Sekta ya mifugo ni
miongoni mwa sekta za kipaumbele katika uwekezaji, Serikali ya Tanzania imekuwa
ikihimiza uwekezaji kwenye sekta hii ambayo imekuwa na tija ya kiuchumi.
Hivi ndivyo kiwanda cha Tanchoice kitakavyohifadhi nyama kwa ajili ya kuuzwa ndani na nchi huku nyingine itasafirishwa kwa ajili ya mauzo katika nchi za nje.
Anaandika Grace Semfuko
Wizara ya Mifugo na
Uvuvi imekuwa ikiweka mikakati ya kuhakikisha afya ya mifugo zinaimarishwa
vyema pamoja na kuwezesha upatikanaji endelevu wa rasilimali za vyakula na maji
kwa ajili ya mifugo.
Mikakati mingine ni kuboresha
biashara ya mifugo ndani na nje, kuimarisha huduma za utafiti wa mifugo, huduma
za ugani na mafunzo kwa wafugaji na maafisa ugani, kuanzisha na kuimarisha
vikundi na vyama vya ushirika vya mazao ya mifugo, kuboresha utekelezaji wa
sera, sheria na kanuni katika sekta ya mifugo pamoja na kuimarisha uratibu na
usimamizi wa wataalamu wa sekta ya mifugo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Kiwanda cha nyama cha Tanchoice alipotembelea kiwanda hicho hivi karibuni.
Katika kuunga mkono
jitihada za Serikali za kuboresha nyororo wa thamani kwenye sekta ya nyama Kampuni
ya Tanchoice Limited imejenga kiwanda kikubwa katika Wilaya ya Kibaha Mkoa wa
Pwani kitakachokuwa na uwezo wa kuchinja mifugo zaidi ya elf 5 kwa siku na
kuzalisha nyama ambayo itauzwa ndani na nje ya nchi.
Kiwanda hicho
kimejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 23 kinakadiriwa kutoa ajira ya zaidi
ya watu 500.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki akitoa neno katika Kiwanda cha nyama cha Tanchoice hivi karibuni baada ya kutembelea hicho.
Kiwanda hicho ambacho
kitakuwa na migawanyo mitano ya machinjio kitakuwa ni kiwanda kikubwa cha nyama
kwa nchi za Afrika Mashariki na cha pili kwa ukubwa Barani Afrika kikitanguliwa
na kile cha nchini Ethiopia ambacho kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 3,000, mbuzi
na kondoo 6,000 na kuzalisha tani 3,000 za nyama kwa siku moja.
Akizungumza mara baada
ya kukagua ujenzi wa kiwanda hicho, Kaimu Msajili wa Bodi ya nyama Tanzania
Iman Sichalwe alisema kiwanda hicho ni kikubwa kwa nchi za Afrika Mashariki na
Kati kwenye Sekta ya mifugo na kwamba kukamilika kwake kutaleta tija kwa
wafugaji na kuinua sekta ya mifugo nchini.
Sichalwe alisema kwa
sasa kiwanda hicho kimefikia asilimia zaidi ya 90 na kwamba muda wowote
kitaanza kufanya kazi kwa hiyo ni nafasi nzuri kwa wafugaji kuchangamkia fursa
hiyo kwa kufanya ufugaji wa kisasa ambao mifugo yake itakidhi mahitaji ya
kiwanda hicho.
“Sehemu ya kufikia
wanyama tayari, sehemu ya kuchinjia tayari mashine zote zimeshafungwa, maabara
na vitu vyote vimekamilika ikiwepo cheti cha kibali cha bodi ya nyama” alisema
Sichalwe.
Meneja uzalishaji wa
Kiwanda hicho Selo Luhongo alisema asilimia 20 ya nyama itakayochinjwa
kiwandani hapo itauzwa ndani ya nchi huku asilimia 80 zilizobakia zitauzwa nje
ya nchi.
“Tumeshafikia asilimia
99.9 ya ukamilishaji wa ujenzi wa kiwanda hiki ili kianze rasmi kazi
iliyokusudiwa, tunawaomba wafugaji na wadau wote wa sekta hii wakiwepo
wafugaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wazingatie kanuni za afya na ustawi
wa wanyama” alisema Luhongo.
Juhudi za Serikali za
kuimarisha sekta ya mifugo na mazao ya nyama zinafanyika ambapo katika hotuba
ya makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya 2020/2021 Bungeni Jijini
Dodoma, Waziri wa Wizara hiyo Luhaga Joelson Mpina alisema idadi ya mifugo nchini
inakadiriwa kuongezeka ikilinganishwa na mwaka 2018/2019 ambapo idadi ya
ng’ombe imeongezeka kutoka milioni 32.23 hadi milioni 33.4, mbuzi kutoka milioni
20 hadi milioni 21.29 na kondoo kutoka milioni 5.5 hadi milioni 5.65.
Kuongezeka kwa idadi
hiyo kunatokana na sera na mifumo thabiti ya utunzaji na ulinzi wa mifugo na
kusababisha kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la nyama kutoka tani 690,629 mwaka
2018/2019 hadi tani 701,679.1 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 1.6
kati ya hizo, tani 486,736.1 za nyama ya ng’ombe, tani 95,964.2 za nyama ya
mbuzi na kondoo, tani 80,601.3 za nyama ya kuku na tani 38,377.4 za nyama ya
nguruwe.
Aidha, ng’ombe walionenepeshwa wameongezeka kutoka ng’ombe 371,200
mwaka 2018/2019 hadi kufikia ng’ombe 512,256 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko
la asilimia 38.
Aidha katika mazao ya
ngozi Waziri Mpina alisema hadi kufikia Aprili 30, 2020 jumla ya kilo za ngozi
16,746,589.36 kutoka kwenye ng’ombe 14,449,075.49, mbuzi 1,775,298.5 na kondoo 522,215.38
zenye thamani ya shilingi bilioni 23.9 zimezalishwa ikilinganishwa na kilo
16,012,800.71 za kutoka kwenye ng’ombe 13,904,620.27, mbuzi 1,653,669.26 na
kondoo 454,511.17 zenye thamani ya shilingi bilioni 22.8 zilizozalishwa mwaka
2018/2019.
Alisema hadi kufikia
Machi 30 mwaka huu Sekali imeingiza zaidi ya shilingi Bilioni 12.9 za mauzo ya
ngozi za wanyama hao kwenye nchi za Ghana, China, Pakistani, Indonesia,
Ethiopia, Nigeria na Italy ikilinganishwa na mauzo ya shilingi bilioni 13.0 ya
mwaka mwaka 2018/2019.
Katika mwaka 2019/2020,
Wizara kupitia Fungu 99 ilitarajia kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 50
ambapo hadi kufikia Aprili 30, 2020 zilikusanywa shilingi Bil. 38.5 sawa na
asilimia 77 ya lengo la makusanyo ya mwaka huo wa fedha.
Aidha Wizara hiyo
imeendelea kupitia Sheria za sekta ya mifugo kwa ajili ya kuboresha mazingira
na kuwezesha ukuaji wa sekta ya mifugo ambapo marekebisho ya Sheria za Ustawi
wa Wanyama na Sheria ya Magonjwa ya Mifugo yamefanyika kupitia Written Laws
Miscelleneous Amendments Act 2019, Act No.14 of 2019
Mapendekezo ya
marekebisho ya Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo
SURA 180 yaliyopo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Written
Laws Miscelleneous Amendments Act 2020) tayari yameshasomwa kwa mara ya kwanza
katika kikao cha Bunge la Mwezi Januari, 2020.
Wizara imeandaa Kanuni
mbalimbali chini ya Sheria ya Magonjwa ya Wanyama na kutangaza katika Gazeti la
Serikali kwa ajili ya kuanza kutumika ili kutatua changamoto mbalimbali katika
Sekta ya Mifugo.
Wizara imefanya
marekebisho ya tozo katika Kanuni za Magonjwa ya Wanyama na kuwasilishwa Wizara
ya Fedha na Mipango. Aidha, kanuni mbalimbali chini ya Sheria ya Veterinari zimeandaliwa
na kutangazwa katika Gazeti la Serikali kwa ajili ya kuanza kutumika.
Mwisho.
0 Comments