Kongamano la Uwekezaji
limemalizika Mkoani Songwe, Kongamano hilo lilikuwa na mafanikio makubwa
kutokana na mwamko wa wawekezaji kushiriki katika Kongamano hilo lililokuwa na
lengo la kuwaweka karibu wafanyabiashara na wawekezaji wa Mkoa huo pamoja na
wafanyabiashara wa mikoa na mataifa mbalimbali Duniani.
Anaripoti Grace Semfuko aliehudhuria Kongamano hilo.
Kongamano hilo lililoandaliwa na
Serikali ya Mkoa wa Songwe kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo
limeleta chachu ya kuimarisha uwekezaji nchini hatua ambayo imefikiwa kufuatia
juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli za
kuimarisha sekta ya viwanda na uwekezani nchini.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC
ni miongoni mwa Taasisi za Serikali zilizokuwa na nguvu katika kongamano hilo
kutokana na ushiriki wake ikiwa ni sehemu ya kazi zake za kila siku za
kuhakikisha uwekezaji Nchini Tanzania unakua kwa kiwango cha hali ya juu.
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ya
TIC ndio ilikuwa mwenyeji katika Kongamano hilo ambapo Meneja wake wa Kanda Bw. Venance Mashiba alisema Kanda hiyo inazo fursa nyingi za uwekezaji ikiwepo kwenye Kilimo,
viwanda, Ujenzi na sekta nyingine nyingi ambapo hatua ya sasa ya TIC ni
kuhakikisha wawekezaji wanapata elimu kuhusiana na kujiunga na Kituo hicho ili
waweze kupata manufaa mengi ikiwepo vivutio vya kikodi.
“Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini
imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi sana, miongoni mwa rasilimali hizo ni
pamoja na sekta ya kilimo, mfano kilimo cha Parachichi, Mahindi na mazao
mengine, hii ni fursa yetu kubwa kwenye mikoa hii, nashauri wawekezaji wajiunge
na kituo ili waweke kupata fursa nyingi” alisema Mashiba.
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
inajumuisha Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Rukwa ambapo kwa rasilimali,
mikoa hii imebarikiwa kuwa na rasilimali za asili ikiwepo Madini mbalimbali,
hali nzuri ya hewa kwa ajili ya kilimo, uvuvi pamoja na maeneo makubwa ya uwekezaji
ambapo wawekezaji kutoka katika mataifa mbalimbali Duniani wanashauriwa
kuwekeza kwenye mikoa hiyo.
Fursa nyingine za uwekezaji
zilizopo kwenye mikoa hiyo ni pamoja na uwekezaji wa viwanda vya madawa na
vifaa tiba pamoja na mafuta ya kipikia.
Aidha Mashiba aliyataja maeneo
mengine ya uwekezaji kuwa ni kwenye uzalishaji wa zao la Kokoa ambapo Tanzania
pekee inazalisha zaidi ya tani elf 10 za Kokoa huku maeneo ya Kyela yakiongoza.
“Kama mnavyofahamu Serikali ya
awamu ya tano inasisitiza uwekezaji kwenye viwanda ili kuweza kusaidia
maendeleo ya viwanda katika nchi yetu, na sisi TIC jukumu letu ni kuhakikisha
tunatekeleza uhamasishaji na ufanikishaji wa ujenzi wa viwanda unaofanywa na
wawekezaji wetu, tumejipanga kwa jambo hilo” alisema Mashiba.
Alisema kuwa eneo la kwanza ni
kuahamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata na kusindika mahindi. “ukiangalia
maeneo ya Songwe, Mbeya, iringa na Rukwa ni mikoa ambayo inaongoza katika uzalishaji
wa zao la mahindi”.
“TIC Nyanda za juu kusini
inahamasisha uwekezaji wa viwanda vya kuchakata na kusindika mpunga, Wilaya ya Kyela
pekee inazalisha tani elf 70 kwa mwaka huku Wilaya ya Mbarali ikizalisha tani
laki 7, Songwe na Kamsamba yakizalisha mpunga kwa kiasi kikubwa sana, kwa hiyo
uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mpunga vitasaidia ongezeko la uwekezaji
katika mikoa ya Kanda hiyo”alisema Mashiba.
0 Comments