Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimepokea ujumbe wa timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo, Maji na Mazingira ya Saudi Arabia ukiongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Jabil Mwadini.
Wataalamu hao wamefika kuangalia mazingira na taratibu za usafirishaji wa mifugo hai ili kujiridhisha watakapoanza kufanya uwekezaji huo baada ya Tanzania kupewa kibali cha kuingiza mifugo hai katika soko la Saudi Arabia.
Balozi wa Tanzania Nchini Saudi Arabia, Mhe. Ali Mwadini, amewasihi wageni hao kufungua fursa katika kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwemo mifugo.
“Tumepata kibali cha kusafirisha nyama pamoja na mifugo hai, hivyo ujio wa ujumbe huu ni fursa kwetu katika kuimarisha uchumi wetu kupitia sekta ya mifugo.” Amesema Mhe. Mwadini.
Kaimu Mkurugenzi Uhamasishaji Uwekezaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Ndg. Revocatus Rasheli ameukaribisha ujumbe huo na kufanya kikao kilichoshirikisha Taasisi za Serikali pamoja na Sekta Binafsi. Mkutano huo umefanyika leo tarehe 11 Agosti, 2022 kwenye ofisi za TIC Makao Makuu.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi huyo alisema, ujumbe huu umefika Tanzania kufuatia Ziara ya Mhe. Liberata Mulamula, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mwezi Machi 2022 alipokutana na Uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maji na Mazingira ya Saudi Arabia waliafikiana kuwa timu ya Wataalamu kutoka Wizara hiyo pamoja na Taasisi zilizopo chini yake watembelee Tanzania kuangalia maeneo ya uwekezaji na ushirikiano.
“Mpaka hivi sasa, nchi ya Saudi Arabia imeweza kuwekeza nchini Tanzania miradi 13 kwa kiwango cha mtaji wa dola milioni 55.2, hivyo uwekezaji wao utaweza kuzalisha ajira nchini.” Amesema Revocatus.
Aidha, wataalamu hao wataangalia fursa za uwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi na namna ya kushirikiana katika sekta ya wanyama pori.
Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (MFA-EAC), Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi Zanzibar (MOBEF), Wizara ya Mifugo na Uvuvi (MOLF), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori (TAWA), Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB), Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Kampuni ya Ranchi Tanzania (NARCO LTD), Mpango wa Kukuza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), OILCOM LTD pamoja na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
0 Comments