Na Grace Semfuko, Dar Es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki amefanya ziara kwenye kiwanda cha kutengeneza Soda cha Pepsi cha SBC Dar es Salaam. Ziara hiyo ilikuwa na mlengo wa kukagua na kuangalia ufanisi wa kiwanda sambamba na changamoto wanazokabiliana nazo katika uwekezaji wao mchini. Mpaka sasa kiwanda kimewekeza mtaji wa Dola za Kimarekani zaidi ya Milioni 373.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki akikagua Soda aina ya Pepsi mara baada ya kuwasili kiwandani hapo na kukagua shughuli za uzalishaji wa kiwanda ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kawaida ya kikazi Desemba 16,2019.(Picha na Grace Semfuko)
Kiwanda hicho kinachoendeshwa na SBC kwa miaka 18 sasa, kina jumla ya wafanyakazi wa kudumu 1,215 na wa mkataba maalum zaidi ya 2,000, kimelipa kodi ya jumla ya shilingi Bilioni 416 za kitanzania ambapo kwa mwaka 2018 pekee kiwanda hicho kimelipa kodi ya shilingi Bilioni 46.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho ambacho kimesajiliwa na kupata huduma za Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC tangu mwaka 2012, Waziri Kairuki amewapongeza kwa ufanisi na uendeshaji wa uwekezaji wao kupitia TIC kwa kuwa imekuwa msaada mkubwa katika changamoto za hapa na pale. Kwa kizingatia hilo, amewataka wawekezaji wengine pia kusajiliwa kwenye Kituo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki angalia Vibandiko vyenye majina ya bidhaa za Soda zinazozalishwa na Kampuni ya Pepsi mara baada ya kuwasili kiwandani hapo na kukagua shughuli za uzalishaji wa kiwanda ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kawaida ya kikazi Desemba 16,2019.(Picha na Grace Semfuko)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiW95bQnP5xU7lfA1y8r4xdto9AWaWLvBXhCUD4vLjdKzEPYXmxYTJrb_jAJd4eKX9ZBy63l9NY0Xf7FIw2iB_0hYisTbsZ0jTa7OYLXsTsX4fEpCRcsl2DITH6lsiC4y-Bl-fCnM29LMM/s640/p5.png)
Kipekee kabisa, Waziri Kairuki ameupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuongeza mnyororo wa thamani kutokana na kununua chupa kutoka katika kiwanda cha Kioo Limited.
“Nawapongeza sana kwa kuwa mmeona kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza mnyororo wa thamani, mnanunua chupa zenu kutoka kampuni ya Kioo Limited, ingekuwa kampuni nyingine wangesema chupa watengeneze wao, mabox watengeneze wao, vizibo wao, lakini nyie mmesema hapana, lazima tugawane majukumu kwa kutoa zabuni kwenye bidhaa za vifungashio kwenye kampuni nyingine zinazoendesha uwekezaji nchini” alisema Kairuki.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki akiwa katika kikao cha majadiliano kuhusu uzalishaji wa Kampuni ya SBC inayomiliki kiwanda cha Pepsi Jijini Dar Es Salaam, Kairuki alifanya ziara kiwandani hapo Desemba 16, 2019 (Picha na Grace Semfuko)
Kampuni ya Pepsi kwa mwaka 2001 ilianza kwa kuuza chupa za soda milioni 2.1, kwa sasa wanazalisha na kuuza zaidi ya milioni 37 kwa mwaka kutokana na uzalishaji wa viwanda vinne vilivyopo Mwanza, Mbeya, Dar Es Salaam na Arusha.
Kwa sasa mpango wa kampuni ni kufungua viwanda Mkoani Dodoma ambapo ekari nane za ujenzi wa kiwanda hicho zimepatikana na mazungumzo ya ujenzi yanaendelea.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki akipata maelezo ya uzalishaji wa bidhaa za soda katika kiwanda cha Pepsi kilichopo Jijini Dar Es Salaam Desemba 16,2019 (Picha na Grace Semfuko)
SBC Tanzania ni kampuni iliyosajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC ambapo imejipanga kuhakikisha inatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwepo upatikanaji wa maji wa uhakika kwenye viwanda vyake nchini Tanzania.
0 Comments