Na Mwandishi wetu, Dar Es Salaam.
Wawekezaji wa Kiwanda cha OK
Plastic Limited cha Vingunguti Jijini Dar Es Salaam ameiomba Serikali kupitia
Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) kusitisha uuzwaji wa malighafi za shaba nje ya
nchi zoezi linalofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wa ndani kwa kuwa
linawapunguzia upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa viwanda vya ndani na hivyo
kupunguza uzalishaji kwenye viwanda vyao.
Kiwanda cha Ok Plastic Limited kilichokuwa
na uwezo wa kuzalisha bidhaa za shaba tano 500 kwa mwezi, hivi sasa kinazalisha
tani 150 tu kutokana na kukosekana kwa malighafi hiyo ndani ya nchi hatua
ambayo amesema inawapa changamoto kubwa kiwandani hapo.
Hayo yalibainishwa na Meneja wa
Kiwanda hicho Bw. Fadil Ghaddar kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki aliyetembelea kiwandani hapo ikiwa
ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ambapo alisema iwapo Serikali itazuia uuzwaji
holela wa bidhaa hiyo nje ya nchi, itaongeza uzalishaji wa viwanda vya ndani.
“Mheshimiwa Waziri, sisi
changamoto yetu kubwa ni malighafi ya shaba kiwandani kwetu, malighafi hii ipo
nyingi nay a kutosha hapa nchini kwani kuna utafiti ulifanywa na Taasisi
ya BICO ya chuo kikuu cha Dar es Salaam
ambao ulionyesha kuna upatikanaji wa kutosha wa bidhaa hiyo, tunakuomba
utuwasilishie ombi letu la kusitisha uuzwaji nje ya nchi wa malighafi hizo,
kwani nasi tunapoagiza hujo nje tunatumia gharama kubwa sana” alisema Bw.
Ghaddar.
Kwa upande wake Waziri Kairuki
alisema amepokea ombi lao hilo na ataliwasilisha kwenye mamlaka zinazohusika.
“Nimelipokea ombi lenu na
nitaliwasilisha kwenye mamlaka zinazohusika, nipende tu kuwahakikishia Serikali
inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kila mara na nyie ni mashahidi
kwani tumeboresha Sera na sheria zetu ili kuwarahisishia uwekezaji wenye tija”
alisema Waziri Kairuki.
Aidha katika hatua nyingine
Waziri Kairuki, amewataka wawekezaji waliosajili miradi yao kwenye Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC), kuwasilisha taarifa za maendeleo na changamoto zao
kila baada ya miezi sita ili ziweze kufanyiwa kazi za uboreshaji na utatuzi wa
changamoto zake.
Kairuki alisema Kanuni za usajili
za TIC zinawataka wawekezaji hao kufanya hivyo na kwamba hatua hiyo inalenga kuwaweka
karibu wawekezaji hao ambao wamekuwa na tija ya kiuchumi kutokana na uzalishaji
wa bidhaa mbalimbali za viwandani na kilimo ambazo hutoa ajira kwa watanzania
na ulipaji kodi unaostahili.
“Nawasihi wawekezaji wote
mliojisajili na TIC, pelekeni taarifa zenu za maendeleo ya miradi yenu kila
baada ya miezi sita ili tujue ni wapi kuna changamoto tuweze kuzitatua, ni kwa
nia njema sana, Serikali yenu ipo na ni sikivu, pia naomba nawapongeza wamiliki
wa kiwanda hiki cha OK kwa ulipaji wa kodi mzuri na mmeajiri watanzania wengi,
na wengine igeni mfano wa kiwanda hiki” alisema Waziri Kairuki.
Kiwanda cha OK Plast Limited tangu
kuanzishwa kwake mwaka 2005 kimekuwa na mafanikio makubwa ya soko la bidhaa
zake nchini Tanzania nan chi jirani ikiwepo Kenya, Kiwanda hiki kimewekeza
nchini kwa mtaji wa Shilingi Bilioni 10 na kinazalisha bidhaa za nyaya za
umeme,betri ingots na mikeka, kimeajiri wafanyakazi 595 wa kitanzania na raia
wa kigeni watano.
Mwisho.
0 Comments