Ni takribani dakika 122 alizotumia Jukwaani Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, akilihutubia Taifa kuelezea
mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wake kwa miaka mitano wakati akilivunja
Bunge la 11 lililodumu kwa miaka hiyo kuanzia
Novemba 20,2015 alipolizindua hadi Juni 16,2020 alipolivunja rasmi, ili kuacha
nafasi ya uchaguzi Mkuu mwingine unaotarajia kufanyika Octoba mwaka huu.
Na Grace Semfuko.
Hotuba hiyo iliyosheheni mafanikio lukuki
ambayo mengi yanaonekana kwa macho, ilileta hisia kwa wananchi wengi wa
Tanzania, huku wengine wakisema, ahadi nyingi za wakati wa kampeni za uchaguzi
uliopita wa mwaka 2015 zimetimizwa kwa asilimia kubwa.
Katika hotuba hiyo ndefu nitaomba niangazie tu
kwenye suala zima la uwekezaji ambalo alisema Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC) katika kipindi cha miaka yake mitano madarakani kimesajili miradi mipya
1,307 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 14.607 ikiwa ni zaidi ya
shilingi trilioni 30.
Miradi hiyo ambayo mingi inafanya kazi na baadhi
yake inaendelea kutekelezwa inatoa ajira ya Watanzania 183,503.
Tukumbuke tu kwamba Rais Magufuli aliahidi
kuimarisha Uwekezaji utakaokuwa na fursa ya kuimarisha uchumi wa Tanzania,
kuboresha maisha ya wakazi waliopo nchini, kuongeza uzalishaji wa viwanda na
mauzo ya nje pamoja na kuongeza wataalamu wa viwanda kwa kutumia teknolojia ya
nje itakayoletwa nchini kupitia wawekezaji wa viwanda.
Rais alisema hatua ya TIC kusajili miradi hiyo
imetokana na maboresho ya mazingira ya biashara nchini Tanzania pamoja na
kuanzisha Wizara maalum ya kushughulikia Uwekezaji.
“Kwa lengo la kukuza uchumi pia tumeendelea
kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ikiwemo kuanza kutekeleza
Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini (Blueprint) na kuanzisha
Wizara Maalum ya Uwekezaji iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tumefanya
marekebisho ya sheria mbalimbali na kupunguza urasimu katika kutoa vibali na
pia kufuta tozo kero 173 ambapo tozo 114 zinahusu sekta ya kilimo, uvuvi na
mifugo; tozo 54 za sekta nyingine mbalimbali; na tozo 5 zilikuwa zinatozwa na
Wakala wa Usalama na Afya mahali pa Kazi” alisema Rais Magufuli.
Alisema kutokana na hatua hizo, mafanikio
makubwa yamepatikana kwenye nyanja za biashara na uwekezaji huku akitolea mfano
biashara ya Tanzania nje ya nchi kuongezeka kutoka shilingi trilioni 11.5 mwaka
2014/2015 hadi kufikia shilingi trilioni 16.6 mwaka 2018/2019.
Aliongeza kuwa “jambo la kufurahisha zaidi ni
kwamba, Tanzania imekuwa na urari chanya wa mauzo ya bidhaa kwenye masoko ya nchi
za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya
Kusini mwa Afrika (SADC), mfano, kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
kutoka mwaka 2015 hadi mwaka 2018, Tanzania imekuwa na urari chanya wa
mauzo ya bidhaa kwa wastani wa Dola za Marekani milioni 288.04. Kuhusu
uwekezaji, Kituo chetu cha Uwekezaji kimesajili miradi mipya 1,307 yenye
thamani ya Dola za Marekani bilioni 14.607, zaidi ya shilingi trilioni 30, na
itakapokamilika itatoa ajira 183,503” alisema
Rais Magufuli Wakati akizindua Bunge hilo la
11 Mwezi Novemba 2015 aliahidi Serikali yake ingeendeleza jitihada za awamu
zilizotangulia za kukuza uchumi pamoja na kukabiliana na matatizo ya umasikini
na ukosefu wa ajira hatua ambayo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ametekeleza
ahadi hiyo, hususan kwa kukuza sekta kuu za uchumi na uzalishaji, ikiwemo
viwanda, kilimo, biashara, madini pamoja na utalii.
Kuhusu viwanda alisema vimejengwa viwanda
vipya 8,477, ambapo vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406, na vidogo sana
4,410 ujenzi ambao umeongeza idadi ya viwanda nchini kutoka 52,633 mwaka 2015 hadi
viwanda 61,110 mwaka 2020 aidha alisema viwanda vipya vilivyojengwa vimeisaidia
kuifanya nchi yetu kujitosheleza kwa baadhi ya bidhaa, ikiwemo saruji, nondo na
bati. Aidha, viwanda vipya vimezalisha ajira 482,601.
Ongezeko
hili la ujenzi wa viwanda pengine linakuja kufuatia kuwepo mazingira mazuri ya
Amani na utulivu yaliyopo nchini kwani ripoti
ya Global Peace Index ya Mwaka 2020 imeitaja Tanzania kushika nafasi ya kwanza
kwa amani na utulivu kwenye eneo la Afrika Mashariki na ya saba kwa nchi za
Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, mwekezaji yoyote hawezi kuwekeza
katika nchi ambayo haina Amani kwani anaweza kuhofia mtaji wake kuwa mashakani.
Rushwa na ufisadi ni miongoni mwa vitu
vinavyotajwa kushusha hali ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali Duniani,
Wawekezaji wanaweza kutoa au kuombwa rushwa ili mradi tu mambo yao yaende sawa,
na rushwa ni kielelezo tosha cha kutojiamini katika uwekezaji wao, kwa hapa
Tanzania ili kuufanya uwekezaji uwe ni wenye tija mambo hayo yalidhibitiwa
katika kipindi hicho na kusababisha kuwepo kwa maadili ya hali ya juu katika
utendaji wa kazi.
“Mheshimiwa
Spika, sambamba na kuimarisha nidhamu
Serikalini, tulizidisha mapambano dhidi ya rushwa, uhujumu uchumi na ufisadi.
Utakumbuka kuwa, wakati nikizindua Bunge hili niliahidi kuanzisha Mahakama ya
Uhujumu Uchumi. Mahakama hiyo ilianzishwa mwaka 2016 na mpaka sasa imepokea
mashauri 407, ambapo mashauri 385 tayari yamesikilizwa. Zaidi ya hapo, katika
kupambana na adui rushwa, Taasisi yetu ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) imeweza kufungua mashauri 2,256; ambapo mashauri 1,926 tayari
yametolewa uamuzi, na Serikali imepata ushindi kwenye mashauri 1,013” alisema
Rais Magufuli.
Mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa
yamefanyika ambapo TAKUKURU ilifanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni
273.38, zikiwemo fedha walizokuwa wamedhulumiwa wakulima, taasisi hiyo pia ilitaifisha
shilingi milioni 899, Dola za Marekani 1,191,651, EURO 4,301,399, nyumba 8
zenye thamani ya shilingi bilioni 11.6, magari matano yenye thamani ya shilingi
milioni 126 pamoja na viwanja vitano.
Aidha, zimerejeshwa pia mali za Serikali
zilizochukuliwa na watu binafsi ama taasisi kinyume cha sheria, zikiwemo nyumba
na majengo 98 ikiwemo Mbeya Hotel, mashamba 23, viwanja 298, kampuni 3, maghala
69. Vile vile, kiasi cha fedha na mali zilizowekewa zuio kusubiria kukamilika
kwa taratibu za kisheria za utaifishaji ni shilingi bilioni 52.7; Dola za
Marekani milioni 55.8; Euro milioni 4.3, magari 75, nyumba 41; viwanja 47 na
mashamba 13.
Uwekezaji pia unahitaji mawasiliano
ya uhakika, sekta hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kufufuliwa kwa
Shirika la mawasiliano la Taifa la TTCL ambapo Rais Magufuli anasema hatua hiyo
imeongeza masafa pamoja na watumiaji wa huduma hiyo.
Hapa
tunaona ni kwa jinsi gani Serikali iliyo makini inavyojali wawekezaji nchini
kwani imeimarisha huduma hizo kwa kuboresha usikivu wa simu kutoka asilimia 79
mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 94 mwezi Disemba 2019 huku idadi ya watumiaji
wa simu za mkononi pamoja na watumiaji data ikiongezeka maradufu, hali hiyo
imechangiwa zaidi na kupungua kwa gharama za kupiga simu kwa dakika moja kutoka
shilingi 267 mwaka 2015 hadi shilingi 40 tu hivi sasa.
Pia
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, limefufuliwa Shirika la Simu (TTCL)
ambalo lilikuwa limekufa pamoja na kuongeza hisa kwenye Kampuni ya Airtel
kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49. Huu ni ushahidi mwingine kwamba kazi aliyotumwa
Rais Magufuli na Watanzania ameifanya kikamilifu.
Aidha
miundombinu mbalimbali ya kurahisisha uwekezaji pia imeimarishwa kwani kuna mambo
mengi yamefanyika ikiwepo ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, upanuzi wa
Bandari kuu za Dar es Salaam, Mtwara na
Tanga na uboreshaji wa usafiri wa maji kwenye Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa
kuboresha bandari zake pamoja na kujenga na kukarabati meli
Mengine
ni ujenzi wa
barabara, mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji wa Mwalimu Julius Nyerere
(Stigler’s Gorge) na mengineyo mingi ikiwepo ujenzi wa vituo vya huduma za afya
na huduma nyinginezo za kijamii.
Aidha kuhusu usafiri wa anga, ujenzi wa Jengo
jipya la Abiria (Terminal III) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu
Nyerere umekamilika na kuendelea na upanuzi wa Viwanja vya Kimataifa vya
Kilimanjaro (KIA) na Abeid Aman Karume kule Zanzibar pamoja na ujenzi wa
viwanja vingine 11 ambavyo vipo katika hatua mbalimbali, na sasa Serikali ipo mbioni
kumpata Mkandarasi wa kujenga Uwanja wa Kimataifa wa Msalato hapa Dodoma.
Kutokana na hatua tulizochukua za kuimarisha
sekta mbalimbali, uchumi wa Tanzania umeendelea kukua vizuri, ambapo kwa
wastani, katika miaka mitano iliyopita, umekua kwa asilimia 6.9 kutoka ukuaji
wa asilimia 6.2 mwaka 2015, huku pato ghafi la Taifa likiongezeka kutoka
shilingi trilioni 94.349 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 139.9 mwaka
2019 kwa bei ya miaka husika, hii sio tu imeifanya nchi kuwa miongoni mwa nchi
zinazokua kwa kasi kiuchumi lakini imeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10
zenye uchumi mkubwa zaidi Barani Afrika.
Aidha mfumuko wa bei za bidhaa pia
umedhibitiwa kutoka asilimia 6.1 mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa asilimia
4.4 huku akiba ya fedha ya kigeni ikiongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni
4.4 zilizokuwa zikitosheleza kununua bidhaa na huduma kwa miezi 4.3 mwaka 2015
hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 5.3 mwezi Aprili, 2020 ambazo
zinatowezesha kununua bidhaa na huduma kwa miezi 6.2. Kiwango hiki ni zaidi ya
lengo lililowekwa kwenye EAC (miezi 4.5) na SADC (miezi 6).
0 Comments