Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Ndg. John Mnali akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya TIC katika kipindi cha mwaka 2021-2022.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 274 kwa kipindi cha Juni 2021 hadi Julai 2022, inayotarajiwa kuzalisha ajira 43,925 ikilinganishwa na ajira 36,470 zilizozalishwa mwaka 2020/2021.
Miradi hiyo ambayo ni ongezeko la asilimia 14.6, ipo katika sekta ya viwanda, usafirishaji, kilimo, ujenzi wa majengo ya biashara, miundombinu ya kiuchumi, taasisi za fedha, rasilimali watu, usafirishaji, utalii na huduma mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), John Mnali, amesema kuwa ongezeko la usajili wa miradi imetokana na Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ujenzi wa miundombinu wezeshi kama barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na umeme pamoja na sera ambayo imeendelea kuwekwa nchini, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
“Mnafahamu, Rais alipoingia madarakani, alieleza kabisa kuwa anataka kuifungua nchi, kwa hiyo wawekezaji wengi wamekuwa wakivutiwa katika kuanzisha miradi mbalimbali ya uwekezaji,” amesema Mnali.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji amebainisha kuwa diplomasia ya uchumi imekuwa chachu katika kuifanya Tanzania kuwa kivutio kikubwa katika kuwekeza barani Afrika kutokana na mazingira wezeshi.
“Kupitia mfumo wa uandikishaji kwa njia ya mtandao, kwa wale wanaoomba cheti cha uwekezaji, wanaweza kupata cheti ndani ya siku tatu ikiwa mradi umekamilisha kila kitu,” ameongeza Mnali.
Katika kipindi cha kuanzia Juni 2021 hadi Julai 2022 uhamasishaji uwekezaji wa nje umeendelea kufanyika kupitia makongamano ya uwekezaji yaliyofanyika Qatar, Doha na ushiriki wa TIC kwenye kongamano na maonesho haya yameleta matokeo chanya ambapo wawekezaji mbalimbali walifika nchini.
0 Comments