Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wanaotaka kuwekeza kando ya Fukwe za Bahari na Maziwa nchini kusoma historia za maeneo hayo ili kuepukana na hasara wanazoweza kuzipata siku za baadae kutokana na mafuriko.
Na Grace Semfuko
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt Samuel Gwamaka alipofanya ziara yake mkoani Kigoma na kutembelea kando ya Ziwa Tanganyika ili kujionea athari za kimazingira kutokana na kuongezeka kwa maji kwenye ziwa hilo.
"Maji yameongezeka kwa Zaidi ya mita 1.3 katika kipindi cha mwaka mmoja, na katika kipindi cha miaka 14 maji haya yameongezeka kwa mita 3.19 jambo ambalo linahatarisha miundombinu na uwekezaji katika fukwe na kuhatarisha biashara pia" alisema Dkt Gwamaka.
Aliwataka Wawekezaji hao kuangalia historia ya maeneo wanayotaka kuwekeza ili kujihakikishia usalama wao pamoja na mitaji yao.
"Pia nawaomba mfuatilie taarifa za historia ya maeneo haya kwa mamlaka ya Bonde la maji kwani wao wanazo taarifa za kutosha kuhus mazingira ya maeneo haya ili muwe na tahadhari kubwa" alisema.
Aliongeza kuwa kumekuwa na mabadiliko ya tabianchi ambayo yana athari kubwa za kimazingira zikiwepo za ongezeko la kina cha maji katika maziwa na Bahari hali inayisababisha mafuriko ambayo yanaharibu miundombinu mbalimbali
Kwa Upande wake Mwekezaji wa fukwe ya Golden Beach Dkt Lameck Yohana alisema kupanuka kwa ziwa Tanganyika kumeathiri uwekezaji huo kutokana na maji kuharibu baadhi ya miundombinu yake.
0 Comments