![]() |
Mkurugenzi Mtendaji akijibu maswali ya washiriki baada ya kuwasilisha hotuba yake |
Suala
la ukuzaji wa kada ya ujasiriamali mdogo na wa kati (SME) siyo tu limesisitizwa
na Ilani ya Chama Tawala, bali pia ni utekelezaji wa majukumu ya Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC) kama lilivyoanishwa na Mpango Mkakati wa Kituo
2016-2021. Ni katika kutekeleza majukumu hayo Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi
Mtendaji wa TIC ameshiriki kama Mgeni Rasmi katika Kongamano la Uchumi na
Uwekezaji lililoandaliwa na UVCCM SENETI Mtwara kwenye ukumbi wa Stella Maris
University Mtwara tarehe 30 Machi, 2019. Lengo la kongamano lilikuwa ni
kujadili uwekezaji unavyotatua changamaoto za ajira kwa vijana.
![]() |
Sehemu ya washiriki wa kongamano |
Hotuba ya mgeni rasmi, ilijawa na maneno ya hamasa kwa vijana
ambapo amewataka kujiamini na kuthubutu katika kuibua na kutekeleza miradi ya
uchumi kwenye sekta za kipaumbele ambazo ni kilimo, viwanda, madini, mifugo na
uvuvi. Washiriki wameelezwa kutafiti na kutambua fursa zinazowazunguka mahali
walipo na kuibua miradi ya uwekezaji inayoweza kutekelezwa kwa lengo la
kutengeneza ajira na kuzalisha bidhaa au huduma zinazolenga kuinufaisha jamii
na Taifa kwa ujumla. Kwa muktadha huo vijana wameelezwa kwamba mtazamo wao wa
kwanza wa kupata ajira iwe ni ile inayotokana na uwekezaji wao wenyewe/
kujiajiri. Hivyo kujiamini na kuthubutu ni hatua kwa vijana katika kutengeneza
ajira badala ya kutegemea dhana iliyozoeleka ya kutafuta ama kusubiri
kuajiriwa.
![]() |
Washiriki waliposimamam kumkaribisha Mgeni Rasmi Geoffrey Mwambe alipokuwa akiingia ukumbini |
Elimu ya uwekezaji na uchumi iliyotolewa kupitia kongamno hilo,
inatafsiriwa kuwa ni mbegu bora ya maendeleo iliyopandwa kwa takribani
washiriki 600 wengi wao wakiwa vijana ambao ni wawekezaji watarajiwa kwa jamii
ya Watanzania na Taifa kiujumla. Kinachotakiwa ni vijana kuanza utekelezaji wa
kuyaishi yote waliyoelekezwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi vya watu
watano sambamba na kusajili kampuni. Baada ya kusajili kampuni wafuate hatua
inayofuata ya kubuni/kuibua miradi mbalimbali ya uchumi kwa utekelezaji. Mwambe
alisema ‘utekelezaji wa uanzishaji wa vikundi ni hatua muhimu kwa vijana
kutokana na ukweli kwamba itawasaidia kunufaika na vyanzo vya fedha za
uwezeshaji kutoka Serikalini na sekta binafsi inayotolewa kupitia kwenye
vikundi kwa ajili ya mitaji ya kutekeleza shughuli/miradi ya kiuchumi na
uwekezaji .
![]() |
Mmoja wa Walimu wa Chuo cha Stella Maris University akichangia hoja juu ya Serikali kusisisitiza utekelezaji wa sera ya kujitegemea kwa wanavyuo kam ilivyokuwa zamani |
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu. Mhe Moses Machali
alitumia kongamano hilo pia kutoa ufafanuzi zaidi ya kwamba vijana waamke
kutumia fursa za uwekezaji zilizopo ili kuibua miradi ya uchumi na uwekezaji
katika maeneo yanayowazunguka. Vijana kuweni na tabia ya kujishughulisha
kutekeleza miradi ya kiuchumi ikilenga maeneo ya uzalishaji, usambazaji na
ulaji. Kwa msisitizo Mhe.Machali alisema ‘Vijana wakati huu ni wa kupambana na
kuthubutu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Ni wajibu wa vijana kuchukua
hatua kwa vitendo katika kuanzisha miradi ambayo itachangia kwenye maeneo
matatu makuu ya uchumi ambayo ni uzalishaji ‘production’ usambazaji
‘distribution’ na ulaji ‘consumption’.
![]() |
Mwanafunzi wa mwaka wa pili akieleza namna ambavyo wanafunzi wanatakiwa kuzingatia elimu wanayopewa ili wanapohitimu waweze kuitumia kivitendo katika sehemu zao za kazi. |
Mwambe amewahakikishia wadau wengine utayari wa Kituo kushiriki
kwenye makongamano ya aina hiyo yenye lengo la kutoa elimu kwa washiriki juu ya
uchumi na uwekezaji kwa manufaa ya nchi yetu. Mwisho, anawakaribisha wadau wote
kutembelea ofisi za TIC zinazopatikana Dar es Salaam Makao Makuu mtaa wa
Shabaan Robert na katika Ofisi za TIC za Kanda zinazopatikana nchini. Lengo ni
kupata miongozo na kushauriana/kujadiliana namna ya kuibua na kuanzisha miradi
ya uwekezaji kupitia fursa zinazopatikana katika maeneo yanayotuzunguka.
Akitambulisha Ofisi za Kanda Mwambe amesema, Ofisi za TIC Kanda ya Kusini
zinapatikana Mtwara Jengo la Mkuu wa Mkoa, Ofisi za TIC Kanda ya Mashariki
zinapatikana Dar es Salama Jengo la TIC Makao Makuu, Ofisi za TIC Kanda ya Kati
zinapatikana Dodoma Jengo la Manispaa, Ofisi za TIC Kanda ya Magharibi
zinapatikana Kigoma Jengo la Mkuu wa Mkoa, ofisi za TIC Kanda ya Kaskazini
zinapatikana Moshi Jengo la Mkuu wa Mkoa, Ofisi za TIC Kanda ya Ziwa
zinapatikana Mwanza Barabara ya Kenyatta na ofisi za TIC Kanda ya Nyanda ya Juu
Kusini zinapatikana Mbeya Jengo la Benki ya NBC.
0 Comments