Header Ads Widget

Ticker

6/recent/ticker-posts

Wahariri wa Habari washauriwa kuvutia uwekezaji Tanzania

Na Grace Semfuko, Dar Es Salaam.
Wahariri wa vyombo vya habari nchini wameshauriwa kusimamia na kuandika habari za kuvutia uwekezaji ili kuongeza kasi ya ujenzi wa viwanda ambavyo vitaajiri Watanzania wengi na kuongeza pato la Taifa litokanalo na kodi za Viwandani. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari wakati wa Semina ya kuwajengea uwezo wa kuandika Habari za Uwekezaji, Semina hiyo ilifanyika Ijumaa Desemba 6,2019.

Hatua hiyo itasaidia kukuza sekta ya uwekezaji kwa kuanzisha miradi ya uwekezaji hatua ambayo inatajwa kuwa kichocheo cha kuongeza pato na kukuza uchumi wa Taifa. Aidha, uwekezaji huo pia utasaidia kuongeza ajira kwa wananchi na kuondokana na utegemezi kwa baadhi ya vijana/wananchi ambao wengi ni nguvu kazi ya Taifa. 


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe wakati akifungua Semina ya siku moja ya Wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyokuwa na lengo la kuwapa elimu na kuwajengea uwezo na uelewa mpana juu ya uwekezaji na  namna ya kuandika habari za kuvutia uwekezaji.

 Baadhi ya Wahariri wa Vyombo vya Habari Nchini wakifuatilia kwa makini Mada ya Uwekezaji iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw.Geoffrey Mwambe, Semina hiyo ilifanyika Ijumaa Desemba 6,2019.

“Suala la kutoa habari za kunadi fursa za uwekezaji nchini ni jukumu la TIC, hata hivyo ili kulifanikisha inashirikiana na wadau mkiwepo Wahariri wa vyombo vya habari na Waandishi wa habari,” alisema Mwambe

Akiendelea na hotuba yake,  Mwambe alisema suala la uwekezaji Duniani ni la ushindani kwa kuwa nchi mbalimbali zikiwepo pia zilizoendelea zinaangalia wawekezaji hao hao. Hivyo, kama timu tunatakiwa kufahamu kuwa jukumu la kuvutia na kuhamasisha uwekezaji linatakiwa lifanywe kwa weledi wa hali ya juu.

Wahariri kama wadau wakubwa wa kuhamaisha na kuvutia uwekezaji nchini, kabla ya kuruhusu habari yeyote ya masuala ya uwekezaji kwenda hewani, ni vema mkajiweka kwenye nafasi ya Utanzania huku akiongeza kuwa wajibu wa Mtanzania yeyote bila kujali sehemu aliyopo ni kuweka uzalendo na maslahi ya nchi mbele ikiwa ni pamoja na kuitangaza ama kuinenea nchi mema. 

 Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw.Geoffrey Mwambe akisisitiza jambo kwa Wahariri wa vyombo vya Habari kuhusu kuandika fursa za kuvutia Uwekezaji,  Semina hiyo ilifanyika Ijumaa Desemba 6,2019.


Akiyataja mema hayo Mwambe amesema kuwa ni pamoja na kunadi fursa za uwekezaji na maliasili zilizopo Tanzania, kukaribisha wawekezaji, kueleza faida za uwekezaji, na namna wawekezaji wanavyosaidiwa na Serikali kuanzisha miradi nchini.

Mwambe alihitimisha kwa kuwaomba Wahariri hao kupuuza kuandika habari za baadhi ya Taasisi, Mamlaka ama mtu yeyote atakayejaribu kubeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuvutia na kuhamasisha wawekezaji kwa maslahi binafsi ama kwa lengo la kuchafua nchi na kukatisha tamaa wawekezaji.

Naye mwakilishi wa Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Elias Malima alisema nchi ipo katika vita ya uchumi, na kuwataka Wahariri kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. John Pombe Magufuli zenye mlengo wa kuipaisha Tanzania kiuchumi na kuongeza kuwa Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali haitasita kukichukulia hatua chombo cha Habari kitakachopotosha masuala ya uwekezaji.



“Uwekezaji ni suala la nchi Wahariri kama sehemu ya wadau tuna wajibu wa kuwa wazalendo kwa kuisemea nchi na endapo atatokea mtu anachezea uwekezaji tupambae nae” alisema Malima.

Miongoni mwa mada zilizowasilishwa ni chanzo cha TIC, Mamlaka ya TIC, Urasimu unavyokwamisha Uwekezaji na Wajibu wa Wanahabari kuandika na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania. Nyingine ni mchango wa tafiti mbalimbali kwenye Uwekezaji na nafasi ya Tanzania kwenye Uwekezaji Duniani; Fursa, Vivutio na Changamoto za Uwekezaji nchini Tanzania; 

 Huduma zinazotolewa ndani ya Mfumo wa Mahala Pamoja katika kufanikisha Uwekezaji. Sheria ya Uwekezaji na Huduma za kitaasisi kwa Wawekezaji; Mradi wa e-regulation unavyosaidia wawekezaji na Jukumu la vyombo vya Habari katika kuhamasisha na kuvutia uwekezaji.

Post a Comment

0 Comments