Marekani (USAID), Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DfID), Taasisi ya Rasilimali za Wanyama ya Umoja wa Afrika (AU-IBAR), Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE), Shirika la Maendeleo ya Uswisi (SDC), Shirika la Ushirikiano la Ujerumani (GIZ), United Nations University (UNU), Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA), na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Sweden (SIDA); na mashirika ya FAO, WHO, IAEA, UNICEF, UNDP, UNIDO, SIDA, ILRI, CIAT, ASARECA na CCARDESA. Pia, natoa shukrani kwa Mifuko ya Kimataifa ya GEF na IFAD kwa michango yao katika kuendeleza Sekta za Mifugo na Uvuvi. 

Mheshimiwa Spika, pia, napenda kushukuru Mashirika na Taasisi za hiari za Bill and Melinda Gates Foundation, World Wide Fund for Nature (WWF), Indian Ocean Commission (IOC), South West Indian Ocean Fisheries Commission (SWIOFC), Heifer Project Tanzania (HPT), Overseas Fisheries Cooperation Foundation of Japan (OFCF), Vetaid, Care International, OXFARM, Welcome Trust, World Vision, FARM Africa, Land O’ Lakes, Building Resources Across Communities (BRAC), World Society for Protection of Animals (WSPA), Global Alliance for Livestock and Veterinary Medicine (GALVmed), Institute of Social Studies (ISS), International Land Coalition (ILC), British Gas International, Sea Sense, Indian Ocean Tuna Commission (IOTC), International Whaling Commission (IWC), SmartFish, Marine Stewardship Council (MSC), Mashirika na Taasisi mbalimbali za humu nchini zinazojihusisha na uendelezaji wa Sekta za Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa namna anavyoliongoza Taifa letu na anavyotusimamia katika kutekeleza majukumu ya Serikali. Nimewahi kukutana na kufanya kazi na viongozi wengi ndani na nje ya nchi yetu lakini Mheshimiwa Rais wewe ni Kiongozi na Mwalimu bora nakushukuru sana. Umenikabidhi majukumu ambayo nimeyatekeleza kikamilifu katika Wizara yangu na kuhakikisha kuwa ahadi ulizozitoa kwa Watanzania wakati unaomba kura mwaka 2015 zimetimia na kuhakikisha kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 imetekelezwa.

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kuwapongeza Wafugaji na Wavuvi wote nchini kwa kazi nzuri wanazofanya za kutunza, kuzalisha na kulinda rasilimali za Taifa. Kazi wanazofanya ni nzuri na za heshima na kwamba Wizara yangu itaendelea kusimamia na kuunga mkono juhudi zao. Pia, niwashukuru wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wote wa Sekta za Mifugo na Uvuvi kwa dhamira yao njema ya kuendeleza sekta hizi muhimu.
17

Mheshimiwa Spika, naomba kurejea tena kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega, Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa msaada wake wa karibu katika kusimamia kazi za Wizara. Aidha, napenda pia nitoe shukrani zangu kwa Katibu Mkuu Uvuvi, Dkt. Rashid Adam Tamatamah na Katibu Mkuu Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel, Wakurugenzi pamoja na Watendaji wote wa Wizara na Taasisi kwa kazi nzuri sana wanazofanya. Nimefurahi sana kufanya kazi nanyi na ninawapongeza kwa kukubali mabadiliko na kukubali kuchapa kazi usiku na mchana kwa kauli mbiu ya “masaa ni namba tu” kwa manufaa ya Taifa letu, mmejinyima mengi kufikia mafanikio haya tunayojivunia. Mwandishi wa Kitabu cha How Successful People lead, John C. Maxwell alisema, nakuu “nobody achieves anything great by giving the minimum. No teams win championship without making sacrifices and giving their best” namuomba Mungu aendelee kuwabariki katika utumishi wenu.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukrani zangu za dhati kwa wananchi wa Jimbo la Kisesa ambao muda wote wameendelea kuniunga mkono katika kutekeleza majukumu yangu ya jimbo na kitaifa, nataka niwahakikishie kuwa nipo tayari kuendelea kuwatumikia kwa juhudi, bidii, maarifa na ujasiri mkubwa na wasiwe na mashaka kunitwisha tena mzigo wa kuwatumikia. Wahenga walisema mzigo mzito mtwishe mnyamwezi na mimi Luhaga Joelson Mpina, kijana wenu wana Kisesa bado niko tayari na timamu kuwa ‘mnyamwezi’ wenu ili niendelee kuwatumikia kwa hiyo nawaomba wananchi wa Kisesa kwenye kumbukumbu zenu muendelee kubakia na jina la Luhaga Joelson Mpina.

Mheshimiwa Spika, wananchi wangu watakumbuka kuwa walinichagua nikiwa bado kijana mdogo hadi sasa sijawahi kuwaangusha, JEMBE LIPO SHAMBANI, muda ukifika niwahisheni ili tuendelee kuyasaka maendeleo ya Jimbo letu kwa udi na uvumba, tumepania na hakunakurudi nyuma.

MUHTASARI WA MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara inaomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya jumla ya shilingi 66,817,518,000 Kati ya fedha hizo, shilingi 32,096,197,000 kwa ajili ya Sekta ya Mifugo na shilingi 34,721,321,000 kwa ajili ya Sekta ya Uvuvi. Mchanganuo wa fedha zinazoombwa kwa kila Fungu  ni kama ifuatavyo: Fungu 99: SektayaMifugo 

Mheshimiwa Spika, Wizara inaomba kutumia jumla ya shilingi 32,096,197,000 kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Sekta ya Mifugo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 27,034,826,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 5,061,371,000ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Mgawanyo wake ni kama ifuatavyo:

(i) Fedha za Matumizi ya Kawaida shilingi 27,034,826,000  Mishahara shilingi 17,130,715,000  Matumizi Mengine (OC) shilingi 9,904,111,000 

(ii) Fedha za Matumizi ya Maendeleo shilingi 5,061,371,000  Fedha za Ndani,shilingi5,061,371,000;na  Fedha za Nje shilingi -Hakuna. 

Sekta ya Uvuvi 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Wizara inaomba jumla ya shilingi 34,721,321,000 kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Sekta ya Uvuvi. Kati ya fedha hizo, shilingi 21,662,107,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 13,059,214,000 ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Mgawanyiko wake ni kama ifuatavyo:

(i) Fedha za Matumizi ya Kawaida shilingi 21,662,107,000.00  Mishahara: Shilingi12,031,696,000.00; na  Matumizi Mengine (OC): Shilingi 9,630,411,000.00. 

(ii)Fedha za Matumizi ya Maendeleo shilingi 13,059,214,000  Fedha za Ndani: Shilingi5,976,856,000.00, na  Fedhaza Nje :Shilingi 7,082,358,000.00

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwako na kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza. Hotuba hii pia inapatikana katika Tovuti ya Wizara: www.mifugouvuvi.go.tz.

Mheshimiwa Spika,naomba kutoa hoja.

Post a Comment

0 Comments