Kampuni
ya Kuunda Mabasi ya Abiria yaanzishwa Kibaha
Na Grace Semfuko, Kibaha.
Kampuni
ya BM Motors iliyopo Kibaha mkoani Pwani, imeingia kwenye orodha ya kampuni
zinazounda na kutengeneza mabasi ya abiria hapa nchini.
Mkurugenzi
wa Kampuni hiyo Bw. Jonas Nyagawa amesema, karakana hiyo iliyojengwa eneo la
Zegereni katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani inatengeneza mabasi yenye
uwezo wa kubeba abiria kati ya 45 hadi 57.
Akiongea
na Maafisa Habari kutoka Idara ya Habari – MAELEZO, amesema, kutoka na na msukumo
wa mazingira wezeshi ya Serikali katika kuunga mkono Sera ya viwanda nchini,
ameweza kufanikisha ndoto yake ya kuanzisha karakana hiyo miezi sita iliyopita.
Amesema,
ni fursa pekee katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Tano inahamasisha
Wananchi kuanzisha viwanda nchini ili kujenga uchumi wa nchi na kuongeza ajira kwa
vijana.
“Serikali
imekuwa ikisisitiza uanzishaji wa viwanda ili nchi yetu ifikie uchumi wa kati na
Wananchi waweze kuwa na kipato cha kati. Ili kufikia azma hiyo lazima kujengwe viwanda
vingi na wananchi nao wapate ajira.”
Bwana
Nyagawa amesema, vifaa vinavyotumika kuunda mabasi hayo vinatoka sehemu mbalimbali,
huku asilimia 55 vikitoka nje ya nchi.
Tangu
karakana hiyo ianze kufanya kazi tayari mabasi mawili yameshaundwa na yako katika
hatua za mwisho za usajili ili kuanza kufanya kazi.
“Kila
kitu kinawezekana, Watanzania wanapaswa kuwa na uthubutu. Karakana hii inaunda mabasi
na sio kwamba vifaa vyote vinatoka nje ya nchi, vingine vinapatikana hapa hapa nchini.”
Amesema.
Kufuatia
uanzishwaji wa kampuni hiyo, hadi sasa imetoa ajira kwa Watanzania 15 huku baadhi
yao wakiongeza ujuzi kutoka kwa Wataalamu wa nje ya nchi wanaofanya kazi na kampuni
hiyo.
Frank
Ngewe ambaye ni fundi mkuu wa karakana hiyo amesema, ujenzi wa karakana hiyo umekuwa
mkombozi mkubwa kwa vijana hususani wale waliopata mafunzo ya uchomeleaji vyuma,
umeme, rangi n.k.
“Kwanza
tunamshukuru Rais wetu na Serikali kwa ujumla kwa kukazania Sera ya Tanzania ya
Viwanda. Watanzania wengi hususan vijana hivi sasa wanapata ajira na kujikwamua
kimaisha kutokana na kuanzishwa kwa viwanda nchini. ”Amefafanua zaidi Bw.
Ngewe.
Kwa
upande wake Elibariki Maleshe ambaye ni fundi bodi wa mabasi katika karakana hiyo
ameeleza kwamba, vijana wanapaswa kuchangamkia fursa za viwanda ili kupata uzoefu
na kujifunza zaidi vitu vipya.
''Vijana
hasa wanaomaliza masomo ya ufundi wanapaswa kujikita kwenye masuala ya viwanda ili
watakapomaliza masomo yao waweze kupata ajira kwenye viwanda vipya vinavyoanzishwa
nchini.''
Wakati
karakana hiyo ikiwa na miezi sita tu tangu ianze kufanya kazi ya kuunda mabasi,
eneo hilo la Zegereni limetengewa zaidi ya ekari elfu moja kwa ajili ya viwanda
vinavyojihusisha na shughuli mbalimbali ikiwa
ni kuiishi Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya viwanda.
MWISHO
0 Comments