Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambae pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi amesema Dunia ipo mbioni kushuhudia kundi kubwa la Wawekezaji watakaokuja kuwekeza nchini kutokana na kuwepo kwa mazingira na Sera nzuri za kuvutia Uwekezaji Nchini Tanzania.
Anaandika Grace Semfuko, Dar Es Salaam.
Dkt Abbasi amesema hatua hiyo pamoja na kuifanya Tanzania kung’ara kiuchumi Duniani pia itaipaisha katika ushindani wa kimataifa kwenye soko la bidhaa bora zinazozalishwa nchini kutoka kwa wawekezaji wa ndani.
Dkt Abbasi alitembelea maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea Jijini Dar Es Salaam ambapo pamoja kufurahishwa na idadi kubwa ya watu waliohudhuria kwenye maonesho hayo alipongeza kazi zinazofanywa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania za kuratibu suala zima la uwekezaji.
“kwenye uchumi wa kipato cha kati Dunia itatuangalia sana na Wawekezaji watakuja sana, tukiwa na mazao, tukiwa na bidhaa nzuri masoko yatakuwepo, kwa sababu kuwa na uchumi wa kipato cha kati ni kwamba unaaminika Duniani, yaani wanakuona huduma zako za kijamii ni nzuri, kwa sababu hawakuchukulii kama ni nchi masikini wanakuchukulia ni nchi tajiri ya kipato cha kati, wawekezaji wanapikuja wanakuwa wanajiamini kwamba tukinunua bidhaa za Tanzania zitakuwa nzuri” amesema Dkt Abbasi.
Amesema ni fursa sasa kwa Watanzania ya kuchapa kazi na kuzalisha kwa wingi bidhaa na kuwataka watumishi wa Umma kuwa waadilifu katika utendaji wao wakazi ili kuongeza ari ya kufanya kazi.
“Watumishi wa Umma naomba tuwe Waaminifu na waadilifu, hatuwezi kuingia kwenye uchumi wa kipato cha kati ukiwa ni yule yule, utendaji wako wa kazi ni ule ule, unaamka saa nne unategemea unakuja kazini, unawahi kuondoka, na kwa wanafunzi hujisomei, hilo halikubaliki, unajua tutaweza kuingia kwenye nchi ya kipato cha kati lakini kuna baadhi ya watu wakawa kipato cha chini kwa sababu ya mtazamo wako wa kukosa uzalendo” amesema Abbasi.
Amesema kuna baadhi ya watu wanasema tukiingia katika kipato cha kati nchi itakuwa haikopesheki na kukosa misaada na kuongeza kuwa jambo hilo sio kweli.
“Si kweli kwamba tukiingia katika kipato cha kati tutakuwa hatukopesheki, kwanza sio lazima tupate misaada yoyote, lakini ukiingia katika kipato cha kati mana yake ni kwamba dunia inaiamini hiyo nchi kuwa ipo vizuri kwa sababu wanaiamini hiyo nchi ina miundfombinu mizuri na soko la uhakika”amesema Dkt Abbasi.
Mwisho.
0 Comments