Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiambatana na timu ya Wataalamu kutoka
Ofisi ya Waziri Mkuu amefanya ziara ya kikazi kwenye ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) tarehe 20
Februari, 2019. Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kukutana na Maafisa wa Taasisi
za Serikali wanaohudumia wawekezaji kupitia Mfumo wa Mahala Pamoja (One Stop
Facilitation Centre-OSFC). Alitumia ziara hiyo kusikiliza namna ambavyo Maafisa
wanavyofanya kazi zao ndani ya Mfumo ili kujifunza na baadae kutoa maagizo ya kuboresha utoaji wa huduma husika kwa
Wawekezaji.
Mhe. Kairuki akisisitiza jambo pembeni yake ni Mkurugenzi Mtendaji Geoffrey Mwambe |
Ziara hiyo imekuja zikiwa zimepita
takribani siku tano tu baada ya Mhe. Waziri kukutana na Watumishi wa TIC na
kufanya nao mkutano kwa kila idara kwa lengo la kujifunza majukumu ya kila
idara, kufahamu changamoto, kupokea
mapendekezo ya kuboresha utekelezaji wa majukumu hayo na kutoa maelekezo ya kuchapa kazi kwa kufuata
misingi ya weledi.
Baada ya Mhe. Waziri kukaribishwa
na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geoffrey Mwambe kwenye ofisi za Huduma za Mahala Pamoja,
alikaa kwa muda wa masaa manne na amekutana na mfanyakazi mmoja mmoja
anayewakilisha Taasisi zinazofanya kazi ndani ya Mfumo wa Mahala Pamoja ambapo
alipokea taarifa ya majukumu na ripoti ya utekelezaji.
Katika ziara hiyo, Waziri amekuta
TIC inatekeleza mfumo wa kielektroniki (TIW) ambao unatumiwa kupokea na kuchakata
maombi ya wateja kwa ajili ya cheti cha uwekezaji. Mhe. Waziri alivutiwa na
taarifa ya kutumika kwa mfumo na akahitaji kufahamu iwapo mfumo unatumika
kwenye ofisi zote za TIC zikiwemo zile za Kanda. Maelezo yalitolewa kwamba kwa
sasa mfumo huo unatumiwa TIC Makao Makuu na kwenye Kanda moja ya Kaskazini na
zoezi lipo mbioni kukamilika kwenye kanda zilizobaki.
Kufuatia maelezo hayo, Mhe.
Kairuki ameagiza TIC ikamilishe ndani ya mwezi mmoja kuunganisha mfumo huo
katika Kanda ambazo bado ili pia ziweze kuchakata maombi ya wawekezaji
kielektroniki. Kwa kufanya hivyo kutaharakisha zoezi la upatikanaji wa cheti
cha uwekezaji na huduma nyingine kwa wawekezaji kiujumla. Ni wazi mfumo huo unasaidia kuondokana na
urasimu, ucheleweshwaji na unarahisisha upatikanaji wa huduma nyingine ambazo
ni upatikanaji wa leseni, cheti na vibali ambavyo mwekezaji anahitaji ili
kuanzisha mradi wa uwekezaji nchini’ Amesema Kairuki’.
Kaimu meneja wa miradi Bi Phina Lyimo akimpa maelezo Mhe. Kairuki juu ya mahitaji ya kusajili mradi na Kituo |
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji
wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe alisema iwapo
Serikali itawezesha taasisi zote zinazohusika na huduma za mahala pamoja kutoa
idhini huduma mbalimbali za uwekezaji ndani ya ofisi za TIC itakuwa ni hatua
kubwa uwekezaji nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC akimfafanulia jambo Mhe Waziri alipokuwa akijifunza kutoka kwa Afisa wa TBS |
“Taasisi zilizopo ndani ya mfumo
wa mahala pamoja zinafanya kazi kubwa, tunachoomba sisi kama TIC ni kwamba
huduma za taasisi hizo kwa wawekezaji zikamilike ndani ya TIC badala ya kwenda
kwenye makao makuu ya ofisi hizo kufuata idhini ya vibali, leseni na vyeti
husika kwa wawekezaji” alisema Mwambe.
Katika mazungumzo yake na
wawakilishi wa idara, Mhe. Waziri aliwataka watendaji wa ardhi ndani ya Kituo
hicho kuweka vizuri takwimu za ardhi ya uwekezaji na kushughulikia changamoto
za upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji .
Mhe. Kairuki akipata maelezo kwa Afisa wa Idara ya Ardhi Bi Mwanamkuu Hashim |
Akiwa katika sehemu ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania TRA Waziri Kairuki aliagiza watendaji hao kuona umuhimu wa utoaji wa
cheti cha walipakodi wakubwa (VAT) ndani ya Kituo ili kurahisisha huduma
kwa wawekezaji.
Mhe. Waziri akipata maelezo kutoka kwa Afisa wa TRA Leonard Mapunda |
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya huduma kwa wawekezaji
Anna Lyimo alisema kwa sasa huduma za mahala pamoja zimekuwa na manufaa makubwa
kwa wawekezaji kutokana na kuwapo kwa taasisi nyingi muhimu Kituoni ambazo zinamuwezesha
kupata huduma husika na kwamba
marekebisho yaliyotajwa na Waziri yatafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo.
“Tumeyapokea maagizo ya Waziri na
tutayafanyia kazi, ni maagizo yenye tija kwa kituo” alisema Kaimu Mkurugenzi
Idara ya Huduma za Mahala Pamaoja wa TIC Anna Lyimo.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma za Mahala Pamaoja wa TIC Anna Lyimo akimfafanulia jambo Mhe. Waziri |
Taasisi za zilizopo ndani ya
mfumo wa Huduma za mahala pamoja kwenye Kituo cha uwekezaji Tanzania TIC
zinajumuisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Baraza la Taifa la usimamizi na
uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA),
Shirika la viwango Tanzania (TBS), Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na wenye
ulemavu, Wizara ya Ardhi, Idara ya Uhamiaji,Wakala wa Usalama na Afya mahala pa
kazi (OSHA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA na Mamlaka ya vitambulisho vya
Taifa (NIDA).
Mhe. Waziri pia alipata nafasi ya kuwasalimia wateja waliokuwa ndani ya mfumo wa mahala pamoja ili kupata huduma |
0 Comments