Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Sera wa Benki Kuu ya Tanzania BOT Dkt Suleiman Missango, amesema ukuaji wa pato la Taifa kwa kiwango kikubwa unatokana na shughuli za uwekezaji,hatua ambayo pamoja na kumnufaisha Mwananchi mmoja mmoja, pia italinufaisha Taifa kiuchumi kwa mapato yatokanayo na kodi mbalimbali.
Anaandika Grace Semfuko

Anaandika Grace Semfuko
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Sera wa Benki Kuu ya Tanzania BOT Dkt Suleiman Missango akitoa maoni yake kwa Afisa Msajili TIC-NIDA Bw. Christopher Bomola wakati alipotembelea banda la Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC wakati wa maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba Jijini Dar Es Salaam Julai 7, 2020
Dkt Missango alitembelea Banda la Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) lililopo kwenye maonesho ya 44 ya kimataifa ya biashara Sabasaba ili kuangalia shughuli zinazofanywa na kituo hicho za kuratibu na kuhamasisha uwekezaji nchini Tanzania.
Amesema katika kutekeleza sera na kuangalia masuala ya kiuchumi suala la uwekezaji ni kitu cha msingi ambapo kuingia katika uchumi wa kati wa nchi kumetokana na shughuli mbalimbali zikiwepo Sera, Uwekezaji, Wananchi kufanya kazi kwa bidi pamoja na Amani na utulivu uliopo nchini.
“Tanzania kuingia kwenye uchumi wa kati ina maana kubwa kwetu kama nchi, hii itavutia Wawekezaji wengi zaidi kutokana na kuwa na uhakika wa soko kubwa na la uhakika la ndani na nje ya nchi, mwekezaji atakuja kwa sababu anajua akija kuwekeza hapa atazalisha na kuuza kwenye soko la ndani ambalo limepanuka kutokana na ongezko la watu, pia Wawekezaji wataongezeka kwa sababu Tanzania inayo Serikali inayoaminika na inayotekeleza Sera zake kwa ufasaha” Alisema Dkt Missango.
Amesema kutokana na kuimarika kwa Sera na mifumo ya uwekezaji kunakofanywa na Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dkt John Pombe Magufuli kunampa fursa mwekezaji kuja kuwekeza kwenye nchi ambayo sasa imeingia katika historia mpya ya kiuchumi na hivyo kuwataka wawekezaji wengi Zaidi kuwekeza Tanzania.
“Rais wetu ana nia ya dhati ya kuhakikisha uchumi unakua na tumeona juhudi hizo, hii inatoa taarifa kwa wawekezaji kwamba waje kuwekeza Tanzania kwa sababu ya mazingira yake mazuri, tunashuhudia sasa hivi kuna sera imara na ambazo hazibadiliki, kuna soko la kutosha la bidhaa na mwekezaji hawezi tu kutegemea soko la nje kuuza bidhaa anazozizalisha hapa nchini” alisema Dkt Missango.
Aidha amemalizia kwa kusema kuwa, Tanzania sio nchi masikini tena na hivyo kuna kila sababu ya kuwekeza.
Mwisho.
0 Comments