Kituo cha Uwekezaji Tanzania -TIC katika kipindi cha Januari 2016 hadi Juni 2020 kimefanikiwa kusajili jumla ya
miradi 1,312 ya uwekezaji yenye mtaji wa thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 20 ikiwa ni takribani Shilingi Trilioni 46 za kitanzania na kutoa ajira ya Watanzania 178,101.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Bw. Geoffrey Mwambe akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar Es Salaam kuhusu mafanikio ya TIC katika kipindi cha Miaka mitano ya Uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Anaandika Grace Semfuko kutoka Dar es Salaam.
Katika usajili huo sekta ya
uzalishaji na usindikaji wa viwanda iliongoza kwa asilimia 54 ya miradi yote na ilitoa ajira kwa watanzania 67,992.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari Jijini Dar Es Salaam kuhusu mafanikio ya miaka mitano ya TIC, Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo hicho Bw. Geoffrey Mwambe, amesema tangu kuingia madarakani kwa
Rais Dkt John Pombe Magufuli, kumekuwa na mafanikio makubwa ya kujivunia kwenye
Sekta ya Uwekezaji.
“Katika Serikali ya awamu ya tano,
Kituo kimeendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano, dira yetu ilikuwa
ni kuwa Kituo bora kabisa Duniani kwa kuvutia uwekezaji wa maendeleo endelevu”alisema
Mwambe.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Bw. Geoffrey Mwambe akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar Es Salaam kuhusu mafanikio ya TIC katika kipindi cha Miaka mitano ya Uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Amesema Tanzania inao uwezo
mkubwa wa kufanya maendeleo ya kasi kwamba ndani ya miaka mitano tu hali ya
uchumi na maendeleo ya Taifa yamebalidika kwa kiwango kikubwa kuliko
ilivyotarajiwa.
“Watanzania tunapaswa kujivunia,
ndani ya miaka mitano tumebadili kabisa hali yetu ya uchumi na maendeleo ya
Taifa, watu wanaokuja hawaamini kwamba hii ni Tanzania ile waliyokuwa wanaijua
awali, ambayo hatukuwa na uwezo wa kutengeneza miundombinu yetu kama Reli ya kisasa
ya SGR, wanabakia tu kuhoji Tanzania mnaweza? Sisi tunasema ndio tunaweza”
alisisitiza Mwambe.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Bw. Geoffrey Mwambe akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar Es Salaam kuhusu mafanikio ya TIC katika kipindi cha Miaka mitano ya Uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Alizungumzia pia uboreshaji wa
TIC kwenye huduma za mahala pamoja (One Stop Facilitation Centre) akisema,
zimeboreshwa kwa kuongeza idadi ya taasisi zinazohudumia Wawekezaji kutoka
taasisi saba mwaka 2015 hadi kufikia 10 mwaka 2020, huku idadi ya watumishi
katika eneo hilo wakiongezeka kutoka 14 wa awali, na kufikia 25 lengo likiwa ni
kumrahisishia Mwekezaji.
Kuhusu kusogeza huduma za Uwekezaji
kwenye maeneo yote nchini Mwambe amesema ofisi za Kanda za TIC zimeongezeka
kutoka kanda tatu zilizokuwepo awali mwaka 2015 na kufikia Kanda Saba kwa mwaka
2020zikiwepo za Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya
Kaskazini, Kati, Magharibi na Mashariki.
Aidha alizungumzia pia hatua ya
TIC ya kuanzisha kamati ya Taifa ya uwezeshaji Uwekezaji (NIFC) ambayo
inahusisha Wakuu wa Taasisi za Serikali zinazotoa vibali na leseni mbalimbali
za uwekezaji yenye jukumu la kusaidia kuondokana na changamoto za sekta hiyo
kwenye maeneo yanayosimamiwa na Taasisi hizo.
Katika hatua nyingine Mwambe
amesema TIC imeboresha mifumo ya kuchakata na kutoa vibali kwa njia ya mtandao
ikiwpo utoaji wa cheti cha vivutio, usajili wa Kampuni pamoja na Vibali vya
kazi na ukaazi lengo likiwa ni kuwa na mkakati wa pamoja wa kushirikiana katika
shughuli zote za uhamasishaji, Uwekezaji na Biashara.
Kwa upande wa tafiti zinazofanywa na kituo
hicho Mwambe amesema umefanyika utafiti kuhusu mwenendo wa mitaji ya uwekezaji
kutoka nje ili kubaini hali halisi ya ukuaji, fursa na changamoto za kisekta
ili kuziboresha huku akizitaja tafiti hizo kuhusika kwenye maeneo ya kilimo,
mifugo, viwanda na mazingira ya biashara kwa ujumla.
Katika mkutano huo na Waandishi
wa Habari Mwambe pia alitoa matokeo ya tafiti za athari za uwekezaji
zilizofanywa kufuatia kuibuka kwa ugonjwa wa Homa kali ya mapafu (COVID-19) kwa
wawekezaji wa miradi iliyosajiliwa na TIC huku akiitaja sekta ya utalii na
viwanda vya uchakataji vinavyotegemea malighafi toka nje ya nchi.
Alisema katika kipindi cha
COVID-19 TIC iliendelea kufanya kazi kwa ustadi mkubwa na kuboresha mifumo ya
utendaji kazi kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa Afya
Mwisho.
0 Comments