Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angelah Kairuki amesema Serikali inaimarisha Uwekezaji katika Sekta ya usafiri wa anga ambao umekuwa na tija ya kiuchumi kutokana na kutumiwa katika usafirishaji wa bidhaa na miundombinu mingine muhimu ya uwekezaji.
Na
Grace Semfuko, Dar Es Salaam.
Kairuki amesema Wawekezaji wengi wamekuwa wakiutumia usafiri huo kwa kusafirisha Teknolojia mpya na za kisasa za uwekezaji, hatua inayosababisha ukuaji wa ajira kutokana na kuongezeka kwa ujenzi wa viwanda vinavyochangia pato la Taifa kwa ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali za uendeshaji.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na Wanachama wa chama cha Wamiliki wa Ndege Tanzania TAOA katika ziara yake ya kikazi ya siku tatu ya kutembelea Makampuni makubwa Jijini Dar Es Salaam.
“Usafiri wa Anga ni muhimu kwa Sekta ya Uwekezaji nchini, Serikali tunaendelea kuimarisha usafiri huu ili kuongeza tija ya kiuchumi na kurahisisha shughuli za uwekezaji maana ni usafiri wa haraka na rahisi, wengi mmeshuhudia ujenzi na ukarabati mkubwa wa viwanja vyetu vya ndege nchini kote, na sasa hivi tunaona jinsi ambavyo Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli anavyopambana kuliimarisha Shirika letu la ndege la ATCL, si hivyo tu bali hata wamiliki binafsi wa ndege nao wamekuwa wakifanya kazi nzuri kwenye sekta hii” alisema Kairuki.
Baadhi wa Wanachama wa Chama cha Wamiliki wa Ndege Tanzania-TAOA wakifuatilia kwa makini mjadala baina yao na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu(Uwekezaji) Angellah Kairuki uliofanyika katika Hotel ya Slipway Jijini Dar Es Salaam Jumatano Septemba 19,2020.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) Hamza Johari amesema Mamlaka hiyo imejidhatiti katika kuhakikisha ubora na usalama wa usafiri huo unazingatiwa na kuwataka wamiliki wake kuzingatia ubora, weledi na umakini katika kuendesha shughuli za usafirishaji.
“Usafiri wa anga ni biashara ambayo inahitaji umakini mkubwa, na ni biashara ambayo inadhibitiwa sana,sisi TCAA tunajali usalama kuliko biashara, kwa sababu kurusha watu juu bila kuzingatia usalama ni hatari, ndege inaweza kuanguka na sio tu kuanguka bali kuangukia kwenye maghorofa au sokoni kwenye watu wengi, na nyinyi wote mnafahamu Tanzania hatujawahi kupata kitu hicho, ni kwa sababu tunadhibiti kweli kweli” alisema Johari.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt.Maduhu Isaac Kazi wakiwa na Maafisa wengine wa TIC na Wizara wakisikiliza mada kutoka kwa Mjumbe wa Chama cha Wamiliki wa Ndege Tanzania-TAOA wakati wa kikao cha pamoja kilichofanyika kwenye hotel ya Slipway Jijini Dar Es Salaam Jumatano Septemba 19, 2020 Jijini Dar Es Salaam.
Mkurugenzi huyo wa TCAA alisema iwapo wanaona kuna Shirika lolote la ndege nchini ambalo halizingatii vigezo vya kiusalama wanalifuatilia kwa karibu na hatimaye kulifungia shughuli zake.
“Kwa hiyo kama mtu anatetereka kwa vigezo hasa vya kiusalama, na kwa sababu hatutaki ajali za namna hiyo, mara nyingi tunaanza kumfuatilia kwa ukaribu sana, na anaposhindwa kuboresha inafikia mahali sasa inabidi hilo shirika tulifunge, kwa hiyo ni usafiri unaohitaji umakini wa hali ya juu, utaalamu wa hali ya juu, weledi wa hali ya juu, na uwezo wa kifedha thabiti”alisema Johari.
Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Dkt. Maduhu Isaac Kazi nae alisema Kituo hicho pia kimesajili Wawekezaji wa Usafiri wa anga ambapo wamekuwa wakifuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kazi zao zinakuwa na tija.
“TIC kama msimamizi wa Wawekezaji hawa, tunahakikisha tunafuatilia kwa karibu uwekezaji wao ili kuangalia kama wanatenda kazi zao ipasavyo, niwahakikishie tu kwamba tunafanya kazi kubwa” alisema Dkt Kazi.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Ndege Tanzania TAOA ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mizigo katika Viwanja vya ndege Swissport Bw.Mrisho Yassin amesema kukutana kwao na Waziri Kairuki ni ishara kubwa kuwa Serikali inathamini mchango wa TAOA katika maendeleo ya Taifa.
Mwisho.
0 Comments