Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki amesema ipo haja kwa makampuni ya simu nchini, kuangalia upya punguzo la bei za tozo mbalimbali za huduma hizo ili kuwarahisishia watumiaji wao.
Na Grace Semfuko, Dar Es Salaam.
Kairuki amesema sekta ya mawasiliano licha ya kuwa na muhimu kwa uchumi wa Taifa, lakini pia Wadau wa Sekta binafsi na Serikali wamekuwa wakitumia simu kwa malipo ya huduma mbalimbali za kifedha.
Aliyasema hayo katika ziara yake ya siku tatu ya kutembelea Wawekezaji walipa kodi wakubwa nchini Tanzania ambapo siku ya kwanza ya ziara yake alitembelea Makampuni manne ya Simu ikiwepo Kampuni ya Vodacom, Airtel, Tigo na Zantel na kusisitiza kuwa huduma za mawasiliano kwa sasa sio anasa tena bali ni muhimu.
“Nimewasisitiza pia wazaidi kuona ni kwa namna gani wanaongeza muda wa marejesho ya mikopo yao na kupunguza riba, lakini pia nimewasisitiza wapunguze bei za mawasiliano kwani simu sasa hivi sio anasa ni huduma muhimu maana hata Serikali tunazitumia kupitia malipo mbalimbali ya fedha” alisema Kairuki.
Aidha alisema katika kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa mazuri, Serikali katika kipindi cha Mwaka 2020/2021 imefuta tozo na kodi mbalimbali zaidi ya 60 huku katika kipindi cha miaka mitano ya Rais Dkt John Pombe Magufuli madarakani hakuna kodi mpya iliyoongezwa.
“Tumewahakikishia maboresho mbalimbali yaliwepo ya kufutwa kwa kodi za tozo mbalimbali, tangu Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli aingia madarakani hakuna kodi mpya iliyoongezeka, na tumefuta tozo mbalimbali 168, lakini hiyo haitoshi, kwa mwaka huu wa 2020/2021 tozo na kodi zaidi ya 60 pia zimefutwa, lengo kubwa ni kuwarahisishia wawekezaji wetu kufanya biashara kwa uhakika” alisema Kairuki.
“Kwa TIC iwapo Wawekezaji wana changamoto zozote milango ipo wazi, kuwahudumia Wawekezaji ni jukumu letu kubwa, kwa hiyo wawasiliane nasi wakati wowote” alisisitiza Dkt. Kazi.
0 Comments