Header Ads Widget

Ticker

6/recent/ticker-posts

Shehena ya Samaki yasafirishwa Ulaya kutokea Mwanza.

Na Grace Semfuko.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Injinia Isack Kamwelwe amezindua safari za ndege za kusafirisha shehena ya minofu ya samaki kutoka Jijini Mwanza hadi  Brassels Ubelgiji na Uholanzi kupitia Shirika la ndege la Rwanda ambapo mei 12 shirika hilo lilisafirisha tani nane za minofu hiyo ambayo itasafirishwa mara moja kwa wiki.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (wa pili kushoto) akikagua boksi la minofu ya samaki kabla ya kuingizwa kwenye ndege kwa ajili ya kusafirishwa moja kwa moja kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza kwenda Brussels nchini Ubelgiji.

Waziri Kamwelwe amewaagiza Wakuu wa Mikoa ya Mwanza,Mara, Simiyu na Kagera kuunda mtandao wa pamoja wa wa kuhakikisha Samaki wote wanaletwa kwenye kiwanda ili kurahisisha upatokanaji wa minofu hiyo na kufikishwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwanza.

Kamwelwe amesema kwa sasa wameanza na zoezi la usafirishaji wa minofu ya samaki ambapo sasa wanajipanga kusafirisha bidhaa za nyama za ng'ombe na mbuzi ambapo amewataka wavuvi wadogo na wafugaji kuchangamkia fursa hiyo.

Katika hatua nyingine Serikali imepokea injini mbili kutoka Nchini Korea Kusini ambazo zitafungwa kwenye Meli mpya ya MV Mwanza.

Akizungumza Jijini Mwanza Waziri Kamwelwe amesema Meli hiyo inayotengenezewa Jijini humo itakuwa ikifanya safari zake  kwenye Mikoa ya Mwanza-Bukoba na nchi jirani za Kenya na Uganda.
Alisema Meli hiyo inagharimu Shilingi Bilioni 159 na inatarajia kukamilika January 2021 na kuwataka wakandarasi wa Gas Entec Co. Ltd, Kangnam Corporation zote kutoka Korea Kusini zikishirikiana na Suma JKT ya Tanzania kuhakikisha zinakamilisha shughuli hiyo kama mkataba unavyoelekeza.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (wa pili kushoto) akikagua boksi la minofu ya samaki kabla ya kuingizwa kwenye ndege kwa ajili ya kusafirishwa moja kwa moja kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza kwenda Brussels nchini Ubelgiji.

Meli hiyo inayotajwa kuwa ni kubwa kuliko zote katika Ukanda wa Maziwa Makuu, itakuwa na mita 92.6, Kimo chake kitakuwa mita 11.2, upana mita 17 na uzito wa tani 3,500 kwa takwimu hizo ndio itakuwa Meli kubwa kuliko zote na itakuwa inatumia masaa saba kutoka Mwanza hadi Bukoba.

Akitoa ufafanuzi wa injini hizo Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (MSCL), Eric Hamisi amesema injini hizo zimenunuliwa kwa Dola za Marekani 39,000,000 sawa na Shilingi Bilioni 89.764 na kila moja ikiwa na tani 35 na uwezo wa kuzalisha KW 2,380.

Viongozi mbalimbali waliojitokeza kushuhudia usafirishaji wa minofu ya samaki yenye uzito wa tani nane kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza moja kwa moja kwenda Brussels Ubelgiji wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Alisema uwezo huo wa injini utaiwezesha meli hiyo kusafiri kwa saa saba kutoka Mwanza hadi Bukoba na kwamba hadi sasa Wakandarasi wanaotengeneza wamelipwa Sh. Bilioni 55.618 sawa na asilimia 64 ya gharama zote.
Mwisho.

Post a Comment

0 Comments