HOTUBA
YA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA KASSIM M.
MAJALIWA (MB.), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA
MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE
KWA
MWAKA 2020/2021
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge
lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Mfuko wa Bunge na Ofisi
ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya
Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2019/2020 na Mwelekeo wa Kazi
za Serikali kwa Mwaka 2020/2021. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu likubali
kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
Taasisi zilizopo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Spika,
wakati tunapojadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa
Mwaka 2019/2020 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2020/2021 hatunabudi
kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kutujaalia afya na
uzima.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2019/2020, Bunge lako Tukufu lilimpoteza aliyekuwa Mbunge wa Jimbo
la Newala Vijijini, Mheshimiwa Rashid Ajali Akbar. Pia naungana na Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Watanzania wenzangu kutoa salam za pole kwa familia ya Marehemu na wanachama wa
CUF kufuatia kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa
Alhaji Khalifa Suleiman Khalifa. Pia kwa masikitiko makubwa niungane na
wananchi wote, familia na wanahabari wote nchini kwa kifo cha Mwandishi wa
Habari Mwandamizi wa Shirika la Habari Tanzania (TBC) ndugu yetu Marin Hassan
Marin kilichotokea leo alfajiri, Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema
peponi – Amina. Vilevile, Taifa letu lilikumbwa na majanga mbalimbali ikiwa ni
pamoja na mafuriko nchini kote na ajali za barabarani ambazo zilisababisha
vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
Mheshimiwa Spika,
sambamba na kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki kwa misiba iliyotokea,
tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu awajaalie afya njema waliopata majeraha na
azipumzishe roho za marehemu mahali pema peponi. Amina! Vilevile, nawashukuru
kwa dhati wale wote waliojitolea kwa hali na mali katika kuwasaidia majeruhi na
wahanga wa matukio hayo.
Mheshimiwa Spika, kama
tunavyofahamu, mwaka huu Serikali ya Awamu ya Tano inahitimisha kipindi cha
kwanza cha miaka mitano kilichoanza Mwaka 2015. Kwa msingi huo, hotuba yangu
itaeleza kwa muhtasari baadhi ya mafanikio makubwa ambayo Serikali imeyapata
katika kipindi cha takriban miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mheshimiwa Spika,
hotuba hii inaainisha baadhi ya kazi zilizotekelezwa na Serikali kwa kuzingatia
mipango na mikakati mbalimbali hususan Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka
Mitano wa Mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Dira
ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025. Mikakati na Mipango hiyo, inatekelezwa
sambamba na mipango mingine ya kikanda na kimataifa kama vile Agenda ya Mwaka
2063 ya Umoja wa Afrika na Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya Mwaka 2030.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, tumeshuhudia mafanikio
makubwa katika kuimarisha miundombinu, huduma za kiuchumi na kijamii, utawala
bora, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi pamoja na kuhamasisha uwekezaji. Ningependa
kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri wa Serikali ya Awamu
ya Tano katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka
2015 hadi 2020. Nawapongeza pia, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mheshimiwa Balozi Seif Ally
Idd, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kusimamia
vyema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika,
kipekee nakushukuru wewe binafsi, pia Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wa
Bunge kwa kuliongoza vyema Bunge lako Tukufu na Wabunge wote katika kuisimamia
Serikali kuhakikisha kuwa inatekeleza wajibu wake ipasavyo wa kuhudumia
wananchi. Vilevile, natoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati za Kudumu za Bunge
kwa kazi kubwa ya kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa,
Wakala, Idara zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kipekee,
nawashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria chini
ya uenyekiti wa Mhe. Mohammed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Jimbo la Rufiji;
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI chini ya uenyekiti wa Mhe. Oscar
Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi na Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Bajeti chini ya uenyekiti wa Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge
wa Jimbo la Maswa Magharibi. Maoni na ushauri wa Kamati hizo umesaidia sana
kuboresha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
Mfuko wa Bunge kwa Mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Spika,
nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa
Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala na Taasisi zote za Serikali
kwa ushirikiano mlionipatia katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Aidha, nawashukuru wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake kwa kutekeleza
majukumu yao kwa weledi mkubwa na hivyo, kuwezesha Serikali kutekeleza kazi
zake kwa tija na ufanisi. Vilevile, nawashukuru kwa michango yenu iliyowezesha
kukamilisha Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Spika, kwa
namna ya pekee kabisa, namshukuru Mhe. Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Jimbo
la Peramiho na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu); Mhe. Angellah Jasmine Kairuki, Mbunge wa Viti Maalum
na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji); Mhe. Anthony Peter
Mavunde, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira); Mhe. Stella Alex Ikupa, Mbunge wa Viti
Maalum na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu);
Makatibu Wakuu Bw. Andrew Wilson Massawe (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu), Bibi Dorothy Aidan Mwaluko (Sera, Uratibu na Uwekezaji) na Bw. Tixon
Tuyangine Nzunda (Waziri Mkuu na Bunge) na Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi
zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu na
Wafanyakazi wote kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia katika kutekeleza majukumu
ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika,
napenda pia kuwashukuru washirika wa maendeleo zikiwemo nchi rafiki, taasisi na
mashirika ya kimataifa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali,
kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga uchumi wa viwanda
na kuiletea nchi yetu maendeleo. Mchango wao umekuwa muhimu kuwezesha nchi yetu
kupiga hatua kubwa kimaendeleo kulingana na mipango tuliyojiwekea.
Mheshimiwa Spika,
ninawashukuru wananchi wote kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya
Tano katika kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Aidha, nawashukuru wananchi wa
Jimbo la Ruangwa kwa kuendelea kushirikiana nami na kwa kuniunga mkono.
Niwapongeze na kuwashukuru kwa kutekeleza shughuli za maendeleo jimboni kwa
ufanisi. Kipekee, namshukuru sana mke wangu mpendwa, Mary; watoto wangu na
familia yangu kwa ujumla kwa upendo wao, uvumilivu na maombi yao wakati wote
ninapotekeleza majukumu yangu ya kitaifa. Nawashukuru sana.
Homa Kali ya Mapafu
Mheshimiwa Spika, hivi
sasa nchi yetu na dunia kwa ujumla inapitia katika kipindi kigumu. Itakumbukwa
kwamba, tarehe 11 Machi 2020, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko
wa Homa Kali ya Mapafu ijulikanayo kama COVID-19 inayosababishwa na virusi vya
CORONA kuwa ni janga la Kimataifa. Aidha, tarehe 16 Machi, 2020 Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli ilitangaza kuwepo kwa mgonjwa wa kwanza nchini.
Mheshimiwa Spika, tangu
kugundulika kwa ugonjwa huo, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali
katika kukabiliana na ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukaguzi,
upimaji na ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini ili kubaini wasafiri
wanaoonesha dalili za ugonjwa au wenye viashiria hatari hata hivyo mashirika
mengi yamesitisha ndege zao kwa kukosa abiria. Abiria waingiao wote hupelekwa
nyumba ya kujitenga kwa gharama zao, tumetenga na hostel ili kuwapunguzia
gharama. Kadhalika, katika kukabiliana na virusi vya CORONA, Serikali ilitoa
maelekezo yafuatayo:
Moja: Kusitisha Mbio za
Mwenge wa Uhuru na kwamba fedha zilizotengwa kwa ajili ya jukumu hilo zitumike
kusaidia hatua za kukabiliana na janga la virusi vya Corona;
Mbili: Kusitisha
michezo yote inayokusanya makundi ya watu ikiwemo ligi kuu ya Tanzania Bara,
ligi daraja la kwanza, ligi daraja la pili na aina nyingine za michezo;
Tatu: Kusitisha
shughuli zote za elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, Sekondari, vyuo vya kati
hadi vyuo vikuu;
Nne: Kusitisha Semina,
Warsha, Makongamano na Mikutano yote ya ndani na ya hadhara yenye kuhusisha
mjumuiko wa watu wengi;
Tano: Kuwatenga abiria
waingiao nchini kwenye maeneo maalum kwa siku 14 ili kufuatilia hali zao mpaka
tutakapojiridhisha kuwa hana ugonjwa;
Sita: Kuwasisitiza
watanzania kufuata kanuni za kudhibiti maambukizi ikiwemo kunawa maji kwa
sabuni, kukinga unapokohoa na kupiga chafya, kutopeana mikono bila sababu,
kukaa au kusimama kwa umbali na jirani yako n.k; na
Saba: Kuwaasa
Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi ya virusi
vya Corona, kusitisha safari hizo, na hatua zingine zitafuata.
Mheshimiwa Spika,
serikali inaendelea na usimamizi wa karibu sambamba na kufanya tathmini na
kuchukua hatua kadhaa. Tumeunda Kamati za kitaifa tatu (3) zinazosimamia
ugonjwa huu, niendelee kusisitiza kuwa sote tuzingatie maelekezo yaliyotolewa
na Serikali toka tulipoanza kampeni ya kupambana na ugonjwa huu. Aidha,
niwatake Watanzania kuzingatia masharti ya afya kwa kufuata ushauri unaotolewa
na wataalam. Mgonjwa akithibitika, atapelekwa eneo maalum bila kujali cheo
chake, atalala palipoandaliwa. Watanzania wenzangu tuendelee kupuuza taarifa za
uzushi zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii.
MAFANIKIO
YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO
Mheshimiwa Spika,
tarehe 20 Novemba 2015 wakati akifungua rasmi Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaahidi wananchi wote kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano itawatumikia na kuwajali.
Mheshimiwa Spika,
katika kutekeleza azma hiyo, ndani ya kipindi cha takriban miaka mitano
mafanikio makubwa yamepatikana na yamesaidia kuimarisha hali ya kiuchumi na
kijamii kwenye Taifa letu. Ujenzi wa miundombinu muhimu ya kiuchumi hususan ya
usafiri na usafirishaji sambamba na uimarishaji wa huduma muhimu za kijamii ni
miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Spika,
ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge Railway),
ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania, ufufuaji wa ushirika na mali za
ushirika mfano, NCU, SHIRECU, WETCU na Mamlaka ya Mkonge Tanzania, ujenzi wa
Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, ulinzi wa maliasili na rasilimali zetu
pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Elimu, Afya na Maji ni kati ya
hatua za msingi zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kufikia
uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo Mwaka 2025.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi hiki cha miaka mitano, tumeshuhudia miradi hiyo muhimu ikiwa
katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kwa mfano, ujenzi wa Reli ya Kati kwa
kiwango cha Kimataifa ambao hadi Machi 2020 umetumia Shilingi trilioni 2.96 na
kukamilika kwa asilimia 75 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro na
asilimia 28 kwa kipande cha Morogoro hadi Makutupora.
Mheshimiwa Spika,
Serikali inatumia gharama kubwa katika kujenga miundombinu hiyo wezeshi ya
kiuchumi kwa lengo la kulifanya Taifa letu kuwa na uchumi imara wa kujitegemea
na wenye kuhimili ushindani. Fedha hizo pia zimekuwa chanzo cha ajira na zabuni
kwa Watanzania zinazowasaidia kuongeza kipato.
Mheshimiwa Spika, mradi
huu utakapokamilika utaongeza ufanisi wa huduma za usafiri na usafirishaji wa
bidhaa na abiria pamoja na kupunguza gharama za uchukuzi. Kadhalika, utachochea
ukuaji wa miji na sekta nyingine kama vile kilimo, viwanda, utalii na biashara.
Vilevile, mradi huu utakuwa chanzo cha ongezeko la mapato ya Serikali
yatakayosaidia katika kuboresha maslahi ya watumishi na huduma za kijamii kama
vile afya, elimu na maji.
Mheshimiwa Spika,
vilevile, ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere
ambalo litakapokamilika litazalisha umeme wa Megawati 2,115. Hadi Machi 2020
mradi huo umegharimu Shilingi trilioni 1.28 na umekamilika kwa asilimia 10.74.
Kukamilika kwa bwawa hilo kutalihakikishia Taifa letu umeme wa uhakika na wa
nafuu zaidi. Aidha, ongezeko hilo la uzalishaji wa umeme litawezesha shughuli
za uzalishaji viwandani kuwa za uhakika, tija, ufanisi na gharama nafuu.
Vilevile, mradi huu utachangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za kuhifadhi
mazingira kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya nishati ya umeme kwa watu
wengi.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imefanikiwa kutekeleza Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA)
ambapo vijiji vilivyounganishiwa umeme nchini vimeongezeka kutoka vijiji 2,118
Mwaka 2015 hadi vijiji 9,001 mwezi Machi 2020. Mradi huo pia umezinufaisha
Taasisi 11,128 zikiwemo za elimu, afya, dini, mashine za kusukuma maji na huduma
za biashara.
Mheshimiwa Spika,
katika kuimarisha huduma za usafiri wa anga, Serikali inaendelea kuliimarisha
Shirika la Ndege la Tanzania. Hadi kufikia Machi, 2020 tayari ndege 8 mpya
zenye thamani ya Shilingi trilioni 1.27 zimepokelewa na kuanza kazi. Kadhalika,
malipo ya awali ya Shilingi bilioni 85.7 kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine
3 mpya yamefanyika. Ununuzi wa ndege hizi, umeongeza ufanisi katika usafiri wa
anga, kuongezeka kwa mapato ya Serikali, kuimarika kwa utalii na kuongezeka kwa
fursa za ajira katika sekta ya huduma.
Mheshimiwa Spika,
bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi imeongezeka kutoka Shilingi
bilioni 31 kwa Mwaka 2015 hadi Shilingi bilioni 269 kwa Mwaka 2019. Serikali
pia imegharamia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya kwa kujenga
zahanati 1,198, ukarabati wa vituo vya afya 487, hospitali za Halmashauri za
Wilaya 69 na hospitali za rufaa za mikoa 10 za Njombe, Simiyu, Mara, Geita,
Songwe, Katavi, Sekou Toure, Mwananyamala, Mawenzi, Manyara, hospitali za rufaa
za kanda 3 za Mtwara, Mbeya na Burigi-Chato na Hospitali Maalum ya Kibong’oto
na Uhuru - Chamwino. Katika kipindi cha Julai 2015 hadi Januari 2020 jumla ya
Shilingi trilioni 3.01 zimetumika kugharamia huduma za afya. Kuongezeka kwa
bajeti ya dawa na uboreshaji wa miundombinu ya afya, kumeleta mapinduzi makubwa
katika sekta ya afya kwa kuimarisha afya za Watanzania.
Mheshimiwa Spika, nyote
mtakubaliana nami kuwa ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya, ununuzi wa
dawa na vifaa vya kisasa vya tiba ni utekelezaji wa dhamira ya dhati ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha kila Mtanzania anapatiwa haki yake ya
kupata matibabu tena katika eneo alipo.
Mheshimiwa Spika,
katika eneo la elimu, Serikali imeongeza mikopo kwa ajili ya elimu ya juu
kutoka Shilingi bilioni 365 Mwaka 2015 hadi Shilingi bilioni 450 Mwaka 2019.
Elimumsingi bila Ada nayo imetekelezwa kwa mafanikio makubwa na kuhakikisha
watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa na kupatiwa elimu.
Mheshimiwa Spika,
utekelezaji mzuri wa Mpango wa Elimumsingi bila Ada, uliwezesha kuongezeka kwa
idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza. Kwa mfano, kabla ya kuanza
kwa Mpango huo Mwaka 2015 ni wanafunzi 1,568,378 walioandikishwa. Aidha, baada
ya kuanza utekelezaji wa Mpango Elimumsingi Bila Ada wanafunzi 2,120,667
waliandikishwa Mwaka 2016. Katika kipindi cha mwaka 2015 hadi Februari 2020
jumla ya Shilingi trilioni 1.2 zimetumika kugharamia Elimumsingi Bila Ada.
Mheshimiwa Spika,
maboresho yanayofanyika kwa upande wa elimumsingi yanazingatia uhitaji wa
miundombinu ya kujifunzia na kufundishia. Kuanzia Mwaka 2015 hadi Februari,
2020 vyumba vya madarasa 166,627, maabara 5,801, nyumba za walimu 57,541,
matundu ya vyoo 231,612 yamejengwa na madawati 2,886,459 yamenunuliwa. Aidha,
idadi ya shule za msingi zenye madarasa ya elimu ya awali imeongezeka kutoka
madarasa 16,889 Mwaka 2015 hadi kufikia madarasa 17,771 Mwaka 2020. Kadhalika,
idadi ya shule za sekondari imeongezeka kutoka shule 4,708 Mwaka 2015 hadi
shule 5,330 Mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika,
utekelezaji wa Mpango wa Elimumsingi Bila Ada unawahakikishia watoto wote wa
kitanzania hususan wale wa hali ya chini kupata haki yao ya msingi ya kupata
elimu. Aidha, Mpango huo umewapunguzia wazazi mzigo wa ada na michango
isiyokuwa ya lazima na hivyo kujielekeza zaidi katika kutafuta na kuwapatia
mahitaji ya msingi vijana wetu kama vile sare za shule na madaftari.
Mheshimiwa Spika, kama
utakavyokumbuka, katika vikao vingi vya Bunge lako Tukufu vilivyotangulia,
changamoto ya maji ni suala lililoongoza kuchangiwa Bungeni na Waheshimiwa
Wabunge. Katika kipindi cha takribani miaka mitano, Serikali yetu sikivu ya
Awamu ya Tano imetekeleza ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji 1,423. Kati ya
miradi hiyo, 792 imekamilika ikihusisha miradi 710 vijijini na miradi 82
mijini. Vilevile, Serikali ilipokea ombi la Waheshimiwa Wabunge na kuanzisha
Mfuko wa Taifa wa Maji na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira
Vijijini (RUWASA). Lengo la Serikali ni kuhakikisha vyombo hivi vinakuwa chanzo
cha uhakika cha upatikanaji wa fedha za kugharamia miradi ya maji na kusimamia
utoaji wa huduma ya maji na usafi wa mazingira. Juhudi hizi kwa pamoja
zitasaidia kusogeza huduma ya maji kwa kasi zaidi karibu na wananchi katika
maeneo ya mijini na vijijini.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha takriban miaka mitano, Serikali imefanikiwa kulinda na
kuendeleza rasilimali na maliasili za Taifa hususan madini na kuhakikisha
zinatumika kwa maslahi mapana ya Taifa na watu wake. Mafanikio hayo, yametokana
na Serikali kutekeleza kwa ufanisi mkubwa Mkakati wa Utekelezaji wa Sheria ya
Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Utajiri na Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017 na
Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya
Utajiri na Maliasili za Nchi ya Mwaka 2017.
Mheshimiwa Spika,
utekelezaji wa mkakati na sheria hiyo umechangia kuongezeka kwa maduhuli ya
Serikali yatokanayo na sekta ya madini mwaka hadi mwaka. Maduhuli ya Serikali
yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 205.2 Mwaka 2015/2016, hadi Shilingi
bilioni 346.6 Mwaka 2018/2019. Aidha, katika Mwaka 2019/2020 Serikali
inatarajia kukusanya Shilingi bilioni 471.
Mheshimiwa Spika,
ukusanyaji wa mapato nao umeongezeka kutoka wastani wa Shilingi bilioni 850 kwa
mwezi Mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa Shilingi trilioni 1.3 Mwaka 2019.
Ongezeko hili limechangiwa na hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali
hususan kuimarisha matumizi ya mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia za
kielektroniki, kuongeza idadi ya walipa kodi na kuibua vyanzo vipya vya mapato.
Aidha, ongezeko hilo limekuwa chachu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo
ambayo imesaidia kuimarisha utoaji wa huduma pamoja na kusogeza huduma hizo
karibu na wananchi.
Mheshimiwa Spika,
nichukue fursa hii kuwashukuru wananchi na walipa kodi wote kwa kuendelea
kuitikia wito wa Serikali wa kulipa kodi kwani hatua hiyo ni muhimu katika
kulifanya Taifa letu kujitegemea. Serikali itaendelea kusimamia matumizi kwa
lengo la kuongeza ufanisi na tija kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Spika,
Serikali pia imefanikiwa kudhibiti matumizi ya hovyo ya fedha za Umma kwa
kuziba mianya ya ukwepaji kodi sambamba na kuhakikisha kwamba wale wote
wanaotakiwa kulipa kodi wanafanya hivyo. Kwa mfano, katika kipindi cha miaka
mitano (2015 – 2019), Serikali imeweza kuokoa Shilingi bilioni 19.83 ya
mishahara kwa kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo watumishi hewa 19,708 na wenye
vyeti vya kughushi 15,411. Msingi huu tunaojenga ni muhimu katika kujenga
uchumi imara na usio tegemezi.
Mheshimiwa Spika,
katika siku ya Mashujaa iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mashujaa Jijini
Dodoma tarehe 25 Julai 2016, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitangaza na kusisitiza azma ya Serikali
kuhamia Dodoma ambapo alisema, nanukuu:
“.......ninazungumza
kutoka kwenye dhamira yangu kabla sijamaliza kipindi changu cha miaka mitano
Serikali yote itakuwa hapa Dodoma.....”
Mheshimiwa Spika,
ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na watanzania kuwa tayari Serikali
imehamia Dodoma. Hadi Machi 2020, jumla ya watumishi 15,361 wa Wizara na
Taasisi za Serikali wamehamia Makao Makuu ya Serikali Dodoma, ujenzi wa awali
wa ofisi za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba umekamilika, maandalizi ya
ujenzi wa majengo ya ofisi za Serikali awamu ya pili na ujenzi wa barabara kwa
kiwango cha lami katika mji huo unaendelea. Vilevile, Serikali imekamilisha
mapitio ya Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma ambao niliuzindua tarehe 13
Februari 2020 kwa ajili ya kusimamia shughuli za upangaji wa Jiji la Dodoma.
Naielekeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kusimamia ipasavyo utekelezaji wa
mpango huo ili kuhakikisha Jiji la Dodoma linaendelezwa kwa kuzingatia Mpango
huo.
Mheshimiwa Spika, nyote
mtakubaliana nami kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa katika usimamizi
madhubuti wa sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa viongozi na watumishi
wa umma. Usimamizi huo, umewezesha viongozi na watendaji wa umma kuwajibika
ipasavyo kwa wananchi ambao ndiyo waajiri wao. Sambamba na hilo, nidhamu
Serikalini imeongezeka kutokana na Serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu
watumishi wazembe, wadanganyifu na wasio waadilifu.
Mheshimiwa Spika,
tunapotaja mafanikio haya tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani uongozi
wake mahiri na wenye uthubutu ndiyo msingi mkuu wa mafanikio yaliyopatikana.
Dhana na falsafa aliyojenga ya Hapa Kazi Tu imesaidia kubadili mtazamo wa
Watanzania wengi ambapo sasa tunashuhudia uwajibikaji wa kiwango cha juu wa mtu
mmoja mmoja, katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na uzalishaji iwe shambani,
ofisini, kiwandani, sokoni na kwingineko badala ya tabia ya awali ya baadhi ya
wananchi wachache kupoteza muda mwingi katika shughuli zisizokuwa na tija kwa
Taifa.
Mheshimiwa Spika,
mafanikio haya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji wa
huduma za jamii yameenda sambamba na uzalishaji wa ajira zipatazo milioni 12.6
zikiwemo ajira za moja kwa moja milioni 11.7 kwenye sekta mbalimbali nchini.
Kwa mfano:
Sekta za Afya, Elimu na
Utawala zimetoa ajira za kudumu kwa kuajiri watumishi 28,403 katika mamlaka za
Serikali za Mitaa,
Mradi wa reli ya kati
kwa kiwango cha kimataifa umewezesha kuzalishwa ajira zipatazo 13,177 za
kitaalam na zisizo za kitalaam. Kati ya hizo, ajira za kitaalam kwa wazawa ni
asilimia 46.5. Pia kupitia mradi huu kumekuwa na utoaji wa zabuni zenye thamani
ya Shilingi bilioni 664.7 kwa wazabuni na wakandarasi wa ndani 640,
Mradi wa umeme wa
mwalimu Nyerere kupitia maporomoko ya mto Rufiji umezalisha jumla ya ajira 3,897
ikiwemo ajira za wazawa 3,422,
Ufufuaji wa shirika la
ndege la Tanzania (ATCL) pamoja na kuboresha viwanja vya ndege jumla ya ajira
2,970,
Ujenzi wa Viwanda
nchini jumla ya ajira zilizozalishwa ni 41,900.
Ujenzi na uboreshaji wa
miundombinu mbalimbali ikiwemo Hospitali za Wilaya, vituo vya afya, Zahanati,
Madarasa, Nyumba na majengo maeneo mapya ya utawala, Miradi ya barabara chini
ya TARURA kwa kutumia force Account jumla ya mafundi 845,348 walipata ajira za
mikataba na muda.
Mheshimiwa Spika, baada
ya kueleza mafanikio hayo, nyote ni mashuhuda kwamba Chama Cha Mapinduzi
kiliahidi na kimetekeleza kwa vitendo na ndiyo maana kinaendelea kuwa Chama cha
mfano na cha kuigwa siyo tu Nchini, bali hata katika Bara la Afrika. Hata
hivyo, mafanikio mengine yataelezwa kwa kina wakati Mawaziri watakapokuwa
wanawasilisha hotuba za bajeti za Wizara zao.
Mheshimiwa Spika, sasa
naomba kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka
2019/2020 na shughuli zitakazotekelezwa na Serikali katika Mwaka 2020/2021.
MPANGO WA MAENDELEO NA
BAJETI YA MWAKA 2020/2021
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2020/2021 yamezingatia Sera na
Miongozo ikiwa ni pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/2021.
Mpango huu ni wa mwisho katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka wa kutekeleza
Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021) wenye dhima ya Kujenga
Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Uchumi na Maendeleo ya Watu.
Mheshimiwa Spika,
Mpango wa Maendeleo na Bajeti wa Mwaka 2020/2021 umezingatia yafuatayo: Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 yenye lengo la kuiwezesha Tanzania kuwa Nchi
ya hadhi ya uchumi wa kipato cha kati inayoongozwa na viwanda ifikapo Mwaka
2025; Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/2017 –
2020/2021; Sera na Mikakati mbalimbali; Malengo ya Maendeleo Endelevu na
Makubaliano ya Kikanda na Kimataifa ambayo Serikali imeyaridhia. Aidha, Ilani
ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 - 2020 imezingatiwa pamoja na
Maelekezo ya Serikali yaliyoainishwa na Mheshimiwa Rais wakati wa uzinduzi
rasmi wa Bunge la 11 mwezi Novemba 2015. Vilevile, Mpango umezingatia hali
halisi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2019/2020; changamoto
zilizojitokeza; hali ya uchumi kitaifa, kikanda na kidunia kwa Mwaka 2019 na
maoteo ya ukuaji wa uchumi kwa Mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika,
nitumie fursa hii kueleza kwa kifupi vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa
Mwaka 2020/2021 ambavyo vimejikita katika masuala makuu manne yafuatayo: Ujenzi
wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda; Kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya
watu; Uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji
na Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo. Katika kufikia
malengo ya Mpango, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika
kutekeleza miradi ya kielelezo ya kimkakati ikiwa ni pamoja na: Ujenzi wa Reli
ya Kati ya Kiwango cha Kimataifa; Mradi wa kufua umeme wa Maji wa Julius
Nyerere – MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL); Mradi wa
Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania);
Uanzishwaji wa kanda maalum za Kiuchumi na Kusomesha wataalam wengi zaidi
katika fani za Ujuzi Adimu na Maalum. Hatua hizo, zitasaidia kufungamanisha
ujenzi wa miundombinu wezeshi na sekta nyingine za kiuchumi ili kuongeza kasi
ya maendeleo, ajira na kipato na hatimaye kuliwezesha Taifa kupiga hatua kubwa
za kimaendeleo.
Mheshimiwa Spika,
nitumie fursa hii kutoa rai kwa Wafanyabiashara, Wawekezaji, Wajasiriamali,
Wabunge, Viongozi na Watendaji wa Serikali, Taasisi za Dini, Asasi za Kiraia,
Washirika wa Maendeleo, na Wananchi wote kwa ujumla, kushirikiana na Serikali
bega kwa bega katika kutekeleza Mpango huu ili azma ya kufikia uchumi wa kati
unaoongozwa na viwanda ifikapo Mwaka 2025 iweze kutimia.
HALI YA UCHUMI
Mheshimiwa Spika,
uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha Januari hadi
Septemba 2019, ukuaji halisi wa Pato la Taifa ulifikia asilimia 6.9. Baadhi ya
shughuli zilizochangia ukuaji huo kwa viwango vikubwa ni pamoja na ujenzi
asilimia 14.8; uchimbaji wa madini na mawe asilimia 12.6; habari na mawasiliano
asilimia 11.0; uchukuzi na uhifadhi wa mizigo asilimia 8.8 na huduma za
usambazaji maji asilimia 8.5.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Januari 2020, mfumuko wa bei ulikuwa
wastani wa asilimia 3.7. Kiwango hiki ni chini ya lengo la Taifa la kipindi cha
muda wa kati la asilimia 5.0, na chini ya malengo ya asilimia 7.0 kwa nchi za
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na asilimia 8.0 kwa Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Hali hii inatokana na utekelezaji madhubuti wa
sera za fedha na za bajeti, uhakika wa upatikanaji wa chakula na utulivu wa
thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine duniani.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha sekta za uzalishaji na
utoaji huduma ili kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa. Vilevile,
Serikali itaendelea kutekeleza mikakati na sera za uchumi jumla ili kudhibiti
kasi ya mfumuko wa bei na kuwa na mwenendo tulivu wa uchumi. Serikali pia,
itaendelea kuimarisha Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa
Mapato (GePG) kwa kuharakisha ufungaji wa mfumo huo katika wizara na taasisi za
Serikali.
HALI
YA SIASA
Mheshimiwa Spika, Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na
maadili ya vyama vya siasa ili kuhakikisha demokrasia ya vyama vingi inaimarika
pamoja na kudumisha amani, utulivu na mshikamano uliopo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaendelea
kusimamia utekelezaji na utoaji elimu kuhusu Sheria ya Vyama vya Siasa, Kanuni
za Maadili ya Vyama vya Siasa, pamoja na Sheria ya Gharama za Uchaguzi katika
Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020. Vilevile, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
itaendelea kufuatilia uhai wa Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu kwa
lengo la kuwawezesha wananchi kushiriki na kutoa michango yao ya mawazo na
fikra kupitia vyama hivyo ili kuimarisha demokrasia na maendeleo nchini.
Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeratibu na kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika
tarehe 24 Novemba 2019. Uchaguzi huo ulihusisha Mitaa 4,263, Vijiji 12,319 na
Vitongoji 64,384. Katika uchaguzi huo, Chama Cha Mapinduzi kilipata ushindi wa
kishindo wa asilimia 99.9 kwa nafasi zote zilizogombewa. Matokeo hayo
yameendelea kudhihirisha imani kubwa waliyonayo wananchi kwa Chama Cha
Mapinduzi. Hivyo, basi natoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi
waliochaguliwa ili kutimiza azma ya kuwaletea maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Tume
ya Taifa ya Uchaguzi imeanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi
Oktoba 2020. Pamoja na mambo mengine, maandalizi hayo yanahusisha Zoezi la
Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika nchi nzima. Awamu ya
kwanza ilizinduliwa tarehe 18 Julai, 2019 Mkoani Kilimanjaro na kukamilika
tarehe 23 Februari, 2020 katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika,
uboreshaji wa daftari hili ulihusisha: Uandikishaji wa Wapiga Kura wapya ambao
wametimiza umri wa miaka 18 au watatimiza umri huo ifikapo siku ya Uchaguzi
Mkuu wa Mwaka 2020; urekebishaji wa taarifa za Wapiga Kura walioandikishwa
katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 pamoja na ufutaji wa taarifa za Wapiga Kura
waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mheshimiwa Spika,
katika zoezi hilo, jumla ya Wapiga Kura 10,285,732 wameandikishwa na kati yao,
Wapiga Kura wapya ni 7,043,247, Wapiga Kura walioboreshewa taarifa zao ni
3,225,778 na Wapiga Kura waliofutwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
kutokana na kupoteza sifa ni 16,707. Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura kwa Awamu ya Pili linatarajiwa kuanza tarehe 5 Aprili 2020 na
kukamilika tarehe 26 Juni 2020. Zoezi hili litaenda sambamba na uhakiki wa
taarifa za wapiga kura katika daftari hilo. Natoa wito kwa Wananchi kujitokeza
kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari hilo, ili
waweze kutumia haki yao ya Kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Mheshimiwa Spika,
niwasihi Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kwa kufuata
sheria, kanuni na taratibu za Nchi. Viongozi wa Vyama vya Siasa waoneshe mfano
wa kuendesha siasa za kistaarabu zenye lengo la kuwaunganisha watanzania na
siyo kuwatenganisha. Hakuna kiongozi aliyewahi kupata sifa nzuri kwa kuwa
chanzo cha mifarakano. Hivyo basi, tudumishe utulivu, amani, mshikamano pamoja
na ustaarabu wetu wa kitanzania katika kipindi chote cha kampeni na Uchaguzi
Mkuu ili kulifanya Taifa letu kuendelea kuwa kisiwa cha amani na mfano wa
kuigwa barani Afrika na duniani kwa ujumla.
BUNGE
Mheshimiwa Spika, Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeendelea kutimiza wajibu wake wa kikatiba
na kikanuni kwa kufanya mikutano mitatu na huu ukiwa ni wa nne kwa mwaka
2019/2020. Ofisi ya Bunge kwa sasa inatekeleza shughuli za Bunge kwa kutumia
TEHAMA kupitia mfumo wa Bunge Mtandao (e-Parliament) uliotengenezwa na
kusimamiwa na wataalam wa ndani wa Ofisi ya Bunge. Hivi sasa Wizara, Idara na
Taasisi za Serikali zinawasilisha taarifa na nyaraka mbalimbali Bungeni kwa
kutumia nakala tete badala ya nakala ngumu. Hatua hii imeweza kupunguza
gharama za uendeshaji hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha cha takribani
Shilingi bilioni 2 kilichokuwa kinatumika kila mwaka katika uandaaji na
uhifadhi wa nyaraka mbalimbali zinazoandaliwa kwa ajili ya utekelezaji wa
shughuli mbalimbali za Bunge. Pia, Ofisi ya Bunge imeweza kuzindua ‘Bunge
Mobile Application’ ambayo imewezesha Waheshimiwa Wabunge pamoja na wadau
mbalimbali kupata kwa urahisi taarifa mbalimbali kama vile orodha ya shughuli
za Bunge (Order Paper), Hansard pamoja na sheria na miswada. Ni matumaini yangu
kwamba Bunge lako Tukufu litaendelea kuisimamia Serikali ili itekeleze majukumu
yake ipasavyo.
MAHAKAMA
Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa gharama nafuu,
Mahakama imeendelea kuimarisha huduma kwa kuweka mifumo na taratibu mbalimbali
za kuwafikia wananchi katika maeneo yote nchini ili kupunguza mlundikano wa
mashauri. Mojawapo ya utaratibu unaotumika ni kuwatumia Mahakimu wenye Mamlaka
ya Ziada (Extended Jurisdiction) kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu ambapo
Mahakimu 195 walipewa Mamlaka hiyo ya ziada. Katika kipindi cha Mwaka 2019 mashauri
1,132 yalisikilizwa na kumalizwa kwa utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika,
Mahakama imeendelea kuboresha miundombinu katika ngazi mbalimbali nchini ikiwa
ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa majengo. Katika kutekeleza hilo, ujenzi wa
majengo ya Mahakama Kuu katika Mikoa ya Kigoma na Mara, Mahakama ya Hakimu
Mkazi katika Mikoa ya Simiyu, Manyara, Geita, Njombe, Mahakama za Wilaya 14,
pamoja na Mahakama za Mwanzo za Mlowo, Magoma, Uyole, Mtowisa, Msanzi na Mkunya
umekamilika.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kulinda, kuheshimu na kuzingatia
haki za binadamu na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa sheria na utoaji Haki kwa
kutumia TEHAMA. Vilevile, Serikali itaendelea kufanya maboresho katika mfumo wa
Haki Jinai ili kuwezesha shughuli za uchunguzi, upelelezi, uendeshaji wa
mashauri na usikilizaji wa mashauri kufanyika kwa ufanisi.
UWEKEZAJI
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuratibu na kusimamia shughuli za kuhamasisha na
kufanikisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuvutia mitaji,
teknolojia na ujuzi ambao ni chachu ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
Serikali imeendelea kuhakikisha mazingira ya uwekezaji na biashara yanakuwa
rafiki.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kutumia vyema uwepo wa fursa nyingi za uwekezaji na kuwepo
kwenye eneo la kimkakati la kijiografia kwa kuhudumia nchi zipatazo 6 ambazo
hazipo kwenye mwambao wa bahari. Hali hii inaifanya nchi yetu kuwa lango la
biashara ya kimataifa hususani katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na
Kati pamoja na Kusini mwa Afrika. Aidha, Serikali inaendelea kuboresha
mazingiza ya uwekezaji na biashara ikiwemo kufanya tathmini ya utekelezaji wa
Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 ili kubaini changamoto za kisera,
kisheria na kiutendaji zitakazopelekea kuhuisha Sera ya Uwekezaji ya Mwaka 1996
na Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1997.
Mheshimiwa Spika,
vilevile, Serikali imeendelea kuratibu utekelezaji wa Kuboresha Mfumo wa
Udhibiti wa Biashara (Blueprint) ambapo kupitia Mpango huo Serikali imefuta
tozo mbalimbali 54 katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 pamoja na kuondoa
mwingiliano wa majukumu kati ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya
Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ili kurahisisha shughuli za uwekezaji na
biashara.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2019/2020 Serikali pia imeratibu mikutano ya mashauriano kati yake
na wawekezaji na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la
kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo. Katika
mikutano hiyo hoja nyingi na changamoto zilipatiwa ufumbuzi na nyingine
kutolewa ufafanuzi ambapo pia wafanyabiashara na wawekezaji walikumbushwa
wajibu wao katika uendeshaji biashara na uwekezaji wao.
Mheshimiwa Spika,
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) kwa kushirikiana na Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliendesha mikutano kati ya
Serikali na wawekezaji kutoka China, Uingereza na Marekani waliowekeza hapa
nchini. Kwa nia ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili na kupata
maoni na ushauri zaidi.
Mheshimiwa Spika,
katika kuongeza njia za kushughulikia malalamiko ya wawekezaji, Serikali kwa
kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeandaa mfumo wa
kielektroniki wa kupokea malalamiko na kupata mrejesho wa wawekezaji (Online
Complaints and Feedback Platform) ambao utaanza kutumika katika Mwaka
2020/2021. Mfumo huo utapokea maoni na ushauri kwa njia ya haraka na kuleta
ufanisi katika kuwahudumia.
Mheshimiwa Spika,
Mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini yameendelea kuimarika.
Taarifa ya Benki ya Dunia ya Wepesi wa Kufanya Biashara (Ease of Doing Business
Report) ya Mwaka 2020 iliyotolewa Oktoba 2019 inaonesha kuwa Tanzania imepanda
kwa nafasi tatu (3) kutoka nafasi ya 144 hadi kufikia nafasi ya 141. Lengo letu
ni kufikia nafasi ya juu kufikia Mwaka 2025. Naziagiza Wizara na Taasisi zote
za Serikali zinazohusika na utekelezaji wa maboresho na kuweka mazingira mazuri
na rafiki ya kuratibu kwa ukaribu ili kufungua fursa zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa kukuza uwekezaji, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea
kuhamasisha Mikoa yote nchini kuandaa Makongamano ya Uwekezaji sambamba na
kuzindua Miongozo ya Uwekezaji ya Mikoa inayobainisha fursa za uwekezaji za
Mikoa pamoja na maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa ili kuhamasisha na kuvutia
uwekezaji zaidi katika Mikoa hiyo. Hadi sasa, Mikoa 14 ya Ruvuma, Songwe,
Pwani, Lindi, Kagera, Mtwara, Geita, Kilimanjaro, Simiyu, Manyara, Dodoma,
Mwanza, Kigoma na Morogoro imezindua miongozo hiyo. Mikoa yote ambayo
haijakamilisha kuandaa miongozo hiyo ifanye hivyo kabla ya Septemba 2020.
Mheshimiwa Spika, Ofisi
ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu makongamano ya uwekezaji yaliyofanyika hapa
nchini kama vile Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na
Uganda, Tanzania na Afrika Kusini; Afrika Mashariki na Sweden na
Makongamano mengine yaliyofanyika nje ya Nchi kama vile Tanzania na Burundi;
“Investment for Africa” lililofanyika nchini Misri; Kongamano lililoandaliwa na
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) lililofanyika Afrika Kusini; na Kongamano
kati ya Pakistani na Afrika lililofanyika nchini Kenya. Tumeendelea kupokea
wawekezaji wanaofika nchini kwa ajili ya kutafuta fursa za uwekezaji kutoka
Nchi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika,
Serikali inahakikisha maeneo ya uwekezaji yanatengwa na kuendelezwa kwa
kuwekewa miundombinu ya msingi ya maji, umeme, mawasiliano na barabara. Hadi
Februari 2020, jumla ya hekta 854,821.61 zimetengwa kwa ajili ya uwekezaji
katika Halmashauri zote nchini.
Mheshimiwa Spika,
kupitia kitengo cha Huduma za Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre)
kilichopo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) chenye watendaji kutoka Taasisi 10
wameendelea kutoa huduma za muda mfupi kwa wawekezaji wetu kupitia Kituo hicho
hadi kufikia Februari 2020, jumla ya miradi 146 yenye thamani ya Dola za
Marekani Milioni 1,514.57 inayotegemewa kutoa ajira za moja kwa moja zipatazo
26,384 ilisajiliwa ambapo miradi 52 sawa na asilimia 36 inamilikiwa na wageni,
miradi 50 sawa na asilimia 34 inamilikiwa na Watanzania na miradi 44 sawa na
asilimia 30 inamilikiwa kwa ubia kati ya wageni na Watanzania. Katika miradi
iliyosajiliwa katika Mwaka huu wa Fedha miradi 95 sawa na asilimia 65 ya miradi
yote inahusisha sekta ya uzalishaji viwandani.
SEKTA ZA
UZALISHAJI
Viwanda
Mheshimiwa Spika, kwa
kutambua umuhimu wa viwanda Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti ili
kuwezesha sekta hii kukua kwa haraka na kutoa mchango mkubwa zaidi katika Pato
la Taifa pamoja na kupunguza umaskini. Katika kutekeleza dhana hii kwa vitendo
katika mwaka 2019/2020, Serikali iliimarisha kiwanda cha Ngozi na Bidhaa za
Ngozi cha Karanga (Moshi) na kuimarisha Shirika la Nyumbu (Pwani) ili kuongeza
uzalishaji ikiwemo wa magari ya zimamoto. Vilevile, ada na tozo 54 zilifutwa
ili kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta hii.
Aidha, uzalishaji katika baadhi ya viwanda ulianza ikiwa ni pamoja na Pipe
Industries Co. Limited (Dar es Salaam), Kiwanda cha Chai cha Kabambe (Njombe),
kiwanda cha Yalin Cashewnut Co. Limited (Mtwara), kiwanda cha 21st Century Food
and Packaging (Dar es Salaam), kiwanda cha kusaga mahindi (MeTL, Dar es
Salaam), kiwanda cha bidhaa za plastiki cha Plasco Pipelines Co. Ltd (Dar es
Salaam), kiwanda cha kupakia na kuhifadhi parachichi, Rungwe Avocado na kiwanda
cha kuchakata parachichi kwa ajili ya kutengeneza mafuta (KUZA Afrika).
Mheshimiwa Spika,
kutokana na jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali za kujenga uchumi
wa viwanda, jumla ya viwanda vipya zaidi ya 4,000 vimejengwa katika mikoa
mbalimbali. Viwanda vilivyojengwa vinazalisha bidhaa za ujenzi; pamoja na
viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ikiwemo nafaka, matunda, mafuta ya
kupikia na bidhaa za ngozi. Ujenzi wa viwanda vipya nchini, katika kipindi cha
Serikali ya awamu ya tano, umechangia kupatikana kwa ajira mpya 482,601 nchi
nzima.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuondoa kero zinazokwamisha ufanisi
na ukuaji wa sekta ya viwanda. Aidha, Serikali itaimarisha ushindani katika
soko kwa kuzingatia sheria na kanuni za ushindani sawa hususan wa bidhaa
zinazozalishwa ndani ya nchi kama vile nondo, mabomba ya plastiki, nguo na
mavazi, bidhaa za ngozi na marumaru. Lengo ni kuimarisha msingi wa ukuaji wa
sekta ya viwanda nchini pamoja na kuvutia sekta binafsi kuwekeza au
kushirikiana na Serikali kuwekeza kwenye viwanda.
Kilimo
Mheshimiwa Spika, sekta
ya kilimo ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula, kupambana na
umaskini, kuongeza ajira pamoja na kuleta maendeleo ya Nchi kwa ujumla. Kwa
kulitambua hilo, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutoa kipaumbele kikubwa
kwenye sekta hiyo kwa lengo la kuwawezesha wakulima kupata pembejeo na zana za
kisasa ili kuongeza tija katika kilimo na hivyo kuleta mageuzi ya kiuchumi.
Hali ya Upatikanaji wa
Chakula
Mheshimiwa Spika,
pamoja na mambo mengine hususan kuimarika kwa hali ya hewa, mageuzi
yanayofanywa katika sekta ya kilimo, yamechangia kuimarika kwa hali ya
upatikanaji wa chakula nchini na upatikanaji wa malighafi za viwanda, sambamba
na kuongeza tija kwa wakulima. Katika msimu wa kilimo wa Mwaka 2018/2019,
uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa ulikuwa tani milioni 16.3 ikilinganishwa
na mahitaji halisi ya tani milioni 13.6. Uzalishaji huo umeihakikishia Nchi
utoshelevu wa chakula kwa asilimia 118 kwa msimu wa kilimo wa Mwaka
2019/2020.
Upatikanaji wa Pembejeo
za Kilimo
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya pembejeo na mbinu bora za kilimo na
teknolojia kwa lengo la kukifanya kilimo chetu kuwa cha kisasa zaidi na chenye
tija. Hadi kufikia Februari 2020, upatikanaji wa mbegu bora za mazao umefikia
tani 71,207 ikilinganishwa na tani 57,023 za msimu wa Mwaka 2018/2019. Kati ya
mbegu hizo, tani 66,031 zimezalishwa nchini ambayo ni sawa na asilimia 93 na
tani 5,175 sawa na asilimia 7 zimeingizwa kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kuimarisha upatikanaji wa mbolea nchini kwa kutumia Mfumo wa Ununuzi
wa Mbolea kwa Pamoja ambao umesaidia kupunguza bei ya mbolea kwa wakulima.
Kutokana na mfumo huo, upatikanaji wa mbolea hadi Februari 2020 umefikia tani
516,813 sawa na asilimia 89 ya lengo la tani 586,604. Kwa kuwa mbolea hizo
hutumika kulingana na hatua mbalimbali za ukuaji wa mazao, Serikali inaendelea
kuhakikisha asilimia 11 iliyobaki inapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa
wakati. Aidha, Serikali imeendelea kuratibu upatikanaji wa viuatilifu ambapo
hadi Januari 2020, jumla ya tani 8,719 za viuatilifu zimeingizwa nchini ili
kudhibiti visumbufu vya mimea na mazao.
Benki ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania (TADB)
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha Julai 2019 hadi Februari 2020, Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB), imetoa mikopo ya Shilingi bilioni 34 kwa miradi ya kilimo 38
na kufanya jumla ya mikopo iliyotolewa kufikia Shilingi bilioni 160.6 toka
Benki ilipoanza utoaji wa mikopo. Mikopo iliyotolewa imewanufaisha wakulima
wadogo, wa kati na wakubwa wapatao milioni 2.1 wa mazao ya kilimo, mifugo na
uvuvi pamoja na viwanda vidogo vya uchakataji wa mazao.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi hicho TADB imetoa mikopo ya ziada ya Shilingi bilioni 31.77
kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo. Mikopo hiyo imewanufaisha
wakulima wapatao 5,080, biashara ndogo na za kati za kilimo zipatazo 30, Vyama
vya Msingi (AMCOS) 20 katika mikoa mbalimbali nchini pamoja na kufanikisha
ununuzi wa matrekta 19 katika mikoa hiyo.
Uzalishaji wa Zao la
Chikichi
Mheshimiwa Spika,
Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini
kwa kuendeleza zao la chikichi sambamba na mazao mengine yanayozalisha mafuta.
Uendelezaji wa zao la chikichi unahusisha kupanda kwa wingi miche mipya yenye
uzalishaji wenye tija. Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini
(TARI) imeanza uzalishaji wa mbegu bora za chikichi aina ya TENERA inayotoa
mafuta mengi. Lengo ni kuzalisha mbegu bora na za kutosha zitakazowezesha
wakulima kuongeza uzalishaji na hivyo kujiongezea kipato na kupunguza matumizi
ya fedha za kigeni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, hadi
tarehe 15 Februari 2020, mbegu 1,525,017 zimezalishwa ambazo zitatosha kupanda
eneo la ekari 30,500. Tayari mbegu 1,026,111 zimesambazwa kwa ajili ya
kuziotesha ili miche bora iweze kusambazwa kwa wakulima. Usambazaji kwa ajili
ya uoteshaji umefanyika katika halmashauri za mkoa wa Kigoma na taasisi
nyingine ikiwemo Magereza ya Kwitanga na Ilagala na JKT Bulombora.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za ugani, kilimo
cha umwagiliaji, ushirika na upatikanaji wa pembejeo ikiwa ni pamoja na mbegu
bora za mazao. Aidha, itajenga na kukarabati miundombinu ya kuhifadhi mazao ya
kilimo na masoko.
Zao la Mkonge
Mheshimiwa Spika, sote
ni mashahidi kuwa zao la Mkonge lilikatiwa tamaa na wakulima na wakulima wengi
waliacha kulima zao hili. Serikali imeanza kuchukua hatua za kufufua kilimo cha
Mkonge na masoko yake. Tunafufua mamlaka ya Mkonge ili itambue mashamba yake na
mali zingine ili ianze kuhamasisha wakulima wadogo na wakubwa na kukaribisha
uwekezaji wa sekta ya Mkonge. Tunaimarisha Taasisi ya Utafiti ya Mlingano ili
izalishe miche zaidi na kuisambaza kwa wakulima. Natoa wito kwa Wizara, Wakuu
wa Mikoa inakolima Mkonge kutambua wakulima wa Mkonge na wapate msaada wa
kitaalam.
Mifugo
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya mifugo nchini ili iweze kutoa mchango
mkubwa zaidi katika Pato la Taifa na kutoa fursa za ajira. Ili kufikia lengo
hili, Serikali imehamasisha wafugaji kuendelea kuimarisha ufugaji wa kisasa,
kuchakata bidhaa za mifugo kwa ajili ya mahitaji ya ndani, ikiwemo lishe bora
na kuuza nje pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi. Aidha, katika
Mwaka 2019/2020, Serikali imekarabati majosho 292, inaendelea na ukarabati wa
majosho 207 na kuendelea na ujenzi wa majosho mapya 84 katika halmashauri
mbalimbali nchini. Hatua hii imewezesha kuongezeka kwa majosho yanayofanya kazi
kutoka 1,486 Mwaka 2018/2019 hadi majosho 1,738 Mwaka 2019/2020. Aidha,
Serikali imenunua lita 12,549 za dawa za kuogesha mifugo.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021 Serikali itaendelea kuhimiza ufugaji wa kisasa pamoja na
kuimarisha afya ya mifugo kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za chanjo na tiba
kwa kuimarisha vituo vya utengenezaji wa chanjo za mifugo. Aidha, Serikali
itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa malisho kwa kutambua, kutenga,
kumilikisha, kusimamia na kuendeleza maeneo ya malisho. Vilevile, huduma za ugani
zitaboreshwa na mafunzo kwa wafugaji na maafisa ugani yatatolewa ili kuwapatia
maarifa na teknolojia mbalimbali kwa lengo la kuongeza tija.
Uvuvi
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuboresha Sekta ndogo ya Uvuvi ili iweze kuchangia
kikamilifu katika Pato la Taifa na ajira kwa ujumla. Hatua zilizochukuliwa ni
pamoja na kuondolewa kwa kodi katika zana na malighafi za uvuvi, kupambana na
uvuvi haramu, kuboreshwa kwa mialo ya kupokelea samaki na kuwa ya kisasa,
kuhamasisha uwekezaji katika ukuzaji wa viumbe maji pamoja na kuhamasisha sekta
binafsi kuwekeza katika viwanda vya kuchakata samaki.
Mheshimwia Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaimarisha sekta ya uvuvi ili kuongeza
mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa na kuwaongezea wavuvi kipato. Hatua
zitakazochukuliwa zitahusisha, utekelezaji wa Mkakati wa kujenga na kuboresha
miundombinu ya uvuvi, mkakati wa kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania, kuweka
mazingira bora katika uvuvi wa bahari kuu kwa kuweka vivutio kwa wawekezaji,
kuendelea kupambana na wavuvi haramu na kuhamasisha matumizi endelevu ya
rasilimali za uvuvi, uhifadhi na uchakataji wa samaki ili kuimarisha mnyororo
wa thamani.
Utalii
Mheshimiwa Spika, sekta
ya utalii nchini imeendelea kuimarika ikichagizwa pamoja na mambo mengine na
uwekezaji mkubwa uliofanyika katika miundombinu ya usafiri na usafirishaji na
utoaji huduma. Katika Mwaka 2019, idadi ya watalii walioingia nchini ilifikia
1,510,151 ikilinganishwa na 1,505,702 Mwaka 2018. Ongezeko la idadi ya watalii
nchini limeongeza mapato ya Serikali yatokanayo na utalii kutoka Dola za
Marekani bilioni 2.4 Mwaka 2018 hadi Dola za Marekani bilioni 2.6 Mwaka 2019.
Mheshimiwa Spika,
katika hatua nyingine ya kuimarisha shughuli za utalii nchini, Serikali
imepandisha hadhi Mapori ya Akiba 6 ambayo ni Burigi (Chato), Ibanda (Kyerwa),
Rumanyika (Karagwe), Nyerere, Mto Ugalla na Kigosi kuwa Hifadhi za Taifa. Lengo
ni kuimarisha Sekta ya Utalii kwa kuwa na maeneo mengi ya hifadhi na vivutio
vya watalii yatakayosaidia kuongeza wigo wa utalii na mapato yatokanayo na
sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuvitangaza vituo vya utalii ndani
na nje ya nchi hususan kwenye masoko ya kimkakati, kuimarisha hifadhi mpya 6 za
Taifa, kukuza wigo wa mazao ya utalii na kuweka mazingira wezeshi ili sekta
binafsi ishiriki kikamilifu katika uwekezaji kwenye utalii. Kadhalika, maeneo
mengine yatakayopewa kipaumbele ni utalii wa meli, mikutano, fukwe, utamaduni,
malikale, ikolojia na jiolojia.
Madini
Mheshimiwa Spika,
usimamizi mzuri wa mikakati na sheria za ulinzi wa rasilimali na maliasili zetu
umekuwa chachu ya kukua na kuimarika kwa sekta ya Madini nchini. Usimamizi huo
umeifanya sekta hiyo kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa Pato la Taifa.
Mathalan, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya Mwaka 2019/2020 mchango wa Sekta
ya madini ulikuwa asilimia 13.7. Katika kipindi hicho, sekta ya madini ilishika
nafasi ya pili katika kuchangia Pato la Taifa baada ya sekta ya ujenzi
iliyochangia asilimia 16.5.
Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia Januari 2020, maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa kupitia Sekta ya
Madini ni Shilingi bilioni 284.4. Kiwango hicho ni sawa na asilimia 60.4 ya
lengo la mwaka la kukusanya Shilingi bilioni 470.89. Mafanikio hayo, ni ishara
tosha ya kuendelea kuimarika kwa sekta hii kufuatia usimamizi thabiti unaowekwa
na Serikali.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeanzisha masoko ya madini nchini kwa lengo la kupata takwimu sahihi
za mauzo ya madini, kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata soko la uhakika, kupata
bei stahiki kwa bidhaa za madini na kuondoa tatizo la utoroshaji na biashara
haramu ya madini. Hatua hiyo imewezesha kuongezeka kwa mapato ya Serikali
kupitia tozo za mrabaha na ada ya ukaguzi wa mauzo ya madini kwenye masoko.
Mheshimiwa Spika, hadi
Januari 2020, jumla ya masoko ya madini 28 na vituo vidogo vya ununuzi wa
madini 28 vimeanzishwa nchini. Kupitia masoko na vituo hivyo, katika kipindi
cha Machi 2019 hadi Januari 2020, jumla ya kilogramu 9,237.34 za dhahabu;
karati 12,973.14 za madini ya almasi; kilogramu 20,099.17 za madini ya bati na
kilogramu 514,683.28 za madini ya vito mbalimbali ziliuzwa na kuipatia Serikali
mapato ya Shilingi bilioni 66.57 ambazo zimetokana na mrabaha, ada ya ukaguzi
na ushuru wa Halmashauri.
Mheshimiwa Spika,
masoko ya madini yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji wa
takwimu sahihi za madini tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa kwake.
Masoko hayo, yana ulinzi na usalama wa kutosha na sifa zote za kimataifa
zinazohitajika katika kuendesha biashara ya madini. Hivyo, natoa rai kwa wadau
wa ndani na nje ya nchi kutumia masoko na vituo hivyo ambavyo vinaendeshwa kwa
misingi ya kisheria kwa kuzingatia ushindani na uwazi wa kibiashara.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha uchimbaji mdogo na wa
kati wa madini nchini; ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini; kuhamasisha
uwekezaji katika Sekta ya Madini; kuimarisha shughuli za ugani na utafiti,
uongezaji thamani madini na masoko.
Nishati
Mheshimiwa Spika, hali
ya upatikanaji wa umeme nchini imeendelea kuimarika na kuchangia katika ukuaji
wa uchumi na ustawi wa Taifa kwa ujumla. Uwezo wa mitambo ya kufua umeme nchini
ni Megawati 1,602.32 ambapo kati ya hizo Megawati 1,565.72 zipo katika Mfumo wa
Gridi ya Taifa na Megawati 36.6 zipo nje ya Mfumo wa Gridi ya Taifa. Aidha,
hali ya maji katika mabwawa ya Mtera, Kidatu, Kihansi, Nyumba ya Mungu na New
Pangani Falls imeendelea kuwa nzuri na hivyo kutuhakikishia kuwa na umeme wa
uhakika.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na kuelezea juu ya mafanikio tuliyoyapata katika utekelezaji wa Mradi wa
Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere hapo awali, Serikali vilevile inatekeleza
Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Rusumo utakaozalisha Megawati 80. Kukamilika kwa
miradi hii na mingine itaimarisha upatikanaji wa umeme nafuu na wa uhakika na
hivyo kuchangia katika maendeleo ya ukuaji wa viwanda na uchumi.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kutekeleza miradi mikubwa na ya
kielelezo ya uzalishaji wa umeme hususan Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius
Nyerere (MW 2,115), upanuzi wa Mradi wa Kinyerezi I (MW 185) pamoja na
kuimarisha mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini. Aidha,
Serikali itaendelea kutekeleza Awamu ya Tatu ya Mradi wa Kupeleka Umeme
Vijijini ili kuhakikisha vijiji vilivyobaki vinapatiwa umeme.
HUDUMA
ZA KIUCHUMI
Ardhi
Mheshimiwa Spika, ardhi
ni rasilimali namba moja katika kuifikia ndoto ya Serikali ya kujenga uchumi wa
viwanda. Kwa msingi huo, Serikali imeendelea kusimamia upimaji wa ardhi,
mipango ya matumizi ya ardhi kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa na umilikishaji
ardhi kwa wananchi. Sambamba na kuimarisha utoaji huduma kwa njia ya
kielektroniki, Serikali inatekeleza mpango wa kusogeza huduma za ardhi karibu
na wananchi. Hadi sasa ofisi za ardhi za mikoa 26 zimeanzishwa pamoja na
kuendelea kuziimarisha ofisi zote za ardhi za Halmashauri kwa kuwapatia mafunzo
wataalam wa sekta ya ardhi na kununua vifaa.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2019/2020, Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya usimikaji wa
Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi katika Ofisi za Ardhi Kanda ya
Dar es Salaam na Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ubungo. Lengo ni
kuharakisha upimaji na utoaji hatimiliki za ardhi ili kuwawezesha wananchi
wengi zaidi kumiliki ardhi kisheria na kutumia hati hizo kupata mikopo katika
taasisi za fedha itakayowezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za
ujasiriamali.
Mipango
ya Matumizi ya Ardhi
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kusimamia upangaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya
ardhi katika ngazi ya Kanda, Wilaya na Vijiji. Lengo la Serikali ni kuharakisha
upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya makazi na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo,
ufugaji, biashara na uwekezaji. Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Februari
2020, mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 132 imeandaliwa katika Wilaya 27.
Mheshimiwa Spika,
sambamba na uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Serikali imeendelea
kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali. Katika Mwaka
2019/2020 Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametoa
kibali kwa vijiji 920 kati ya vijiji 975 vilivyokuwemo ndani ya hifadhi na
mapori ya akiba kuhalalishwa rasmi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na
kijamii. Hatua hiyo itapunguza migogoro iliyokuwa ikiendelea katika maeneo
mbalimbali nchini na hivyo kuwawezesha wananchi kutumia muda mwingi katika
shughuli za uzalishaji.
Miundombinu
ya Usafiri na Usafirishaji
Mheshimiwa Spika, sekta
ya miundombinu hususan ya usafiri na usafirishaji ndio kiunganishi cha sekta za
uchumi wa nchi ili kuwezesha shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma
katika jamii. Kuimarika kwa sekta hii, ni kichocheo muhimu katika kukua kwa
uchumi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kwa
kutambua umuhimu wa sekta hii Serikali ya Awamu ya Tano ilichukua hatua za
makusudi kuanza ujenzi mkubwa wa barabara, madaraja, vivuko, ufufuaji na ujenzi
wa reli mpya, uimarishaji wa usafiri wa majini, na uboreshaji wa usafiri
wa anga ili kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kurahisisha huduma za uchukuzi na
usafirishaji wa watu na bidhaa.
Barabara na Madaraja
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2019/2020, Serikali imepata mafanikio makubwa katika kujenga
mtandao wa barabara za kiwango cha lami nchini. Serikali imeendelea kuhakikisha
mikoa yote inaunganishwa na mtandao wa barabara za lami ili kurahisisha
usafirishaji wa watu na bidhaa.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi hicho jumla ya kilomita 399.07 za barabara kuu na barabara za
mikoa zilijengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, kilomita 56 za barabara kuu
zilifanyiwa ukarabati kwa kiwango cha lami na kilomita 84 za barabara za mikoa
zilifanyiwa ukarabati kwa kiwango cha changarawe. Hadi kufikia Februari 2020,
jumla ya kilomita 6,960 zimefanyiwa matengenezo ya kawaida, kilomita 1,444
zimefanyiwa matengenezo maalum na madaraja 416 yamefanyiwa matengenezo.
Mheshimiwa Spika,
katika kuondoa msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam, Serikali inaendelea
na ujenzi wa barabara ya njia 8 kutoka Kimara hadi Kibaha yenye urefu wa
Kilomita 19 ambapo ujenzi umefikia asilimia 63. Mradi mwingine ni ujenzi wa
Ubungo Interchange ambao umefikia asilimia 65.
Mheshimiwa Spika,
miradi mingine inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa Daraja la Tanzanite
(Salender) lenye urefu wa Kilomita 6.2 uliofikia asilimia 25 na kuanza
maandalizi ya ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi lenye urefu wa kilomita 3.2
na upana wa mita 28.45. Aidha, kati ya Julai 2019 hadi Januari 2020 Serikali
imetoa Shilingi bilioni 703.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara na
madaraja nchini.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa
niliyoitaja pamoja na mingine inayoendelea. Vilevile, Serikali itaanza ujenzi
wa barabara na madaraja mapya ili kuwahakikishia wananchi, wawekezaji na
wafanyabiashara huduma bora na za uhakika za usafirishaji katika kipindi chote
cha mwaka.
Reli
Mheshimiwa Spika, kama
nilivyoeleza hapo awali, moja ya mafanikio makubwa tuliyoyapata katika eneo la
reli ni kuendelea na ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa. Nikiri
pia kuwa, katika kipindi hiki, Serikali inajivunia kurejesha huduma ya reli
kati ya Dar es Salaam na Moshi ambayo ilisimama kwa zaidi ya miaka 20 na
kufufuliwa kwa huduma ya reli kati ya Tanga na Moshi iliyosimama kwa takribani
miaka 12 ambapo hadi Machi 2020 jumla ya abiria 33,459 na mizigo tani 5,080
imesafirishwa kupitia reli hizo. Aidha, ukarabati wa reli ya kati kutoka Dar es
Salaam hadi Isaka nao unaendelea kwa kuondoa reli zote nyepesi na kuweka reli
mpya nzito. Ukarabati huo umewezesha kurejea kwa huduma za usafiri wa abiria na
mizigo na hivyo kurahisisha usafirishaji, kupunguza kero ya usafiri na ajali za
barabarani.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itakamilisha ujenzi wa reli ya kati kwa
kiwango cha kimataifa kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro na kuendelea na
ujenzi wa kipande cha Morogoro – Makutupora sambamba na kukarabati miundombinu
mingine ya reli.
Bandari
Mheshimiwa Spika,
katika eneo la bandari, Serikali imeendelea kuboresha na kuimarisha miundombinu
ya bandari zilizopo katika mwambao wa pwani na maziwa kwa lengo la kuendeleza
huduma ya usafiri wa majini ndani ya nchi na nchi jirani. Katika Mwaka
2019/2020, Serikali imekamilisha ujenzi wa gati namba 1, 2, 3 na gati la
kupakia na kupakua magari (RoRo Berth) katika Bandari ya Dar es Salaam. Kazi ya
ukarabati wa gati namba 5 hadi 7 inaendelea.
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa Bandari ya Mtwara, ujenzi wa Gati lenye urefu wa mita 300 umefikia
asilimia 60 wakati ukarabati wa Gati namba 2 na uongezaji wa kina cha Bandari
ya Tanga unaendelea na umefikia asilimia 60. Ujenzi na ukarabati wa bandari
zetu utaifanya nchi yetu kuendelea kuwa lango muhimu la uagizaji na uingizaji
bidhaa kuelekea nchi jirani.
Ujenzi
wa Meli
Mheshimiwa Spika,
Serikali inafanyia kazi changamoto ya utoaji wa huduma za usafiri katika Maziwa
Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa. Kwa upande wa ziwa Nyasa, tayari ujenzi
wa Meli ya MV Mbeya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo
umekamilika. Vilevile, tarehe 8 Desemba 2019, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa chelezo, meli mpya ya MV Mwanza na
ukarabati wa Meli za MV Victoria na MV Butiama.
Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia Februari 2020, ujenzi wa meli ya MV Mwanza itakayokuwa na uwezo wa
kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo ulikuwa umefikia asilimia 52. Aidha,
ujenzi wa chelezo umefikia asilimia 80, ukarabati wa meli za MV Victoria
asilimia 75 na MV Butiama asilimia 70. Katika Mwaka 2020/2021, Serikali
itaendelea kuboresha huduma za usafiri kwa njia ya maji ikiwa ni pamoja na
kukamilisha miradi inayoendelea, kukarabati vyombo vilivyopo na kununua vyombo
vipya.
Usafiri
wa Anga na Viwanja vya Ndege
Mheshimiwa Spika,
pamoja na mafanikio niliyoyaeleza hapo awali kuhusu kufufua Shirika la Ndege
Tanzania, katika Mwaka 2019/2020 Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa anga la
Tanzania ni salama ili kuimarisha utoaji wa huduma za usafiri wa anga. Aidha,
Serikali inakamilisha usimikaji wa mfumo wa rada 4 za kuongozea ndege za kiraia
katika viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Mwanza na Songwe.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuboresha viwanja vya ndege mbalimbali vilivyopo nchini.
Hadi kufikia Februari, 2020 Serikali imekamilisha ujenzi wa jengo la tatu la
abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere. Kukamilika
kwa jengo hilo kunawezesha kuwahudumia abiria milioni 6 kwa mwaka na hivyo
kuongeza mapato. Serikali pia, imekamilisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha
Mwanza na inaendelea na ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja huo. Jengo hilo
ambalo litagharimu Shilingi bilioni 13.26 litahudumia abiria 400,000 kwa mwaka.
Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya
Mtwara, Songea, Geita, Nachingwea, Iringa na Musoma.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuboresha usafiri wa anga nchini
ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kitovu cha usafiri wa anga kwa nchi za
Afrika Mashariki na Kati. Katika kufanikisha azma hiyo, Serikali itaendelea
kuhakikisha kuwa usalama na miundombinu ya viwanja vya ndege inaboreshwa.
Mawasiliano
Mheshimiwa Spika,
katika eneo la mawasiliano Serikali imeendelea na zoezi la usajili wa laini za
simu kwa njia ya biometria Nchi nzima. Hadi mwisho wa mwezi Februari, 2020
jumla ya laini milioni 31.4 kati ya laini milioni 43.9 zilikuwa zimesajiliwa.
Idadi hii ni sawa na asilimia 71 ya zoezi zima la usajili. Nitoe wito kwa
wananchi waliopata namba za vitambulisho vya Taifa kukamilisha usajili wa laini
zao kwa njia ya biometria ili waendelee kupata huduma za mawasiliano. Zoezi
hili lina umuhimu kwa Taifa kwani linasaidia kuimarisha usalama wa watumiaji wa
huduma za mawasiliano nchini na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
Serikali pia, imeendelea kusimamia mtambo wa Telecommunications Traffic
Monitoring System (TTMS) ili kuhakikisha kuwa tunapata mapato stahiki kutokana
na huduma za mawasiliano. Mfumo huu umeongeza ufanisi katika kusimamia huduma
ya mawasiliano ya simu nchini. Katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Februari,
2020 jumla ya miamala bilioni 2 yenye thamani ya Shilingi trilioni 12.2
imefanyika ambapo Serikali imepata mapato ya Shilingi bilioni 7.3.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kushirikiana na makampuni ya simu
kuboresha huduma za mawasiliano hususan maeneo ya pembezoni ili kuongeza kasi
ya mawasiliano ya kimtandao kwa wananchi wa maeneo hayo. Aidha, Serikali
itaendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kufikisha huduma
katika Makao Makuu ya Wilaya zote nchini pamoja na kuanza ujenzi wa Kituo cha
Data Dodoma.
HUDUMA
ZA JAMII
Elimu
Mheshimiwa Spika, elimu
ya kisasa na hasa yenye mwelekeo wa sayansi na teknolojia ina nafasi ya pekee
katika kufanikisha ujenzi wa msingi wa uchumi wa kisasa wa Taifa
linalojitegemea. Kwa kutambua umuhimu huo na kama nilivyoeleza awali Serikali
ilianzisha na kutekeleza Mpango wa Elimumsingi Bila Ada ili kuhakikisha kila
mtoto mwenye umri wa kwenda shule anaandikishwa.
Mheshimiwa Spika,
katika hatua nyingine ya kuboresha elimu ya sekondari ninayo furaha kuliarifu
Bunge lako Tukufu kuwa tarehe 31 Machi, 2020 Benki ya Dunia imeridhia kuipatia
Tanzania mkopo wa Dola za Marekani Milioni 500 sawa na takriban shilingi
trilioni 1.14 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa maboresho ya elimu ya sekondari
nchini.
Mheshimiwa Spika, Benki
ya Dunia imeridhia kuipatia Tanzani mkopo huo baada ya kuridhishwa na
utekelezaji wa sera ya Elimumsingi Bila Ada. Hivyo, mpango huu utaimarisha
usalama wa watoto shuleni, kuongeza uandikishaji katika shule za sekondari na
elimu mbadala, kuimarisha mafunzo kwa walimu na matumizi ya TEHAMA katika
kufundisha hususan masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Spika,
utekelezaji wa mpango huo utaongeza wigo wa elimu ya sekondari hususan kwa
watoto wa kike na kuwawezesha wavulana na wasichana kukamilisha elimu hiyo.
Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sera ya Elimumsingi Bila Ada kwa
lengo la kuwawezesha watoto wetu wa kike kupata elimu ya sekondari na stadi za
kazi, kuondoa vikwazo kwa watoto wa kike kupata elimu ya sekondari, kuimarisha
matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji pamoja na uratibu,
usimamizi na tathmini ya ubora wa elimu ya sekondari.
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa elimu ya juu, Serikali imeongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu na kutoa kipaumbele kwa watu wenye mahitaji maalum.
Katika Mwaka 2019/2020, Serikali imeongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu
kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi 130,883 ikilinganishwa na wanafunzi 122,754 kwa
Mwaka 2018/2019. Aidha, Shilingi bilioni 450 zilitumika katika kipindi
hicho ikilinganishwa na Shilingi bilioni 424.8 kwa Mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango wa
Elimumsingi Bila Ada, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuhimiza
uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi hususan katika kuboresha
miundombinu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuendeleza rasilimali watu
ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu.
Maji
Upatikanaji wa Maji
Vijijini
Mheshimiwa Spika,
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kutekeleza Programu
ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma ya
maji safi na salama kwa wananchi wote hususan wale wanaoishi maeneo ya
vijijini. Katika Mwaka 2019/2020, jumla ya miradi 94 ya maji yenye vituo vya kuchotea
maji 2,495 katika maeneo mbalimbali vijijini imekamilika. Aidha, miradi 558 ipo
katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na juhudi kubwa za Serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo, hadi
Desemba 2019, upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo ya vijijini umefikia
asilimia 64.8. Vilevile, ili kuboresha utoaji wa huduma ya maji vijijini,
Serikali imeanzisha Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini
(RUWASA) wenye jukumu la kutekeleza miradi na kusimamia utoaji wa huduma za
maji na usafi wa mazingira vijijini.
Upatikanaji wa Maji
Mijini
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa maji mijini, Serikali imetekeleza miradi mipya ya maji katika Jiji la
Dodoma na Dar es Salaam pamoja na maeneo ya Kibaha, Bagamoyo na Kisarawe.
Aidha, Serikali pia imeboresha miundombinu ya upatikanaji wa huduma ya maji
katika miji mikuu ya mikoa, wilaya, miji midogo na maeneo yanayohudumiwa na
miradi ya maji ya kitaifa ya Chalinze, Mugango – Kiabakari, Maswa,
Wanging’ombe, Masasi - Nachingwea na Kahama – Shinyanga. Utekelezaji wa miradi
hiyo umewezesha upatikanaji wa maji katika miji ya mikoa kufikia asilimia 85.
Afya
Ujenzi
na Ukarabati wa Hospitali
Mheshimiwa Spika,
Serikali inaendelea na miradi ya ujenzi wa hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwemo
ujenzi wa hospitali za Mikoa mipya ya Geita, Simiyu, Songwe, Katavi, Njombe
(Mgondechi). Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa hospitali za Mikoa ya
Mara, Singida na Shinyanga pamoja na ujenzi wa hospitali za Wilaya katika
Halmashauri 70 nchini. Vilevile, Serikali inajenga Hospitali ya Uhuru wilayani
Chamwino, Dodoma na hospitali za rufaa za kanda za Mtwara, Mbeya na Burigi -
Chato.
Huduma za Afya za
Kibingwa
Mheshimiwa Spika,
Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kibingwa bobezi (super specialist)
katika Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali Maalum na Hospitali ya Taifa.
Utoaji wa huduma hizo umewezesha wananchi wengi kupata huduma ambazo awali
zilikuwa zinapatikana nje ya Nchi. Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2020,
Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Benjamini Mkapa, MOI na
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete zimetoa huduma mbalimbali za kibingwa kwa
wagonjwa wa ndani na nje ya Nchi.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020, idadi ya wagonjwa waliopata
huduma za kibingwa bobezi katika hospitali hizo ni 1,970. Kati yao, wagonjwa 18
walipata huduma za kupandikiza figo, 330 walipata huduma ya upasuaji wa uti wa
mgongo, 730 upasuaji wa ubongo, 507 upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, 610
upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo, 101 upasuaji wa mishipa ya damu na watoto
284 walifanyiwa upasuaji wa vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Mheshimiwa Spika,
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imetoa tiba mionzi kwa wagonjwa 110,979
ikilinganishwa na wagonjwa 52,890 Mwaka 2018. Kati ya wagonjwa hao, 5,788
walipatiwa tiba ya mionzi. Ongezeko la tiba mionzi kwa wagonjwa limetokana na
uwepo wa mitambo mipya miwili kwa ajili ya tiba ya saratani (LINAC) ambayo
imesaidia kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri tiba mionzi kutoka wiki nne Mwaka
2018 hadi wiki mbili Mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya afya
ikiwemo ukarabati na ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati. Vilevile,
itaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba pamoja na
kuboresha huduma za kibingwa za afya na ubobezi katika Hospitali ya Taifa,
Hospitali Maalum na Hospitali za Rufaa za Kanda ili kuziwezesha kutoa huduma
bora zaidi za kibingwa nchini.
Huduma
kwa Watu Wenye Ulemavu
Mheshimiwa Spika, watu
wenye ulemavu wanayo haki kwa mujibu wa Katiba ya kutambuliwa utu wao,
kuendelezwa, kuheshimiwa na kulindwa dhidi ya vitendo vinavyoshusha utu wao
ikiwemo ubaguzi, uonevu, ukatili na mila potofu. Katika Mwaka 2019/2020,
Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa miongozo na mipango mbalimbali inayolenga
kuongeza upatikanaji wa haki na ustawi wa Watu Wenye Ulemavu na kuhakikisha
huduma zinazotolewa katika ngazi zote kwa ajili ya Watu Wenye Ulemavu na wenye mahitaji maalum
zinatolewa kwa haki na usawa.
Mheshimiwa Spika,
katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili Watu Wenye Ulemavu hususan
kiuchumi, Serikali imezielekeza Halmashauri kutenga asilimia 2 ya mapato yake
ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa Watu Wenye Ulemavu. Kupitia mikopo hiyo
jumla ya vikundi 160 vya Watu Wenye Ulemavu vimeundwa na vilipatiwa mikopo
yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.87. Pamoja na hatua tuliyofikia napenda
kutoa rai kwa Halmashauri zote nchini kutoa fedha hizi ili ziweze kutatua
changamoto za kiuchumi zinazowakabili Watu Wenye Ulemavu kama ilivyokusudiwa na
Serikali.
Mheshimiwa Spika,
vilevile, Serikali imefanikiwa kuanzisha Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu na
kufungua akaunti kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi ikiwa ni pamoja na
kuwajengea uwezo wa kuanzisha miradi mbalimbali ya uzalishaji. Serikali
itatumia Mfuko huo kuratibu upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka kwa wadau
ili kuhakikisha Mfuko huo unakidhi malengo ya uanzishwaji wake.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia, iliwezesha uendeshaji wa Baraza la Ushauri la Taifa la Watu Wenye Ulemavu ambalo limekuwa likitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na 9. ya Mwaka 2010. Aidha, wajumbe wa Baraza hilo wamepatiwa mafunzo kuhusu Sera, Sheria, miongozo na mipango inayowahusu Watu Wenye Ulemavu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuweka mazingira
wezeshi na rafiki kwa Watu Wenye Ulemavu ili kushiriki kikamilifu katika
maendeleo ya Taifa. Baadhi ya shughuli zitakazopewa kipaumbele ni pamoja na
kukamilisha maandalizi ya Mfuko wa Taifa wa Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu,
kuratibu maadhimisho ya Siku za Kitaifa na Kimataifa za Watu Wenye Ulemavu na
kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Baraza la Taifa la Ushauri kwa Watu Wenye
Ulemavu. Vilevile, Serikali itaendeleza vyuo vya mafunzo ya ufundi kwa Watu
Wenye Ulemavu.
ULINZI
NA USALAMA
Mheshimiwa Spika, hali
ya amani na usalama ndani ya mipaka ya Tanzania ni shwari. Vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama vinatekeleza majukumu yake ya kulinda mipaka ya Nchi,
kudumisha amani, usalama wa raia na mali zao pamoja na kufundisha wananchi
ulinzi wa umma. Serikali imeendelea kuliimarisha na kuliongezea uwezo Jeshi la
Wananchi wa Tanzania kwa kulipatia vifaa na zana bora za kisasa pamoja na kutoa
mafunzo na mazoezi stahiki kwa wanajeshi ili kuliwezesha Jeshi kutekeleza
majukumu yake ya msingi ya ulinzi wa mipaka ya Nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimekuwa na mchango mkubwa katika
kukabiliana na majanga na matukio yenye kuleta athari kwa watu na mali zao na
kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi hususan ujenzi, uendelezaji viwanda
na shughuli za kilimo. Nitumie fursa hii kuvipongeza vyombo hivyo hususan Jeshi
la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Magereza kwa kushiriki ipasavyo katika
ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao na kutokana na
juhudi hizo, hali ya ulinzi na usalama imeendelea kuimarika na uhalifu kupungua
kwa asilimia 2.8 kwa makosa makubwa ya jinai ikilinganishwa na Mwaka 2018/2019.
Halikadhalika, ajali za barabarani zimepungua kwa asilimia 25.7 ikilinganishwa
na Mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Spika,
katika kukabiliana na changamoto ya uhamiaji haramu, Serikali ipo katika hatua
za mwisho za uwekaji wa mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mipaka (e-Border
Management System). Kukamilika kwa mfumo huo kutawezesha utoaji wa huduma bora
za uhamiaji, kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka na kuongeza udhibiti katika
ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.
Mheshimiwa Spika,
nitumie fursa hii kuwakumbusha wananchi wote kwamba msingi wa usalama wa raia
na mali zao ni jukumu letu sote. Hivyo, ni muhimu wananchi wote tushirikiane na
vyombo vya ulinzi na usalama kubaini wahalifu pamoja na vitendo
vinavyohatarisha usalama wetu kwa kutoa taarifa kwenye vyombo husika.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kulinda mipaka ya nchi yetu,
kuimarisha usalama wa raia na mali zao ili kuhakikisha wananchi wanaishi na
kufanya shughuli za maendeleo kwa amani. Vilevile Serikali itaendelea kuboresha
mazingira ya kazi na zana za kisasa zinazoendana na teknolojia ya kisasa pamoja
na kuendelea kuhamasisha na kuelimisha wananchi juu ya masuala ya ulinzi,
uzalendo, usalama na umuhimu wa kushiriki katika ulinzi.
USIMAMIZI
WA KAZI NA WAFANYAKAZI
Kazi
na Wafanyakazi
Mheshimiwa Spika, azma
ya Serikali ni kuona wafanyakazi na wananchi kwa ujumla wanafanya kazi za staha
na katika mazingira yanayokubalika. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali
imeendelea kusimamia viwango vya kazi na wafanyakazi, afya na usalama mahali pa
kazi, na kusimamia Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri.
Mheshimiwa Spika,
katika kusimamia viwango vya kazi na wafanyakazi, Serikali imeendelea kusimamia
utekelezaji wa Sheria za Kazi kwa kufanya kaguzi na kutoa elimu kwa wafanyakazi
na waajiri. Aidha, mpaka kufikia mwezi Februari, 2020 kaguzi 3,663 zilifanyika
katika maeneo mbalimbali ya kazi, ikiwa ni sawa na asilimia 76.3 ya lengo
lililopangwa. Kupitia kaguzi hizo, waajiri 36 na raia wa kigeni 82 walifikishwa
Mahakamani kwa kukiuka sheria za kazi ambapo, baada ya kupatikana na hatia
walitozwa faini ya jumla ya Shilingi milioni 872.
Mheshimiwa Spika,
sambamba na hilo Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya
Kuratibu Ajira za Wageni Nchini. Hadi kufikia mwezi Februari, 2020 jumla ya
vibali vya kazi 6,625 vilitolewa kwa wageni na maombi 984 ya vibali vya kazi
yalikataliwa kutokana na kutokidhi vigezo na masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa
Sheria. Vilevile, katika jitihada za kuongeza ufanisi, Serikali imejenga Mfumo
wa Kielektroniki wa Vibali vya Kazi (On Line Work Permit Application and
Information System) pamoja na kuanza kutoa mafunzo ya matumizi yake kabla ya
kuzinduliwa na kuanza kutumika.
Afya na Usalama Mahali
pa Kazi
Mheshimiwa Spika,
katika kusimamia na kudhibiti afya na usalama Mahali pa Kazi, Serikali kupitia
Wakala wa Afya na Usalama mahali pa Kazi imeendelea kufanya kaguzi mbalimbali
katika maeneo ya kazi. Aidha, kwa Mwaka 2019/2020, jumla ya sehemu za kazi
2,270 zilisajiliwa, kaguzi 8,662 zilifanyika na wafanyakazi 93,575 walipimwa
afya.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha utendaji kazi wenye
tija kwa kuboresha vitendea kazi, kuongeza na kuwajengea uwezo watumishi. Hadi
kufikia mwezi Machi 2020, Serikali imetoa ajira mpya na mbadala 6,975 na
kuwapandisha vyeo Watumishi 290,625 wa Kada mbalimbali. Aidha, Serikali imelipa
Shilingi bilioni 130.4 kwa Watumishi wa Umma 100,684 waliokuwa wanadai madeni
mbalimbali na uhakiki wa Watumishi 36,981 wenye madeni ya Shilingi bilioni
88.389 unaendelea. Uhakiki huo ukikamilika madeni hayo yatalipwa.
Mheshimiwa Spika,
nitumie fursa hii kuwashukuru wafanyakazi wote kwa mchango wao mkubwa katika
kujenga Taifa letu. Napenda kuwahakikishia watumishi wote kuwa, katika mwaka
2020/2021, Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kufanya kazi ili
Watumishi wa Umma wafanye kazi kwa weledi, juhudi, uadilifu na uwajibikaji.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004 kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi. Katika
kutekeleza azma hiyo, Serikali imefanikiwa kuongeza ushiriki wa Watanzania
kwenye miradi ya kielelezo na kimkakati ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati
kwa Kiwango cha Kimataifa na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere
ambapo Watanzania 250,000 wameajiriwa katika nafasi mbalimbali zenye ujuzi wa
juu, kati na chini, ikilinganishwa na wageni 1,338. Idadi hiyo ni sawa na
asilimia 99 ya ajira zote kwenye miradi hiyo. Aidha, Shilingi bilioni 170
zililipwa kwa kampuni za kitanzania ambazo zilipata kazi katika miradi ya
kielelezo na kimkakati inayotekelezwa nchini.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuzitumia Taasisi zake za ndani za
masuala ya ujuzi na teknolojia zikiwemo Vyuo vya VETA, Chuo cha Ufundi Dar es
salaam (DIT), Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam (DMI) na vyuo vya ufundi vya Don
Bosco katika kuandaa na kufundisha programu zitakazowezesha Watanzania
kushiriki katika miradi ya kimkakati, kujiajiri na kuajiriwa katika
maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika,
kufuatia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuwa kila Halmashauri itenge
asilimia 10 ya makusanyo yake kwa Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu,
Halmashauri zilitenga jumla ya Shilingi bilioni 54.1 na kutoa jumla ya Shilingi
bilioni 25.4 kwa Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu. Kati ya fedha hizo;
Shilingi 12.9 bilioni zilitolewa kwa wanawake, Shilingi 9.5 bilioni zilitolewa
kwa vijana na Shilingi bilioni 2.9 zilitolewa kwa watu wenye ulemavu. Napenda
kusisitiza Halmashauri zote nchini kuendelea kutenga na kutoa mikopo hiyo kwa
walengwa ili waweze kuinua hali zao kiuchumi na kuongeza mchango wao katika
kujenga uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2019/2020, Serikali imeendelea kusimamia uanzishwaji wa vituo
maalum vya uwezeshaji katika mikoa mbalimbali nchini. Lengo ni kuwawezesha
wananchi kupata taarifa mbalimbali kuhusu fursa za uwezeshaji, usajili na
uendelezaji wa biashara, upatikanaji wa mitaji na mafunzo ya kuongeza thamani
ya mazao na bidhaa mbalimbali.
Mfuko wa Taifa wa
Maendeleo ya Vijana
Mheshimiwa Spika, ili
kutumia kundi la vijana kama fursa muhimu kwa maendeleo ya Taifa, Serikali
imeendelea na uboreshaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Katika Mwaka
2019/2020, Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana umetoa mikopo yenye thamani ya
Shilingi bilioni 3.2 ambapo vikundi 586 vyenye jumla ya vijana 4,222 kutoka
katika Halmashauri 155 walipata mikopo hiyo.
Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF)
Mheshimiwa Spika, mnamo
tarehe 17 Februari 2020, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Kipindi cha Pili cha Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini katika Awamu ya Tatu ya TASAF utakaotekelezwa Tanzania
Bara na Zanzibar. Kuzinduliwa kwa kipindi hiki cha Pili cha Mpango huo,
kunadhihirisha nia ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kutetea wanyonge na
wasiojiweza.
Mheshimiwa Spika,
Mpango huu umewezesha kaya maskini kuongeza kipato, fursa na uwezo wa
kugharamia mahitaji muhimu pamoja na kujenga rasilimali watu. Mathalan, kipindi
cha Kwanza cha TASAF Awamu ya Tatu kilihudumia kaya milioni 1.1 zenye watu
milioni 5.2 katika Halmashauri 159 za Tanzania Bara na wilaya zote za
Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
kupitia Mpango huu wa TASAF kaya maskini zimemudu kujiunga na Mfuko wa Bima ya
Afya ya Jamii pamoja na kujikwamua dhidi ya umaskini. Kwa mfano, asilimia 32 ya
kaya zilijiunga na Bima ya Afya ya Jamii ikilinganishwa na asilimia 11 kabla ya
mpango wa TASAF. Aidha, katika kipindi cha Mwaka 2011/2012 hadi 2017/2018
umaskini wa mahitaji ya msingi kwa Tanzania Bara, ulipungua kwa asilimia 1.8 na
wa chakula kwa asilimia 1.7. Aidha, takwimu zinaonesha pia kuwa, umaskini
uliokithiri umepungua kutoka asilimia 28.2 hadi asilimia 26.4. Kupungua huko
kumechangiwa na utekelezaji wa mpango wa TASAF wa kunusuru kaya maskini.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itafanya utambuzi na uhakiki wa hali za ustawi
wa maisha ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Halmashauri
101. Lengo ni kubaini kaya ambazo si maskini tena sambamba na kuandikisha kaya
mpya 235,647 ambazo hazikufikiwa katika kipindi cha kwanza cha Mpango. Natoa
wito kwa wote waliopewa dhamana ya kutekeleza Mpango huu kufanya kazi kwa
uadilifu, weledi na uaminifu mkubwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Ukuzaji Ujuzi
Mheshimiwa Spika, suala
la ukuzaji ujuzi wa nguvukazi nchini ni miongoni mwa ajenda muhimu ya kisera
katika kuwezesha wananchi kujikwamua kiuchumi. Serikali imeendelea kuwezesha
wananchi wake kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini kwa lengo la kuwapatia
ujuzi na stadi za kazi hasa kundi la vijana, wanawake na Watu Wenye Ulemavu.
Ujuzi huo, utawawezesha kumudu ushindani katika soko la ajira na hivyo
kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2019/2020, jumla ya vijana 30,099 wamewezeshwa kupata ujuzi
kupitia programu hiyo. Kati yao, vijana 5,875 wamepata mafunzo ya uanagenzi
katika fani za ufundi stadi katika maeneo mbalimbali. Mafunzo haya yamefanyika
katika Mikoa 13 ya Tanzania Bara ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma,
Lindi, Geita, Mara, Kilimanjaro, Iringa, Morogoro, Kagera, Singida, Shinyanga
na Ruvuma. Aidha, jumla ya vijana 5,395 wamepewa mafunzo na kurasimishiwa ujuzi
walioupata kupitia mfumo usio rasmi wa mafunzo kupitia VETA katika fani za
uashi, useremala, ushonaji, ufundi bomba, uchomeleaji na uungaji vyuma, ufundi
magari, ufundi umeme, ukarabati wa bodi za magari, upishi na uhudumu katika
hoteli.
Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha wahitimu wa elimu ya juu wanapata uzoefu wa kazi ili
kuwawezesha kupata ajira, jumla ya wahitimu 2,115 wamewezeshwa kupata mafunzo
ya uzoefu kazini kupitia viwanda na kampuni mbalimbali nchini. Kati yao,
wahitimu 100 wa fani ya kilimo wamewezeshwa kwenda nchini Israeli kuhudhuria
mafunzo ya uzoefu kazini katika kilimo cha kisasa kwa muda wa mwaka mmoja.
Aidha, vijana wengine 3,200 wataanza mafunzo mwezi huu wa Aprili 2020. Nichukue
fursa hii kuzishukuru taasisi za umma na binafsi ambazo zinaendelea kutoa
nafasi za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi na wahitimu wetu.
Mheshimia Spika, kwa Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri na stadi za kazi kwa vijana katika fani mbalimbali. Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika nyanja mbalimbali ili kukuza ujuzi wa rasilimali watu.
Ukuzaji wa Fursa za
Ajira
Mheshimiwa Spika,
sambamba na ukuzaji ujuzi, Serikali pia imeendelea kuratibu juhudi za ukuzaji
wa fursa za ajira. Katika kipindi cha Julai hadi Februari 2020, jumla ya ajira
1,577,622 zimezalishwa katika sekta mbalimbali ambapo ajira 579,518
zimezalishwa na sekta rasmi na ajira 998,104 zimezalishwa na sekta isiyo rasmi.
Serikali pia, imeendelea na utoaji wa huduma za ajira ili kuwezesha watafutakazi
kumudu ushindani wa soko la ajira. Hadi kufikia tarehe 31 Januari 2020, jumla
ya watafutakazi 6,756 wamesajiliwa na Kitengo cha Huduma za Ajira ili kupatiwa
huduma mbalimbali za ajira hususan, ushauri nasihi (vocational guidance and
employment counselling) na mafunzo ya kumudu ushindani katika soko la ajira.
Watafutakazi waliopatiwa huduma ya ushauri nasihi pamoja na mafunzo hayo
walikuwa 5,266.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya
ukuzaji wa fursa za ajira. Mikakati hiyo ni pamoja na kuwawezesha vijana
wabunifu na makundi mbalimbali ya vijana na wanawake kuanzisha shughuli za
uzalishaji mali na ujasiriamali ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine na
kuimarisha mifumo ya taarifa za soko la ajira na mitaji ili kuwezesha vijana
kutumia fursa hizo.
HIFADHI YA JAMII
Usimamizi na Udhibiti
wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2019/2020, Serikali imeendelea kutekeleza programu ya maboresho ya
Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kuhakikisha kuwa Kinga ya Jamii inawafikia
wananchi walio wengi. Maboresho yaliyofanyika yamelenga kuongeza ufanisi
katika sekta ya hifadhi ya jamii. Vilevile, Serikali imeanza kutekeleza kipindi
cha Mpito cha miaka mitano (2019 – 2023) cha kuendelea kuboresha Sekta ya
Hifadhi ya Jamii hususan suala la pensheni kwa wanachama wa Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii.
Mifuko ya Pensheni
Mheshimiwa Spika,
Mifuko ya Pensheni ya NSSF na PSSSF imekuwa ikifanya kazi muhimu ya kulipa
pensheni pamoja na mafao mengine kwa wastaafu katika sekta za umma na binafsi.
Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019, Mifuko hiyo ililipa pensheni,
malipo ya mkupuo pamoja na mafao mengine yenye jumla ya Shilingi trilioni 1.4
kwa wanachama 206,897 na wastani wa Shilingi bilioni 51.7 zimelipwa kila mwezi
kwa wastaafu kama pensheni.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaboresha uchakataji wa mafao ili kulipa
mafao stahiki na kwa wakati; na kuimarisha ukusanyaji wa michango na mapato
yatokanayo na uwekezaji na Mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha utendaji kazi.
MASUALA MTAMBUKA
Vita Dhidi ya
Rushwa
Mheshimiwa Spika,
jitihada za kuinua uchumi na kuongeza huduma za jamii hazitaleta manufaa kwa
wananchi na kuondoa umasikini iwapo adui rushwa ataendelea kulitafuna Taifa
letu. Rushwa ni adui wa haki, maendeleo na ustawi wa wananchi, pia ni moja ya
changamoto kubwa inayoikabili Nchi yetu na dunia kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kwa
kutambua hilo, Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza mikakati mbalimbali ya
kupambana na rushwa ambayo imeweza kupunguza vitendo vya rushwa kwa kiasi
kikubwa nchini. Mikakati hiyo ni pamoja na Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na
Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Tatu wa Mwaka 2017 - 2022. Hii inadhihirishwa na
matokeo ya tafiti zilizofanywa Mwaka 2019 na Taasisi za Kitaifa na Kimataifa na
kuonesha kuwa Tanzania inafanya vizuri katika kudhibiti vitendo vya rushwa na
ufisadi. Aidha, kiashiria cha Corruption Perception Index (CPI) cha taasisi ya
Transparency International kimeonesha Tanzania imefikia kiwango cha asilimia 37
na kushika nafasi ya 96 kati ya nchi 180 ikilinganishwa na kiwango cha asilimia
30 katika nafasi ya 119 Mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2019/2020, Serikali imeokoa kiasi cha Shilingi bilioni 47.3
zikiwa ni thamani ya mali na fedha taslimu zilizotokana na operesheni
mbalimbali za kiuchunguzi zilizofanyika nchini. Serikali pia, ilifanya
ufuatiliaji katika miradi 244 ya maendeleo iliyohusisha sekta za Afya, Elimu,
Maji, Ujenzi na Nishati yenye thamani ya Shilingi trilioni 9.86 ili kuhakikisha
inatekelezwa kulingana na thamani halisi ya fedha.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha mifumo mbalimbali kwenye
Sekta za Umma katika ngazi zote nchini ili kubaini na kupendekeza njia
madhubuti za kuziba mianya ya rushwa na kuboresha utoaji wa huduma kwa
wananchi. Aidha, Serikali itaendelea kufuatilia miradi ya maendeleo ili
kuhakikisha inatekelezwa kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa kwa ajili
hiyo.
Mapambano Dhidi ya
UKIMWI
Mheshimiwa Spika, Serikali
kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Nne wa Taifa
wa Kudhibiti UKIMWI wa Mwaka 2018/2019 - 2022/2023 ambao unalenga kutekeleza
malengo ya dunia yenye mwelekeo wa kupambana na UKIMWI ili kufikia TISINI TATU
(90:90:90). Katika kutekeleza malengo hayo, lengo la 90 ya kwanza ni
kuhakikisha asilimia 90 ya watu wanapima na kujua hali zao ambapo hadi Desemba
2019 wenye VVU na waliopima na kujua hali zao ilikuwa asilimia 80.1
ikilinganishwa na asilimia 75 kwa Mwaka 2018. Lengo la 90 ya pili ni
kuhakikisha asilimia 90 ya waliokutwa na VVU wanaanzishiwa dawa za kufubaza VVU
ambapo walioanza dawa za ARV na kubaki katika dawa ni asilimia 98.8
ikilinganishwa na asilimia 98 kwa Mwaka 2018. Lengo la 90 ya tatu ni
kuhakikisha asilimia 90 ya wanaoanzishiwa dawa za ARV kinga zao za mwili
zinaimarika ambapo lengo hili limefikiwa kwa asilimia 92 ikilinganishwa na
asilimia 88 kwa Mwaka 2018.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na juhudi za dhati zilizofanywa na Serikali, hali ya maambukizi ya
UKIMWI inaonesha kuna Watanzania takribani milioni 1.6 wanaoishi na VVU ambapo
kiwango cha maambukizi kimeshuka kutoka asilimia 7 ya Mwaka 2014 hadi kufikia
asilimia 4.7 kwa Mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika,
mafanikio hayo yamechangiwa na jitihada mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja
na kupitia miongozo na Sheria mbalimbali ambapo umri wa vijana kupima VVU bila
ya kuambatana na wazazi au walezi wao umeshushwa kutoka miaka 18 hadi 15.
Aidha, dawa mpya ya ARV yenye ufanisi (Dolutegravir) imeruhusiwa kuingizwa
na kutumika nchini ambapo hadi Desemba 2019 asilimia 53 ya watu wanaoishi na
virusi vya UKIMWI (WAVIU) wameanza kutumia dawa hiyo. Serikali pia imeridhia
mfumo wa watu kujipima wenyewe.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kufanya jitihada za kupunguza kasi
ya maambukizi katika jamii kwa kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali muhimu kwa
ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI; kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU
kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuimarisha huduma za elimu ya UKIMWI.
Mapambano Dhidi ya Dawa
za Kulevya
Mheshimiwa Spika,
Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kuigwa kimataifa katika kudhibiti na
kupambana na dawa za kulevya. Nchi yetu imefanikiwa kwa ufanisi mkubwa
kudhibiti uzalishaji, uuzaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Mafanikio hayo, yamewezesha waathirika wengi hasa vijana kubadilika na
kujihusisha katika shughuli za uzalishaji mali pamoja na kuipatia sifa Tanzania
kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika,
katika kikao cha 63 cha Kamisheni ya Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Dawa za Kulevya na Uhalifu kilichofanyika Machi 2020,
Tanzania ilipongezwa kwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza
miongozo ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020 Serikali ilifanikiwa kukamata
watuhumiwa wa dawa za kulevya 6,350. Katika kipindi hicho, kilogramu 34.986 za
heroine na kilogramu 1.556 za cocaine zilikamatwa. Kadhalika, tani 10.559 za
bangi, tani 6.016 za mirungi na mashamba ya bangi 9 yenye jumla ya ekari 4.25
yaliteketezwa.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na kukamata watuhumiwa na madawa ya kulevya, Serikali imeendelea kutoa
elimu kwa umma kuhusu athari za matumizi ya dawa za kulevya kupitia vyombo vya
habari na mitandao ya kijamii. Elimu kuhusu dawa za kulevya na UKIMWI pia
imetolewa kwa wasanii 600 pamoja na makundi maalum ikiwemo Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na viongozi wa mbio za Mwenge. Elimu hiyo,
imesaidia kujenga uelewa wa pamoja juu ya athari na namna ya kupambana na
kudhibiti dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Spika,
katika hatua nyingine, Serikali imefanya ukaguzi wa kampuni 58 zinazojihusisha
na biashara ya kemikali bashirifu na usafirishaji wa vifurushi. Kupitia ukaguzi
huo, imegundulika kuwa baadhi ya kampuni hizo hutumia majina bandia katika
kuingiza kemikali bashirifu na kusafirisha vifurushi vya dawa za kulevya.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imefanikiwa kukamata watuhumiwa 7
na zaidi ya kilo 890 za dawa za kulevya aina ya mirungi katika Ofisi za Posta
zilizokuwa na majina bandia kama vile mlonge na majani ya chai zikisafirishwa
kwenda nchi za Ulaya, Marekani na Canada.
Mheshimiwa Spika,
katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imeimarisha ukaguzi katika kampuni
zinazosafirisha vifurushi kwenda nje ya nchi zikiwemo Ofisi za Posta. Aidha,
katika kuboresha shughuli za ukaguzi wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye
asili ya kulevya, Serikali imeandaa miongozo ya ukaguzi na uchukuaji sampuli itakayosaidia
kufanya ukaguzi wenye ufanisi kubaini usafirishaji dawa za kulevya, kemikali
bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa tiba dhidi ya waathirika wa dawa za kulevya, Serikali inapanua wigo
wa utoaji huduma za tiba kwa kujenga na kuanzisha vituo vya utoaji wa huduma ya
methadone katika Mikoa ya Tanga na Pwani. Hadi sasa, zaidi ya watumiaji 8,200
wanapata huduma za tiba ya methadone kila siku katika vituo vilivyopo katika
mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Tanga na Pwani.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kudhibiti uingizaji, usafirishaji
na matumizi ya dawa za kulevya kwa kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya
matumizi na biashara ya dawa za kulevya na kuongeza huduma za tiba kwa
waathirika wa dawa za kulevya.
Uratibu wa Maafa
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha Mwaka 2019/2020, Nchi yetu imekumbwa na maafa mbalimbali
ikiwemo mafuriko, maporomoko ya ardhi na majanga ya moto. Wananchi wa Bonde la
Mto Rufiji wamepata athari ya mafuriko ambako serikali kupitia Mkoa na Wilaya,
pia Ofisi ya Waziri Mkuu inashirikiana na Viongozi wa Wilaya kutoa huduma
kadiri tathmini inavyoendelea. Maeneo mengi nchini yameendelea kupata mafuriko
na kuathiri shughuli za wananchi. Kufuatia hali hiyo, Serikali imechukua hatua
mbalimbali katika kukabili na kurejesha hali ikiwa ni pamoja na kujenga
miundombinu ya barabara, umeme, reli na majengo ya umma yaliyoathirika na kutoa
misaada ya kibinadamu kwa waathirika.
Mheshimiwa Spika,
Serikali pia imeendelea kutoa elimu kwa umma pamoja na kuzijengea uwezo Kamati
za Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote. Lengo ni kuongeza uelewa na kuimarisha
ustahimilivu dhidi ya majanga kwa kupunguza vihatarishi na vyanzo vinavyoweza
kusababisha maafa. Aidha, kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha
nchini, naelekeza wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wananchi
walioweka makazi katika maeneo hatarishi ikiwemo kandokando ya mito na mabonde
wanahama mara moja katika maeneo hayo ili kupunguza madhara yanayoendelea
kujitokeza katika jamii.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya utoaji wa
taarifa za tahadhari za awali na kuzingatia Wasifu wa Janga la Mafuriko na
Ukame nchini. Wasifu huo, unajumuisha taarifa za ramani ya maeneo hatarishi,
rasilimali, miundombinu muhimu katika maeneo hayo, hatari ya kudhurika na
makadirio ya hasara za kiuchumi kutokana na madhara ya mafuriko na ukame.
Mazingira
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na uharibifu wa
mazingira ikiwemo kuhamasisha upandaji miti, usafi na utunzaji wa mazingira
sambamba na kuanza mradi wa usambazaji gesi majumbani na kupiga marufuku
matumizi ya mifuko ya plastiki.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2019/2020, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa usambazaji wa
gesi majumbani, viwandani na katika magari. Hadi kufikia Desemba 2019, Serikali
imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya usambazaji gesi asilia na kuunganisha
nyumba 125 na Taasisi 4 mkoani Mtwara. Aidha, viwanda 48 vimeunganishwa na gesi
asilia ikiwemo viwanda vya Coca Cola, Tanzania Breweries Ltd, Kiwanda cha
Cement cha Wazo Hill vilivyopo Dar es Salaam na kiwanda cha Saruji cha Dangote
kilichopo Mtwara. Halikadhalika, ujenzi wa miundombinu ya kuunganisha nyumba
185 na Taasisi 4 jijini Dar es Salaam nao umekamilika.
Mheshimiwa Spika,
Serikali pia imefanikiwa kusimamia utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko
ya plastiki hapa nchini. Katika Mwaka 2019/2020, tani 259.2 za mifuko ya
plastiki zilikusanywa nchi nzima. Kati ya hizo, tani 171.5 ziliteketezwa na
tani 86.7 zilirejelezwa katika viwanda mbalimbali hapa nchini. Aidha, Serikali
imeendelea kusimamia ubora na matumizi ya mifuko mbadala.
Mheshimiwa Spika, katazo la mifuko ya plastiki limetoa fursa za kuzalisha mifuko mbadala ambapo wadau wengi wamejitokeza kuwekeza katika sekta hiyo. Kwa mfano, hadi sasa idadi ya viwanda vipya vinavyozalisha mifuko mbadala vimefikia 7. Kati ya hivyo viwanda 6 vipo Dar es Salaam na kimoja kipo Arusha.
Mheshimiwa Spika,
nitumie fursa hii kuziagiza Halmashauri zote nchini kuendelea kutunza mazingira
ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli mbalimbali za
kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, pamoja na mambo mengine, Serikali itaendelea na zoezi
la kuunganisha viwanda na nyumba nyingi zaidi kwenye mtandao wa matumizi ya
gesi asilia katika Mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara. Vilevile, Serikali
itaimarisha juhudi za kuhifadhi na kulinda mazingira kwa kutekeleza miradi
mbalimbali.
MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kushirikiana vyema na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuuendeleza na kuudumisha Muungano
wetu. Katika Mwaka 2019/2020, vikao mbalimbali vya Wataalam na Makatibu Wakuu
vilifanyika na kujadili masuala ya uvuvi kwenye ukanda wa bahari kuu, na hoja
za fedha na biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara. Aidha, maandalizi ya
vikao vya pamoja vya Mawaziri wa SMT na SMZ yamefanyika ikiwemo na kuundwa kwa
kamati ya kitaifa inayoratibu ugonjwa wa Corona.
Mheshimiwa Spika,
nitumie fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kuenzi dhamira
ya Waasisi wa Muungano.
Mheshimiwa Spika, ndugu
zetu Wachina wanao msemo maarufu usemao, “When we drink water from the well, we
should not forget those who dug it.” Msemo huu humaanisha kuwa, tunapokunywa
maji kutoka kwenye kisima basi tusisahau fadhila za waliochimba kisima hicho.
Hivyo basi, nasi hatuna budi kuendelea kuenzi na kuheshimu juhudi za Waasisi wa
Muungano wetu Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati
Mzee Abeid Amani Karume kwa kutuachia alama ya Muungano ambao umekuwa funzo kwa
mataifa mengine. Kwa msingi huo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza
wajibu wake wa kikatiba na kisheria wa kuuenzi na kuulinda Muungano wetu
sambamba na kudumisha amani na utulivu katika pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Spika,
nitumie fursa hii pia kuwashukuru wananchi wote wa Unguja na Pemba ambao sio tu
walinipokea vizuri, lakini pia walinipatia ushirikiano mkubwa wakati wa ziara
yangu ya kikazi mwezi Januari 2020 kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015 hadi 2020 kwa upande wa
Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea
kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuimarisha ziara na
ushiriki wa viongozi wakuu katika matukio muhimu ya kitaifa sambamba na kufanya
mikutano ya mashauriano ya viongozi na watendaji kwa lengo la kuimarisha
Muungano wetu.
UHUSIANO WA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika,
Tanzania imeendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika kutekeleza majukumu yake
mbalimbali ya kidiplomasia kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Sheria, Kanuni na
Taratibu zilizopo. Aidha, mahusiano kati ya Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa
yameendelea kuimarika.
Mheshimiwa Spika,
kuimarika kwa mahusiano na ushawishi wetu kwa Jumuiya ya Kimataifa kumewezesha
Tanzania kuanzisha Balozi mpya 2 katika nchi rafiki katika Mwaka 2019/2020.
Balozi hizo ni Windhoek – Namibia na Havana – Cuba. Sanjari na hilo, Tanzania
imeendelea kuridhia na kutekeleza Itifaki na Mikataba mbalimbali ya Kikanda na
Kimataifa.
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Tanzania itaendelea kuridhia na kutekeleza mikataba mbalimbali
ya kimataifa na kikanda sambamba na kuheshimu misingi ya mahusiano na mataifa
mengine duniani. Aidha, kupitia ushirikiano mzuri uliopo na ushawishi wetu
kwenye jumuiya za kikanda na kimataifa, Tanzania italinda uhuru wa kujiamulia
mambo yake yenyewe, na kujenga umoja na mtangamano wa kikanda wa Bara la
Afrika. Halikadhalika, Tanzania itashiriki kikamilifu katika kuendeleza siasa
ya kutofungamana na upande wowote kama dira na msimamo wetu katika mahusiano
baina yetu na Nchi nyingine katika Jumuiya ya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, kwa
upande mwingine Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kukuza ushirikiano
kwenye nyanja za biashara, uwekezaji, masoko ya bidhaa zetu, utalii na lugha ya
Kiswahili ili kuchochea maendeleo ya Nchi.
HABARI, UTAMADUNI NA
MICHEZO
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2019/2020 Serikali imeendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha
upatikanaji wa habari, kurasimisha kazi za kitamaduni, sanaa na ubunifu na
kuhakikisha watendaji wa kazi hizo wanapata maslahi yanayoendana na kazi zao.
Aidha, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba lugha ya Kiswahili inaendelezwa
ndani na nje ya Nchi na kutumika kama bidhaa ya soko na chanzo cha ajira kwa
wataalam wa lugha yetu ya Kiswahili.
Mheshimiwa Spika,
Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Tanzania tarehe 17 na 18 Agosti, 2019
jijini Dar es Salaam ulipitisha lugha adhimu ya Kiswahili kuwa moja ya lugha
rasmi za Jumuiya hiyo. Serikali imeandaa Miongozo ya Ufundishaji Kiswahili kwa
Wageni na kubainisha mahitaji ya uandaaji wa Mitaala ya kufundishia Kiswahili
katika Nchi za kigeni. Aidha, kupitia kanzidata ya usajili wa Wataalam wa
Kiswahili iliyopo Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), jumla ya wataalam
1,159 wamesajiliwa hadi mwezi Machi, 2020.
Mheshimiwa Spika,
nitumie fursa hii kulipongeza Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kufuatia
maboresho muhimu kwenye mfumo wa urushaji matangazo. Tarehe 30 Machi, 2020 TBC
iliweka jiwe la msingi wa ujenzi wa jengo la studio na kuzindua programu tumizi
na tovuti ya Safari Channel. Maboresho hayo yataimarisha mfumo mzima wa
urushaji matangazo hususan taarifa ya habari (Aridhio).
Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya
Huduma za Habari Na. 12 ya Mwaka 2016 na kuratibu na kusimamia maendeleo ya
michezo nchini ikiwemo ushiriki wa timu za Taifa katika mashindano mbalimbali
ya Kimataifa.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, kama
nilivyotangulia kueleza, katika kipindi cha takriban miaka mitano tangu
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iingie madarakani
tumeshuhudia mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Spika, mafanikio
hayo ni ishara tosha kwa Watanzania kwamba ahadi za Chama Cha Mapinduzi ndani
ya kipindi cha miaka mitano (2015 hadi 2020) zinatekelezwa vyema na kwa
mafanikio makubwa. Hivyo basi, katika Mwaka 2020/2021, Serikali pamoja na mambo
mengine, itaweka mkazo katika masuala yafuatayo:
Mosi: Kuimarisha na
kudumisha amani, utulivu, mshikamano na umoja wa kitaifa uliopo ili kuleta
maendeleo endelevu hususan tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2020;
Pili: Kulinda uhuru wa kujiamulia mambo yetu wenyewe
bila kuingiliwa; mipaka ya Nchi; haki; kuimarisha ujirani mwema na kuunga mkono
Sera ya Kutofungamana na Upande wowote kama dira na msimamo wetu katika
mahusiano na Nchi nyingine katika Jumuiya ya Kimataifa;
Tatu: Kudhibiti upotevu
wa mapato kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa
mapato na utoaji huduma hususan kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo
la kuondoa urasimu usio wa lazima pamoja na kuwahudumia wananchi wote kwa tija
tena bila ubaguzi wa aina yoyote;
Nne: Kuendelea
kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji;
Tano: Kuhimiza
uwajibikaji wa watendaji wa Serikali katika ufuatiliaji wa miradi ya kielelezo
hususan ujenzi wa miundombinu muhimu ya usafiri na usafirishaji, ikiwemo reli,
bandari, ujenzi wa meli, vivuko, viwanja vya ndege, barabara na madaraja;
Sita: Kuwatumikia
Watanzania wote kwa kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao
sambamba na kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii kwa kukamilisha na
kuendelea na ujenzi wa miradi ya miundombinu ya maji, afya na elimu;
Saba: Kuimarisha
uzalishaji na usambazaji wa nishati ya uhakika kwa kukamilisha Ujenzi wa Bwawa
la Kufua Umeme wa MW 2,115 la Julius Nyerere na kuhakikisha vijiji vilivyobaki
katika utekelezaji wa mradi wa REA III vinapatiwa umeme;
Nane: Kuongeza kasi ya
upimaji wa ardhi, mashamba na maeneo ya makazi, uwekezaji na ujenzi wa viwanda
ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira zaidi kwa
watanzania;
Tisa: Kusimamia
kikamilifu matumizi sahihi na yenye tija ya rasilimali zilizopo ili zitumike
kwenye maeneo yanayochochea ukuaji uchumi na utoaji huduma bora kwa wananchi;
na
Kumi: Kuhimiza
Watanzania kufuata maelekezo ya Serikali kuhusu kujikinga, kudhibiti na
kutosambaza virusi vya Corona ili kupunguza athari za kijamii na kiuchumi
zinazoweza kujitokeza kutokana na maambukizi hayo. Serikali kwa upande wake
inashirikiana kwa karibu na Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na
kutokomeza maambukizi ya virusi hivyo vya Corona.
Mheshimiwa Spika, natoa
wito kwa kila mwananchi kuendelea kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na
Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi mahiri na thabiti wa
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, tija na ufanisi,
uaminifu na kupiga vita rushwa.
MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA
2020/2021
Mheshimiwa Spika, kwa
Mwaka 2020/2021, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba
Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi bilioni mia tatu kumi na mbili,
milioni mia nane na mbili na mia tano ishirini elfu (312,802,520,000); kati ya
fedha hizo, Shilingi bilioni themanini na nane, milioni mia nne ishirini na tisa
na mia moja hamsini na sita elfu (88,429,156,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya
Kawaida na Shilingi bilioni mia mbili ishirini na nne, milioni mia tatu sabini
na tatu na mia tatu sitini na nne elfu (224,373,364,000) ni kwa ajili ya
Matumizi ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika,
Vilevile naliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi bilioni mia
moja ishirini na moja, milioni mia saba themanini na sita na mia mbili hamsini
na saba elfu (121,786,257,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo,
Shilingi bilioni mia moja kumi na tatu, milioni mia tano sitini na saba na mia
sita arobaini na saba elfu (113,567,647,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya
Kawaida na Shilingi bilioni nane, milioni mia mbili kumi na nane na mia sita na
kumi elfu (8,218,610,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa hoja.
0 Comments