Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) Dkt. Maduhu Isaac Kazi amewataka Wawekezaji wakubwa wa Viwanda vya uzalishaji wa unga wa ngano kuanzisha mashamba ya kilimo cha bidhaa hiyo ambayo kwa asilimia kubwa wanaiagiza kutoka nje ya nchi.
Dkt. Kazi amesema hatua ya viwanda ya kuagiza malighafi ya ngano kutoka nje ya nchi ili wazalishe unga hairidhishi na hivyo kuwaomba wazalishe nchini ili kuongeza mnyororo wa thamani ambao utaleta tija ya kiuchumi.
Aliyasema hayo katika ziara ya Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki alipotembelea kiwanda cha kuzalisha unga wa ngano, unga wa sembe na Sabubi cha Azania Group kilichopo Tabata Jijini Dar Es Salaam ambacho kinaagiza nje malighafi ya ngano kwa asilimia 90.
“Mnafanya kazi nzuri ya kuzalisha unga hapa, lakini nimeona kuna changamoto kubwa ya uagizaji wa malighafi hiyo kutoka nje kwa asilimia 90, niwaombe sana nyie na viwanda vingine muangalie uwezekano sasa wa kuanzisha mashamba makubwa ya ngano ili muwe na mnyororo mzima wa thamani katika uzalishaji wenu viwandani” alisema Dkt. Kazi
Dkt Kazi alielezea kutoridhishwa kwake na uagizwaji huo na akasema upo umuhimu mkubwa wa kulinda uchumi wa ndani kwa kutoagiza malighafi ambazo uwezo wa kuzalisha nchini upo.
“Nimejionea mengi kutoka kwa wawekezaji wetu tuliowatembelea, kuna hatua ambazo sisi kama TIC tutachukua ili kuzidi kuimarisha mazingira ya uwekezaji, lakini sijafurahishwa kabisa na hatua ya Azania Group wanavyoagiza malighafi ya ngano kutoka nje kwa asilimia 90, ni vizuri wawekeze kwenye kilimo cha ngano na kuhamasisha wakulima zaidi ili kuokoa fedha za kigeni” alisema Dkt Kazi.
Alisema ni muhimu Wawekezaji wakatumia malighafi za ndani kwa kuwa zinapunguza matumizi ya fedha za kigeni lakini pia zinakuza uchumi wa nchi kwa kuwekeza zaidi kwa wananchi hasa kwenye kilimo.
Dkt Kazi aliishari Kampuni ya Azania Group kuwekeza katika kilimo cha ngano ili kupunguza kiwango cha kuagiza ngano nje ya nchi.
Aliishauri Kampuni hiyo kuiga mfano wa viwanda vya Sukari na mvinyo ambao hutumia malighafi zinazozalishwa na wakulima wa maeneo viwanda vilipo huku akitolea mfano wakulima wa zao la Zabibu na Miwa ambao wakizalisha wanaviuzia viwanda husika.
Aidha Dkt. Kazi aliwahakikishia Wawekezaji Nchini kuwa TIC ipo wazi muda wote katika kufanya majukumu yake na endapo Mwekezaji ana tatizo awasiliane naoi li kuweza kutatua changamoto zao.
Kwa upande wake Waziri Kairuki amesema iwapo wawekezaji hao watazalisha ndani malighafi ya ngano wataweza kuinua pato la Taifa kupitia kilimo na kuingia kwenye soko la Dunia la malighafi hiyo.
“Unajua kuzalisha bidhaa hii ya ngano hapa nchini kutakuwa na tija kubwa ya kiuchumi kwani malighafi itakayozalishwa itaweza kuuzwa na nje pia, wakati Serikali inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda nchini, nanyi Wawekezaji mjitahidi kuzalisha malighafi ya ngano kwa kiasi kikubwa ili kuinua uchumi wa ndani, uwekezaji huu utatusaidia kuokoa fedha za kigeni na kulinda ajira za Watanzania na hatimaye kuingia kwenye soko la Dunia la malighafi” alisema Kairuki.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Azania Group Bw. Fuad Awadh akazungumzia changamoto za kikodi mipakani wanaposafirisha bidhaa zao nje ya nchi na akaiomba Serikali kukaa meza ya pamoja katika kujadili mapendekezo ya kibajeti ili kuzipa kipaumbele bidhaa za ndani zinazosafirishwa nje ya nchi kuuzwa.
“Kweli tuna CTI inayotuwakilisha kwenye vikao vya Serikali vya Bajeti, lakini sisi wafanyabiashara, ambao tupo kwenye fani kuna tatizo, tunashindana na wenzetu kwenye nchi jirani, hii inatupa wakati mgumu sana, tunaomba angalau tupate fursa ya kuzungumza kwenye vikao hivi, CTI wanatusemea na ni kweli wanapata mawazo yetu, lakini wao ni watendaji tu, tutakapokwenda sisi wenyewe kuzungumza naamini tutasema mawazo mazuri ya kuhusu viwanda vyetu viweze kuuza kwenye nchi jirani kwa usalama zaidi”
Alisema na kuongeza kuwa Nchi za Afrika Mashariki pekee zina soko kubwa lenye zaidi ya watu milioni 150 na hivyo ipo haja ya Mamlaka za Serikali kuwaangalia mipakani wakati wanaposafirisha bidhaa hizo.
“Soko la Afrika Mashariki pekee lina Watu zaidi ya Milioni 150, tusilipoteze na kubaki na soko la ndani pekee, haitakuwa busara, mimi naona kuna umuhimu Serikali kupitia Wizara yako ya Uwekezaji Mheshimiwa Angellah Kairuki na Wizara ya Viwanda na biashara mtushirikishe sisi wafanyabiashara ambao tupo kwenye nchi hii tutoe maoni wakati mnapanga viwango vya kodi” alisisitiza.
Waziri Kairuki aliahidi kuyafanyia kazi mapendekezo ya Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa Makampuni ya Azania.
Katika Ziara yake Kairuki alitembelea pia Kampuni ya kutengeneza vinywaji vikali ya Tanzania Distillers maarufu kama Konyagi, Kampuni ya Sandvik inayozalisha mitambo ya kuchimba madini na vifaa vya ujenzi, na Kiwanda cha kuzalisha Unga wa Sembe, Ngano, Sabuni na Mafuta ya Kipikia cha Azania kilichopo Jijini Dar Es Salaam ambacho kilianza kujengwa January 2018 na kukamilika Julai 2019 chenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 30.
0 Comments