Anaripoti Grace Semfuko, Dar es Salaam.
Amesema iwapo Wanawake kwa uwingi wao watawekeza, wataweza kuimarisha uchumi wa nchi kutokana na kuwa na nguvu kubwa ya kusimamia miradi pamoja na uaminifu wa shughuli za uendeshaji wa kiuchumi.
Waziri Kairuki ameyasema hayo Machi 6 wakati akifungua kongamano la siku ya Wanawake Duniani kwenye chuo kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) lililoandaliwa na Taasisi ya Taaluma za Jinsia ya Chuo hicho na kufanyika kwenye ukumbi wa Nkrumah.
Amesema Wanawake ni Taifa kubwa hivyo wakiwekeza wataweza kuinua pato na familia zao kwa ujumla.
“Ni vema tukaendelea kuwakumbusha kuwa tunatambua jitihada za wanawake wengine ambao wamemekuwa na mchango mkubwa katika Taifa letu, Wanawake ambao wameweza kujikomboa kiwamawazo, kifikra, kiuchumi na kisiasa, Wanawake wa Tanzania tunaweza kuwekeza, tusibaki nyuma” alisema Kairuki.
“Mtakubaliana nami kuwa licha ya hatua mbalimbali za mafanikio katika kumtambua na kumshirikisha mwanamke katika nafasi mbalimbali kwenye jamii zetu bado kuna kazi kubwa ya kufanya, tunatakiwa kuwa na jitihada za makusudi ili kuhakikisha nafasi na maslahi ya Mwanamke katika jamii inaendelea kutetewa kikamilifu” aliongeza Waziri huyo.
Alisema Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikiwapa kipaumbele Wanawake katika suala zima la uwezeshwaji wa kiuchumi kwa kuweka sera na sheria mbalimbali ambazo utekelezaji wake unampa fursa Mwanamke ya kujikwamua kiuchumi.
Aliyataja maeneo ambayo Serikali imeyaboresha ili kumpa fursa Mwanamke kuwa ni pamoja na uwezeshaji wanawake kiuchumi, kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, kuboresha huduma za afya ya uzazi, kuingiza masuala ya kijinsia katika Sera, sheria na bajeti, kuongeza ushiriki wa Wanawake katika ngazi za kutoa maamuzi, na haki katika masuala mbalimbali ya ypatikanaji wa kisheria.
Aidha alisema tangu kufanyika kwa mkutano mkuu wa wanawake Beijing Nchini China ambao ulikuwa na maadhimio 12 ya kumwinua na kutetea haki za wanawake, Serikali ya Tanzania imeyapa kipaumbele mambo hayo ambayo sasa yamekuwa na manufaa makubwa kwa wanawake.
“Mkutano huo wa Beijing mwaka 1995 ulikuwa na maadhimio makubwa 12 yakihusiana na haki na usawa wa maendeleo ya Wanawake, na sisi kama Serikali tumeweza kuweka msingi wa uwezeshaji na uimarishaji wa mikakati ya kusaidia ukombozi wa wanawake na Wasichana kwani mnaona hata kwenye elimu tunafanya hivyo” alisema Kairuki.
Mwisho.
0 Comments