Header Ads Widget

Ticker

6/recent/ticker-posts

TIC Nyanda za Juu Kusini yajipanga kuhakikisha Wawekezaji wanajisajili


Na Grace Semfuko, Songwe.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC kimejipanga kuhakikisha wawekezaji wote wanajisajili kwenye kituo hicho ili kupata fursa na taarifa mbalimbali za uwekezaji, kisheria na msaada wa huduma za kikodi sambamba na kupata cheti.

Hayo yalisemwa Mkoani Songwe kwenye Kongamano la siku tatu la uwekezaji lililofanyika kwenye viwanja vya michezo vya CCM katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na Mratibu wa Idara ya Huduma za Uwekezaji wa TIC Bw. Aboubakar Ndwata na kuongeza kuwa kuna faida nyingi kwa wawekezaji kujisajili kwenye kituo hicho.

“TIC ni chombo pekee cha kuratibu uwekezaji hapa nchini hivyo tunayo kazi kubwa kuhakikisha elimu inawafikia wawekezaji wa ndani, wan je na wananchi kwa ujumla kuhusiana na mazingira ya uwekezaji na faida watakazozipata wanapojisajili TIC” alisema Bw. Ndwata.

Alisema katika Mkoa wa Songwe TIC itajikita zaidi kuwaelimisha wananchi pamoja na wawekezaji juu ya mazingira ya uwekezaji hapa nchini na umuhimu wa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu  za uwekezaji.

Ndwata alisema Kongamano la uwekezaji Mkoani Songwe lilikuwa na umuhimu mkubwa katika kutangaza vivutio mbalimbali vya uwekezaji vilivyopo mkoani humo kwenye sekta mbalimbali muhimu za kiuchumi na kijamii.

“TIC kushirikiana na Mkoa wa Songwe pamoja na wadau wengine kutoka sekta binafsi tulihakikisha tunawakutanisha wawekezaji wakubwa pamoja na wajasiriamali wadogo na wananchi wa Songwe na mikoa ya karibu” alisema.

Ndwata alisema kuwa lengo ni kutangaza vivutio vya uwekezaji na fursa zilizopo katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

Alisema Mkoa wa Songwe unao utajiri mkubwa kwa fursa za kiuwekezaji na hivyo TIC kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa na wadau wa sekta binafsi wataweza kuzitangaza fursa hizo.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Generali Mstaafu Nicodemus Mwangela aliwashukuru wawekezaji na wafanyabiashara walioshiriki katika Kongamano hilo.


Post a Comment

0 Comments