Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC
kwa kushirikiana na Serikali Mkoani Mtwara wanaangalia uwezekano wa kumhamishia
eneo lingine mwekezaji wa kampuni ya Sukari ya SJ Limited ya India kufuatia
aneo la awali alilokuwa akifanyia shughuli zake kukumbwa na mafuriko ya maji ya
Mto Ruvuma kwa asilimia 90 kwa muda wa miaezi miwili mpaka sasa.
Anaripoti Grace Semfuko
Eneo la Kilambo mpakani mwa
Tanzania na msumbiji ndipo Mwekezaji huyo alipewa kwa ajili ya kilimo cha miwa
na ujenzi wa kiwanda cha sukari, ambapo kwa sasa eneo hilo limeonekana kuwa na
dosari ya mafuriko na hivyo kuwalazimu watendaji hao wa Serikali kuangalia eneo
mbadala.
Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe akifafanua jambo wakati akikagua eneo la uwekezaji la Ludipe lenye zaidi ya ekari elf kumi, eneo hili ni shamba la ufugaji na linamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha
uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe amefanya ziara ya ghafla Mkoani
Mtwara ya kukagua athari za mafuriko ya Mto Ruvuma zilizolikumba eneo hilo
lenye zaidi ya ekari 3,000 zilizotengwa kwa ajili ya kilimo cha miwa na ujenzi
wa kiwanda cha Sukari ambapo ekari 500 zilikuwa zimeanza kazi kwa kuoteshwa
vitalu vyenye miche laki tatu ambazo zote zimesombwa na maji.
Akizungumza Mkoani hapa Mwambe
amesema ipo haja kwa mwekezaji huyu kutafutiwa eneo mbadala la kufanyia
uzalishaji kutokana na eneo la sasa kukumbwa na mafuriko hayo na hivyo kuathiri
shughuli za uzalishaji.
Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe akikagua eneo mbadala la uwekezaji ambalo linatakiwa kupewa Mwekezaji wa Kampuni ya sukari ya SJ ili aendelee na uzalishaji baada ya eneo la awali la Kilambo ambalo walianza uzalishaji kuingiwa na mafuriko ya mto Ruvuma
“Nimefanya ziara ya ghafla Mkoani
hapa ili kuangalia athari za mafuriko haya, nilipata barua na taarifa kutoka
kwa mwekezaji wa SJ Sugar Private Limited ya India pamoja na Halmashauri ya
Mtwara, huu ni uwekezaji wa kilimo cha miwa na kuweka kiwanda cha sukari
ambacho kitakuwa ni cha kwanza cha uzalishaji wa sukari kwenye ukanda wa
kusini, tuliwaleta Mtwara wakapewa eneo Kilambo sasa kwa bahati mbaya mwaka huu
wakapata mafuriko” alisema Mwambe.
“Karibu 90% ya eneo zima
lilifunikwa na maji kwa muda wa miezi miwili, miche yote waliyoipanda imekufa,
hivyo kutokana na uharibifu huo wanahofia kwa miaka mingine ijayo kiwanda
kitakachojengwa kinaweza kuathiriwa na mafuriko, sasa wameomba eneo lingine,
tuliwasiliana na Halmashauri ya Wilaya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na Mkuu
wa Wilaya ya Mtwara,kwa hiyo nikaona nije kushauriana ili kuona namna ya
kumpatia eneo lingine, na kwa bahati nzuri maeneo yapo” alisema Mwambe.
Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe akikagua eneo mbadala la uwekezaji ambalo linatakiwa kupewa Mwekezaji wa Kampuni ya sukari ya SJ ili aendelee na uzalishaji baada ya eneo la awali la Kilambo ambalo walianza uzalishaji kuingiwa na mafuriko ya mto Ruvuma
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw. Evod
Mmanda amesema eneo kwa ajili ya uwezezaji huo lipo na wanaangalia utaratibu wa
kuhamisha shughuli hizo.
“huu ni uwekezaji mkubwa hapa
Mkoani kwetu na kwenye Wilaya yangu, tunaangalia taratibu za kumhamisha
mwekezaji huyu ili aweze kufanya shughuli zake, zaidi ya wakazi 1,500 watapata
ajira hapa na tutaongeza kiwango cha uchumi” alisema Mmanda.
Athari za mafuriko hayo
zimesababisha zaidi ya wananchi 150 kukosa ajira.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Sukari ya SJ akimwonyesha jambo kwenye simu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe katika eneo la Kilambo lililoathiriwa na mafuriko ya mto Ruvuma
Wawekezaji hao wa kampuni ya SJ
Limited wanakusudia kujenga Kiwanda cha Sukari Mkoani Mtwara kitakachozalisha
tani 10,000 kwa mwaka ambapo walianza kupanda miwa kwa ajili ya uzalishaji wa
bidhaa hiyo hatua ilitofanya TIC pamoja na Serikali kuangalia eneo mbadala la
kuwahamishia wawekezaji hao ili waweze kufanya shughuli zao.
Kwa mwaka 2019 mahitaji ya sukari
ni tani 620 na uzalishaji ni tani 320 hatua ambayo inapelekea upungufu wa tani
laki tatu hivyo uzalishaji wa tani elf kumi za sukari utasaidia kupunguza nakisi
hiyo.
Mwisho.
0 Comments