Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)Mussa Zungu amewataka Wamiliki wa Mgodi wa Dhahabu Barrick North Mara kutumia teknolojia rafiki iitwayo CIP Gold processing ili kulinda mazingira ya Tanzania na kujipunguzia gharama za utunzaji wa mazingira katika mgodi huo.
Waziri Zungu aliyasema hayo juzi baada ya kukagua bwawa la mgodi linalohifadhi tope sumu katika kiwanda hicho huku akiwa ameambatana na Waziri wa Madini Dotto Biteko, Naibu Waziri wa Ardhu, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula, Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Profesa Esnati Chagu na Watendaji wa NEMC.
“Muhimu teknolojia hii itumike kutibu tope sumu katika migodi yote kwani athari zake ni kubwa endapo sumu hii itaingia katika mito na kuhatarisha Afya za Wananchi” alisema Waziri Zungu.
Alisema ni kweli Serikali inathamini Uwekezaji ili kukuza uchumi lakini Uwekezaji lazima uzingatie Sheria na Kanuni za kutunza na kuhifadhi mazingira ya nchi ili yapatikane maendeleo endelevu.
“Tumejiridhisha usalama wa maji taka upon a mara kwa mara tunahakikisha tunafanya ukaguzi ili maji taka haya yasiwaathiri Wananchi waliouzunguka mgodi huu”alisema Zungu na kuongeza kuwa migodi ina kila sababu ya kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira katika kutibu maji taka yake kwani kwa kufanya hivyo kutalinda afya za Wananchi wanaozunguka migodi na kuondoa migogoro kati ya wawekezaji na wananchi” alisema.
Alisema ameambatana na Naibu Waziri wa Ardhi na Waziri wa Madini kwa lengo la kusikiliza changamoto za wananchi na Wawekezaji ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo.
Aidha Waziri Biteko amekabidhu hundi ya Shilingi Bilioni 34 ambayo alisema ni fidia kwa Wananchi wa eneo la Nyamongo ili kuondoa migogoro kati ya Wananchi na Kampuni ya Barrick.
“Baada ya Malipo haya tunaamini hakutakuwepo na mgogoro tena, kadhalika Serikali haitawavumilia watu watakaochochea migogoro kati ya wananchi na mgodi huu”alisema Waziri Biteko.
Nae Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula amewataka Wananchi kufuata taratibu za mipango miji kupitia Halmashauri zao ili kuepukana na ujenzi holela ambao unakwamisha juhudi za kuhifadhi na kutunza mazingira.
“ Nawaomba Wananchi achene tabia ya kujenga nyumba za kutegesha ili baadae mlipwe fidia, kumbukeni kwa mba kwa kufanya hivyo kunaweza kuwakosesha haki zenu za msingi kutokana na kutofuata taratibu za mipangomiji”alisema Mabula.
Nae Mkurugenzi wa NEMC Dkt Samuel Gwamaka amewahakikishia Watanzania kwamba baraza lake linafanyia kazi malalamiko ya Wananchi wanaozunguka migodi na kwamba NEMC inakagua migodi yote nchini ili kuona iwapo taratibu za kulinda mazingira zinafuatwa.
“Barrick North Mara ni miongoni mwa migodi tunayoifuatilia ili kuhakikisha uendeshaji wake hauleti madhara kwenye mazingira na wananchi wa maeneo ya jirani” alisema Dkt Gwamaka.
ReplyForward
|
0 Comments