Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe amesema ipo haja
kwa Wadau kuunganisha Utalii wa upandaji wa Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi iliyopo Wilayani Same ili kuongeza tija ya kiuchumi
kwa kutangaza vivutio vilivyopo kwenye hifadhi hiyo.
Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Tanapa Kamishna Msaidizi Abel Mtui akiwaonyesha Wanyama Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe (Katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Bi Rosemary Senyamule walipotembelea hifadhi hiyo hivi karibuni.
Anaandika Grace Semfuko kutoka Hai,
Kilimanjaro.
Aliyasema hayo katika ziara yake kwenye hifadhi hiyo iliyokuwa na lengo la kuangalia vivutio vya
uwekezaji vilivyopo hususan kwenye sekta ya utalii.
Alisema
kutokana na kuwa na idadi ndogo ya Watalii wanaoingia katika hifadhi hiyo
ukilinganisha na wanaotembelea Mlima Kilimanjaro, kuna haja ya kuunganisha
utalii huo na kuwa katika masoko ya pamoja ambayo pamoja na kusaidia kuitangaza
hifadhi hiyo, pia itasaidia kuongeza pato kwenye Sekta ya Utalii nchini.
“Hifadhi
ya Mkomazi inavyo vivutio vingi vya utalii, ina wanyama wote wakiwepo wanyama
wakubwa watano wanaotambulika ulimwenguni kote, ina maeneo ya mwinuko ambayo
unaweza kuona wanyama kwa urahisi, na pia Wawekezaji wa Sekta ya Utalii wakija
hapa watapata manufaa makubwa kwani watapata walichokusudia kukiona” alisema Mwambe.
“Tunafikiri
kuna uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Utalii ambao unatakiwa ufanyike katika
hifadhi yetu hii na kwenye zote tulizonazo nchini kwetu, fursa na uwezo huo tunao
kwani kwa hapa Mkomazi pekee tunaona ni jinsi gani TANAPA walivyojipanga kusimamia hifadhi
hii, wametenga na kubainisha maeneo ambayo wawekezaji wanaweza kuja kuwekeza” aliongeza Mwambe.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Bw. Geoffrey Mwambe akionyesha Twiga (hayupo pichani) katika hifadhi ya Taifa ya Mkomazi iliyopo Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.
Aidha Mwambe aliwaomba viongozi wa Mikoa na Wilaya Nchini, kuendelea kuibua fursa za uwekezaji zilizopo kwenye maeneo yao, ili Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kiweze kuzitengenezea mpango maalum wa kuvutia uwekezaji.
“Sio
kazi rahisi sana kumleta Mwekezaji, lakini inakua ni afadhali kama kunakuwa na
maandalizi ili tujue Mwekezaji akawekeze wapi na kwa masharti gani, mfano tunajua
kwenye maeneo ya hifadhi kuna taratibu zake zinazosimamiwa na TANAPA ambazo
zinatusaidia sisi namna ya kutafuta wawekezaji na kuwapa mwongozo ambao ni
rahisi, sio mwekezaji anatoka zake huko, umeshamshawishi anakuja hapa anakutana
na masharti mapya kabisa ambayo hayakuwepo katika taarifa zetu, tunakuwa kama tunamvunja
moyo” alisema Mwambe.
Kwa
upande wake Kamishna Msaidizi wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi Abel Mtui alisema
hifadhi hiyo inavyo vivutio muhimu na kuwakaribisha wawekezaji watakaowekeza
kwenye eneo la Hotel na Camps kwa utaratibu uliowekwa na Shirika la Hifadhi za
Taifa Tanzania (TANAPA.).
Faru Debora, ni mmoja wa Faru wa maajabu anaepatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Taifa ya Mkomazi, Faru huyu analijua jina lake na ukimwita anasikia na anakufuata mahali ulipo.
Aidha
alisema ili kuongeza idadi ya vivutio hifadhi hiyo inatarajia kuanzisha utalii
wa mnyama aina ya Faru kama zao jipya la utalii nchini na kuongeza kuwa ni hifadhi pekee Tanzania kuwa na aina ya utalii
huo lengo likiwa ni kukuza sekta hiyo na kwamba hifadhi hiyo itakuwa ya kwanza kuwa na
utaratibu wa kuona faru weusi ambao walikuwa hatarini kutoweka hali
aliyoitaja kuwa ni fursa nzuri kwa wageni wote kutoka mataifa mbalimbali Duniani kuja
na kufanya utalii Nchini Tanzania.
“
Kwa zaidi miaka 20 hifadhi hii ilikuwa na mradi wa uzalishaji faru lengo likiwa
ni kuongeza idadi ya mnyama huyo ambaye alikuwa ametoweka katika maeneo mengi na
matarajio yetu ni kuwa na wageni wengi Zaidi kwa mwaka” alisema.
Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ipo katika
mikoa miwili ya Kilimanjaro na Tanga, ndani ya Wilaya za Same, Lushoto na
Korogwe kwa kiasi kidogo, hifadhi hii ilianzishwa kama pori la akiba
lililomegwa kutoka katika Pori kubwa la Akiba la Ruvu mnamo mwaka 1951, Hifadhi
ya Mkomazi ilipewa hadhi ya hifadhi ya Taifa Mwaka 2007.
Jirani ya hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kuna pori la akiba la Wanyapori la Umba katika Mkoa wa Tanga, pori hilo lina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 3,234, kwa pamoja Mkomazi na Umba ni maeneo ambayo yamepakana na Nchi Jirani ya Kenya katika hidadhi ya Tsavo.
Jirani ya hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kuna pori la akiba la Wanyapori la Umba katika Mkoa wa Tanga, pori hilo lina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 3,234, kwa pamoja Mkomazi na Umba ni maeneo ambayo yamepakana na Nchi Jirani ya Kenya katika hidadhi ya Tsavo.
Hifadhi hii ya Taifa ya Tsavo Mashariki ni moja ya hifadhi kubwa zaidi na kongwe nchini Kenya iliyotambaa eneo la kilomita za mraba 11,747. Ilifunguliwa mnamo April 1948, na iko
karibu na kijiji cha Voi katika Kaunti ya Taita-Taveta. Hifadhi hii
imegawanywa katika sehemu za mashariki na magharibi na barabara na reli ya
A109. Jina lake ambalo linatokana mto Tsavo,
ambao unatiririka kutoka magharibi hadi mashariki kupitia hifadhi hii, iko
mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya milima ya Chyulu na hifadhi ya wanyama ya Mkomazi nchini Tanzania.
Mwisho.
0 Comments