Na Grace Semfuko,TIC.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji
Angellah Kairuki, amesema ipo haja kwa wawekezaji wa Sekta ya Mafuta na Gesi,
kutoka katika Mataifa mbalimbali Duniani kuona umuhimu wa kuwekeza nchini
Tanzania kwa kuwa kuna sera na mazingira mazuri ya Uwekezaji.
Kairuki alikuwa Mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa, katika ufunguzi wa Kongamano la
tatu la Kimataifa la Mafuta na Gesi lililofanyika Jijini Dar Es Salaam kwenye
ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) Oktoba 2 na 3 mwaka
2019 na kuhudhuriwa na zaidi ya wadau 500 kutoka katika nchi 67 Duniani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki (katikati) akimpa Kitabu cha Wageni Makamu wa Rais Mstaafu Dkt Mohammed Gharib Bilal alipotembelea banda la Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC, wakati wa maonesho ya tatu ya Kimataifa ya Wadau wa Mafuta na Gesi yaliyofanyika Octoba 2 na 3 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC), Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa TIC Bw.Matthew Mnali.
(Picha na Latiffah Kigoda-Afisa Habari TIC, October 2,2019)
"Sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu sehemu ya Uwekezaji
tunasimamia na kuhakikisha mazingira mazuri ya uwekezaji yanakuwepo wakati
wote, wawekezaji wazawa na wageni "hii ni fursa yenu sasa, muwekeze kwenye sekta
ya Mafuta na Gesi ili kama nchi tuweze kupiga hatua Zaidi"alisema Kairuki.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Matthew Mnali alipotembelea banda la kituo hicho wakati wa maonesho ya tatu ya Kimataifa ya Wadau wa Mafuta na Gesi yaliyofanyika Octoba 2 na 3 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC).
(Picha na Latiffah Kigoda-Afisa Habari TIC, October 2,2019)
Aidha alisema Serikali inashirikiana na sekta binafsi katika
kufanikisha mazingira ya uwekezaji nchini na kushauri makundi mbalimbali
wakiwepo Wanawake, kuona fursa za uwekezaji kwenye Mafuta na Gesi, rasilimali
ambazo zina umuhimu na tija
Nae Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani alisema Serikali imeimarisha
na kuweka mazingira wezeshi ya shughuli za utafutaji na uendeshaji wa sekta ya
gesi na mafuta hatua ambayo itaendeleza uchumi wa viwanda na hatimaye kuinua
Maisha ya Watanzania.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki akifafanua jambo kuhusu Uwekezaji kwa Makamu wa Rais Mstaafu Dkt Mohammed Gharib Bilal na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani wakiwa katika Banda la Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC wakati wa maonesho ya tatu ya Kimataifa ya Wadau wa Mafuta na Gesi yaliyofanyika Octoba 2 na 3 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC).
(Picha na Latiffah Kigoda-Afisa Habari TIC, October 2,2019)
Waziri Kalemani alizitaja faida zinazotokana na gesi kuwa
imechangia pato la Taifa ambapo kwa mwaka 2018, pato hilo limeongezeka na
kufikia asilimia 2% kutoka asilimia 0.9% ya mwaka 2017 huku akiongeza kuwa,
ukuaji huo unatokana na matumizi mbalimbali ya rasilimali hiyo, ikiwepo
uanzishwaji wa Viwanda na ajira, Matumizi ya gesi za Magari na
majumbani,kuzalisha umeme na utunzaji wa mazingira.
Waziri Kalemani aliongeza kuwa gesi iliyopo nchini Tanzania ina
ujazo wa Cubic Feet 57.54 kiwango ambacho ni kikubwa na kinahitaji uwekezaji
endelevu ikiwepo uzalishaji wa umeme na hivyo wawekezaji waione fursa hiyo.
Mwisho.

0 Comments