Na Grace Semfuko, Dar Es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua nafasi na michango wa Mwanamke katika Jamii na ujenzi wa Taifa, na kwamba inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha uwepo wa fursa sawa za ushiriki wa Mwanamke katika shighuli zote za maendeleo.
Waziri Kairuki ameyasema hayo Machi 6 wakati akifungua kongamano la siku ya Wanawake Duniani kwenye chuo kikuu cha Dar Es Salaam lililoandaliwa na Taasisi ya Taaluma za Jinsia ya Chuo hicho lililofanyika kwenye ukumbu wa Nkrumah Jijini Dar Es Salaam.
Kairuki amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha usawa wa kijinsia katika kumwinua Mwanamke kiuchumi, zikiwepo za kisheria na kisera.
Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuandaa na kutekeleza mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto uliozinduliwa mwaka 2016, ambao pamoja na mambo mengine unahimiza jamii kuachana na mila na desturi ambazo zinachochea ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Aidha Pia Kairuki amesema mwaka 2018 Serikali imefanya marekebisho ya sheria ya fedha kwa kuweka kipengele cha kuzibana Manispaa na Halmashauri za Wilaya kutenga fedha kwa ajili ya kukopesha makundi maalum yakiwepo ya Wanawake, Vijana na Walemavu.
“Tumewezesha marekebisho ya sheria ya fedha ya Serikali za mitaa ambayo yalifanyika mwaka 2018 ambapo sasa kuna sharti la kisheria kwa Halmashauri zetu za Wilaya kuchangia asilimia kumi (10%) ya mapato ya ndani, kwa ajili ya kutoa mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu” alisema Kairuki.
Aliongeza kuwa imetungwa Sera ya Elimu yam waka 2014 ambayo inasisitiza umuhimu wa masuala ya kijisia kwenye elimu ikiwepo masomo ya sayansi na hisabati ambapo pia kwa mwaka 2015, Serikali ya awamu ya tano ilifanya marekebisho ya sheria ya elimu ili kuwalinda wanafunzi wa kike dhidi ya mimba na ndoa za utotoni na kuwapatia fursa Zaidi za kujiendeleza kielimu.
Siku ya Wanawake Duniani hufanyika Machi 8 ya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu wa 2020, nchini Tanzania siku hiyo inaadhimishwa Kitaifa Mkoani Simiyu huku kaulimbiu yake ikiwa ni “Kizazi cha haki na usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu”
Mwisho.
0 Comments