HOTUBA YA MHE. DKT.
JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA
KULIHUTUBIA KWA MARA YA MWISHO BUNGE LA KUMI NA MOJA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, UKUMBI WA BUNGE, DODOMA, TAREHE 16 JUNI, 2020
Mheshimiwa Spika;Awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aliyetujalia uhai na kutuwezesha kuiona siku ya leo. Kama, Mheshimiwa Spika unavyofahamu, wapo wenzetu ambao tulikuwa nao wakati wa kuzindua Bunge hili, lakini leo hatuko nao. Wametangulia mbele za haki. Hivyo basi, kwa heshima yao naomba tusimame kwa dakika moja kuwakumbuka. Mwenyezi Mungu azipumzishe roho zao mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Spika,
kabla sijaendelea zaidi, naomba kutambua uwepo wa viongozi mbalimbali kwenye
Ukumbi huu. Nimefurahi kuwaona Waheshimiwa Marais wetu Wastaafu wote wapo hapa,
pamoja na Makamu wa Rais Wastaafu na pia Mawaziri Wakuu wastaafu, akiwemo
Mheshimiwa Lowasa na Mheshimiwa Sumaye. Hii ndiyo Tanzania.
Kwa namna ya pekee,
napenda nikushukuru wewe, Mheshimiwa Spika, Job Ndugai, Mbunge wa Kongwa, kwa
kunipa kibali cha kuja kulihutubia Bunge hili. Aidha, nawashukuru Naibu Spika,
Mheshimiwa Tulia Ackson, pamoja na Wenyeviti wa Bunge, Mheshimiwa Andrew Chenge
na Mheshimiwa Najma Giga, kwa ushirikiano wenu. Ahsanteni sana. Hiki ni
kielelezo cha uhusiano mzuri uliokuwepo kati ya mihimili yetu mitatu katika
kipindi chote cha miaka mitano iliyopita.
Nitumie fursa hii
pia kueleza kuwa, tangu nimeingia ndani ya Bunge hili leo nimeshuhudia
mabadiliko mengi makubwa, tofauti na ilivyokuwa wakati mimi nikiwa
Mbunge. Hivi sasa nimeona hata Waheshimiwa Wabunge wanatumia vifaa vya
kisasa kama vile tablets. Enzi zetu, vifaa hivyo, havikuwepo. Hivyo basi,
nakupongeza sana Mheshimiwa Spika kwa ubunifu huu; na nawapongeza pia
Waheshimiwa Wabunge kwa kuweza kuvitumia vifaa hivi; na hivyo kulifanya Bunge
lenu kuwa la kisasa namna hii.
Mheshimiwa Spika;
Tarehe 20 Novemba
2015, nilikuja hapa kulizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Leo tena, kwa madhumuni ya kutimiza matakwa ya Katiba yetu, nimekuja
kulihutubia kwa mara ya mwisho, ili hatimaye kuweza kuruhusu kuanza kwa
mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika
mwezi Oktoba 2020.
Utakumbuka,
Mheshimiwa Spika, kuwa wakati nikizindua Bunge lako Tukufu, nilitumia fursa
hiyo pia kutoa mwelekeo, kueleza malengo na pia kutaja vipaumbele vya Serikali
ya Awamu ya Tano. Siku ile, nakumbuka, nilieleza mambo mengi sana, ambayo
nafarijika kuona kuwa mengi tumefanikiwa kuyatekeleza, kama ambavyo Waheshimiwa
Mawaziri mbalimbali walieleza wakati wakiwasilisha Bajeti zao. Namshukuru pia
Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambaye naye wakati wa kuwasilisha Hotuba ya Bajeti
ya Serikali alitoa ufafanuzi wa mafanikio tuliyoyapata. Aidha, jana, Mheshimiwa
Waziri Mkuu alitoa maelezo ya kina kuhusu mafanikio yaliyopatikana.
Kwa ujumla, naweza
kusema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumeweza kutimiza wajibu
wetu wa kuwatumikia Watanzania kwa kiasi kikubwa. Na tumeweza kufanya hivyo
kutokana na ushirikiano mkubwa tulioupata kutoka kwa Watanzania wote.
Nitumie fursa hii kuwashukuru ninyi Waheshimiwa Wabunge kwa kuishauri vyema na
pia kuisimamia vizuri Serikali katika kutekeleza majukumu yake. Aidha,
nawashukuru Waheshimiwa Madiwani kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa shughuli
mbalimbali za maendeleo kwenye maeneo yao. Kama mnavyofahamu, Madiwani ni
kiungo muhimu kati ya wananchi na Serikali; lakini pia kati yenu Waheshimiwa
Wabunge pamoja na wananchi. Hivyo, hatuna budi kuwashukuru Waheshimiwa Madiwani
wetu.
Napenda pia nitumie
fursa hii kuwashukuru watangulizi wangu - kuanzia Awamu ya Kwanza iliyoongozwa
na Baba ya Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; Awamu ya Pili,
iliyoongozwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi; Awamu ya Tatu ya Mzee Benjamin William
Mkapa pamoja na Awamu ya Nne ya Mzee Jakaya Mrisho Kikwete– kwa kuweka misingi
imara na kutengeneza mazingira yaliyowezesha kupatikana mafanikio hayo
mbalimbali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Na katika hilo,
nawashukuru pia viongozi wetu wakuu wastaafu; Mzee wetu Mwinyi (Mzee Ruksa),
Mzee wetu Mkapa (Mzee wa Ukweli na Uwazi) na Mzee Kikwete (Mzee wa Ari Mpya,
Nguvu Mpya na Kasi Mpya) kwa ushauri wao mbalimbali waliotupatia katika kipindi
chote cha miaka mitano iliyopita. Nikiri tu kwamba ushauri wao umenisaidia sana
mimi binafsi pamoja na Serikali ninayoingoza. Nawashukuru pia Makamu wa Rais
Wastaafu, Marais wa Zanzibar Wastaafu na Mawaziri Wakuu Wastaafu kwa
ushirikiano wao.
Mheshimiwa Spika;
Kama
utakavyokumbuka, mojawapo ya ahadi kubwa niliyoitoa wakati wa kuzindua Bunge
ilikuwa kudumisha amani, umoja, mshikamano, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar
pamoja na Muungano wetu; na halikadhalika kuimarisha amani, ulinzi, usalama na
utulivu wa nchi yetu. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba
tumeitimiza ahadi hiyo kwa vitendo.
Watanzania tumebaki
kuwa wamoja na tumeendelea kushirikiana licha ya tofauti zetu za dini, kabila,
rangi, ufuasi vyama vya siasa au mahali tunakotoka. Muungano wetu pia
umeendelea kuimarika. Tumeweza kushughulikia baadhi ya changamoto za Muungano
na kufikia makubaliano, ikiwemo kuhusu suala la gharama za kushusha mizigo
{landing fees) na pia kufuta kodi ya ongezeko la thamani pamoja na malimbikizo
ya kodi hiyo ya shilingi bilioni 22.9 ambayo Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO)
lilikuwa likidaiwa na TANESCO. Tumefanikiwa pia kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar.
Kuhusu amani,
ulinzi na usalama, nchi yetu imeendelea kuwa Kisiwa cha Amani na mipaka yake
imebaki kuwa salama. Utakumbuka kuwa, wakati tukiingia madarakani, kulikuwepo
na wimbi kubwa la uhalifu wa kutumia silaha pamoja na vitendo vingine vya
kihalifu, ikiwemo matukio ya mauaji kule Kibiti na Rufiji. Hata hivyo, kutokana
na kazi kubwa iliyofanywa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, vitendo vyote
hivyo vilikomeshwa, na nchi yetu sasa ipo salama. Na katika kuthibitisha hilo,
Ripoti ya Global Peace Index ya Mwaka 2020 imeitaja Tanzania kushika nafasi ya
kwanza kwa amani na utulivu kwenye eneo la Afrika Mashariki na ya saba kwa nchi
za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa niaba yenu na kwa niaba ya
Watanzania wote, navipongeza sana vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi
kubwa na nzuri wanayoifanya ya kusimamia amani nchini. Nawashukuru pia
Watanzania kwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi cha
miaka mitano iliyopita, tumejitahidi pia kuimarisha maadili, nidhamu na
utendaji kazi Serikalini. Kama tulivyoahdi, hatukuwa na mzaha kwa viongozi na
watumishi wazembe, walioshindwa kufanya kazi kwa weledi, nidhamu, maarifa na
uadilifu. Viongozi na watumishi wa namna hiyo walichukuliwa hatua za kinidhamu,
ikiwemo “kuwatumbua”, kuwashusha vyeo na mishahara, au kuwapa onyo kali.
Kwa mujibu wa
takwimu zilizopo, jumla ya watumishi 32,555 wamechukuliwa hatua mbalimbali,
wakiwemo watumishi 15,508 ambao waliachishwa kazi kwa kukutwa na vyeti vya
kughushi. Aidha, tulifuta ajira hewa 19,708 zilizoigharimu Serikali kila mwezi
kiasi cha shilingi bilioni 19.8. Hatua hii ilitoa fursa ya kuajiri watumishi
wapya wenye sifa wapatao 74,173. Vilevile, kufuatia hatua tulizochukua,
tuliwapandisha vyeo watumishi 306,917 na kulipa madeni ya watumishi ya
mishahara na yasiyo ya mishahara yenye thamani ya shilingi bilioni 472.6 (ya
kimshahara shilingi bilioni 114.5 na yasiyo ya kimshahara shilingi bilioni
358.1). Waheshimiwa Wabunge, tulifanya haya kwa lengo kulinda heshima ya
wafanyakazi na kuleta nidhamu kwenye utumishi wa umma.
Sambamba na
kuimarisha nidhamu Serikalini, tulizidisha mapambano dhidi ya rushwa, uhujumu
uchumi na ufisadi. Utakumbuka kuwa, wakati nikizindua Bunge hili niliahidi
kuanzisha Mahakama ya Uhujumu Uchumi. Mahakama hiyo ilianzishwa mwaka 2016 na
mpaka sasa imepokea mashauri 407, ambapo mashauri 385 tayari yamesikilizwa.
Zaidi ya hapo, katika kupambana na adui rushwa, Taasisi yetu ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeweza kufungua mashauri 2,256; ambapo mashauri
1,926 tayari yametolewa uamuzi, na Serikali imepata ushindi kwenye mashauri
1,013.
Katika kipindi cha
miaka mitano iliyopita pia TAKUKURU imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi
bilioni 273.38, zikiwemo fedha walizokuwa wamedhulumiwa wakulima. Aidha,
TAKUKURU imetaifisha fedha taslim shilingi milioni 899, Dola za Marekani
1,191,651, EURO 4,301,399, nyumba 8 zenye thamani ya shilingi bilioni 11.6,
magari matano yenye thamani ya shilingi milioni 126 pamoja na viwanja vitano
(5). Aidha, tumeweza kurejesha mali za Serikali zilizochukuliwa na watu binafsi
ama taasisi kinyume cha sheria, zikiwemo nyumba na majengo 98 (ikiwemo Mbeya
Hotel), mashamba 23, viwanja 298, kampuni 3, maghala 69. Vile vile, kiasi cha
fedha na mali zilizowekewa zuio kusubiria kukamilika kwa taratibu za kisheria
za utaifishaji ni shilingi bilioni 52.7; Dola za Marekani milioni 55.8; Euro
milioni 4.3, magari 75, nyumba 41; viwanja 47 na mashamba 13.
Hii, bila shaka,
inaonesha dhamira yetu isiyo na mashaka ya kupambana na rushwa na ufisadi.
Naupongeza Muhimili wa Mahakama, TAKUKURU, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,
Jeshi la Polisi pamoja na wananchi kwa ujumla kwa kufanikisha mapambano haya.
Lakini, nitumie fursa hii pia kuipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na
Dawa za Kulevya kwa kufanikiwa kudhibiti na kuvunja mitandao ya biashara hiyo
haramu hapa nchini. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, jumla ya tani
97.99 za bangi, tani 85.84 za mirungi, kilo 567.96 za heroin na kilo 23.383 za
cocaine zimekamatwa pamoja na watuhumiwa 37,104. Hatua hizi ndizo zilifanya
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na
Uhalifu (UNODC), mwaka jana, kuipongeza nchi yetu kwa kupunguza uingizaji wa
dawa za kulevya kwa asilimia 90. Lakini niseme, mafanikio haya yasingepatikana
kama pasingekuwa na Sheria nzuri zilizopitishwa na Bunge hili. Hivyo basi,
nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri mliyoifanya. Nawashukuru
pia Watanzania kwa ushirikiano waliotoa katika kukabiliana na biashara hii
haramu.
Mheshimiwa Spika;
Wakati nikizindua
Bunge hili, nilieleza kwa kirefu sana kuhusu kutoridhishwa kwangu na hali ya
ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Hivyo basi, katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita, tumejitahidi kushughulikia suala hilo, kwa kusimamia uadilifu kwa
watumishi waliopewa dhamana ya kukusanya mapato, kuimarisha sheria za kodi,
mifumo ya TEHAMA, kupanua wigo wa walipa kodi, kupunguza misamaha na kuziba
mianya ya ukwepaji kodi, n.k.
Kutokana na hatua
hizo, ukusanyaji wa mapato umeimarika. Mathalan, ukusanyaji wa mapato ya kodi
kwa mwezi umeongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 mwaka 2015 hadi
shilingi trilioni 1.3 hivi sasa; na mwezi Disemba 2019, TRA ilikusanya shilingi
trilioni 1.987, kiwango ambacho ni cha juu kabisa kuwahi kukusanywa kwenye
historia ya nchi yetu. Kwa upande wa mapato yasiyo ya kodi, nayo yameongezeka
kutoka chini ya shilingi bilioni 688.7 mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi
trilioni 2.4 mwaka 2018/2019. Halikadhalika, mapato ya ndani ya Halmashauri
yameongezeka kutoka shilingi bilioni 402.66 Mwaka 2015/2016 hadi shilingi
bilioni 661 Mwaka wa Fedha 2018/2019. Hii imefanya mapato ya ndani kwa
ujumla, kuongezeka kutoka shilingi trilioni 11.0 mwaka 2014/2015 hadi shilingi
trilioni 18.5 Mwaka wa Fedha 2018/2019.
Sambamba na
kuongeza ukusanyaji wa mapato, tumedhibiti matumizi ya fedha za Serikali kwa
kuzuia au kupunguza safari za nje zisizo za lazima, semina, warsha,
makongamano, matamasha na udanganyifu kwenye manunuzi. Aidha, tulipitia upya
muundo wa Serikali ili kuongeza ufanisi na kubana matumizi yasiyo ya lazima.
Katika zoezi hilo, tuliweza kupunguza idadi ya wizara kutoka 29 hadi 22; na pia
kuunganisha taasisi, idara na vitengo mbalimbali. Vilevile, tumepitia miundo ya
wizara, taasisi na idara zinazojitegemea 116 na kufanikiwa kuokoa kiasi cha
shilingi bilioni 17.4. Tumeunganisha pia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoka
mitano kuwa miwili kwa lengo hilo hilo la kuongeza ufanisi na kupunguza gharama
za uendeshaji. Mabadiliko yote haya yalifanyika baada ya kupata baraka za Bunge
hili Tukufu. Hivyo basi, nina haki kabisa ya kusema “ahsanteni sana Waheshimiwa
Wabunge”. Bila ya ninyi, haya yote yasingefanyika.
Mheshimiwa Spika;
Kwa sababu ya
kuongezeka kwa mapato na kudhibiti matumizi, Serikali iliweza kuongeza bajeti
ya maendeleo kutoka wastani wa asilimia 26 hadi asilimia 40. Hii ndiyo
imetuwezesha kuboresha huduma mbalimbali za jamii na kutekeleza miradi mikubwa
ya maendeleo. Kwa upande wa huduma za jamii, tumepanua wigo na kuboresha
upatikanaji wa huduma za elimu, afya pamoja na maji. Kwenye elimu, kama
unavyofahamu, tulianza kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari
ambapo mpaka mwezi Februari 2020 tulikuwa tumetumia shilingi trilioni 1.01
kugharamia.
Lakini, mbali na
kutoa elimu bure, tumeongeza idadi ya shule za msingi kutoka 16,899 mwaka 2015
hadi 17,804 mwaka huu; na shule za sekondari kutoka 4,708 mwaka 2015 hadi shule
5,330 mwaka 2020. Vilevile, tumekarabati shule kongwe za sekondari 73 kati ya
89, tumejenga mabweni 253 na vyumba vya maabara ya 227. Aidha, tumetoa
vifaa kwenye maabara zipatazo 2,956 na tumepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la
uhaba wa madawati, ambapo idadi yake imeongezeka kutoka madawati 3,024,311 mwaka
2015 hadi kufikia 8,095,207; sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 200.
Kwa upande wa Vyuo
vya Ualimu, tumekarabati vyuo 18, tumejenga upya vyuo viwili (Murutunguru na
Kabanga) na halikadhalika tumepeleka kompyuta 1,550 kwenye vyuo vyote 35 vya
ualimu kwa lengo la kuimarisha ufundishaji wa masomo ya TEHAMA. Kuhusu ngazi
nyingine za elimu, tumeongeza Vyuo vya Ufundi (VETA) kutoka 672 mwaka 2015 hadi
712 mwaka 2020; na pia tumekarabati na kuboresha vifaa na miundombinu ya
kufundishia katika vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi (FDC). Vilevile, tumejenga
hosteli, kumbi za mihadhari, mabwalo ya chakula na maktaba kwenye vyuo vikuu.
Tumeongeza pia bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 348.7
mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 450 mwaka huu wa Fedha 2019/2020.
Kutokana na hatua
hizo, uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza umeongozeka maradufu kutoka
wastani wa wanafunzi milioni 1 mwaka 2015 hadi kufikia milioni 1.6 hivi sasa.
Aidha, idadi ya wanafunzi wa kidato cha I – IV imeongezeka kutoka 1,648,359
mwaka 2015 hadi 2,185,037. Idadi ya wanafunzi wa VETA imeongezeka kutoka
117,067 mwaka 2015 hadi 226,767 mwaka 2020; na idadi ya wanafunzi wa Vyuo vya
Maendeleo ya Wananchi (FDC) imeongezeka kutoka 6,693 mwaka 2016/17 hadi 9,736
mwaka 2018/19. Kwa upande wa vyuo vikuu, idadi ya wanafunzi wanaojiunga mwaka
wa kwanza imeongezeka kutoka 65,064 mwaka 2015 hadi 87,813 mwaka 2020; na wenye
kupata mikopo wameongezeka kutoka 98,300 mwaka 2014/2015 hadi 130,883 mwaka
2019/2020. Kwa taarifa hii Waheshimiwa Wabunge, naamini nitakuwa sijakosea
nikisema, kazi kubwa imefanyika kwenye sekta ya elimu.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa sekta
ya afya, tumeongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya 1,769, zikiwemo
zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 71, hospitali za mikoa
10, ikiwemo Hospitali ya Mkoa wa Mara, (Mwalimu Nyerere Memorial Hospital) ambayo
ujenzi wake ulikwama tangu miaka ya 1970. Vilevile, tumejenga hospitali za
rufaa za kanda 3. Hii imefanya vituo vya kutolea huduma za afya kuongezeka
kutoka 7,014 mwaka 2015 hadi kufikia 8,783 hivi sasa.
Zaidi ya hapo,
tumeajiri watumishi wapya wa afya wapatao 14,479, wakiwemo madaktari wapya
1,000 tuliowaajiri hivi karibuni. Hii imeongeza idadi ya watumishi wa afya
nchini kutoka 86,152 mwaka 2015 hadi 100,631 mwaka 2020. Tumeimarisha pia
upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, ambapo tuliongeza bajeti yake kutoka shilingi
bilioni 31 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 270 hivi sasa; na pia tumenunua na
kusambaza magari ya kubeba wagonjwa (Ambulances) 117. Vilevile, tumefanikiwa
kusomesha madaktari bingwa 301 ambao wamewezesha kuimarisha matibabu ya
kibingwa nchini, hususan kwa magonjwa ya moyo, masikio, figo, mifupa, ubongo,
kansa, n.k.
Kutokana na hatua
hizo, idadi ya akinamama wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za
afya imeongezeka kutoka asilimia 64 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 83 hivi
sasa; vifo vya watoto wachanga (wenye chini ya siku 28) vimepungua kutoka
wastani wa vifo 25 hadi vifo 7 kwa kila vizazi hai 1,000; na idadi ya rufaa za
kwenda nje ya nchi zimepungua kwa asilimia 95. Aidha, kutokana na kuimarishwa
kwa matibabu ya kibingwa, baadhi ya wagonjwa kutoka mataifa jirani wameanza
kuja kutibiwa nchini, hususan magonjwa ya moyo. Hii inadhihirisha kuwa,
tumefanya kazi kubwa sana katika kuboresha na kuimarisha sekta ya afya nchini.
Ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi.
Kuhusu maji, tumetekeleza
miradi ya maji 1,423, ambapo miradi 1,268 ni ya vijijini na 155 ni ya mijini.
Miongoni mwa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa ni wa kutoa maji Ziwa
Victoria kwenda Nzega, Tabora na Igunga; Mradi wa Maji wa Arusha pamoja na
mradi wa kupeleka maji kwenye miji 28 unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi
trilioni 1.2. Miradi mingine ya maji ilielezwa vizuri kwenye Hotuba ya Waziri
wa Maji wakati wa kuwasilisha Bajeti. Na kutokana na jitihada zilizofanyika,
upatikanaji wa majisafi na salama vijijini umeongezeka kutoka asilimia 47 mwaka
2015 hadi kufikia asilimia 70.1 mwaka 2020; na kwa mijini kutoka asilimia 74
mwaka 2015 hadi asilimia 84 mwaka 2020.
Tumeimarisha pia
huduma za mawasiliano, hususan kwa kuboresha usikivu wa simu kutoka asilimia 79
mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 94 mwezi Disemba 2019. Aidha, idadi ya
watumiaji wa simu za mkononi pamoja na watumiaji data imeongezeka maradufu. Na
hali hiyo imechangiwa zaidi na kupungua kwa gharama za kupiga simu kwa dakika
moja kutoka shilingi 267 mwaka 2015 hadi shilingi 40 tu hivi sasa.
Sambamba na hayo,
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kufufua Shirika letu la
Simu (TTCL) ambalo lilikuwa limekufa pamoja na kuongeza hisa zetu kwenye
Kampuni ya Airtel kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49. Huu ni ushahidi mwingine
kwamba kazi tuliyotumwa na Watanzania tumeifanya kikamilifu.
Mheshimiwa Spika;
Mbali na kuboresha
huduma za jamii, tumetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hususan katika
ujenzi, uchukuzi na nishati ya umeme. Tumekamilisha ujenzi wa barabara zenye
urefu wa takriban kilometa 3,500 na hivyo kuifanya nchi yetu iwe na kilometa
12,964 za barabara za lami. Barabara nyingine zenye urefu wa zaidi ya kilometa
2,000 zinaendelea kujengwa. Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi
yetu, tumejenga barabara za juu (flyover na interchange) Dar es Salaam ili
kupunguza tatizo la msongamano wa magari na pia tumekamilisha ujenzi wa
madaraja makubwa 13, likiwepo Daraja la Nyerere – Kigamboni, Daraja la Magufuli
katika Mto Kilombero pamoja na Daraja la Sibiti; na wakati huo huo ujenzi wa
madaraja mengine makubwa unaendelea, likiwemo Daraja la Kigongo - Busisi lenye
urefu wa kilometa 3.2, Daraja la Salender lenye urefu wa kilometa 1.03 pamoja
na Daraja la Wami lenye urefu wa meta 513.5.
Kwa ujumla, katika Awamu hii, hakuna Mkoa au Wilaya ambayo haikupatiwa fedha za kujenga barabara za lami. Makao Makuu ya Mikoa na Wilaya karibu zote sasa yanameremeta kwa lami na taa za barabarani. Na ahadi yetu ya kuunganisha Mikoa kwa barabara za lami nayo imetekelezwa kwa asilimia kubwa; na kwa Mikoa ya Rukwa-Katavi, Katavi-Tabora, Singida-Tabora, Tabora-Kigoma na Kigoma-Kagera nayo inaendelea kuunganishwa. Mathalan, barabara ya Mpanda – Tabora kilometa 359 wakandarasi wanne wanaendelea kujenga kwa kiwango cha lami; na barabara ya Manyoni – Tabora inakamilishwa kujengwa kwa lami. Vilevile, barabara ya kutoka Mpanda kwenda Kigoma na Kigoma hadi Nyakanazi zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hakika, kazi kubwa imefanyika.
Sambamba na kujenga
barabara, tunakamilisha Awamu ya Kwanza ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar
es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa kilometa 300 na ujenzi wa Awamu ya Pili
kutoka Morogoro hadi Makutupora umbali wa kilometa 422 umefikia asilimia 30.
Miradi hii miwili inagharimu shilingi trilioni 7.062. Ujenzi wa sehemu ya
Mwanza – Isaka – Dodoma ipo kwenye maandalizi. Tumekarabati pia reli ya zamani
kutoka Dar es Salaam hadi Isaka kilometa 970 na halikadhalika tumefufua usafiri
wa reli ya Dar es Salaam –Tanga – Moshi - Arusha, ambao ulisimama kwa takriban
miaka 20. Lakini, katika kipindi cha miaka mitano, tumefanikiwa kurudisha tena
usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga, Moshi hadi Arusha. Huu ni
uthibitisho kuwa kazi kubwa imefanyika.
Kwa upande wa
usafiri wa maji, hivi sasa tunafanya upanuzi wa Bandari zetu kuu za Dar es
Salaam, Mtwara na Tanga. Vilevile, tumeboresha usafiri wa maji kwenye Maziwa
yetu Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa kuboresha bandari zake pamoja
na kujenga na kukarabati meli. Kwenye Ziwa Victoria tumekarabati meli tano za
Mv. Victoria, Mv. Butiama, Mv. Clarias, Mv. Umoja na Mv. Wimbi; na tunaendelea
na ujenzi wa meli mpya kubwa ya “Mv. Mwanza, Hapa Kazi tu” itakayokuwa na uwezo
wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo. Kwenye Ziwa Victoria pia
tumejenga Chelezo kubwa kuliko zote kwenye Ziwa Victoria ili kujenga na
kukarabati meli.
Kwa upande wa Ziwa
Tanganyika, tumekarabati meli ya mafuta ya MT. Sangara na tupo mbioni kuanza
ukarabati wa MV Liemba. Kwenye Ziwa Nyasa tumejenga meli mpya ya kubeba abiria
200 na mizigo tani 200. Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba wenzetu kule
Zanzibar wamenunua meli kubwa mbili kwa ajili ya kutoa huduma katika Bahari ya
Hindi. Aidha, mipango ya kujenga meli mpya kwa ajili ya kutoa huduma kati ya
Bandari ya Mtwara na Comoro na kati ya Bandari ya Kalema na karemi nchini DRC,
nayo inaendelea. Sambamba na hayo, tumejenga vivuko vipya na kukarabati vivuko
vya zamani vipatavyo 17.
Kuhusu usafiri wa
anga, tumekamilisha ujenzi wa Jengo jipya la Abiria (Terminal III) katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere na tunaendelea na upanuzi wa
Viwanja vya Kimataifa vya Kilimanjaro (KIA) na Abeid Aman Karume kule Zanzibar.
Vilevile, ujenzi wa viwanja vingine 11 upo katika hatua mbalimbali, na tupo
mbioni kumpata Mkandarasi wa kujenga Uwanja wa Kimataifa wa Msalato hapa
Dodoma.
Tumekamilisha pia
ujenzi rada Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza; na kule Songwe/Mbeya ujenzi
wake unakaribia kukamilika. Sambamba na hilo, tumefufua Shirika letu la Ndege
(ATCL) kwa kununua ndege mpya 11, ambapo 8 tayari zimewasili. Hii imeongeza
idadi ya wasafiri wa anga nchini kutoka milioni 4.8 mwaka 2015 hadi milioni 5.8
mwaka 2018. Na faida nyingine ya kuwa na ndege tumeiona katika kipindi hiki cha
mlipuko wa ugonjwa wa corona, ambapo kwa kutumia ndege zetu tumeweza
kuwarejesha Watanzania wenzetu waliokwama nchi mbalimbali, ikiwemo India. Kama
tusingekuwa na ndege zetu, ingekuwa vigumu kuwarejesha Watanzania hao.
Ukiachilia mbali
uimarishaji wa miundombinu ya usafiri, tumeboresha upatikanaji wa nishati ya
umeme. Tumekamilisha Mradi wa Kinyerezi II, ambao umetuongezea Megawati 240; na
tunakaribia kukamilisha upanuzi wa mtambo wa Kinyerezi I utakaozalisha Megawati
325 kutoka Megawati 150 za sasa. Muhimu zaidi, tumeanza kutekeleza Mradi mkubwa
wa Bwawa la Nyerere kwenye Bonde la Mto Rufiji. Mradi huu unagharimu shilingi
trilioni 6.5 na utakapokamilika utazalisha umeme Megawati 2115, ambazo sio tu
zitatuhakikishia umeme wa kutosha na wa gharama nafuu lakini pia utatusaidia
kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi
makubwa ya kuni na mkaa. Tunaendelea pia kutekeleza miradi mingine kwa kutumia
vyanzo mbalimbali, ikiwemo maji, gesi asilia, jua, upepo, n.k. Aidha,
tumekamilisha miradi mikubwa ya kusafirisha umeme, ikiwemo Mradi wa Iringa –
Shinyanga; Makambako – Songea; Lindi – Mtwara; n.k.; pamoja na kuendelea
kutekeleza Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini, ambapo tumeongeza idadi ya vijiji
vilivyofikishiwa umeme kutoka 2,018 mwaka 2015 hadi vijiji 9,112 mwezi Aprili
2020. Nchi yetu ina vijiji 12,268; hivyo tumebakisha vijiji 3,156 tu kufikisha
umeme kwenye vijiji vyote nchini.
Kutokana na hatua tulizochukua, idadi ya watumiaji wa umeme (energy access) imeongezeka kutoka asilimia 35 hadi asilimia 85. Na hii imechagizwa na ushushaji wa gharama za kuunganisha umeme kutoka shilingi 177,000 hadi shilingi 27,000. Mafanikio mengine tuliyoyapata kwenye sekta ya nishati ni kupunguza tatizo la kukatikakatika kwa umeme. Katika kipindi chote cha miaka mitano nchi yetu haikuwahi kuingia gizani. Zaidi ya hapo, tumeokoa kiasi kikubwa cha fedha kwa kuzima mitambo ya kuzalisha umeme wa mafuta. Kwa mfano, kwa kuzima mitambo ya IPTL, Aggreko na Symbion tumeokoa shilingi bilioni 719 kwa mwaka. Hii ndiyo imesaidia TANESCO sasa ianze kujiendesha yenyewe.
Mheshimiwa Spika;
Wakati nikizindua
Bunge hili, nakumbuka niliahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ingeendeleza
jitihada za Awamu zilizotangulia za kukuza uchumi pamoja na kukabiliana na
matatizo ya umasikini na ukosefu wa ajira. Hivyo basi, katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita, tumejitahidi kutekeleza ahadi hiyo; hususan kwa kukuza sekta
zetu kuu za uchumi na uzalishaji, ikiwemo viwanda, kilimo, biashara, madini
pamoja na utalii. Kuhusu viwanda, tumejenga viwanda vipya 8,477, ambapo vikubwa
ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406, na vidogo sana 4,410. Hii imeongeza idadi
ya viwanda nchini kutoka 52,633 mwaka 2015 hadi viwanda 61,110 mwaka 2020.
Viwanda vipya vilivyojengwa vimeisaidia kuifanya nchi yetu kujitosheleza kwa
baadhi ya bidhaa, ikiwemo saruji, nondo na bati. Aidha, viwanda vipya
vimezalisha ajira 482,601.
Sambamba na kujenga
viwanda, tumeendelea kuweka mkazo kwenye sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji. Kama
unavyofahamu, sekta hii bado ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu.
Inachangia takriban asilimia 25 ya fedha za kigeni, asilimia 30 ya Pato la
Taifa, asilimia 65 ya malighafi za viwandani, asilimia 70 ya ajira zote nchini
na asilimia 100 ya mahitaji yetu ya chakula.
Hivyo basi, katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita tumeendelea kuipa kipaumbele sekta hiyo.
Tumeongeza upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo (mbegu bora, mbolea,
viatilifu, matrekta), tumeongeza uzalishaji wa miche ya mazao ya kimkakati,
tumejenga na kukarabati skimu za umwagiliaji, vihenge vya kuhifadhi mazao,
tumetafuta masoko na kuviimarisha vyama vya ushirika. Vilevile, tumeongeza
maeneo ya ufugaji kutoka hekta milioni 1.4 mwaka 2015 hadi hekta milioni 5
mwaka 2020 na hivyo kusaidia kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Tumejenga pia majosho mapya 104; tumeongeza idadi ya ng’ombe waliohamilishwa
kutoka 105,000 mwaka 2015 hadi 514,700 mwaka 2020, tumetoa chanjo ya mifugo na
kusambaza dawa za kuogeshea mifugo.
Tumeimarisha pia
ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi kwa kuanzisha Kanda Kuu tatu: Ziwa
Victoria, Tanganyika na Pwani; pamoja na kudhibiti matumizi ya zana haramu.
(Nakumbuka kuna wakati Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Mhe. Mpina alikuwa akitembea
na rula hadi kwenye migahawa). Zaidi ya hapo, tumehamasisha na kufanikiwa
kuongeza idadi wafugaji samaki kutoka 18,843 mwaka 2015 hadi 26,474 mwaka 2020;
tumeongeza idadi ya mabwawa kutoka 22,545 hadi 26,445; vizimba vya kufugia
samaki (fish cages) kutoka 109 hadi 431; na uzalishaji wa vifaranga kutoka
8,090,000 hadi 14,531,487.
Sambamba na hayo,
mwaka 2017, tulizindua Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP – II) wenye
malengo wa kukifanya kilimo chetu kuwa cha kisasa, cha kibiashara na chenye
tija. Vilevile, tumeiongezea mtaji Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) wa
shilingi bilioni 208 kupitia mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Serikali pia imeipatia TADB Dola za Marekani milioni 25.0 (sawa na shilingi
bilioni 57.8) ili kuendesha Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (SCGS) wenye
lengo la kuchagiza mabenki na taasisi za fedha kuongeza utoaji wa mikopo kwa
wakulima wadogo na makampuni madogo na ya kati ya kilimo (SMEs). Hii ina maana
kuwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imeipa TADB shilingi
bilioni 324.8 na hivyo kuiwezesha Benki hiyo kutoa mikopo ya moja kwa moja kwa
wakulima, wafugaji na wavuvi yenye thamani ya shilingi bilioni 166.9 kwa riba
nafuu.
Kutokana na hatua
hizi, mafanikio makubwa yamepatikana. Mathalan, uzalishaji wa mazao ya chakula
umeongezeka kutoka tani 15,528,820 mwaka 2015/2016 hadi tani 16,891,974 mwaka
2018/2019. Mahitaji yetu ya chakula kwa mwaka ni chini ya tani milioni 14. Kwa
upande wa mazao ya biashara, uzalishaji umeongezeka kutoka tani 796,502 hadi
tani 1,144,1631. Kwenye uvuvi, sangara kwenye Ziwa Victoria wameongezeka kutoka
tani 417,936 mwaka 2016 hadi tani 816,964 mwaka 2020, na urefu wa sangara
umeongezeka kutoka wastani wa sentimeta 16 hadi sentimeta 25.2. Vilevile, mauzo
ya samaki wetu nje ya nchi yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 379
mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 692 mwaka 2019. Haya sio mambo madogo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa lengo la kukuza
uchumi pia tumeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini,
ikiwemo kuanza kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini
(Blueprint) na kuanzisha Wizara Maalum ya Uwekezaji iliyopo chini ya Ofisi ya
Waziri Mkuu. Tumefanya marekebisho ya sheria mbalimbali na kupunguza urasimu
katika kutoa vibali na pia kufuta tozo kero 173 ambapo tozo 114 zinahusu sekta
ya kilimo, uvuvi na mifugo; tozo 54 za sekta nyingine mbalimbali; na tozo 5
zilikuwa zinatozwa na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa Kazi.
Kutokana na hatua
hizo, mafanikio makubwa yamepatikana kwenye nyanja za biashara na uwekezaji.
Biashara yetu ya nje imeongezeka kutoka shilingi trilioni 11.5 mwaka 2014/2015
hadi kufikia shilingi trilioni 16.6 mwaka 2018/2019. Jambo la kufurahisha zaidi
ni kwamba, Tanzania imekuwa na urari chanya wa mauzo ya bidhaa kwenye masoko ya
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na nchi za Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Mfano, kwa upande wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, kutoka mwaka 2015 hadi mwaka 2018, Tanzania imekuwa na urari
chanya wa mauzo ya bidhaa kwa wastani wa Dola za Marekani milioni 288.04.
Kuhusu uwekezaji, Kituo chetu cha Uwekezaji kimesajili miradi mipya 1,307 yenye
thamani ya Dola za Marekani bilioni 14.607, zaidi ya shilingi trilioni 30, na
itakapokamilika itatoa ajira 183,503.
Mheshimiwa Spika;
Kwenye sekta ya
madini, mageuzi makubwa sana yamefanyika, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Wizara
mahsusi ya Madini, kudhibiti utoroshaji na usafirishaji wa madini ghafi nje ya
nchi, kuanzisha masoko ya madini kwenye kila Mkoa, kuongeza ushiriki wa
wafanyabiashara wetu wadogo kwenye mnyororo wa uchumi wa madini na kuwafutia
ama kuwapunguzia viwango vya kodi. Zaidi ya hapo na muhimu zaidi, mwezi Julai
2017, tulipitisha Sheria ya Kulinda Rasilimali za Taifa (The Natural Wealth and
Resources – Permanent Sovereignty - Act 2017), ikiwemo madini. Nakushukuru sana
wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupitisha Sheria
hii muhimu sana kwa Taifa letu. Kwa hakika, mmeingia kwenye vitabu vya historia
vya nchi yetu na naamini vizazi hadi vizazi vitawakumbuka.
Kupitishwa kwa
Sheria hiyo ndiko kumewezesha kwa mara ya kwanza Watanzania kumiliki rasilimali
zao kwa nguvu za kisheria. Na Sheria hiyo pia ndiyo imefanikisha kuanzishwa kwa
Kampuni ya Twiga Minerals Company, ambayo Serikali yetu inamiliki hisa asilimia
16 na Kampuni ya Barrick asilimia 84 ya Hisa, na halikadhalika kutolewa kwa
malipo ya fidia ya Dola za Marekani milioni 100 kati ya Dola za Marekani 300
ambazo Kampuni ya Barrick ilikubali kutulipa kufuatia majadiliano tuliyofanya.
Napenda pia nikushukuru wewe, Mheshimiwa Spika, kwa Kuunda Kamati Maalum ya
Bunge ya Kuchunguza Utoroshaji wa Madini ya Tanzanite, ambayo ilitoa ushauri wa
kujenga Ukuta wa kilometa 25 katika Mgodi wa Mirerani, ambao Serikali
iliutekeleza.
Kutokana na hatua
mbalimbali tulizochukua, sekta ya madini sasa imeanza kukua kwa kasi kubwa,
ambapo mwaka jana (2019) iliongoza kwa ukuaji (kwa asilimia 17.7), ikifuatiwa
na ujenzi asilimia 14.1. Aidha, mapato yatokanayo na madini nayo yameongezeka.
Mathalan, kwenye mwaka wa Fedha 2018/2019 zilikusanywa shilingi bilioni 346
kutoka shilingi bilioni 194 mwaka 2016/2017. Kwenye Mwaka huu wa fedha
(2019/2020) tunatarajia tukusanye shilingi bilioni 470, ambapo mwezi Aprili
2020 pekee, licha ya kuwepo kwa tatizo la ugonjwa wa corona, tumekusanya shilingi
bilioni 58. Haijawahi kutokea. Kiwango cha juu kabisa tulichowahi kukikusanya
kwa mwezi ilikuwa shilingi bilioni 43.
Mafanikio mengine
tuliyoyapa kwenye sekta ya madini ni kutolewa kwa leseni 221 za uchenjuaji
madini, leseni 4 za uyeyushaji madini (smelting) na leseni 4 za usafishaji
madini (refining). Vilevile, tumetenga hekta 38,567 kwa ajili ya uchimbaji
mdogo na kuwapatia mafunzo wachimbaji wadogo 10,338. Kwa ujumla, hivi sasa
wachimbaji wadogo hawabughudhiwi. Mtakumbuka, zamani wachimbaji wadogo
waliendesha shughuli zao kama wakimbizi. Sisi tukasema, hatutaki kuona wananchi
wetu wakiwa wakimbizi ndani ya Taifa lao. Na kweli, kwa hatua tulizochukua,
tumeweza kujenga heshima kwa wananchi kwa kuwawezesha kutengeneza maisha yao
bila bugudha.
Kuhusu utalii,
tumechukua hatua mbalimbali za kukuza sekta hiyo ikiwemo kuanza kutekeleza
Mpango wa Uendelezaji Utalii Nyanda za Kusini, kuanzisha hifadhi mpya 5
(Hifadhi ya Nyerere, Chato – Burigi, Ibanda-Kyerwa, na Rumanyika-Karagwe) na
kuongeza jitihada za kutangaza vivutio tulivyonavyo kimataifa, ikiwemo
kuanzisha Chaneli Maalum ya Utalii ya Televisheni ya Taifa. Aidha, kama
tulivyoahidi, tumezidisha mapambano dhidi ya ujangili kwa kuanzisha Jeshi Usu
na hivyo kusaidia kuongezeka kwa idadi ya wanyama waliokuwa kwenye hatari ya
kutoweka kama vile faru na tembo. Mathalan, idadi ya faru imeongezeka kutoka
162 mwaka 2015 hadi 190 mwaka 2019; na tembo wameongezeka kutoka 43,330 mwaka
2014 hadi 51,299 mwaka 2019.
Kufuatia hatua
hizo, idadi ya watalii na mapato yameongezeka. Kwa mfano, mwaka 2019 tulipokea
watalii 1,510,151 kutoka watalii 1,137,182 mwaka 2015. Aidha, mapato
yaliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi kufikia Dola
za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2019. Kama isingekuwa tatizo la kuibuka kwa janga
la korona, naamini mwaka huu pia idadi ya watalii na mapato yake yangeongezeka.
Sekta nyingine,
ambayo haijasemwa sana lakini kwa sasa ina mchango mkubwa kwenye uchumi wetu ni
sanaa na utamaduni. Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2018,
shughuli za Sanaa na Burudani ziliongoza kwa ukuaji mwaka 2018 ambapo ilikua
kwa asilimia 13.7 na mwaka 2019 ilishika nafasi ya tatu kwa ukuaji wa asilimia
11.2. Hongereni sana wasanii wetu mbalimbali, hususan wa Bongo Fleva na Filamu.
Kazi zenu sio tu zinaburudisha na kuchangia ukuaji uchumi, lakini pia
zinaitangaza nchi yetu kimataifa. Na katika hilo, naipongeza Timu yetu Taifa ya
Soka, ambayo baada ya takriban miaka 39 kupita, hatimaye mwaka jana (2019)
ilifanikiwa kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Afrika. Nawapongeza pia
wanamichezo wengine waliopeperusha vyema bendera yetu katika miaka mitano
iliyopita, hususan katika ndondi na riadha. Mheshimiwa Spika, kutokana na
mchango mkubwa unatolewa na wasanii na wanamichezo nchini, Serikali imejipanga,
katika miaka mitano ijayo, kuweka mkazo mkubwa zaidi kwenye sekta hii ambayo
imewaajiri vijana wetu wengi.
Sekta nyingine
tulizoshughulikia na kutoa mchango kwenye ukuaji uchumi ni ulinzi, sayansi na
teknolojia, habari, misitu, ufugaji nyuki, mazingira; n.k. Kwenye ulinzi,
mathalan, tumeviimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi,
Polisi, Idara ya Usalama, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto, TAKUKURU na Mamlaka ya
Kudhibiti Madawa Kulevya, kwa kuvipatia vifaa na zana za kisasa). Kwa upande wa
sayansi na teknolojia, tumeanzisha vituo mahiri vya mafunzo kwa taasisi za
elimu ili kuzalisha vijana wenye uwezo unaohitajika Kitaifa, Kikanda na
Kimataifa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 75. Taasisi hizo ni: Taasisi
ya Teknolojia Dar es Salaam itakayobobea katika TEHAMA na Taasisi ya Teknolojia
Mwanza itakayobobea kwenye masuala ya Ngozi), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji
kitakachobobea katika taaluma za anga na Chuo cha Ufundi Arusha kitabobea
katika nishati. Kwa sababu ya ufinyu wa muda sitoweza kuzielezea sekta zote.
Itoshe tu kusema, Serikali imejitahidi kuimarisha sekta zote ili kukuza uchumi
nchini.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na hatua
tulizochukua za kuimarisha sekta mbalimbali, uchumi wa nchi yetu umeendelea
kukua vizuri, ambapo kwa wastani, katika miaka mitano iliyopita, umekua kwa
asilimia 6.9 kutoka ukuaji wa asilimia 6.2 mwaka 2015. Pato ghafi la Taifa
limeongezeka kutoka shilingi trilioni 94.349 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi
trilioni 139.9 mwaka 2019; kwa bei ya miaka husika (yaani current prices). Hii
sio tu imetufanya tuwe miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi lakini
imeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 zenye uchumi mkubwa zaidi Barani
Afrika.
Tumefanikiwa pia
kudhibiti mfumuko wa bei, kutoka asilimia 6.1 mwaka 2015 hadi kufikia wastani
wa asilimia 4.4. Sambamba na hilo, akiba ya fedha ya kigeni imeongezeka kutoka
Dola za Marekani bilioni 4.4 zilizokuwa zikitosheleza kununua bidhaa na huduma
kwa miezi 4.3 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 5.3 mwezi
Aprili, 2020 ambazo zinatowezesha kununua bidhaa na huduma kwa miezi 6.2.
Kiwango hiki ni zaidi ya lengo lililowekwa kwenye EAC (miezi 4.5) na SADC
(miezi 6).
Kwa upande wa
mapambano dhidi ya umasikini, umasikini wa kipato umepungua hadi kufikia asilimia
26.4 mwaka 2017/2018. Na kwa lengo la kuendelea kupambana na umaskini, mwezi
Februari 2020, tumezindua Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Mpango wa
Kunusuru Kaya Masikini (TASAF III), ambao utagharimu shilingi trilioni 2.032.
Kuhusu kukabiliana na tatizo la ajira, kupitia jitihada zilizofanyika, ikiwemo
utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, tumefanikiwa kutengeneza ajira
zipatazo 6,032,299. Kati ya ajira hizo, 1,975,723 zimezalishwa na sekta rasmi
na ajira 4,056,576 zimezalishwa na sekta isiyo rasmi.
Mheshimiwa Spika;
Mafanikio mengine
tumeyapata kwenye nyanja za sheria na utoaji haki. Katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita, tumejitahidi kupunguza vitendo vya rushwa, ucheleweshaji na
ubambikaji kesi, pamoja na tatizo la mlundikano wa wafungwa. Mathalan, ili
kukabiliana na tatizo la ucheleweshaji wa kesi, Serikali iliteua Majaji wapya
17 wa Mahakama ya Rufani, Majaji 52 wa Mahakama Kuu na kuajiri watumishi wa
mahakama 859, wakiwemo mahakimu 396. Aidha, tumejenga Mahakama Kuu mpya 2 (Mara
na Kigoma); na kukarabati nyingine nne Dar es Salaam, Mbeya, Shinyanga na
Sumbawanga. Tumejenga pia Mahakama za Hakimu Mkazi 5, za Wilaya 15 pamoja na
Mahakama za Mwanzo 18, na halikadhalika tumeanzisha Mahakama ya Kutembea
(mobile court), ambayo imeanza kufanya kazi kwenye Mikoa ya Dar es Salaam na
Mwanza na mpaka mwezi Machi 2020 ilishasajili mashauri 337 na kusikiliza
mashauri 274. Naipongeza Mahakama kwa kuchukua hatua za kupunguza mrundikano wa
kesi, ikiwemo kuimarisha matumizi ya TEHAMA ambayo sio tu imeharakisha
uendeshaji wa mashauri lakini pia imepunguza tatizo la rushwa kwa watumishi wa
Mahakama.
Vilevile, katika
jitihada za kukabiliana na tatizo la ucheleweshaji kesi, nilisaini Hati ya
kuiimarisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na pia
kuanzisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Uwekaji saini Hati hiyo umeongeza
tija na kuleta ufanisi mkubwa katika usimamizi na uendeshaji wa mashauri
Mahakamani na pia kwenye Mabaraza ya Usuluhishi ndani na nje ya nchi. Zaidi ya
hapo, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumewasamehe wafungwa 42,774
waliokuwa wakitumikia vifungo mbalimbali na hivyo kupunguza mlundikano
magerezani. Aidha, katika zoezi la ukaguzi na kusikiliza changamoto za wafungwa
na mahabusu, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imewafutia kesi mahabusu 2,812.
Nitumie fursa hii
kumpongeza sana Mheshimiwa Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi, Waheshimiwa Majaji
wengine, Mahakimu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa
ya Mashtaka pamoja na Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuimarisha mfumo wa utoaji
haki nchini.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi cha
miaka mitano iliyopita, tumeshughulikia pia kero mbalimbali za wananchi,
hususan wakulima, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara, wafanyakazi,
wajasiliamali; na bila kusahau migogoro ya ardhi. Kwa upande wa wakulima,
wavuvi, wafugaji na wafanyabiashara; kama nilivyosema awali, tumefuta takriban
tozo 114 zilizokuwa zikikwamisha shughuli zao. Kwa wafanyakazi, tayari
nimeshaeleza kuhusu upandishaji vyeo na malipo ya madeni mbalimbali. Zaidi ya
hapo, tumepunguza kodi ya mapato kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9 na kulipa
deni la shilingi trilioni 1.2 ambalo Serikali ilikuwa ikidaiwa na Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii; na hivyo kuwezesha wastaafu kuendelea kulipwa mafao yao.
Kwa upande wa
wajasiliamali wadogo, wakiwemo machinga, mama lishe, waendesha bodaboda na
bajaji, tumejitahidi kuwawekea utaratibu mzuri wa kuendesha shughuli bila ya
kubughudhiwa kwa kuwapatia vitambulisho maalum vilivyotolewa kwa gharama nafuu.
Mwaka jana (2019) jumla ya wajasiliamali wadogo 1,591,085 walipatiwa
vitambulisho na hivyo kuwafanya waondokane na usumbufu uliokuwepo. Mtakumbuka,
zamani, kabla ya utaratibu huo kuanza, wajasiliamali wadogo walikuwa
wakibugudhiwa sana na mgambo, ikiwemo kunyang’anywa mali zao. Hivyo, kwa
kuanzisha utaratibu wa kutoa vitambulisho hivyo, tumedhihirisha kuwa Serikali
ya Awamu ya Tano ipo kwa ajili ya wanyonge.
Sambamba na kutoa
vitambulisho kwa wajasiliamali wadogo, tumetunga Sheria yenye kuzitaka
halmashauri zote kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya kutoa mikopo
isiyo na riba kwa wanawake (asilimia 4), vijana (asilimia 4) na wenye ulemavu
(asilimia 2), ambapo hadi mwezi Machi kiasi cha shilingi bilioni 93.2 kilikuwa
kimetolewa.
Kero nyingine
tuliyoshughulikia ni ya migogoro ya ardhi. Baadhi ya hatua tulizochukua ni
kuanzisha Ofisi za Ardhi kwenye Mikoa yote, ambapo sasa huduma zote za
upangaji, upimaji, umilikishaji, utathmini pamoja na usajili wa hati, nyaraka,
ramani na michoro zinapatikana. Hii imeongeza kasi ya urasimishaji makazi ya
wananchi na pia utoaji hati. Jumla ya maeneo ya viwanja yaliyorasimishwa ni
764,158 na tumetoa hatimiliki za kimila 515,474. Kubwa zaidi, ni uamuzi
uliofanywa na Serikali wa kuvirasimisha vijiji 920 kati ya 975 vilivyokuwa
kwenye maeneo ya hifadhi.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi cha
miaka mitano iliyopita, tumeimarisha pia uhusiano na ushirikiano na mataifa ya
nje pamoja na taasisi za kimataifa. Hii ndiyo sababu tuliweza kuwapokea
viongozi wa nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa, ikiwemo Vietnam, India,
uturuki, Afrika Kusini, DRC, Ethiopia, Misri, Rwanda, Zambia, Zimbabwe, Uganda,
IMF, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, IFAD, n.k.
Katika kipindi
hicho pia tumefungua Balozi mpya 8 (Algeria, Cuba, Israel, Korea, Qatar,
Namibia, Sudan na Uturuki). Aidha, nchi mbili, Ethiopia na Poland, nazo
zimefungua Balozi zao hapa nchini. Sambamba na hayo, tumeendelea kushiriki
katika shughuli na mipango mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo ulinzi wa amani,
ambapo kwa sasa tuna askari wapatao 2,303 katika nchi za DRC, Jamhuri ya Afrika
ya Kati, Lebanon, Sudan na Sudan Kusini. Zaidi ya hapo, nchi yetu imeaminiwa
kuongoza jumuiya mbili za kikanda, Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanzia 2016
hadi 2017 na pia kuongoza SADC kuanzia Agosti 2019 hadi mwezi Agosti 2020
tutakapokabidhi. Na moja ya mafanikio tuliyoyapata katika kuongoza taasisi
hizo, ni kuzishawishi Nchi Wanachama kuridhia lugha ya Kiswahili kutumika
kwenye Taasisi hizo.
Mheshimiwa Spika;
Katika Ibara 151
(c) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020, Chama Cha Mapinduzi
kiliahidi, nanukuu “kusimamia azma ya Serikali ya kuhakikisha majengo yote ya
Wizara za Serikali yanajengwa Dodoma badala ya Dar es Salaam”, mwisho wa
kunukuu. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa ahadi hiyo
tumeitekeleza. Sio tu kwamba majengo ya Wizara zote yamejengwa Dodoma, bali
Serikali yote tayari imehamia, ambapo tarehe 13 Aprili, 2019 nilizindua Mji wa
Serikali pale Mtumba. Hii ina maana kuwa tumetekeleza ahadi yetu zaidi ya
tulivyoahidi. Nina imani, kwa kutekeleza ndoto hiyo iliyodumu kwa miaka 47, sio
tu tumemuenzi Baba wa Taifa lakini pia Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu
TANU waliofikia uamuzi ya kuhamishia Makao Makuu ya nchi Dodoma mwaka 1973.
Hivyo, naamini, Mheshimiwa Spika utanisemehe nikisema “CCM Oyee”. Hapo nilikuwa
nachomekea tu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kifupi sana,
haya ni baadhi tu ya mafanikio tuliyoyapata. Lakini, kama nilivyosema awali,
tumefanya mengi, ambayo kama ningeamua kuyaeleze yote hapa, tunaweza kukesha.
Kwa bahati nzuri, Watanzania wengi wameona na wanayajua. Hivyo basi, nina imani
wataendelea kutuamini na kutupa dhamana ya kuongoza nchi yetu katika kipindi
cha miaka mitano ijayo.
Na binafsi naamini,
kutokana na misingi imara tuliyoiweka ya ukuaji uchumi pamoja na uzoefu mkubwa
tulioupata, endapo wananchi wataendelea kutuamini na kutuchagua kuongoza nchi
yetu katika miaka mitano ijayo, tutafanya mambo mengine makubwa zaidi na hatimaye
kufanikiwa kutimiza ndoto na dhamira yetu ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya
uchumi wa kati wenye kuongozwa na viwanda pamoja na huduma za kiuchumi
(economic services) ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na mafanikio
yaliyopatikana, zilijitokeza baadhi ya changamoto. Kama ujuavyo, hapa dunia sio
rahisi kufanya jambo lisikumbane na changamoto ama vikwazo. Hivyo basi, sisi
pia, katika miaka hii mitano, tumekumbana na changamoto/vikwazo mbalimbali;
lakini kikubwa zaidi ni kuibuka kwa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na
virusi vya corona.
Napenda nitumie
fursa hii kulishukuru Bunge hili Tukufu kwa kupitisha Azimio la kunipongeza;
japo ukweli ni kwamba pongezi hizi zinatustahili Watanzania wote, ikiwa ni
pamoja na Bunge hili. Pamoja na hofu kubwa iliyokuwa imetawala, Bunge hili
liliendelea na vikao vyake kama kawaida kwa lengo la kuwatumikia Watanzania;
ingawa nafahamu wapo wachache walikimbia. Lakini niseme tu kwamba, kukimbia
haikuwa jambo sahihi kwa sababu matatizo au changamoto hazikimbiwi. Kukimbia
matatizo au changamoto ni ishara ya udhaifu, ni ishara ya woga lakini pia ni
ishara ya kutojiamini. Siku zote njia sahihi ya kukabiliana na matatizo ni
kukabiliana nayo.
Na hii ndiyo sababu
sisi, tuliamua kukabiliana na ugonjwa wa corona, huku tukiwa tumemtanguliza
Mwenyezi Mungu. Na tunashukuru, kwa kufanya hivyo, tumeweza mpaka sasa, kwa
kiasi kikubwa, sio tu kufanikiwa kuushinda ugonjwa huo lakini pia kupunguza
athari zake, zikiwemo athari za kiuchumi. Kama mnavyofahamu, Benki ya Dunia pamoja
na Shirika la Fedha Dunia, yamebashiri kwamba asilimia 60 ya nchi za Afrika
zilizopo Kusini mwa Janga la Sahara zitashuhudia ukuaji hasi wa uchumi mwaka
huu (2020). Hata hivyo, sisi Tanzania, kutokana na hatua tulizochukua, uchumi
wetu unatarajiwa kuendelea kukua vizuri kwa asilimia 5.5. Zaidi ya hapo,
tumeweza kulinda ajira za wananchi wetu, tuna uhakika wa usalama wa chakula na
pia tumeweza kuendelea na utekelezaji wa miradi yetu mikubwa ya kimkakati. Na
hii inadhihirisha kuwa maamuzi yetu yalikuwa sahihi na maamuzi ya Bunge hili
kuendelea na vikao nayo yalikuwa sahihi sana. Hongera sana Mheshimiwa Spika na
hongereni sana Waheshimiwa Wabunge.
Nitumie fursa hii,
kwa mara nyingine tena, kurudia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuliepusha Taifa
letu dhidi ya ugonjwa wa corona. Nawashukuru pia viongozi wa dini pamoja na
madhehebu mbalimbali kwa kuitikia wito wa Serikali wa kufanya maombi maalum ya
kumwomba Mwenyezi Mungu kutuepusha na Janga la Corona. Dua na maombi yao
yamedhihirisha kuwa penye hakuna linaloshindikana. Namshukuru na kumpongeza
Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja wajumbe wote wa Kamati ya Kitaifa ya kukabiliana
na ugonjwa wa corona. Kwa namna ya pekee, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya,
Ummy Mwalimu kwa kufanya kazi kwa ujasiri mkubwa sana. Vilevile, navishukuru
vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na madaktari na wauguzi wetu kwa kazi kubwa
na nzuri waliyoifanya na wanaoendelea kuifanya ya kuwahudumia wagonjwa wa
corona.
Na kutokana na hali
ya ugonjwa wa corona nchini kuendelea vizuri, napenda kutumia fursa hii
kutangaza kuwa, kuanzia tarehe 29 Juni, 2020 shule zote kuanzia za awali,
zifunguliwe na pia shughuli nyingine zote ambazo tulizizuia nazo zifunguliwe.
Maisha ni lazima yarudi kama ilivyokuwa zamani. Hata hivyo, naendelea kuwasihi
Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari na pia kuzingatia ushauri unaotolewa na
wataalam wetu wa afya.
Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge;
Kabla ya
kuhitimisha hotuba yangu napenda nirudie kuwashukuru Watanzania wote, wa
makundi yote, wakiwemo wakulima, wafanyakazi, wafugaji, wavuvi,
wafanyabiashara; kwa kuiunga mkono Serikali yetu, hususan kwa kudumisha amani
na mshikamano, kuchapa kazi kwa bidii, kulipa kodi; lakini pia kwa kuwa tayari
kufunga mkanda ili kuijenga Tanzania mpya. Nawashukuru pia viongozi wenzangu
wote wa Serikali tulioshirikiana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Namshukuru Makamu wa Rais, Mwanamama shupavu na jasiri, Mama Samia Suluhu
Hassan kwa kunisaidia majukumu; Namshukuru Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed
Shein, kwa ushauri na ushirikiano alionipa; namshukuru na kumpongeza pia
Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa heshima na unyenyekevu wake,
uchapaji kazi wake mzuri na kutanguliza mbele maslahi ya taifa. Kwa hakika,
amenisaidia sana. Aidha, namshukuru Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi
Seif Ali Iddi, pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi, Mheshimiwa Balozi John Kijazi,
kwa kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka. Vilevile, nawashukuru Waheshimiwa
Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kufanya kazi bila kuchoka. Nawashukuru pia Makatibu
Wakuu; Wakuu wa Mikoa; Makatibu Tawala wa Mikoa; Wakuu wa Wilaya; Makatibu
Tawala wa Wilaya; Wakurugenzi wa Wilaya, Manispaa na Majiji; Maafisa Tarafa;
Watendaji wa Kata na Vijiji, Mabalozi wa nyumba kumi pamoja na watumishi wote
wa Serikali kwa kufanikisha kupatikana kwa mafanikio yote niliyoyataja. Kwa
ujumla wao, wote wamenisaidia sana kwenye kufanya kazi.
0 Comments