KILIMO
CHA VANILA
Na Grace Semfuko.
Fursa za Uwekezaji kwenye zao la
Vanila nchini Tanzania zipo kwenye Mikoa ya Kagera, Mbeya, Morogoro,
Kilimanjaro na Arusha.
Mkoa wa Kagera kwa asilimia kubwa
hulimwa zaidi Mkoani Kagera.
Zao la
vanilla ni moja ya zao la viungo ambalo asili yake ni Kusini Mashariki ya Mexico
na sehemu nyingine za Amerika ya Kati. Vanilla hulimwa katika nchi mbalimbali
duniani. Nchi zinazolima kwa wingi ni pamoja na Madagascar, Comoro, Tahiti,
Uganda, India na nchi nyingine za Amerika ya Kati.
Mmea wa Vanilla.
Tanzania
ni miongoni mwa nchi zinazolima vanilla katika Afrika. Zao hili lilianza
kuingia nchini kutoka Uganda mnamo mwaka 1954 kupitia kwa mkulima mmoja wa
kijiji cha Kiilima wilaya ya Bukoba Vijijini. Vanilla imeanza kulimwa
kibiashara hasa katika mkoa wa Kagera mwaka wa 1992.
Katika
mkoa wa Kagera, kilimo cha Vanilla kimehamasishwa zaidi na Chama cha Maendeleo
Ya Wakulima kinachofahamika kama MAYAWA. Chama hiki kimekuwa kikihimiza
uzalishaji na usindikaji wa Vanilla ambayo huuzwa kupitia kampuni zilizopo
Uganda.
Mmea wa
Vanilla huzaa maharage (mapodo) ambayo hukaushwa kwa njia maalum inayowezesha
kupatikana kwa Kemikali inayoitwa Vanillini. Kemikali hiyo hutumika
katika kuongeza laadha na harufu nzuri kwenye vyakula na vinywaji mbalimbali.
Pia hutumika katika viwanda vinvyotengeneza Vipodozi na Dawa za matibabu ya
binadamu.
Kwa
matumizi ya kawaida, Vanilla huweza kutumika katika vinywaji kama Chai, Maziwa
na kama kiungo kwenye mapishi ya Vyakula mbalimbali.
Pia zao
hilo hutumika katika viwanda vinavyotengeneza vipodozi na dawa za matibabu ya
binaadam.
Inakadiriwa
vkuwa kilo moja ya vanilla kutoka shambani kwa hapa Tanzania huuzwa kati ya sh
120,000 hadi laki mbili.
Mavuno ya
kwanza ya zao hilo huanza kati ya miaka miwili na nusu hadi mitatu na mmea na
kuzaa kilo moja tu na unapofikia umri wa miaka mine hadi nane mavuno huongezeka
na kufikia kilo tatu hadi tano kwa mmea mmoja.
Mavuno huanza
kupungua mmea unapofikia umri wa miaka 15 na kuendelea.
Inakadiriwa
kuwa hekta moja ya shamba la vanilla lililotunzwa vizuri hutoa mavuno ya tani
tatu hadi tano za mapodo mabichi nah ii ni
sawa na wastani wa kilo 500 hadi 800 za mapodo yaliyokaushwa, hivyo kwa bei ya
hapa nchini mkulima anaweza kujipatia zaidi ya shilingi milioni 60 kwa mwaka.
Kwa mujibu
wa Mtandao wa Food Business News bei ya soko la Dunia ya zao la vanilla Dola za
Marekani 475 hadi 500 sawa na shilingi milioni moja hadi 1.1 za kitanzania kwa
kilo moja.
Maeneo ya
Tanzania yanayoweza kulima zao la vanilla ni pamoja na wilaya za Mbeya
Vijijini, Tukuyu, Morogoro Vijijini, Mvomero, Muheza, Arumeru
na Ukerewe.
UMBILE LA
MMEA NA MAZINGIRA YANAYOFAA
Mmea wa
Vanilla upo katika familia ya Okidi (Orchidaceae) ambayo ina genera zipatazo
700. Kati ya hizo, genera moja itwaayo vanilla ndio yenye umuhimu wa
kiuchumi. Genera ya Vanilla ina aina au jamii zipatazo 110, kati ya hizo
ni mbili ambazo huzalishwa kibiashara. Aina hizo ni Bourbon ya nchini Mexico na
Tahitian ya visiwa vya Tahiti.
Mmea
wa Vanilla ni rando teke linalotambaa ambalo ni la kudumu. Mmea huu hukua na
kutambaa katika mti mwingine hadi kufikia urefu wa mita 10 hadi 15 na zaidi
kutegemea na mazingira.
Mizizi ya zao la Vanilla.
Mizizi
ya mmea huu ni mirefu ina rangi nyeupe, myembamba yenye kipenyo cha milimita
mbili. Mizizi hutokea kwenye fundo la shina lililo ndani ya udongo na hutambaa
sambamba na tabaka la udongo wenye rutuba. Pia hutokea katika vifundo vya shina
sambamba na majani ambayo hujishikiza katika miti ya kuegemea.
Shina.
Shina
la vanilla lina rangi ya kijani, refu lenye vifundo na kipenyo cha sentimeta
moja hadi mbili. Nafasi kati ya fundo na fundo ni sentimita tano (5) hadi 15.
Majani.
Majani
yana rangi ya kijani iliyokolea, yenye umbile la bapa, lenye ncha, nene na
kubwa. Huota kwa kupishana katika shina, yana urefu wa sentimita nane hadi 25
na upana wa sentimita mbili hadi nane, na yana rangi ya kijani iliyokolea.
Maua.
Maua
yana rangi mchanganyiko wa kijani na njano na kipenyo cha sentimita 10. Huota
katika vifungu vyenye maua kati ya 18 hadi 30.
Matunda
Matunda
yana umbile la podo la harage lenye rangi ya kijani likiwa changa. Hubadilika
kuwa rangi ya njano, hatimaye kahawia kadri linavyokomaa. Podo lina urefu wa
sentmeta 10 hadi 25, kipenyo cha sentimeta nane hadi 15 na lina mbegu ndogo
sana ambazo huonekana linapokomaa.
Mmea wa Vanilla.
Mazingira
Yanayofaa katika Uzalishaji wa Zao la Vanilla
Mmea
wa vanilla una asili ya msituni hivyo huhitaji kuoteshwa katika sehemu yenye
kivuli na mvua ya kutosha. Ili zao hili liweze kukua vizuri linahitaji
mazingira yafuatayo:
Mvua
Mmea
wa Vanilla huhitaji kiasi cha mvua cha milimita 1250 hadi 2500 kwa mwaka. Pia
zao hili huhitaji kipindi cha miezi mawili cha ukame ili kuweza kusisisimka na
kutoa vitumba vya maua.
Joto
Zao
hili hustawi vizuri katika maeneo yenye nyuzi joto 20 hadi 30 za Sentigredi.
Pia huweza kustahimili nyuzi joto 32 za Sentigredi. Lakini hukua vizuri
zaidi katika kiwango cha nyuzi joto 27 za Sentigredi.
Mwinuko
Zao
hili hustawi vizuri katika maeneo yenye mwinuko wa mita 0 hadi 600 kutoka usawa
wa bahari. Pia hustawi katika maeneo yenye mwinuko unaofikia mita 1500 katika
nchi za joto (tropiki).
Udongo
Mmea
wa vanilla una mizizi ambayo hutambaa katika sehemu ya juu ya udongo. Hivyo,
huhitaji udongo mwepesi wa tifutifu, wenye rutuba ya kutosha na usiotuamisha
maji.
Mwanga
Mmea
wa vanilla huathirika kwa jua na husababisha kuungua kwa majani, hivyo huhitaji
kivuli cha asilimia 50 hadi 75 ili uweze kukua vizuri. Kivuli kinaweza
kupatikana kwa kupanda miti au kwa kutengenezwa kitaalamu.
UZALISHAJI
WA ZAO LA VANILA
Vanilla
huzalishwa kwa kupandikiza marando moja kwa moja shambani au kwa kukuzwa kwanza
kwenye kitalu na baadaye kupandikizwa shambani. Kabla ya kupanda inatakiwa
kuzingatia yafuatayo:
Uchaguzi wa Shamba
Shamba
la kupanda vanilla inafaa liwe mahali pasipo na upepo mkali ili kuepuka
kuanguka kwa miti ya kuegemea na kukatika kwa mimea. Ni muhimu kupanda miti ya
kuzuia upepo ikiwa mahali hapo pana upepo mkali. Shamba hilo pia liwe na udongo
usiotuamisha maji, mwepesi na ambao unaruhusu mizizi kupenya kwa urahisi.
Aidha,
shamba lisiwe na magugu mabaya (kwa mfano kwekwe/sangare) ambayo hulazimu
kutumia jembe mara kwa mara wakati wa palizi. Kutumia jembe huweza kusababisha
kukatika au kuharibu mizizi na kuhatarisha ukuaji wa mmea.
Utayarishaji wa
Shamba
Utayarishaji
wa shamba huhusisha shughuli mbalimbali kama vile usafishaji wa shamba,
utayarishaji wa mashimo na uwekaji wa mbolea.
Kusafisha Shamba
Shamba
lisafishwe kwa kulima, kungÃoa visiki, magugu mabaya na kutifua hadi kina
kisichopungua sentimita 30.
Kutayarisha Mashimo
Mashimo
yatayarishwe miezi miwili hadi mitatu sambamba na usafishaji wa shamba. Yawe na
kina cha sentimita 30 na upana wa sentimita 60 hadi 90. Nafasi kati ya mstari
na mstari iwe mita mbili na nusu hadi mita tatu na kati ya shimo na shimo iwe
mita moja na nusu hadi mbili. Udongo wa juu utengwe na ule wa chini.
Uwekaji wa Mbolea
Mbolea
za asili kama mboji, vunde au samadi ichanganywe vema na udongo wa juu na
kujazwa kwenye shimo kwa kipimo cha debe moja hadi mbili kwa kila shimo.
Mifumo ya Upandaji
Zao
la vanilla huweza kupandwa shambani kwa kutumia mifumo mikuu mitatu ifuatayo:
(i) Vanilla Pekee
Mfumo
huu unahusisha upandaji wa mmea wa vanilla na miti ya kuegemea tu ambayo hutoa
kivuli kwa mimea.
(ii) Vanilla na Migomba
Mfumo
huu unawezesha kuotesha vanilla katika shamba la migomba, ambapo rando hupandwa pamoja na mti wa kuegemea ndani ya shamba la migomba. Na hivyo kukuwezesha kufanya kilimo cha migomba na vanilla katika shamba moja kwa wakati mmoja
(iii)Vanilla na Miti ya
Kivuli
Katika
mfumo huu vanilla huoteshwa katika shamba la miti ya kivuli, ambapo mmea
hupandwa na miti ya kuegemea katikati ya miti ya kivuli.
Kumbuka: Mfumo wa pili na wa tatu unapendekezwa zaidi
kutokana na matokeo yake mazuri.
Upandaji wa Miti ya
Kuegemea (miega)
Miti
ya kuegemea hupandwa miezi miwili hadi mitatu kabla ya kupanda rando la vanilla
ili iweze kuchipua, kutoa kivuli na kuwa na uwezo wa kuhimili mimea.
(i) Sifa za Miega
Miti
inayofaa kutumika kwa kuegemea iwe na sifa zifuatazo:
·
Uwezo
wa kukua haraka bila kuathiri mmea wa vanilla.
·
Uwezo
wa kutoa kivuli kinachofaa.
·
Uwezo
wa kuchipua haraka inapopunguzwa.
·
Uwezo
wa kuchipua matawi kwa chini ili kupandishia marando kwa urahisi.
·
Uwezekano
wa kuoteshwa kwa urahisi.
Miti
yenye sifa hizo ni pamoja na mibono (Jatropha carcus) na Gilirisidia.
Miti mingine inayoweza kutumika kwa kivuli na kuegemea ni pamoja na Erythrina
spp na Bauhania spp.
(ii) Kupanda Miega ya
Mibono
Miti inayotumika
zaidi katika mashamba ya vanilla ni jamii ya Jatropha. Miti hii huoteshwa kwa
kutumia mbegu au kipande cha tawi kwa umbali wa sentimita 30 kutoka katika
shimo la kupandia vanilla. Tawi la mbono lenye urefu wa sentimita 120 hadi
150 hupandwa katika kina cha sentimita10 hadi 15.
Mmea wa Vanilla uliojishikiza kwenye mti.
Upandaji wa Vanilla
Mmea wa vanilla hupandwa mwanzoni mwa msimu wa mvua ili kuhakikisha upatikanaji wa unyevu ardhini. Hupandwa kwa kutumia rando lenye urefu wa kati ya sentimita 100 hadi 150 (futi tatu na nusu hadi tano) kutoka kwenye mmea unaokuwa vizuri, usio na magonjwa na wenye pingili ndefu. Rando lenye sifa hizo hukua haraka na kutoa maua mapema (miaka 2). Rando fupi halikui haraka na huchukua muda mrefu kutoa maua (miaka 2 hadi 3).
Kutayarisha Marando
· Kata rando kwa kutumia kisu kikali kwa kufuata vipimo (sentimita 100 hadi 150).
· Ondoa majani matatu hadi matano katika sehemu ya chini ya rando itayofukiwa kwenye udongo.
· Ning’iniza rando lililokatwa kwenye kivuli kwa muda wa siku saba hadi 10 kabla ya kupanda ili kupunguza utomvu na kulipa nguvu ya kuchipua na kuhimili hali ya shambani.
Jinsi ya Kupanda
Upandaji wa vanilla hufanywa kwa kutumia hatua zifuatazo:
· Andaa nyasi kavu (matandazo) ambazo zitatumika mara baada ya kupanda.
· Tengeneza kifereji chenye kina cha sentimita 10 hadi 12 katikati ya shimo lenye mbolea lililokwisha tengenezwa.
· Laza sehemu ya rando iliyotolewa majani katika kifereji hicho, acha sehemu yenye majani juu ya ardhi.
· Fukia rando kwenye kifereji kwa udongo na gandamiza taratibu ili lishikamane na udongo.
· Funga sehemu ya juu ya rando kwa kutumia kamba katika umbile la nane kwenye mti wa kuegemea.
· Weka matandazo kuzunguka kila shina lililopandwa.
Kumbuka:
· Utaratibu huu wa kupanda hutumika katika aina zote za mifumo ya kuzalisha vanilla, na hutofautiana kwa nafasi za upandaji kati ya mfumo mmoja na mwingine.
· Shamba la vanilla pekee katika miaka ya mwanzoni, huweza kuchanganywa katikati ya mistari na mazao mengine ya muda mfupi kama mazao ya jamii ya mikunde.
Utunzaji wa Shamba
Vanilla huhitaji kutunzwa vizuri ili iweze kukua vizuri na kutoa mavuno yenye ubora wa hali ya juu. Huduma muhimu katika uzalishaji wa vanilla ni kama ifuatavyo:
Kutengeneza Kivuli
Mmea wa vanilla huhitaji kivuli ili uweze kukua vizuri. Hivyo ni muhimu kupanda miti ya kivuli kabla ya kustawisha vanilla. Katika ukuaji wake kuanzia inapopandwa hadi inapokaribia kutoa maua huhitaji kivuli cha kutosha kinachoweza kuzuia jua kali na kuruhusu mwanga (asilimia 60 hadi 70).
Kipindi cha kusisimua kivuli kipunguzwe zaidi na kufikia asilimia 55 hadi 50. Kivuli kitengenezwe kwa kupunguza matawi ya miti ya miega na ya kivuli ili kupata kivuli kinachofaa.
Kumbuka: Kivuli kizito huathiri ukuaji wa mmea.
Kuweka Matandazo
Utandazaji wa nyasi ni muhimu katika shamba la vanila kutokana na tabia ya ukuaji wa mizizi ambayo huota katika kina cha sentimita 5 hadi 10, hivyo huhitaji kulindwa isiharibiwe. Matandazo yawekwe kuzunguka mashina ya mimea ili kuhifadhi unyevu, kuzuia uotaji wa magugu, na kulinda mizizi isiharibiwe wakati wa palizi.
Kumbuka: Matandazo yawe makavu na yasiwe na mbegu za magugu.
Palizi
Palizi hufanyika wakati wowote magugu yanapoota shambani. Inashauriwa kufanya palizi kabla ya mvua kunyesha ili mmea uweze kutumia maji ya mvua ipasavyo. Palizi ifanyike wakati wowote magugu yanapoota shambani, kwa kungÃoa magugu kutumia mikono ili kuepuka kujeruhi mizizi jembe linapotumika.
Kuning’iniza Marando
Mmea wa vanilla uliokua vizuri huota matawi (marando) mengi na marefu. Marando hayo huelekezwa kwenye matawi ya miti ya kuegemea na kuningÃinizwa. Rando linapofikia urefu wa sentimita 150 hadi 180 liningÃinizwe katika matawi ya miega ili liendelee kukua kuelekea chini. Endapo kuna upepo mkali, marando yafungwe kwenye miega kwa muda ili yasivunjike.
Kulisha Marando
Kulisha marando ni kitendo cha kufukia ardhini sehemu ya kipande cha rando ili kiweze kutoa mizizi na kuongeza nguvu ya kuchukua chakula kutoka kwenye udongo. Kazi hii hufanywa baada ya rando lililoningÃinizwa kurefuka sana kiasi cha kutambaa ardhini, katika hatua hii mmea huweza kuwa na umri wa miezi sita hadi tisa kutegemea na utunzaji.
Jinsi ya Kulisha
· Ondoa majani matatu hadi manne kwenye rando lililoingÃinizwa na kurefuka sana.
· Fukia kwenye udongo, karibu na shina sehemu iliyoondolewa majani.
· Weka matandazo katika sehemu iliyofukiwa ili kuhifadhi unyevu.
· Funga sehemu ya juu ya rando katika mti wa kuegemea ili liendelee kukua.
· Marando mawili hadi mitatu yalishwe kwa wakati mmoja na mengine yaachwe kwa ajili ya kutoa maua na kupata marando ya kupanda.
Kumbuka: Kulisha kufanyike wakati wa mvua ili marando yaweze kutoa mizizi kwa urahisi. Kazi hii irudiwe kila wakati ili rando mama litakapokatika machipukizi yake yaendelea kukua.
Soma kilimo cha tangawizi
Soma kilimo cha tangawizi
Kusisimua
Kusisimua ni kitendo cha kuufanya mmea kuwa katika hali ya kuweza kutoa maua. Kitendo hiki kifanywe wakati mmea ukiwa umefikia umri wa mwaka 1 na nusu au zaidi, na hufanywa wakati wa kiangazi ili kuepuka kupata matawi mengi badala ya vitumba vya maua. Mmea usiosisimuliwa hautoi maua au hutoa maua machache na kusisimua mapema kunaweza kuuchosha mmea.
Jinsi ya Kusisimua
· Chagua matawi matatu hadi matano yanayoningÃinia. Kusisimua matawi mengi kunaweza kuudhoofisha mmea au kuzaa maharage madogo.
· Kata ncha ya rando ili kuwezesha vitumba vya maua kukua na kuwa tayari kufunguka au kutoa maua.
Ukataji wa ncha huweza kufanyika kama ifuatavyo:
· Kukata ncha ndogo (mdomo wa rando) kwa mkono. Hii hufanyika kwa rando fupi linaloningÃnia.
· Kukata rando kwa kisu kikali, kwa rando linaloningÃnia ambalo halijafikia urefu wa kupanda.
· Kukata rando kwa kisu kikali kwa rando refu linaloningÃinia (lenye urefu wa kuweza kupandwa, sentimita100-150).
Uchavushaji
Ni kitendo cha kuunganisha chavua kutoka katika sehemu dume ya ua na kuweka katika sehemu jike ya ua, hufanyika baada ya maua kuchanua.
Uchanuaji wa Maua
Mmea wa Vanilla hutoa maua miezi miwili hadi mitatu baada ya kusisimuliwa. Maua huchanua kwa kipindi cha masaa matatu hadi manne kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana kwa muda wa miezi miwili hadi mitatu kutegemea unyevu uliopo kwenye udongo na kiwango cha Jua.
Ua huchanua kwa muda huo na hudondoka baada ya siku 1 ikiwa halikupata chavua. Hivyo ni muhimu uchavushaji ufanyike kwa haraka na kwa uangalifu mkubwa.
Jinsi ya Kuchavusha
Mmea wa vanilla, ili uweze kutoa matunda inabidi uchavushwe. Ua la vanilla kwa kawaida huchavushwa na nyuki jamii ya melapona ambao hawapo hapa nchini. Nyuki hao hupatikana Mexico na katika nchi nyingine za Amerika ya Kati. Hivyo uchavushaji hufanywa kwa mikono kwani umbile la ua haliruhusu nyuki wa aina nyingine kufanya uchavushaji.
Soma kilimo cha binzari
Soma kilimo cha binzari
Uchavushaji hufanywa kwa kufuata hatua zifuatazo:
· Gawa petali ya ua la vanilla katika sehemu mbili kwa kutumia pini, sindano, au mwiba. Hakikisha vifaa hivyo ni safi.
· Kunjua sehemu jike ya ua (stigima) kwa kuelekea juu ili kuwezesha kulala sambamba kwenye sehemu dume ya ua (stameni).
· Unganisha stameni na stigima na kubana taratibu kwa dole gumba kwa nusu dakika ili kuruhusu chavua kuingia kwenye stigima.
Ua lililochavushwa vizuri, hubaki likiningÃinia kwenye kikonyo chake. Ikiwa uchavushaji haukufanikiwa, ua hudondoka baada ya siku moja au mbili. Kiasi cha maua au mapodo nane hadi 12 yaachwe katika kila kitumba. Aidha vitumba vinne hadi nane viruhusiwe kukua katika kila rando na visizidi 20 kwa mmea.
Ndugu yangu mkulima hivi ndivyo vanilla inavyolimwa, ni shughuri nzito sana lakini inalipa sana, kama ilivyo kawaida: mvumilivu hula mbivu. Sasa badilishana nasi uzoefu wako wa kilimo hiki kwa ku-coment hapa chini huku ukisubiri muendelezo wa kilimo cha vanilla.
Ndugu yangu mkulima hivi ndivyo vanilla inavyolimwa, ni shughuri nzito sana lakini inalipa sana, kama ilivyo kawaida: mvumilivu hula mbivu. Sasa badilishana nasi uzoefu wako wa kilimo hiki kwa ku-coment hapa chini huku ukisubiri muendelezo wa kilimo cha vanilla.
VANILLA MKOANI KAGERA
Uchumi wa Mkoa wa Kagera kwa muda mrefu umekuwa ukitegemea sana mazao ya asili mazao ya biashara kama kahawa, chai, tumbaku, ndizi na sasa miwa. Mazao haya licha ya kuwa na changamoto nyingi za masoko na magonjwa na uwekezaji wake unahitaji gharama kubwa na bado bei ya mazao haya kwa mkulima ni ndogo kulingana na gharama za uzalishaji, Mkoa unaendelea kuhimiza wakulima kuzingatia kanuni za kilimo bora cha kisasa na cha kibiashara katika kuzalisha mazao haya ilikufikia uchumi wa kati na wa viwanda. Aidha, tunahimiza wananchi kuwa namtazamo wa kuzalisha mazao mengine ikiwemo VANILA ili kujiongezea kipato zaidi.
Tunaendelea kuwahamasisha wananchi hasa wakulima kulima kwa wingi zao la Vanilla na kujipatia kipato na mkoa kuwa kinara wa uzalishaji wa Vanila.
Zao hili la vanilla kwasasa linashirikisha wakulima wasiopungua 6,000 kwa Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba Karagwe na Kyerwa. Aidha, inakisiwa kuwa kiasi cha vanilla kinachozalishwa Mkoani hapa kwasasa ni wastani wa tani 15 kwa mwaka, ukilinganisha na uzalishaji wa juu uliowahi kuripotiwa wa tani 105. Bei ya kilo moja ya vanilla kwa msimu uliyopita ilikuwa na wastani wa Tsh. 65,000/= katika Mkoa wa Kagera. Kwa mwaka jana 2017 inakadiriwa zaidi ya Tsh 800,000,000/= (million mia nane) ziliweza kulipwa kwa wakulima kutokana na mauzo ya maharage ya vanilla.
Imeangaliwa na Grace Semfuko kwa hisani ya mitandao.
0 Comments