Header Ads Widget

Ticker

6/recent/ticker-posts

Changamkieni Fursa za Uwekezaji wa Alizeti-Kairuki


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki ametoa rai kwa Watanzania kuwekeza katika sekta kilimo cha zao la Alizeti na mafuta ya kula  kutokana na kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa soko lilipo nchini na nje ya nchi.

Ametoa rai hiyo Mei 28, 2020 alipotembelea na kukagua kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula ya Alizeti cha Sunbelt kilichopo katika eneo la Zuzu Jijini Dodoma.

Lengo la ziara hiyo ni kukagua, kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji nchini.

Waziri Kairuki alipongeza uwekezaji wa kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha tani 25 kwa siku.

"Niwapongeze kwa uwekezaji huu mkubwa mlioufanya katika eneo hili tangu mwaka 2015, hii inaleta chachu kwa wawekezaji wazawa kuona fursa ya soko la malighafi wanazozalisha hasa kwenye zao la alizeti" alisema Waziri Kairuki.

Aliongeza kuwa ni vyema Watanzania wakaendelea kuchangamkia fursa ya kilimo cha zao la Alizeti kwa kuzingatia uhitaji mkubwa wa mafuta ya kula nchini, kwani nchi imekuwa ikipoteza Zaidi ya shilingi Bilioni 443 kwa mwaka kutokana na kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi.

Aidha Waziri Kairuki alibainisha kuwa uwekezaji huo ni miongoni mwa fursa muhimu na kuwataka wenye uwezo wa kulima zao hilo kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo kutokana na zao hilo kustawi Zaidi kwenye ukanda huo.

Alitumia fursa hiyo kuendelea kuwasihi wataalamu wa masuala ya kilimo kutoa elimu kwa umma kuhusu kilimo cha zao hilo ili kutumia mbinu za kisasa na zenye kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Akitoa taarifa ya kiwanda hicho Meneja Biashara na maendeleo wa Kiwanda hicho Bw. Krishna Urs alieleza changamoto wanayokabiliana nayo kuwa ni pamoja na uhaba wa malighafi kwa ajili uzalishaji wa mafuta na kuendelea kutoa wito kwa wadau kutumia fursa ya kilimo cha zao la alizeti ili kuendana na mahitaji halisi.

"Ni muhimu kuwekeza Zaidi katika alizeti kwa sababu soko lake lipo, na hii itatatua changamoto ya kuzalisha kwa uchache na kuwafikia wananchi wengi na hatimaye kupata soko katika nchi za nje" alisema Krishna. 
Nae Afisa Viwango wa kiwanda hicho Upendo Mganda alisema uwekezaji huo umesaidia kutoa ajira kwa wananchi wengi wa eneo hilo.

"Tunashukuru uwepo wa KIiwanda hiki kwani kimetusaidia kupata ajira na wazawa wa eneo hili wanatuuzia malighafi na kufaidika na kilimo chao" alisema Mganda.

Alisema kiwanda hicho kimekuwa na tija kubwa kutokana na kuweza kuzalisha tani 25 kwa siku na kinafanya vizuri sokoni kwani mafuta yanayozalishwa hapo hayana kemikali zenye athari kwa watumiaji.

Post a Comment

0 Comments