Header Ads Widget

Ticker

6/recent/ticker-posts

TIC yashiriki Maonesho ya NANENANE Kanda zote Tanzania

Maonesho ya Wakulima maarufu kama NANENANE ya Ishirini na Nane (28) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993, yameanza nchini kwenye Kanda nane (8) kuanzia tarehe 31 Julai -Agosti 8, 2020. Kanda hizo ni Kanda ya Mashariki (Morogoro), Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Magharibi (Tabora), Kanda ya Kusini (Lindi), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Ziwa Mashariki (Simiyu) na Kanda ya Ziwa Magharibi (Mwanza).


Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ni miongoni mwa Taasisi za Serikali zinazoshiriki maonyesho hayo na uwakilishi wake upo kwenye Kanda zote kupitia Ofisi zake za Kanda. Lengo ni kutoa elimu ya uwekezaji kwa umma, kutoa taarifa/maelezo na ufafanuzi kwa wadau kuhusiana na shughuli za Kituo na masuala mbalimbali  yahusuyo uwekezaji.

Kauli mbiu ya Maonesho hayo kwa Mwaka 2020 inasema “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020“. Imeelezwa  kuwa Mwaka 2020 ni Mwaka wa Uchaguzi Mkuu  hivyo, Kaulimbiu inatoa hamasa kwa wananchi kuchagua viongozi bora watakaokuwa chachu ya kuleta mapinduzi kwa ajili ya maendeleo ya sekta za kilimo,ufugaji na uvuvi ili kuinua ustawi wa maisha ya wakulima, wafugaji, wavuvi na Taifa kiujumla.

Tunawakaribisha wadau wote kutembelea mabanda ya TIC kwenye maonesho ya NANENANE, Kanda zote ili kujifunza uwekezaji-biashara  katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi ili kujiletea mapinduzi ya uchumi ikiwemo kukidhi mahitaji ya viwanda, masoko na familia. 

Maadhimisho ya Sikukuu ya wakulima NANENANE Kitaifa yanafanyika katika viwanja vya Nyakabindi, Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu na yamefunguliwa na Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan terehe 1 Agosti,2020.

 

Post a Comment

0 Comments