Anaandika Grace Semfuko
TADB inaendelea
kuwasaidia Wakulima na kuwapa kipaumbele wawekezaji wazawa.
Hayo yalisemwa na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki
mwishoni mwa wiki alipofanya ziara katika kiwanda cha kuchakata mbegu za
Alizeti cha Qstek Wilayani Manyoni Mkoa wa Singida ambapo aliipongeza Benki
hiyo kwa kueleza kuwa imekuwa ikiwainua Wakulima na wawekezaji wadogo tofauti
na taasisi zingine za fedha.
Aliipongeza Benki hiyo
kwa kutoa mkopo wa shilingi Bilioni 2.2 kwa wawekezaji hao wa Qstek kwa ajili
ya uwekezaji wao,kiwanda kitakachokuwa na uwezo wa kuchakata mbegu za alizeti
tani 6,000 kwa mwaka na kuzalisha mafuta ya kula yenye ubora tani 2,500 kwa
mwaka.
“Niwapongeze sana TADB kwa namna mnavyowashika
mkono Wakulima, mtaji wa shilingi Bilioni 2.2 mlioutoa hapa ni mkubwa, niwasihi
muendelee kuwawezesha zaidi hadi watakaposimama kabisa, nafahamu pia mmewezesha
wakulima 829 na mnao mpango wa kuwawezesha wengine laki mbili” alisema Kairuki.
“Onesheni mfano wa
kuwasaidia Wakulima na Vijana wetu ili kwa pamoja tuweze kufikia malengo na
ndoto za Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli kwamba ifikapo 2025 tufikie uchumi
wa kati unaotegemea viwanda” alisisitiza Waziri Kairuki.
Aliongeza kuwa Serikali
imeweka unafuu wa kikodi kwa wawekezaji ili kuvutia uwekezaji na kuwataka
Wakurugenzi wa Halmashauri Nchini kutenga maeneo ya uwekezaji na kutowakwamisha
wawekezaji wanaotaka kuwekeza viwanda na miradi mbalimbali.
Mkurugenzi wa Benki ya
TADB Japhet Justine alisema mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umegharimu shilingi
Bilioni 3huku wao kama wadau wa maendeleo wametoa shilingi Bilioni 1.5 kwa
ajili ya kusaidia gharama za ujenzi wa
majengo ya kiwanda na shilingi milioni 718 kwa ajili ya kusaidia kuanzisha
uzalishaji.
Alisema Tanzania kwa
viwanda vya mafuta vilivyopo inazalisha tani 201,000 bado havitoshi na kuongeza
kuwa njia pekee ya kufanya mapinduzi katika katika sekta ya mafuta ni kuwezesha
wakulima wadogowadogo kufanya kilimo cha kisasa.
“Tunapaswa kuwasaidia
Wakulima wadogo wadogo na sisi kama benki ya maendeleo ya kilimo tumeshaanza
kuchukua hatua ya kuhakikisha wakulima hawa wanahama kutoka kwenye ule mfumo wa
kutumia mbegu ambazo walizitumia mwaka jana na msimu mpya ukianza wanazitumia
tena, tayaru tumeshaanza kulifanyia kazi suala hilo” alisema.
Aliongeza kuwa “tunaamini
tukihamasisha kuwainua wakulima wadogowadogo, tutawainua wengi hapa Manyoni na
sehemu nyingine nchini, kwa hiyo nikuahidi tutaendelea kushirikiana na Mkoa wa
Singida kuwainua wakulima wa alizeti ambao tunaamini wakiinuka wao na Singida
imenyanyuka” aliongeza.
Alisema huo ni mkopo
wao wa pili kuutoa ndani ya mkoa huo ambapo tayari wametoa zaidi ya shilingi
milioni 600 kwa wakulima wadogowadogo waliokuwa wanazalisha alizeti pamoja nan
a hizo shilingi Bilioni 2.2 kwa ajili ya kiwanda hicho cha Qstek lengo ni
kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi inayoongoza kuuza mafuta ya alizeti nje ya
nchi.
Mkurugenzi wa kiwanda
hicho Emmanuel Nagunwa aliishukuru Serikali kwa kuwawezesha kuanzisha kiwanda
hichoambacho kitaongeza wigo wa biashara ya zao la alizeti na kuchochea mapato
kupitia kodi mbalimbali zinazotokana na uzalishaji wa kiwanda hicho.
0 Comments