Na Grace Semfuko.
Ripoti ya utafiti wa Benki ya Dunia ya Doing Business
2020 imetoa matokeo ya tathimini ya mazingira ya uwekezaji duniani kwa
nchi 190 na kuonesha Tanzania kupanda na kufikia nafasi tatu ambapo sasa ipo
nafasi ya 141 mwaka 2019 ikilinganishwa na nafasi ya 144 kwa mwaka 2018.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Mamlaka ya Rufaa za
Manunuzi ya Umma kuboresha mifumo ya utoaji huduma ambapo maamuzi ya utoaji wa
tenda yanafanyika kwa siku 18, na ugawaji wa tenda ni ndani ya siku 41.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha
Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe Jijini Dar Es Salaam wakati
akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na maendeleo ya uwekezaji Nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maendeleo ya sekta ya uwekezaji katika ukumbi wa kituo hicho Oktoba 28,2019. (Picha na Grace Semfuko)
“Sasa hivi tumepanda na kuwa nafasi ya 141 kutoka
nafasi ya 144, hii ni hatua kubwa, nah ii imetokana na hatua ya Serikali ya
awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli ya kuimarisha mazingira ya
uwekezaji”
Aidha Mwambe alibainisha kuwa ripoti ya Utafiti wa Taasisi ya usimamizi
na uwekezaji wa kifedha Afrika ABSA imetoa orodha mpya ya mwezi Oktoba, 2019 ya masoko ya uwekezaji na kuonesha Tanzania
ipo nafasi ya saba ikilinganishwa na mwaka 2018 ilipokuwa kwenye nafasi ya 15
kati ya nchi 20 za Afrika zenye mazingira mazuri ya uwekezaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (Hawapo Pichani) kuhusu maendeleo ya sekta ya uwekezaji katika ukumbi wa kituo hicho Oktoba 28,2019. (Picha na Grace Semfuko)
“Uzoefu wa ‘Absa Group’ katika mambo ya Fedha na Uwekezaji na matokeo
ya utafiti wake, yanatudhihirishia kuwa juhudi zinazofanya na serikali za
kuboresha mazingira ya uwekezaji zinaifanya Tanzania kuwa kivutio bora cha uwekezaji
kwenye bara la Afrika” alisema Mwambe.
Alibainisha kuwa tafiti kubwa za kimataifa zinaonyesha mazingira na hali
ya uwekezaji nchini itaendelea kuimarika huku akitolea mfano uchumi wa Tanzania
kuendelea kukua kwa kasi kubwa ya asilimia 7.0 kwa miaka minne mfululizo, ambapo
kwa sasa nchi inashika nafasi ya tano kati ya Mataifa 10 Duniani yenye uchumi
unaokua kwa kasi kutokana na hatua za makusudi
zinazochukuliwa na serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kukuza
sekta binafsi ambayo ni injini ya ukuaji wa uchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe akisikiliza maswali kutoka kwa Waandishi wa Habari waliotaka kufahamu maendeleo ya sekta ya uwekezaji katika ukumbi wa kituo hicho Oktoba 28,2019. (Picha na Grace Semfuko)
Akizungumzia taarifa
ya miradi iliyosajiliwa na kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC kuanzia January
hadi Septemba 2019, Mwambe alisema jumla ya miradi 227 yenye thamani ya Zaidi
ya Dola za Marekani Bil.2 imesajiliwa miradi ambayo imetoa ajira kwa watanzania
38,816 huku Sekta ya Viwanda ikiongoza kwa kusajiri miradi 128 ikifuatiwa na
usafirishaji yenye miradi 29 na sekta ya huduma za kijamii ikiwa na miradi 18.
Aidha
ameendelea kuwashauri Wawekezaji Duniani kuja kuwekeza nchini Tanzania kutokana
na uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji na usalama na
kufafanua kuwa Serikali inaendelea na
maboresha ya miundombinu ya kufanikisha uwekezaji ikiwemo usafiri wa barabara,
anga, reli, nishati, upatikanaji wa maji safi na salama, maeneo ya uwekezaji na
maboresho ya Huduma za Mahala Pamoja kwa wawekezaji kupitia ofisi ya TIC.
Mwisho.
0 Comments