Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki, amewataka wawekezaji
waliosajili miradi yao kwenye Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kuwasilisha
taarifa za maendeleo na changamoto zao kila baada ya miezi sita ili ziweze
kufanyiwa kazi za uboreshaji na utatuzi wa changamoto zake kwa wakati.
Anaandika Grace Semfuko, Dar es Salaam.
Kairuki alisema Kanuni za usajili
za TIC zinawataka wawekezaji hao kufanya hivyo na kwamba hatua hiyo inalenga
kuwaweka karibu wawekezaji hao ambao wamekuwa na tija ya kiuchumi kutokana na
uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani na kilimo ambazo hutoa ajira kwa
watanzania na ulipaji kodi unaostahili.
Aliyasema hayo alipotembelea
kiwanda cha OK Plastic Limited kilichopo Vingunguti Jijini Dar Es Salaam kinachochakata
bidhaa(vyuma) chakavu na kuzalisha rodi za shaba, nyaya za umeme, betri ingots na mikeka ambacho kimeajiri
wafanyakazi 595 wa kitanzania na raia wa kigeni watano.
“Nawasihi wawekezaji wote
mliojisajili na TIC, pelekeni taarifa zenu za maendeleo ya miradi yenu kila
baada ya miezi sita ili tujue ni wapi kuna changamoto tuweze kuzitatua kwa
wakati, ni kwa nia njema sana, Serikali yenu ipo na ni sikivu, pia naomba niwapongeza
wamiliki wa kiwanda hiki cha OK kwa ulipaji wa kodi mzuri na mmeajiri
watanzania wengi, na wengine igeni mfano wa kiwanda hiki” alisema Waziri
Kairuki.
Meneja wa kiwanda hicho Bw.Fadil
Ghaddar alisema uwekezaji wao kwa sasa umefikia shilingi Bil 10 na kwamba tangu
kuanzishwa kwake mwaka 2005 wamepata mafanikio makubwa ikiwepo soko la uhakika
la ndani ya nchi pamoja na baadhi ya nchi jirani ikiwepo Kenya.
Mbali na uzalishaji wa bidhaa
hizo, kiwanda hicho pia kinatoa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za
metali kwa vijana waajiriwa wao ili kuwajenga kiuchumi kwa kuanzisha viwanda
vyao pindi wanapoamua kuacha kufanya kazi kiwandani hapo.
Kiwanda hicho kinalipa kodi ya
mapato ya zaidi ya shilingi Bilioni 2 kwa mwaka, lakini wanasema changamoto yao
kubwa ni upatikanaji wa malighafi za uzalishaji wa bidhaa na wameiomba Serikali
iweke mikakati ya kuhakikisha kwamba viwanda vya ndani vinapata malighafi
kwanza ya kutosheleza au kuweka zuio kabla ya uuzwaji wa malighafi hizo nje ya
nchi ambapo Waziri Kairuki alisema
amelipokea ombi hilo na ataliwasilisha kwenye mamlaka zinazohusika ili ziweze
kulifanyia kazi.
“Mheshimiwa Waziri, hapa
kiwandani tunayo changamoto ya upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji
wa bidhaa hizi, hali hii imetufanya kupunguza uzalishaji kutoka tani 500 za
shaba kwa mwezi hadi kufikia tani 150 tu, utafiti uliofanywa na Taasisi ya BICO
ya chuo kikuu cha Dar es Salaam hivi karibuni ulionyesha kuna upatikanaji wa
kutosha wa bidhaa chakavu za shaba nchini kiasi cha kutosheleza viwanda vya
ndani, lakini tunakwama kupata malighafi hiyo kwa sababu inauzwa nje, tunaiomba
Serikali izuie ili tupate sisi” alisema Ghaddar.
Alisema wanatumia fedha nyingi
kuagiza malighafi za shaba kutoka nje ya nchi na kwamba iwapo Serikali itazuia
bidhaa hizo kuuzwa nje ya nchi itakuwa ni nafuu kwao.
Mwisho.
0 Comments