Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Bw. Geoffrey Mwambe ametembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kwenye Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro ambapo alijionea vivutio mbalimbali vya Utalii huku kimojawapo kikiwa ni eneo la mradi wa kuzalisha Mbwa Mwitu ambao wanatajwa kuwa hatarini kutoweka kutokana na magonjwa, kuuwawa kwa sumu kutokana na tabia zao za kula mifugo inayofugwa na binaadamu.
Na Grace Semfuko, Same.
Akiwa katika Hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Hifadhi ya Mkomazi Abel Mtui alisema mradi wa kuzalisha Mbwa Mwitu unaosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA katika hifadhi hiyo ya Mkomazi umekuja mahsusi ili kuwalinda Wanyama hao muhimu kwa utalii katika hifadhi hiyo.
Mbwa Mwitu wanaotunzwa katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi iliyopo Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.
Mradi huo wa kuzalisha mbwa mwitu ulianzishwa na TANAPA kwa kushirikiana na Taasisi ya wanyamapori ya Tanzania Wildlife Protection Fund mwaka 1995 ambapo mpaka sasa tayari mbwa 215 waliozalishwa kupitia mradi huo wametolewa kwa ajili ya kuvutia utalii.
"Hawa mbwa wanauwawa sana na binaadamu kwa sababu wanadai kuwasababishia hasara ya kula mifugo yao, kuna wakati wanawekewa hadi sumu na wanakufa sana, tunatoa elimu kwa jamii kuhusu kuwatunza mbwa hawa, mfano Loliondo tumehusisha jamii ya kule kuhusu utalii wa mazingira ya mazalia ya mbwa, na sasa wanafikiria kuwahamishia mbali na mifugo yao, kwa hiyo jamii lazima ishirikishwe ili kuondokana na mauaji ya malipizi" alisema Mtui.
Mbwa Mwitu wakipata chakula katika hifadhi hiyo ya Mkomazi
"Mradi huu umekuwa na mafanikio makubwa lakini unaweza usiwaone hawa mbwa hapa kwa sababu wanatembea sana na wanaenda mbali mno, kwa siku wanaweza kutembea Zaidi ya kilomita 60, sisi tunawazalisha hapa lakini tukiwatoa tu unaweza kuwakuta kwenye hifadhi zingine huko, mfano hata hapa kuna mbwa waliokuja kutoka Serengeti" alisema Mtui.
Mbwa Mwitu wakiwa katika hifadhi ya Taifa ya Mkomazi iliyopo Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.
Alisema Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi inaendeleza mradi wa kuongeza Mbwa Mwitu waliokuwa hatarini kutoweka kutokana na athari za kibinaadamu na kwamba wakazi waishio jirani na hifadhi hiyo wanapewa elimu ya kuwalinda Wanyama hao muhimu katika sekta ya utalii pamoja na afya ya hifadhi za mazingira ya Mkomazi.
Kamishna Msaidizi wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi iliyopo Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro Abel Mtui (aliyesimama) akitoa maelezo ya Hifadhi hiyo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe na ujumbe wake walipowasili katika hifadhi hiyo ili kuangalia vivutio vua uwekezaji katika sekta ya utalii.
Mbwa hawa wanatajwa kuwa na tabia zinazofanana na mbwa wa kawaida ambao tunaishi nao majumbani, mbwa hawa walikuwa hatarini kutoweka kutokana na kudhuriwa na binaadamu kwa sababu ya tabia zao zinazotajwa kutowapendeza wanadamu hao.
kutokana na hatari hiyo ya kutoweka kwa viumbe hawa hifadhi ya Taifa ya Mkomazi imeamua kuja na mkakati wa kuwahifadhi na sasa wameanza kuongezeka kutokana na kuzaliana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe akisoma moja ya jarida linalohusu habari za Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
0 Comments