Katika
jitihada za kutafuta/kuhamasisha na kuvutia wawekezaji nchini, Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Bw. Geoffrey Mwambe yupo nchini
Uholanzi ambapo amepokelewa na Mwenyeji wake Mhe. Irene Kasyanju Balozi wa
Tanznaia Uholanzi kwa lengo la kufanya ziara ya kikazi itakayochukua takribani
siku tano kuanzia tarehe 4 Februari, 2019. Akiwa na Mhe. Balozi, Mwambe
atakutana na uongozi wa makampuni makubwa yenye nia ya kuwekeza Tanzania na
kufanya nao mazungumzo ya kimkakati yenye lengo la kuwavutia kuja kuwekeza
Tanzania kwenye sekta za kipaumbele.
Katika hatua za awali,
Mkurugenzi Mtendaji pamoja na Mhe. Balozi wamefanya mazungumzo na Bw. Kees
Blokland Mkurugenzi wa Biashara aliyeambatana na maafisa wengine wawili kutoka
kampuni ya Trade and Development Holding B.V. (TDH). TDH ni kampuni kubwa na
maarufu nchini Uholanzi inayojihusisha na biashara ya korosho duniani. Kampuni
hii imewahi kufanya biashara ya korosho nchini Tanzania na sasa imefanya
uwekezaji kwenye viwanda vya korosho nchini Burkina Faso na Benin.
Kwa kuzingatia hayo, Mkurugenzi
Mtendaji amefanya mazungumzo na uongozi wa kampuni hiyo ili kuwakaribisha kwa
mara nyingine kufikiria kuja Tanzania kwa ajili ya kuwekeza katika zao la
korosho. Mkurugenzi wa TDH amesema anatambua ubora wa korosho kutoka Tanzania
na mazingira ya uwekezaji yaliyopo kwa sasa. Kwa niaba ya kampuni hiyo
ameonesha utayari wa kurejea nchini kwa ajili ya kuwekeza katika zao la korosha
hususan kujenga kiwanda cha kubangua korosho. Katika hatua za awali, kampuni
hii itawasilisha andiko mradi (Business
Proposal) likielezea nia ya kujenga kiwanda cha korosho nchini. Hata hivyo
jambo litafanyika baada ya kampuni ya TDH kukamilisha majadiliano na Taasisi za
kifedha nchini Uholanzi ‘The Netherlands
Development Finance Company’ (FMO).
Ujio
wa kampuni hiyo utakuwa wa manufaa kwa Taifa kwani utaleta mabadiliko chanya
katika zao la korosho kwa kuwa kiungo cha kuongeza chachu kwenye mnyororo wa thamani
wa zao hilo la biashara.
0 Comments