Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Mtwara, Tanzania
Waziri
Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema mtu yoyote anayekwaza wawekezaji
nchini Tanzania atachukuliwa hatua kali, hivyo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa
Mtwara Gelasius Byakanwa amchukulie hatua Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Mtwara, Bw. Maisha Selemani Mtipa baada ya kumtaka mwekezaji alipe sh. milioni
31.6 kwa ajili ya gharama za vikao ili aweze kupatiwa eneo.
Ametoa agizo hilo
Ijumaa, Novemba 01, 2019, wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji na Maonesho
ya Biashara mkoa wa Mtwara lililofanyika kwenye Viwanja vya Chuo cha Ualimu
Mtwara. “Yoyote anayekwaza uwekezaji nchini kwa kuwasumbua wawekezaji
tutamshughulikia kabla ya kuwasumbua wawekezaji.” Amesema Bw. Mtipa
amemwandikia barua mwekezaji wa kampuni ya MBR Internation Company Limited
akimtaka alipe sh. milioni 31.6 kwa ajili ya kulipa kamati mbalimbali zikiwemo
sh. milioni 1.95 kwa kamati ya Menejimenti ya Halmashauri.
Waziri Mkuu amesema
“fedha nyingine sh. milioni 2.27 kwa kamati ya kugawa ardhi ya wilaya, sh.
milioni 4.43 kamati ya Uchumi Ujenzi na Mazingira, Kamati ya Fedha, Utawala na
Mipango
sh. milioni 5.14 na sh milioni 17.79 Baraza la madiwani ili wagawane tu, huu ni
utaratibu wa wapi? huku ni kufukuza na kukwaza wawekezaji.”
Waziri Mkuu amesema
Serikali imeshaondoa tozo zaidi ya 150 zilizokuwa zinakwaza wawekezaji kupata
uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo haitaki kusikia mahali popote
panawekwa tozo zenye kuwakwaza wawekezaji. Amesema hatua zitakazochukuliwa kwa
Bw. Mtipa ziwe fundisho kwa halmashauri zote nchini.
Mapema, Waziri Mkuu
alizungumzia uuzwaji wa korosho na kuagiza kwamba mfumo uliotumika katika mnada
wa kwanza wa uuzwaji wa zao la korosho uliofanyika Alhamisi, Oktoba 31, 2019
ndio unaopaswa kuendelea, hivyo ameagiza wahusika wausimamie vizuri ili
usiingie dosari.
Waziri Mkuu amesema,
Serikali ilibaini changamoto katika uuzwaji wa mazao mengine ya pamba na kahawa
ya uwepo wa watu ambao wananunua mazao nje ya mfumo kama kangomba, hivyo ni muhimu
wakadhibitiwa ili fedha zote ziende kwa wakulima. Pia Waziri Mkuu aliagiza
maandalizi yawe yanakwenda pamoja na msimu kama suala la magunia wasiachiwe
watu wa ushirika pekee bali Wakuu wa Mikoa na Wilaya nao washiriki katika
kutatua tatizo hilo ili minada ifanyike kikamilifu.
Pia chama kikuu cha
ushirika pamoja na vyama vya msingi wazuie kuwepo kwa makato ya hovyo ambayo
yalishaondolewa na Serikali ili kuhakikisha mkulima haumizwi kwa kupunguzwa kwa
malipo yake. Amewataka viongozi hao wasimamie mtiririko wa fedha kutoka
kwa wafanyabiashara kwenda kwa mkulima na wahakikishe zinaingizwa katika
akaunti za wakulima. Pia sheria ya ununuzi isimamiwe baada ya mnunuzi kupewa
zabuni anatakiwa alipe ndani ya siku nne. “Sheria hii itaondoa watu wa kati na
kumwezesha mkulima kulipwa fedha zake kwa wakati.”
Kwa upande wake, Mkuu wa
Mkoa amesema amesema wanunuzi wote wametakiwa wahakikishe wakulima wanalipwa
kwa wakati. “Bei ya chini katika mnada wa korosho uliofanyika Mtwara ilikuwa
sh. 2,409 na bei ya juu ilikuwa 2,559 na hali inaonesha uhitaji wa korosho
duniani ni mkubwa kutokana na ubora wake.”
Amesema chama cha
ushirika cha TANECU waliingiza sokoni tani 13,000 huku mahitaji yakiwa ni tani
40,000 na chama cha ushirika cha MAMCU walipelela sokoni tani 7,000 na mahitaji
yalikuwa tani 22,000 hivyo wafanyabiashara wengi walikosa korosho.
Akizungumziakuhusu
kilimo cha zao la korosho, Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa mkoa wa
Mtwara kuwa wasibweteke kwani mikoa mingine nayo imeanza kulima korosho, hivyo
waweke mikakati mizuri ili zao la korosho liendelee kuwa zao kuu la biashara
kwa mkoa. Amesema Serikali kwa upande wake, itaendelea kuweka mazingira rafiki
na miundombinu wezeshi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza
mkoani Mtwara.
“Tusisahau kuwa Mkoa wa
Mtwara ni korosho na korosho ndiyo mkoa. Hili linadhihirishwa na usemi wa wenyeji
kuwa korosho ni dhahabu ya kijani. Mtwara ndiyo mzalishaji mkubwa wa korosho
Tanzania, huzalisha zaidi ya asilimia 65 ya korosho zote nchini.”
Kadhalika, Waziri Mkuu
ametumia fursa hiyo kuwaasa wawekezaji wote kwamba waondoe hofu kuhusu kuwekeza
Mtwara kwa sababu mkoa wa Mtwara wa sasa ni tofauti na Mtwara ile waliyokuwa
wanaisikia zamani, uchumi wake unakuwa.
Waziri Mkuu amesema
ushiriki wao kwenye kongamano hilo unaonesha utayari walionao katika kuiunga
mkono Serikali kwa lengo la kuwaletea maendeleo na kujenga Tanzania ya Uchumi
wa Viwanda ambayo wote wanaitamani.
Kongamano hili na
mengine yaliyofanyika kwenye mikoa mbalimbali ni utekelezaji wa agizo la Waziri
Mkuu alilolitoa wakati anafungua Kongamano la tatu la uwezeshaji wananchi
kiuchumi jijini Dodoma Juni 18, 2018, ambapo aliagiza mikoa yote kuandaa
Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa. “Niendelee kusisitiza tena kwa mikoa ambayo bado
haijatekeleza agizo hili la kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji ifanye hivyo mapema.”
Wakati huo huo, Waziri
Mkuu amesema, licha ya Serikali kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye miradi ya
kijamii katika Mkoa wa Mtwara, pia imewekeza kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ambayo
inachochea kukua kwa uchumi kwa haraka. Waziri Mkuu ameitaja miradi hiyo
ni pamoja na upanuzi wa uwanja wa ndege na bandari ya Mtwara; ujenzi wa
barabara ya lami kutoka Mtwara hadi Nanyumbu mpakani na Msumbiji; ufufuaji na
ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho.
Miradi mingine ni ujenzi
wa reli kutoka Mtwara hadi Songea kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe kutoka
Mchuchuma na chuma kutoka Liganga na kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia
gesi asilia na vyanzo vingine. Ufunguzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi -
Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki, Waziri wa Kilimo Josephat
Hasunga, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, Mkuu wa Mkoa wa
Lindi, Godfrey Zambi, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme na watendaji
wengine wa Serikali.
0 Comments